Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari Itigi, Miaka 35 ya Huduma Kwa Maskini
Na Padre Justin Boniface Mwanyelo, C.PP.S., na Ndahani Lugunya, Itigi-Singida, Tanzania
Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari-Itigi, Jimbo Katoliki la Singida inayosimamiwa na kuendeshwa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania, inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 35 tangu ilipoanza kutoa huduma za afya tarehe 15 Mei 1989. Kilele cha Maadhimisho hayo kimetanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye viunga vya Hospitali hiyo ya Rufaa, na kuongozwa na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC huku akishirikiana na Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida. Askofu mkuu Nyaisonga amesema, Injili imeendelea kuhubiriwa kwa njia ya huduma mbalimbali za afya zinazotolewa na Wakristo na wasio wakristo. Kanisa linajivunia miaka 35 ya kupigania afya na maisha bora, jambo la kumshukuru Mungu na kuwapongeza wahudumu wa Hospitali hii. Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. wakisukumwa na kauli mbiu ya: Elimisha, Tibu na Fariji walianza rasmi kutoa huduma za afya Itigi, Manyoni, Singida nchini Tanzania tarehe 15 Septemba 1987. Lengo kuu likiwa ni kutoa huduma kwa maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbalimbali. Dira ya Hospitali hii ni kielelezo cha shauku ya kuwa ni kitovu cha ufanisi wa huduma bora za afya na mafunzo kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema mambo yasiyokinzana na kanuni na mafundisho ya Kanisa Katoliki, daima wakifuata agizo la Kristo Yesu la kuhubiri Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kwa kuendelea kujikita: “katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki” kama anavyoandika Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa 2Kor 6:6.
Hizi ni kanuni msingi zinazoongoza tiba inayotolewa kwenye Hospitali za Kanisa Katoliki. Kuhusu kaulimbiu ya “Elimisha, Tibu na Fariji” imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa katika kipindi cha miaka 35 ya maisha na utume wake, kwa sababu Hospitali hii ilianza kama Zahanati tu, jambo la kumshukuru Mungu kutoka vitanda 100 vya awali hadi kufikia vitanda zaidi ya 300 si haba. Kuna wengine walianza kutoa huduma ya afya kama hii, lakini wameishia njiani, kumbe, kuha kila sababu ya kumshuruku Mungu kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa. Hii ni hospitali inayojali utu, heshima na haki msingi za wagonjwa, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu Ukanda wa Kati kuitumia kikamilifu, ili izidi kuwa ni chombo cha elimu bora ya afya. Kwa upande wake Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., amewataka watumishi na wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari, kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa na kwamba, Hospitali hii imekuwa ni msaada mkubwa kwa maskini na wanyonge, jambo la kumshukuru Mungu. Amelishukuru Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia kwa kuendelea kushikamana na Kanda ya Tanzania katika huduma. Ameiombea Hospitali hii heri na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili iendelee kuwa ni chemchemi ya baraka na faraja na kwamba, Jimbo Katoliki la Singida litaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, ili kuhakikisha kwamba, Hospitali hii inaendelea kuwa ni kitovu cha kuelimisha, kufariji na kutibu. Amesema, huu ni utume wa watu wengi, kumbe, ameishukuru pia Serikali ya Mkoa wa Singida kwa ushirikiano wake.
