Baba Mtakatifu Francisko Ampongeza Askofu Mkuu Ruwa'ichi Kwa Jubilei Ya Miaka 25 ya Uaskofu
Na Celina Munde, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania
Askofu mkuu Angelo Accattino Balozi wa Vatican nchini Tanzania amempongeza Askofu mkuu Ruwa’ichi kwa kazi kubwa ya uinjilishaji aliyoifanya katika Majimbo mbalimbali nchini Tanzania hadi kufikisha Miaka 25 ya Uaskofu wake. Aidha amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Uaskofu. Baba Mtakatifu amemtakia utume mwema, afya njema na uthabiti katika kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam, daima akiwa chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Wazazi na walezi wametakiwa kutambua umuhimu wa elimu jamii na elimu jumuishi ili kumtokomeza adui ujinga kwani sifa ya mtu mwenye elimu ni yule anayejifunza kwa kusikiliza kutoka kwa watu wengine. Wito huo umetolewa na Askofu Wolfugang Pissa wa Jimbo Katoliki la Lindi, katika adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja takatifu ya Uaskofu wa Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., wa Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam katika viwanja vya Msimbazi Center, Jimboni Dar es Salaam. Askofu Pissa amempongeza Askofu mkuu Ruwa’ichi kwa miaka hiyo 25 ya Uaskofu na kubainisha kuwa Askofu mkuu Ruwa’ichi ni mtu mwenye kujifunza kutokana na kufanya kazi katika zaidi ya majimbo manne aliyofanya utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Askofu mkuu Ruwa’ichi ana kipaji cha kufundisha na kwamba, ni mfano bora wa kuigwa na changamoto kwa jamii ya watanzania kujikita katika malezi na makuzi bora ya watoto wa kizazi hiki.
Huu ni wajibu na dhamana kwa watanzania wote kusimama kidete kupambana na adui ujinga kwa kuwafundisha watoto wao maarifa, nidhamu na utu wema, hususan katika dhama hizi za ubabaifu. “Adui ujinga hatujamshinda Tanzania, tuanze sasa bado hatujachelewa tusisubiri tu walimu shuleni, nasema hivi kwa sababu wazazi na walezi leo hii hawana muda kabisa na hili sio jambo zuri” alisema Askofu Pissa. Kuna tabia ya watu wengi kutosikiliza mambo ya kweli au ya maisha ya kiroho na hivyo kujikuta wakifuata nafsi zao kwa kupenda sana miungu mali, badala ya kuangalia na kutimiza mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Viongozi wa Kanisa watambue kwamba, wao ni kioo cha jamii na mfano bora wa kuigwa, kumbe, wanapaswa kusimamia ukweli na kamwe wasiwe ni watu kulalamika kwa kila jambo. Wakitekeleza dhamana na wajibu wao katika misingi ya ukweli na uwazi, Kanisa litapiga hatua katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na huo utakuwa ni mtaji wa kwenda mbinguni. Aidha amemtia moyo Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., anaposherehekea Jubilei ya miaka 25 ya Daraja takatifu ya Uaskofu, aendelee kubaki na msimamo wake; huku akisali na, kuomba hekima ya Mungu imsaidie kulipeleka Kanisa alilokabidhiwa na Mungu ili kulifikisha mbinguni ndilo jambo pekee aliloitiwa huku akisaidiana na Mapadre wengine. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasimamie: Haki, Usawa, Utu, Heshima; wasimame kidete kulinda utambulisho wa Kanisa, Imani na Mafundisho ya Kanisa. Viongozi wa kanisa wajitambue na kutambua wajibu wao.
