Tafuta

Tarehe 13 Mei 2024, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, imezindua maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwake. Tarehe 13 Mei 2024, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, imezindua maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwake. 

Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida: Huduma Bora

Tarehe 13 Mei 2024, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, imezindua maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwake kwa kutoa tiba bure, kuwapatia wananchi nafasi ya kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali pamoja na kutoa huduma za kijamii. Maadhimisho haya yatafikia kilele chake Jumamosi tarehe 18 Mei 2024. Kutujuza zaidi, tunaye Padre Justin Boniface, Mkurugenzi wa Hospitali anayefafanua maana: kutibu, kufariji na kuelimisha! Yaani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. wakisukumwa na kauli mbiu ya: Elimisha, Tibu na Fariji walianza rasmi kutoa huduma za afya Itigi, Manyoni, Singida nchini Tanzania tarehe 15 Septemba 1987. Lengo kuu likiwa ni kutoa huduma kwa maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Itigi ya wakati huo si Itigi ya Mwaka 2024 kuna mabadiliko makubwa. Nia hii njema ilizidi kukuwa na baada ya miaka miwili huduma hii ilipanuka na hivyo kufunguliwa rasmi kwa Hospitali ya Mtakatifu Gaspari na Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi tarehe 15 Mei 1989. Miaka 35 ya uwepo wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, imeendelea kupanuka na kukua katika shughuli na huduma zake na tarehe 12 Oktoba 2010 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kuipandisha hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa ngazi ya mkoa. Hospitali ina jumla ya vitanda 320. Katika wodi kuu nne ambazo ni: Wodi ya magonjwa mchanganyiko (Medical ward), Wodi ya Upasuaji (Surgical ward), Wodi ya Uzazi na Magonjwa ya Kike (Obstetrics & Gynaecology), Wodi ya watoto chini ya miaka 12 (Paediatrics ward) na Wodi maalum na ya magonjwa ya mlipuko ((Privates & Isolation).

Katika kipindi cha Miaka 35 huduma zimeboreka maradufu
Katika kipindi cha Miaka 35 huduma zimeboreka maradufu

Kwa hivi sasa Hospitali ina jumla ya watumishi 297. Hospitali inao madaktari bingwa 5. Ili kuboresha zaidi huduma ya tiba kwa wagonjwa, kwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari, ikaanzisha Chuo cha Uuguzi cha Mtakatifu Gaspari na kuzinduliwa rasmi tarehe 4 Septemba 2016. Chuo hiki kinapatika ndani ya eneo la Hospitali ya Mtakatifu Gaspari na kila mwaka “hufundisha wauguzi wa kesho.” Kuanzia Novemba 2, 2020, shule hiyo iliinuliwa kwa viwango vya Chuo, na kuwa Chuo cha Mtakatifu Gaspari cha Sayansi ya Afya na Ushirika na hivyo kuongozwa na kauli mbiu “Tufanye mengi, vizuri na kwa haraka.” Tarehe 13 Mei 2024, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari, imezindua maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwake kwa kutoa tiba bure, kuwapatia wananchi nafasi ya kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali pamoja na kutoa huduma za kijamii. Maadhimisho haya yatafikia kilele chake Jumamosi tarehe 18 Mei 2024.

Chuo cha Mt. Gaspari cha Sayansi ya Afya na Ushirika
Chuo cha Mt. Gaspari cha Sayansi ya Afya na Ushirika

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican Padre Justin Boniface, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana nao katika kumshukuru Mungu na kuendelea kuomba neema na baraka zake, ili awawezeshe kutoa huduma bora zaidi kwa watu wa Mungu Kanda ya Kati, kwa kuzingatia kauli: “Elimisha, Tibu na Fariji. Kutibu ni nafasi ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia watu wake kwa kuwa na utaalam wa kuganga, kutibu na kuponya maradhi yanayomsumbua mwanadamu. Faraja ya kweli ni Kristo Yesu. Kumbe, mchakato wa uinjilishaji wa kina unawasaidia watu wa Mungu kuona sura ya ufunuo wa: faraja, huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.

Kumbukizi ya Miaka 35 ya huduma bora ya afya kwa watu wa Mungu.
Kumbukizi ya Miaka 35 ya huduma bora ya afya kwa watu wa Mungu.

Kwa hakika, upendo wa Kristo kwa waja wake ndicho kilele cha faraja yenyewe na kwamba, hata katika mateso, Mwenyezi Mungu kamwe hamwachi mja wake. Changamoto zilizoibuliwa kwenye sekta ya afya zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na kukazia umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika udugu wa kibinadamu. Elimu maana yake ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye, kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano ya kijamii sanjari na hofu ya Mungu. Kumbe baada ya kugundua shida na changamoto zinazowakabili wagonjwa, wanaelimishwa ili kuchukua tahadhari, kinga na kujipatia tiba pamoja na kujenga utamaduni wa kuwajali wengine.

Hospitali ya Mt. Gaspari
14 May 2024, 14:54