Ekaristi Takatifu ni adhimisho la uwepo hai wa Bwana Wetu Yesu Kristo katika mwili na damu yake chini ya maumbo ya mkate na divai. Ekaristi Takatifu ni adhimisho la uwepo hai wa Bwana Wetu Yesu Kristo katika mwili na damu yake chini ya maumbo ya mkate na divai. 

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Chanzo na Kilele cha Maisha na Utume wa Kanisa

Ekaristi ndiyo jumla na muhtasari wa imani yetu nzima (KKK 1327). Imani yetu na fumbo zima la wokovu wa mwanadamu vimelala juu ya Ekaristi Takatifu. Ndiyo ishara thabiti ya ushirika katika uzima wa kimungu na adhimisho lake ni ishara ya muunganiko na Liturujia ya mbinguni. Ekaristi ndio chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo.; ni chemchemi ya neema na baraka zote; ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo. Ekaristi Takatifu ni Kristo Yesu Mwenyewe!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Ekaristi Takatifu Mwaka B wa kiliturujia. Kawaida sherehe hii inaadhimishwa Alhamisi Kuu. Lakini inarudiwa siku ya Alhamisi baada ya sherehe ya Utatu Mtakatifu. Lakini kwa sababu za kiuchungaji inahamishiwa Jumapili baada ya sherehe ya Utatu Mtakatifu. Mama Kanisa ameamua hivyo ili kuwapa watoto wake nafasi ya kufurahia, kumsifu, kumwabudu na kumpa Mungu heshima katika Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa maandamano yanayofanyika baada ya Misa ili kuliishi, kulitafakari na kuonyesha umuhimu na uhitaji wa Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho. Ekaristi Takatifu ni adhimisho la uwepo hai wa Bwana Wetu Yesu Kristo katika mwili na damu yake chini ya maumbo ya mkate na divai.  Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kuwa Ekaristi ndiyo jumla na muhtasari wa imani yetu nzima (KKK 1327). Imani yetu na fumbo zima la wokovu wa mwanadamu vimelala juu ya Ekaristi Takatifu. Ndiyo ishara thabiti ya ushirika katika uzima wa kimungu na adhimisho lake ni ishara ya muunganiko na Liturujia ya mbinguni. Ekaristi ndio chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Ndiyo maana wimbo wa mwanzo unafungua maadhimisho haya ukisema; “Nimewalisha kwa unono wa ngano na kuwashibisha kwa asali itokayo mwambani” (Zab.80:17). Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kutoka (24:3-8). Somo hili linatueleza jinsi Mungu alivyofanya Agano na Israeli taifa lake teule, chini ya uongozi wa Musa. Agano hili liliashiriwa kwa watu kunyunyiziwa damu ya ng’ombe kama alama na ishara tu ya Agano Jipya na la milele lililofanyika na Kristo Yesu kwa kumwaga damu yake msalabani. Nasi tunashirikishwa katika Agano hili kwa njia ya ubatizo. Mzaburi alipotafakari uaminifu wa Mungu kwa Agano lake na wanadamu alistaajabia na kuimba zaburi hii ya wimbo wa katikati akisema; “Nimrudishie Bwana nini, kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; na kulitangaza jina la Bwana. Ina thamani machoni pa Bwana, mauti ya wacha Mungu wake. Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako, umevifungua vifungo vyangu. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, na kulitangaza jina la Bwana. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana, naam, mbele ya watu wake wote” (Zab. 116 :12-13, 15-18).

Maandamano ya Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wa imani kwa Yesu wa Ekaristi
Maandamano ya Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wa imani kwa Yesu wa Ekaristi