Katika Adhimisho hilo ameshiriki pia Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Chesco Peter Msaga C.PP.S., Padri Terenzio Pastore, C.PP.S., Mwakilishi wa Mkuu wa Kanda ya Italia, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Tanzania Padri Vedastus Ngowi C.PP.S, Mkurugenzi wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar-Itigi Padri Justine Boniface C.PP.S., Mapadri na Watawa mbalimbali wa kike na kiume. Wakati huo huo, Serikali ya Mkoa wa Singida imewahakishia Wadau wa Maendeleo ikiwemo Uongozi wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar ya Halmashauri ya Itigi Wilayani Manyoni kuwa itaendelea kudumisha ushirikiano uliotukuka katika shughuli mbalimbali wanazofanya ikiwemo utoaji wa huduma bora za msingi na za kibingwa za afya kwa wananchi wa mkoa huo. Mkuu wa mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, ametoa kauli hiyo tarehe 14 Mei 2024 wakati anazungumza katika maadhimisho ya Miaka 35 ya Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari, Itigi, Manyoni, Sindiga, Tanzania. Halima Dendego, amesema amefurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Viongozi na Watendaji wa Hospitali hiyo katika utoaji wa huduma za kiwango cha juu za afya ikiwemo mama na mtoto pamoja na uboreshaji majengo na vifaa tiba. “Baraka na mkono wa Mungu uwe pamoja nasi na tuendelee kumwomba ili aendelee kutubariki zaidi ya hapa, Mhe. Halima Dendego. Mkuu wa mkoa huyo amesema yeye na watendaji wake wataendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mashirika yenye nia njema ya kuwaletea maendeleo ya uhakika wananchi wa mkoani Singida yanafikia malengo yao kwa kutoa huduma zao bila usumbufu wowote. Aidha amesisitiza Viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari, Itigi, Manyoni, kama wanachangamoto yoyote ambayo inaweza kusababisha kudumaza au kuchelewesha utoaji wa huduma za afya kwenye Hospitali hiyo wamweleze ili aweze kuzitafutia majawabu haraka iwezekanavyo ili wananchi waendelee kupata huduma bora za kisasa za afya.
Na Padre Justin Boniface, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspari: Hospitali ya Mtakatifu Gaspari ipo katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida katika Jimbo Katoliki la Singida. Hospitali ya Mt. Gaspari inamilikiwa na kusimamiwa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu na iko katika Jimbo Katoliki la Singida. Dira ya hospitali ni kuwa Kitovu cha Ufanisi wa Huduma Bora za Afya na Mafunzo kwa Kuzingatia Kanuni za afya zisizokinzana na kanuni za Kikatoliki. Dhima ya Hospitali: Kutibu, Kufariji na Kuelimisha. (Kutoa Huduma za Hali ya Juu za Tiba, Elimu na Utafiti ulio makini kwa jamii zilizo pembezoni kulinganna na Kanuni za Afya zisizokinzana na Mafundisho ya Kanisa Katoliki. Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu walianza kutoa huduma za Afya Itigi katika level ya Zahanati iliyofunguliwa rasmi na Fr. Dino Gioia, C.PP. S tarehe 24, September 1987. Mnamo tarehe 15 Mae, 1989 Hospitali ya Mtakatifu Gaspari ilifunguliwa rasmi na aliyekua Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Ali Hassan Mwinyi. Wakati huo hospitali ilikua na wastani wa vitanda mia moja (100). Ilikuwa inatoa huduma za msingi pamoja na huduma za kibingwa katika fani za upasuaji (general surgery), huduma za Watoto (paediatriacs), na huduma za uzazi na magonjwa ya wakina mama: (obstetrics and gynaecology). KUKUA KWA HOSPITALI: Miaka michache baadae hospitali ilipanuliwa na kuongeza jengo la wodi ya magonjwa ya ndani (medical ward) lenye vitanda 64 na hivyo uwezo wa hospitali ukawa ni vitanda 164. Mwaka 2003, Upanuzi wa hospitali uliendelea kutokana na mahitaji ambapo jengo la Watoto (paediatric complex) lilifunguliwa rasmi tar 22, Novemba, 2023 likiwa na vitanda 156 na hivyo idadi ya vitanda kwa hospitali nzima kuwa 320. Mwaka 2010 kutokana na ukubwa wa hospitali na huduma zinazotolewa, serikali iliipandisha hadhi hospitali ya Mt. Gaspar na kuwa Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa (kutoka hospitali ngazi ya Wilaya).