Kwa upande wake Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., ambaye ndiye Mjubilei wa miaka 25 ya uaskofu amesema katika majimbo aliyohudumia amebaini kwamba Kanisa Katoliki nchini Tanzania bado ni changa na lenye vijana wengi, lenye uhai mkubwa lakini lenye changamoto kubwa hasa vijana hawana mizizi katika Ukristo. Hivyo ametoa wito kwa wanaowahudumia kwa mambo ya kichungaji kusafiri nao wakiwasaidia kuifundisha imani na Neno la Mungu ili wakite mizizi katika Mungu na imani thabiti. Amesema Kanisa la Tanzania linawahitaji vijana lakini wanalojukumu kubwa la kuwalea na kuwasaidia ili waumiliki ukristo wao. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap katika maisha na utume wake wa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu amejitambua kwamba, yeye ni mlezi, mwalimu na kiongozi, mambo ambayo ameyapatia kipaumbele cha pekee kabisa. Katika miaka 43 ya Daraja Takatifu ya Upadre, alibahatika kuwa Paroko kwa miezi mitano tu na miaka mingine yote amekuwa akihudumu shuleni na ofisini, dhamana na utume, uliomwezesha kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii. Alipata fursa ya kutembelea nchi 38 Barani Asia, Ulaya, Marekani na Amerika ya Kusini akiwa Mshauri wa mkuu wa Shirika na huko kote alipata nafasi ya kuchangamana na watu wa hali tofauti tofuti na ilimfunza kufanya kazi za kutembelea vigango, jumuiya na familia binafsi. Hivyo amesema hakuna mtu anayekuwa Askofu kwa matakwa yake, bali ni kwa neema na mapenzi ya Mungu pekee. Kwa upande wake Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, amewashukuru wale wote waliohudhuria katika sherehe hii ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Askofu mkuu Ruwa’ichi alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Amempongeza Askofu mkuu Philip Arnold S. Anyolo wa Jimbo kuu la Nairobi kwa kushirikiana bega kwa bega na Askofu mkuu Ruwa’ichi katika kazi za kitume.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa wito kwa Watanzania kuhakikisha matumizi adili ya rasilimali za nchi kama njia ya kumshukuru Mungu. Makamu wa Rais ametoa wito huo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi (OFMCap) iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi Centre Jimbo kuu la Dar es Salaam. Amesema Viongozi na watumishi wa Serikali wanayo nafasi kubwa ya kusimamia vyema matumizi ya rasilimali za nchi na kuwaongoza watanzania katika kuhakikisha mazingira mazuri ya nchi yanatunzwa na kurekebishwa pale ambapo tayari yameharibiwa kwa uchomaji moto ovyo wa misitu, uharibifu wa vyanzo vya maji, uchafunzi wa mazingira ya mito na bahari. Amesema ni vema kumshukuru Mungu kwa neema zake kwa kusali au kumtolea maombi ya shukurani pamoja na kutimiza wajibu wa kutunza na kustawisha fadhila zote ambazo Mungu ametutendea. Amesema Watanzania wanaweza kumshukuru Mwenyezi Mungu vizuri zaidi kwa kuthamini na kuitunza nchi nzuri ya Tanzania waliyokirimiwa.
Amewasihi Watanzania kuwajibika kumshukuru Mungu kwa amani na mtangamano katika Taifa kwa miaka 63 ya uhuru na kuwezesha kuishi kwa ushirikiano baina ya watu wa imani, rangi, kabila na itikadi za kisiasa tofauti tofauti. Amesema ni baraka za kushukuru kwa kuwa na Taifa lenye ardhi nzuri, maziwa, mito na vijito, bahari, misitu, mabonde na milima, madini ya aina mbalimbali, wanyama wa kufugwa na wa porini, ndege, wadudu, neema ya mvua na hali ya hewa nzuri. Makamu wa Rais amesema ni wajibu kushukuru kwa kuwa shukurani inafungua milango iliyofungwa hususan pale binadamu anapokabiliwa na ugumu wa maisha, magonjwa, biashara kudorora, changamoto za kazi na mara zote Mungu humpa anayeshukuru zaidi ya kile anachoshukuru kukipokea kwani shukrani inaonesha kwamba, mtoa shukrani anatambua mchango wa mwenyezi Mungu katika maisha yake. Makamu wa Rais amempongeza Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., kwa kutimiza miaka 25 ya Uaskofu na kukumbuka kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye amemjalia neema nyingi na kumwezesha kutekeleza utume wake kikamilifu kwa miaka yote 43 ya Upadre wake ambayo 25 amekuwa Askofu. Aidha amempongeza kwa mchango mkubwa katika kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (Saint Augustine University of Tanzania;SAUT) na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Mtwara, Songea na Moshi.