Somo la pili ni la Waraka kwa Waebrania (9:11-15). Somo hili linatueleza jinsi na namna ukuhani wa Kristo ulivyo msingi wa Agano Jipya nao ni bora kuliko ukuhani wa Agano la Kale. Kwa sababu Kristo alitolea damu yake mwenyewe katika madhabahu ya mbinguni siyo duniani na kwa sadaka hiyo amezitakasa roho za watu wote. Na hii ndiyo sadaka ya mwili na damu yake pale msalabani. Injili ni ilivyoandikwa na Marko (14:12-16, 22-26). Sehemu hii ya Injili inatueleza jinsi Yesu Kristo alivyoiweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu – mwili na damu yake ishara wazi ya Agano Jipya na la milele – katika mlo wa kipasaka, siku ya Alhamisi Kuu kabla ya kukamatwa, kuteswa na kufa msalabani (1Cor. 11:23-26, KKK. 1337). Marko anasimulia akisema; “Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa akisema; Twaeni; huu ndio mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi”. Ekaristi Takatifu ni ukumbusho wa mateso ya Yesu. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umetuachia ukumbusho wa mateso yako katika sakramenti ya ajabu. Tunakuomba utujalie kuyaheshimu mafumbo matakatifu ya mwili na damu ya mwanao, tupate daima neema ya ukombozi wako ndani yetu.” Hii ndiyo amana ya Ekaristi Takatifu, kilele cha maisha ya utume wa Kanisa na chemchemi ya neema na baraka zote, ndiyo sadaka ya shukrani ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo, ukumbusho wa mateso kifo na ufufuko wa Bwana. Ekaristi Takatifu ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo. Utakatifu wake umo katika usakramenti wake. Ekaristi Takatifu ni sakramenti ya sakramenti, alama wazi aliyoiweka Yesu Kristo mwenyewe ili kutuletea neema ya wokovu. Tofauti na sakramenti zingine, Ekaristi Takatifu ni Kristo mwenyewe katika maumbo ya mkate na divai. Uwepo wa Kristo katika Ekaristi Takatifu unaiinua juu zaidi sakramenti hii kuliko sakramenti zingine ukiwa ndio utimilifu wa maisha ya kiroho na ndio mwisho ambao sakramenti zote hulenga kwani ndani yake kuna mwili na damu ya Yesu Kristo, kweli, halisi na uwamo kamili pamoja na roho na umungu na hivi ni Kristo mzima kabisa (Rejea KKK 1211, 1374).

Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho
Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho

Inakuwaje mkate kuwa mwili wake Yesu na divai kuwa damu yake Yesu? Mababa wa Mtaguso wa Trento wanasema hivi: “Kwa sababu Kristo Mkombozi wetu ndiye alisema mwenyewe kwamba ulikuwa ni mwili wake kweli ambao alikuwa anautoa sadaka kwa namna ya mkate na damu kweli kwa namna ya divai, imekuwa tayari imethibitishwa kwa Kanisa la Mungu, kwamba kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate na divai kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na ya kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake. Uwepo huu huanza dakika ya mageuzo na hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwepo. Hivyo Kristo yupo mzima na mkamilifu katika kila mojawapo ya maumbo ya mkate na divai na ni mzima na mkamilifu katika kila sehemu yao, kwa jinsi hii kwamba kuimega Ekaristi Takatifu hakumgawanyi Kristo hata kidogo”, uwepo wa Yesu unabaki kwenye kila kipande kidogo kilichovunjika na hata katika kila tone la damu yake uwepo wa Yesu umo kamili kabisa kama katika Ekaristi Takatifu nzima (KKK 1376-1377). Kumbe basi, Ekaristi Takatifu ni kitovu, chemchemu na kilele cha maisha yote ya Kanisa na Kanisa haliwezi kitu pasipo Ekaristi Takatifu. Katika Ekaristi Takatifu mna kila hazina ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe, Pasaka wetu. Ndiyo maana katika Ekaristi Takatifu tendo la Mungu kuutakatifuza ulimwengu na kilele cha tendo la watu kumwabudu Mungu katika Kristo hufanyika. Hivyo Ekaristi Takatifu ndiyo ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja wa Taifa la Mungu ambao unalifanya Kanisa liwepo. Kwa njia ya adhimisho la Ekaristi Takatifu tunaungana tayari sisi wenyewe na liturujia ya mbinguni na tunaanza kushiriki uzima wa milele (KKK 1322–1323, 1324–1327, 1407, 1409; DS 3364).

