Jimbo Kuu la Tabora: Daraja la Ushemasi na Upadre 2 Mei 2024
Na Frt. Lazaro Felix Mahangale
Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja; Upadre na Ushemasi. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa ya kudumu na hivyo kufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya “Shemasi”, yaani Mtumishi wa wote! Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre katika maadhimisho ya Mafumbo ya Mungu na kwa namna ya pekee, Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Mashemasi ni wahudumu wa Neno la Mungu kwa kutangaza na kuhubiri Injili; kwa kusimamia na kubariki ndoa; kwa kuongoza mazishi na hasa zaidi kwa kujitoa kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kwa niaba ya Kanisa. Ni katika muktadha huu, Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, tarehe 2 Mei 2024 anatarajiwa kutoa Daraja takatifu la ushemasi kwa: Frt. Abel Paul Luhende, Frt. Clement Mathew Masuhuko, Frt. Emmanuel Joseph Mashenene, Frt. Emmanuel Gervas Jilungu, Frt. Francis Masumbuko Tesha, Frt. Francisko Milembe Rutaha, Frt. John Kulwa Mathew, Frt. Lazaro Felix Mahangale na Frt. Paul Usiga Kagolo. Pamoja nao ni Shemasi Constantine Elias Kagudi atakayepatiwa Daraja Takatifu ya Upadre.
Ifuatayo ni historia ya Jandokasisi Lazaro Felix Mahangale wa Parokia ya Urambo, Jimbo Kuu Katoliki la Tabora. Nilizaliwa tarehe 06/11/1994 katika Kijiji cha Mapambano – wilaya ya Urambo Mkoani Tabora. Mimi ni mtoto wa tano kati ya watoto nane wa baba Felix Ernest Mahangale na mama Hilaria Lazaro Gwasa. Nilipatiwa Sakramenti ya Ubatizo: 01/12/1995. Komunyo ya kwanza: 25/05/2008, na Kipaimara: 15/08/2010, Sakramenti zote hizi nilipatiwa katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Urambo, Jimbo kuu la Tabora. Historia ya wito wangu: Katika makuzi yangu hata kuanza safari ya wito wa kuwa Padre, ni watu wengi sana wameshiriki kunisaidia kuitikia wito huu. Tukianzia miaka ya mwanzoni nikiwa na miaka 3-8 hivi, nilikuwa nikiishi kwa Babu na Bibi wazazi wa Mama yangu katika kijiji kinachoitwa Kapalamasa, Parokia ya Ndono, Jimbo Kuu la Tabora. Huko niliishi nikifanya kazi ya kuchunga mifugo ya Babu yangu kama vile; ng’ombe, kondoo, na mbuzi. Hakukuwa na suala la kuenda shule, kwani kijiji hicho hakikuwa na shule kwa wakati huo. Ilitokea kama bahati tu, pale ambapo wanakijiji waliona umuhimu wa watoto kupata elimu, hivyo wakajitolea kuandaa eneo na kujenga kijengo kidogo cha kufundishiwa. Haikuwa rahisi, kwani hakukuwa na mwalimu mwenye ujuzi. Ndipo mama mmoja aliamua kujitolea kutufundisha akilenga na kuhakikisha kwamba anatusaidia tuweze kusoma na kuandika. Mwaka 2002 tulipaswa kumaliza na kuanza shule ya msingi Ndono. Ijapokuwa nilikuwa tayari nimefahamu kusoma na kuandika, mwalimu alipendekeza nisiende shule ya msingi badala yake niendelee na chekechea hadi mwaka utakaofuata. Jambo hili lilinisikitisha sana, likanifanya nikate tamaa badala yake nikaendelea na kazi yangu ya kuchunga mifugo ya Babu. Maisha ya kwa Babu na Bibi yalinisaidia kuendelea kukua katika imani, kwani ilikuwa kila ifikapo usiku mara baada ya chakula, tulisali sala ya usiku pamoja kama familia huku tukimalizia kwa wimbo wa “Kwa Heri Yesu Mpenzi Mwema”, wimbo niliotokea kuupenda zaidi na zaidi. Mbali na kusali kila siku nyumbani, kila ifikapo Jumapili wote tuliokuwa tukiishi kwa Babu tulipaswa kwenda kusali. Parokia ilikuwa mbali kidogo na nyumbani. Kuna wakati tuliona kuwa ni mateso lakini ilikuwa ni amri kwamba wote tunapaswa kwenda kusali. Wakati wa usiku, pindi tungojeapo chakula kiive, kulikuwa na desturi ya kukaa na Babu tukiota moto, akitusimulia mambo ya zamani, na zaidi mambo yahusuyo dini enzi zake. Haya yote yalinijenga katika imani.