Mwaka 2014, Hospitali iliongeza huduma za upasuaji kwa Watoto kwa kufungua rasmi jengo la upasuaji kwa watoto (paediatric operating theatre) katika jengo la Watoto. Jengo hili lilibarikiwa na Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo tarehe 07 Februari, 2014. Huduma zetu ziliendelea kupanuka ambapo mwaka 2019 huduma za “CT-Scan na Endoscopy” zilizinduliwa rasmi katika hospitali yetu na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan wakati huo akiwa Makamu wa Rais. Mwaka 2022 tulianza kutumia mfumo wa kompyuta (electronic health management system -ehms) katika idara zote kwenye hospitali yetu. Hii imesaidia sana katika kurahisha huduma, kutunza kumbukumbu za wagonjwa na kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali za hospitali kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa. Mwaka 2022 Hospitali ilifungua kliniki ya kisasa meno pamoja na upanuzi wa huduma za matibabu ya mazoezi (physiotherapy). Mwaka 2023, tulifungua rasmi idara ya Huduma za Dharura (Emergency department) na idara ya wagonjwa walioko kwenye uangalizi maalum (ICU). Hii imeasaidia sana kuboresha huduma na kupunguza vifo vinavyozuilika. Mwaka huu wa 2024 hospitali imefanya maboresho na ukarabati wa jingo na wodi ya kinamama (maternity ward) ambapo imeweka vifaa vya kisasa, kuongeza HDU (High Dependent Unit) na NCU (Neonatal/Newborn Care Unit) katika wodi ya wazazi. Vilevile mwaka huu wa 2024 hospitali imeanza ujenzi wa idara ya kusafisha figo (Dialysis unit) kwa kushirikiana na AHN (Africa Healthcare Network) unaotegemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa sita 2024.
Kwa kuzingatia dhima ya Hospitali {Mwaka 2006, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu walianzisha Chuo cha Uuguzi cha Mtakatifu Gaspari kilicho sajiliwa kama “St. Gaspar School of Nursing” kilichopo ndani ya eneo la hospitali ambapo hospitali ya Mtakatifu Gaspari hutumika kama hospitali ya mafunzo kwa chuo. Mwaka 2020 chuo kilipandishwa hadhi na kuwa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Mtakatifu Gaspari. (Kilichosajiliwa kama St. Gaspar College of Nursing and Allied Sciences) Kwa sasa chuo kinatoa kozi za uuguzi na ukunga katika ngazi ya diploma, kozi ya Utabibu, kozi ya Diploma ya Maabara (Diploma in Laboratory Technology) na Chuo kikombioni kuanzisha kozi ya Ufamasia ngazi ya diploma. (diploma in Pharmaceutical Sciences).} HUDUMA: Kwa sasa Hospitali inatoa huduma za afya ya msingi pamoja na huduma za kibingwa katika idara ya Watoto, Uzazi na Magonjwa ya kina mama, Magonjwa ya ndani (internal medicine), Upasuaji, Kurekebisha viungo na makovu (Plastic and Reconstructive surgery), Upasuaji wa Kurekebisha Mdomo Sungura (Cleft lip and palate surgeries) bure, Matibabu ya Miguu Kifundo (Club – foot management) bure, na Dignostic and Interventional Endoscopy). Pia Hospitali imeongeza mashine na wataalam katika idara ya Radiologia na Maabara ambapo tunafanya karibia vipimo vyote muhimu vinavyomwezesha daktari kuweza kumtibu mgonjwa kwa uhakika zaidi. Vilevile tunatoa huduma za kliniki tembezi kwa wamama wajawazito na Watoto chini ya miaka mitano bure katika vijiji vilivyopo mbali na hospitali yetu na ambako hakuna zahanati (mfano Kazikazi station nk). Hata hivyo, hivi karibuni Hospitali imeanza kutoa pia huduma za kibingwa za klinic tembezi (outreach services) katika halmashauri ya Itigi ambapo tunatoa huduma kwa wananchi waliopo vijiji vya mbali na hospitali yetu ambao kwa sababu moja ama nyingine wanashindwa kufika hapa hospitalini kupata huduma hizi.
MIPANGO YA BAADAYE (FUTURE PLANS): Ili kuendelea kuhudumia jamii inayoizunguka hospitali kwa ukamilifu Zaidi hospitali inampango wa Kuongeza madaktari bingwa wa mifupa (orthopaedic surgeon), masikio, pua na koo (ENT surgeon), mfumo wa mkojo (Urologist) pathologia (Pathologist), macho (Ophthalmologist) na Kuanzisha huduma za upasuaji wa matundu (Laparascopic surgeries), huduma za Histopathology, huduma za matibabu ya saratani kwa Watoto (paediatric oncology unit) na kuwa na mtambo wa kuzalishia oksijen kwa matumizi ya wagonjwa na kwa ajili ya hospitali jirani.