Maandamano ya Ekaristi Takatifu: Uwepo wa Kristo kati ya waja wake
Maandamano ya Ekaristi Takatifu: Uwepo wa Kristo kati ya waja wake

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unatilia makazo kuwa Ekaristi Takatifu ni “Chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo” (Lumen gentium 11), “chemchemi na kilele cha uinjilishaji wote” (Presbyterorum Ordinis 5). Kumbe Ekaristi inaunda Kanisa na Kanisa linaitengeneza Ekaristi, na ndimo linamochota nguvu ya kiroho. Hivyo hakuna jumuiya ya Kikristo inayoweza kujengwa na kusimama imara bila adhimisho la Sakramanti Kuu ya Ekaristi Takatifu (Presbyterorum Ordinis 6). Katika Ekaristi Takatifu fumbo la Ukombozi wetu linawekwa hai na kufikia kilele chake, kama inavyotamkwa katika maneno ya konsekrasio: “Huu ndio Mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu na Hii ndiyo Damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu”, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” (Lk 22:19-20). Hivyo basi ili mkristo awe na muunganiko kamili na Kristo Yesu, anapaswa kupokea Ekaristi Takatifu ili kwayo kuwezeshwa kushiriki katika uzima ule ule wa Kristo kama anavyosema Yesu mwenyewe; “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yn 6:56-57). Kwa vile ni sadaka, Ekaristi Takatifu hutolewa kwa waamini wote, wazima na wafu, kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na kupata rehema ya Mungu. Kumbe katika sadaka ya Ekaristi Takatifu, Kanisa hutolea maisha ya waamini, masifu yao, mateso yao, sala zao, kazi zao na kuyaunganisha na yale ya Kristo kwa Mungu Baba. Kanisa la Mbinguni pia linaungana na matoleo ya Kristo. Ekaristi Takatifu ikiwa ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, inatuunganisha na watu wote kwa muda wote bila kujali tofauti zetu. Ni wazi, maana Kristo mwenyewe anasema; “aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu nami ndani yake.” Kwa kuwa tunakuwa kile tunachokula, tukila mwili na kunywa damu ya Kristo tunakuwa na ukristo ndani mwetu tunakuwa kitu kimoja, ndiyo maana tunaitwa wakristo. Mbele ya Ekaristi Takatifu, tofauti zetu za kisiasa, kikabila, kivyama, kitaifa, kirangi hazina nafasi kwa kuwa kila mmoja ana Ukristo ndani yake. Hivyo, mkristo kumwinulia upanga mkristo mwingine ni kujiinulia upanga mwenyewe na kumwinulia Kristo upanga. Hivi ndivyo alivyomwambia Paulo alipokuwa anawatesa Wakristo; “Ni mimi Kristo unayenitesa” (Mdo 9:5) na anasisistiza kwamba; “Chochote ulichowatenda hawa wadogo umenitendea mimi” (Mt. 25:40; KKK 1391–1397, 1416).

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Ekaristi Takatifu inatupatia msamaha wa dhambi nasi tunasameheana na kuwa wamoja kwani adhimisho la Ekaristi Takatifu ni tendo la toba linalotutakasa na dhambi ndogondogo, na kutupatia nguvu katika vita dhidi ya mwovu na kutuepusha na nafasi za dhambi. Mtakatifu Ambrosi anasema; “Ekaristi Takatifu ni mkate wetu wa kila siku kwa ajili ya dhambi zetu za kila siku, inatupatia silaha bora dhidi ya vishawishi”. Lakini kwa habari ya dhambi za mauti, Sakramenti ya Kitubio ni ya lazima haiepukiki. Ndiyo maana Didache – mafundisho ya mitume – inasema hivi; “Ifikapo siku ya Bwana baada ya kukusanyika na kuwa pamoja, mtamega na kutoa Ekaristi, baada ya kuungama makosa yenu, kusudi sadaka yenu iweze kuwa safi. Lakini asiruhusiwe mtu yeyote aliye na ugomvi na jirani yake ajiunge nanyi mpaka awe amefanya usuluhisho, la sivyo sadaka yenu ni batili” (Didache 9, 14, 1-2). Kumbe, ni hasara kubwa sana kutokupokea Ekaristi Takatifu kwa kuwa umejiwekea vizuizi, umejifungia. Wale wasiopokea Ekaristi Takatifu nawasihi fanyeni bidii kubomoa kuta za vizuizi mpokee Ekaristi Takatifu, ili muungane na jamii ya waamini katika Ekaristi Takatifu na kuwa kweli wakristo. Tukiwa na tofauti katika familia, katika nafasi za kazi, katika vyama vyetu vya siasa, tuiangalie Ekaristi Takatifu ili iwe sababu yetu ya kuthaminiana, kuheshimiana na kupendana kwa kuwa Ekaristi Takatifu inatuunganisha inatufanya tuwe wamoja katika Kristo. Tumsifu Yesu Kristo.

Ekaristi Takatifu
30 May 2024, 08:24