Mwaka huo huo wa 2002 mwishoni, nilirudi kijijini kwa wazazi ambako mwaka uliofuata 2003 nilianza rasmi shule ya Msingi Kasisi hadi nilipohitimu mnamo mwaka 2009. Nikiwa Darasa la tano, nilianza kusikia wito juu ya upadre, hii ni kutokana na namna nilivyovutiwa na huduma za Mapadre waliokuwa wakija Kigangoni kwetu kwa misa hususani siku za jumapili. Ndipo, mwaka 2009 nikiwa darasa la Saba, niliandika Barua yangu ya kwanza kwa Paroko (Pd. William Monela), nikimweleza juu ya nia yangu ya kutaka kujiunga seminari kwa malezi ya Upadre. Nilipokea majibu chanya, lakini baadae haikuwa rahisi, kwani baada ya muda mfupi, Paroko yule akawa amepatiwa uhamisho wa kwenda parokia nyingine kwa utume. Mwaka uliofuata 2010 nililazimika kuanza masomo ya Sekondari katika shule ya Kata inayojulikana kama Matwiga Sekondari iliyopo wilaya ya Urambo Mkoani Tabora, hapo nilisoma kuanzia mnamo mwaka 2010-2013. Nikiwa kidato cha Pili, niliteuliwa kuwa Katekista msaidizi wa TYCS na Kidato cha tatu kuwa Katekista Mkuu wa TYCS na Katibu wa tawi la TYCS shuleni. Uongozi huo uliendelea kunijenga na kuniimarisha kukua katika imani na ujasiri wa kusimama mbele za watu, kwani; kama Kateskista, nilipasika kuandaa Tafakari kila wiki kwa ajili ya kipindi cha dini na mafundisho kwa ajili ya wanafunzi wenzangu. Pili, kama Katibu, nilipasika kuhakikisha kundi la TYCS shuleni linaendelea kuimarika vyema na kuhakikisha wanafunzi wakatoliki wanakuwa mfano kwa wengine. Mwaka 2012 nikiwa Kidato cha tatu, niliandika barua ya pili kwa Paroko (Pd. John Mungoni) aliyekuwepo wakati huo, nikimwelezea nia yangu ya kutaka kujiunga na seminari kwa ajili ya kuanza safari ya wito wa Upadre. Ijapokuwa majibu yalikuwa chanya, hata hivyo sikufanikiwa.
