Mama Evaline Malisa Ntenga: Wekezeni Katika Majiundo Makini ya Makatekista
Na Mama Evaline Malisa Ntenga, Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania.
Makatekista ni wadau wakuu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Wao wamekuwa mstari wa mbele katika Uinjilishaji wa awali Barani Afrika na wanaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwatayarisha wakatekumeni ili kupokea Sakramenti za Kanisa. Makatekista wameonesha umuhimu wa pekee katika kuzisimamia na kuziongoza Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, shule ya Neno la Mungu, ukarimu na upendo kwa familia ya Mungu. Kwa njia ya mifano bora ya Makatekista kutoka sehemu mbalimbali Barani Afrika, Kanisa Barani Afrika limeweza kuzamisha mizizi katika maisha na vipaumbele vya watu. Mchango wa Makatekista bado ni muhimu na endelevu anasema Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume: Dhamana ya Afrika, “Africae Munus.” Maaskofu mahalia wanapaswa kuhakikisha kwamba Makatekista wanapewa majiundo awali na endelevu: kiakili, kimafundisho, kimaadili na kichungaji, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa mahalia pia linapaswa kuhakikisha kwamba, Makatekista wanapata mahitaji yao msingi ili kuziwezesha familia zao kusonga mbele kimaendeleo. Makatekista waoneshe upendo na ukarimu; uaminifu na udumifu katika maisha na utume wao. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Neno la Mungu na Mafundisho ya Kanisa na kwa njia hii wataweza kutoa katekesi safi na kuongoza vyema vikundi vya sala na tafakari ya Neno la Mungu. Ikiwa kama Makatekista watakuwa waaminifu kwa utume wao, watasaidia kuchangia utakatifu wao binafsi pamoja na kusaidia kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza zaidi kwa Makatekista ili waweze kutekeleza vyema dhamana na utume wao kwa Kanisa.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, ni juu ya walei, kutokana na wito wao, kuutafuta ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadiri ya Mungu, wakijitahidi kuyatakatifuza malimwengu kama kutoka ndani, mithili ya chachu, katika kuyatimiza majukumu yao wenyewe, wakiongozwa na roho ya kiinjili, hivyo wamshuhudie Kristo kwa wengine, waking’aa hasa kwa ushuhuda wa maisha yao, imani, matumaini na mapendo. Waamini walei wanaweza kushirikishwa zaidi katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume. Makatekista wanaitwa kuwa ni wataalamu na wahudumu wa jumuiya ya waamini katika kutangaza, kushuhudia na kurithisha imani katika hatua mbalimbali. Waanzie hatua ya kwanza ya kutangaza Injili, “Kerygma”, kufundisha maisha mapya katika Kristo Yesu sanjari na kuwandaa waamini kwa ajili ya kupokea Sakramenti za Kanisa na hatimaye, kuendelea na majiundo endelevu ili kila mwamini aweze kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu anayemuuliza habari za tumaini lililo ndani mwake; lakini kwa upole na kwa hofu. Rej. 1Pet.3:15. Makatekista wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa imani, waalimu, wandani wa imani na walimu wanaofundisha kwa niaba ya Kanisa. Yote haya yanaweza kutekelezwa kwa njia ya sala, masomo na ushiriki wa moja kwa moja katika maisha ya jumuiya yanayoweza kukuza utambulisho na uwajibikaji wake wote.