Katika hali ya Kukata tamaa, Mungu anaonesha njia: Mwaka 2014 wakati nikisubiri kupangiwa shule ya kwenda kusoma Advance, ilitokea kama bahati, hii kila ninapoifikiria naichukulia kuwa kama yule towashi wa Kandake aliyekosa uelekeo na matumaini baada ya kusoma na kutoelewa kile anachokisoma hadi pale Mungu alipomtuma Filipo amwelekeze (rej. Mdo 8:26-40). Kwangu ilikuwa kwamba, katika hali ya kukata tamaa na kuanza kufikiria juu ya njia nyingine ya kuelekea, Sista mmoja (Sr. Happy Mushi) mtawa wa shirika la Mabinti wa Maria – Tabora, alifika katika zahanati ya kijijini kwetu kutoa huduma za afya. Kila Jumapili alijumuika nasi Kigangoni kwa ibada. Hapo nilimweleza lengo na nia yangu na kumuomba kama angaliweza kunisaidia kuniunganisha na watu wanaohusika ili nijiunge na seminari. Swali lake lilikuwa: “unataka kuwa Padre wa Shirika au wa Jimbo”? Swali hili lilinishtua kidogo, kwani, mimi niliwaona Mapadre wakija kigangoni, bila kujua kumbe, kuna wa shirika na mapadre wa Jimbo. Baada ya maelezo na ufafanuzi wa kina, nilimuomba aniunganishe na Jimbo Kuu Tabora. Sista aliongea na Mkurugenzi wa Miito wa Jimbo kuu la Tabora, ambaye tulianza kuwasiliana naye, na kwenda kumtembelea mara kwa mara akinielekeza nini napaswa kufanya ili kujiunga na Jimbo Kuu la Tabora. Kiu ya Kuwa Padre Mtawa wa Shirika: Mwaka 2014 mwezi Mei, nilipangiwa kwenda kusoma kidato cha tano na cha sita katika Shule ya Sekondari Kifaru iliyopo wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro. Kama ilivyokuwa kwa shule ya Sekondari Matwiga, hapo pia nilichaguliwa kuwa Katekista Mkuu wa TYCS. Nikiwa huko, Mapadre wa Mashirika mbalimbali walizidi kuja kutangaza mashirika yao na kuwataka wanafunzi wanaosikia sauti ya Mungu wajiunge nao. Nilivutiwa na shirika moja, linalojulikana kama “Divine Word,” au Neno la Mungu. Mimi pamoja na rafiki yangu (Stephen Basasa) aliyekuwa Kidato cha sita, kwa pamoja tuliafikiana kujiunga na shirika hilo. Lakini kwa upande wangu, haikuwa rahisi kwani, juhudi ziligonga mwamba mara baada ya Mkurugenzi aliyekuwepo wa shirika hilo kuhamishwa na kupewa utume mwingine nje ya nchi.
Rasmi, Malezi ya Upadre Jimbo Kuu la Tabora: Baada ya kushindwa kujiunga na shirika, nilimtafuta Mkurugenzi wa miito wa Jimbo Kuu la Tabora na kunipokea rasmi mwezi Mei mwaka 2016 na kujiunga nyumba ya Malezi ya Askofu Mkuu Mario Mgulunde, iliyopo Kipalapala. Huko niliishi maisha ya Jumuiya na kujifunza mengi hususani kutoka kwa wenzangu waliopitia seminari ndogo. Nilijifunza maisha ya sala, jumuiya, historia ya jimbo, n.k. Mwezi Agosti mwaka 2016 nilitumwa kwenda kusoma Falsafa katika Seminari ya LUMENI CHRISTI INSTITUTE, iliyopo jijini Arusha ikiwa chini ya Shirika la Wamisionari wa Mtakatifu Francis wa Sales. Nilisoma hadi mnamo mwaka 2019 nilipohitimu rasmi masomo yangu ya falsafa, na baadaye kutumwa kwa Masomo ya Taalimungu katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea Jimbo kuu la Dar es Salaam kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2019 hadi Machi 2020. Mwezi Julai, Mwaka 2020 nilitumwa kwenda masomoni Roma nchini Italia kwa masomo ya Taalimungu kwa muda wa miaka mitatu, katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu alimaarufu kama (Pontificia Università della Santa Croce) hadi nilipohitimu rasmi tarehe 19 Juni 2023 na kurudi Jimboni Tabora kwa mwaka wa Kichungaji.
Kuhusu Ushemasi na daraja ya Upadre: Tarehe 2 mwezi Mei 2024, wafuatao tutapatiwa daraja takatifu la ushemasi: Frt. Abel Paul Luhende, Frt. Clement Mathew Masuhuko, Frt. Emmanuel Joseph Mashenene, Frt. Emmanuel Gervas Jilungu, Frt. Francis Masumbuko Tesha, Frt. Francisko Milembe Rutaha, Frt. John Kulwa Mathew, Frt. Lazaro Felix Mahangale na Frt. Paul Usiga Kagolo. Pamoja nasi, ni Shemasi Constantine Elias Kagudi atakayepatiwa daraja la Upadre. Tunayo furaha, huku tukifahamu wazi kwamba majukumu tunayokwenda kukabidhiwa ni majukumu mazito ya kuwapeleka watu kwa Mungu na kumdhihirisha Mungu kwa watu. Hivyo, sisi tunazidi kuomba Neema ya Mungu ipate kutuongoza tukitambua wazi kwamba kwa nguvu zetu wenyewe hatuwezi. Katika haya yote, ninaona utendaji wa Mungu, na ndio sababu nikachagua kauli mbiu itokayo katika sala ya baba yetu isemayo “Fiat Voluntas tua”, yaani “Mapenzi yako Yatimizwe” (Mt 6:10), iniongoze katika kuishi daraja takatifu la Ushemasi ninaloliendea na baadaye upadre. Imani yangu ni kwamba, katika safari hii, magumu ni mengi, vikwazo ni vingi. Ni Mungu tu ndiye aliyetuongoza hadi kufikia hatua hii. Kama alivyoniita kutoka kuchunga mifugo ya Babu yangu, sina budi kuendelea kumsihi kwamba, mapenzi yake yaendelee kutimizwa na si mapenzi yangu. Namshukuru sana mwenyezi Mungu kwa safari hii, ambayo bado naendelea kumuomba, hitimisho lake nilifikie nalo si lingine bali ni utakatifu.
SHUKRANI: Safari yoyote ya mafanikio inahusisha kundi kubwa la watu. Hili naliona katika safari ya wito wangu. Nawashukuru wote walionisaidia na wanaoendelea kunisaidia kwa namna mbalimbali kuendelea kuitikia wito huu. Kwa namna ya pekee, napenda kuwashukuru wazazi wangu kwa malezi yao, na maongozi yao. Walinirithisha imani, wakaendelea kuhakikisha nakua katika imani, Mungu awabariki. Namshukuru kwa namna ya pekee Sr. Happy Mushi, aliyenisaidia kujiunga na Jimbo Kuu la Tabora na akaendelea kunilea na kunisindikiza kwa sala zake, Mungu ambariki daima. Nawashukuru dada na kaka zangu, ndugu, jamaa na marafiki wote, ni wengi kutaja mmoja mmoja lakini nasema asante kwa yote. Nawashukuru walezi wote niliopita mikononi mwao: Mapadre wa Shirika la Mt. Francisko wa Sales, Mapadre walezi, Seminari ya Segerea na Mapadre wa Opus Dei (Kazi ya Mungu) kwa malezi yao kwangu. Kwa namna ya pekee shukrani kwa niaba ya wote tutakaopatiwa daraja la ushemasi; ziwafikie kwa kipekee Mkurugenzi wetu wa miito Pd. Ponsiano Kibobera, na Mlezi wetu Pd. Andrea Mlele Mtaki aliyepo masomoni Roma, Italia kwa malezi yao mpaka kuweza kufikia hatua hii. Shukrani hizi ziwaendee pia Maparoko wetu na Mapadre wote wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora kwa malezi yao. Pia, tunawashukuru waamini wote ambao wamejitoa kwa hali na mali, sehemu zote ambazo tulipita kufanya utume, Mungu awabariki wote. Shukrani za pekee kwa Mhashamu Askofu Mkuu mstaafu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, yeye ambaye aliridhia kutupokea na kuanza malezi katika Kanisa Mahalia Jimbo Kuu la Tabora. Mungu ambariki ili azidi kutuongoza na kuturithisha hekima zake daima. Tunamshukuru pia Mwadhama, Protase Kard. Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, yeye ambaye atatupatia daraja la ushemasi, tunamwombea kwa Mungu awe na afya njema azidi kutuongoza siku zote katika kuyafanya mapenzi ya Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.!