Ni katika muktadha huu, katika Sherehe ya Pentekoste, tarehe 19 Mei 2024 Chuo cha Katekesi cha Mtakatifu Francisko Ksaveri, Chuo Kikuu cha Dodoma, UDOM, Jijini Dodoma, Makatekista 44 wamehitimu masomo yao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa Kanisa la Tanzania. Hiki ni Chuo kinachoendeshwa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania. Katika mahubiri yake, Padre Tito Philip Shirima, C.PP.S., amewataka Makatekista na vijana katika ujumla wao, kuhakikisha kwamba, wanajibidiisha kutambua na kuendeleza karama zao, walizokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya Kumi na Mbili ya Chuo cha Katekesi cha Mtakatifu Francisko Ksaveri, Chuo Kikuu cha Dodoma, UDOM. Katika hotuba yake amekazia mambo makuu ambayo yanapaswa kuwa ni msingi wa mwenendo wao wa Kikristo wanapoingia kwenye awamu nyingine ya maisha: kwa kutafuta, kufanya kazi na kushiriki katika medani mbalimbali za maisha. Kumbe wanapaswa kujikita katika maadili na utu wema; Kutokuchagua kazi, uvumilivu, kutafuta fursa za kuwahudumia watu wa Mungu na kupanda mbegu njema ya imani, matumaini na mapendo katika jamii, ili hatimaye, waweze kuandika jina jema. Maadili ni msingi wa maisha ya Kikristo yanayopata chimbuko lake katika: Biblia, Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Uadilifu unamwezesha mwamini kuishi katika ukweli na uaminifu. Mama Evaline Malisa Ntenga, anasema, kazi inamtambulisha mwanadamu na kumwezesha kutekeleza karama na mapaji mbalimbali aliyokirimiwa katika maisha yake. Kwa njia ya kazi, mwanadamu anashiriki pia katika mpango wa kazi ya uumbaji na hivyo kushiriki pia katika mchakato wa mshikamano na jirani zake. Licha ya shida, lakini inamwezesha mtu kukua na kukomaa, pamoja na kutekeleza ndoto za maisha yake, Kumbe, wasipende kuchagua kazi, bali wahakikishe kwamba, wanatumia vyema talanta walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu, kwa uaminifu, ubunifu na moyo wa huduma, hali inayoakisi upendo. Makatekista hawa wahakikishe wanapanda mbegu ya imani, matumaini, mapendo; na utu wema.
Mama Evaline Malisa Ntenga, Hotuba Kamili. Tumsifu Yesu Kristo, Mheshimiwa Baba Paroko/Paroko Msaidizi, viongozi wa Jimbo Kuu la Dodoma, viongozi wa Halmashauri ya Walei Dekania, viongozi wa Halmashauri ya Walei Parokia, viongozi wa Kamati Tendaji za Vigango vyote kutoka katika Parokia yetu, wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana, Tumsifu Yesu Kristo…... Salamu na shukurani: Awali ya yote, napenda kumshukuru Mungu mwingi wa rehema kwa zawadi ya uhai na afya njema inayotuwezesha kushiriki katika siku hii adhimu ya mahafali ya kumi na mbili ya wanafunzi wa UDOM katika Kigango chetu cha Mtakatifu Bernado kwa mwaka huu wa masomo 2023/2024. Wapendwa wahitimu, nimepokea risala yenu kwa moyo mkunjufu na ninawapongeza kwa mafanikio mliyoyapata pamoja na changamoto mlizozitaja. Kwa kweli, ni dhahiri kwamba mnapiga hatua kubwa katika kueneza na kukuza imani katoliki katika kigango chenu. Mafanikio yenu katika kuandaa misa takatifu, kusaidia wahitaji, na kujitoa kwa moyo katika masuala ya kiuchumi na kiimani ni mfano wa kuigwa. Kuhusu historia na shughuli za kigango: Historia ya Kigango cha Mtakatifu Bernado inavutia sana na inaonyesha jinsi mmejitolea kuendeleza imani. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012, mmekuwa mkiendelea kupanuka na sasa mna waumini zaidi ya 800. Hongereni sana kwa juhudi zenu na kwa viongozi wote wa kigango kwa kazi nzuri mnayoifanya. Shughuli mnazozifanya, kama kuratibu misa takatifu, ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu, na sala za jioni, ni muhimu sana kwa ukuaji wa kiroho wa waamini. Kabla sijajikita sana katika kuijibu risala yenu, naomba niseme mambo kadhaa ambayo nafikiri ni muhimu kwenu kuwa nayo, hasa katika kipindi hiki ambacho mko katika hatua ya kuingia kwenye awamu nyingine ya maisha – maisha ya kutafuta, kufanya kazi na kushiriki katika mambo mbalimbali ya kifamilia, kanisa, kijamii na kitaifa pia.
Ningependa kujadili baadhi ya maadili muhimu ambayo ni msingi wa mwendo wetu na Kristo: Maadili, Uadilifu, Kutochagua kazi, Uvumilivu, kutafuta fursa za kuhudumia, na kupanda mbegu njema/za matumaini katika jamii zetu.Andika jina lako Vizuri: Make your own Brand: Andika jina lako vizuri. Kuna mtu anapenda jina lake liandikwe vibaya? Nikitaja jina – Say Raphael --- Trust/Uaminifu, What are your values? Which value resonate most with you? How do you measure your self worthy? In God i trust! Everything has its time. Humility/humble – unyenyekevu. Aim high – strech, must be ambitious, who dares wins, whatever youdo, do it hard….only on positive things. Team spirit. Time Management consciousness show respect to others Maadili ni msingi wa maisha ya Kikristo. Dira yetu ya maadili inaongozwa na mafundisho ya Yesu Kristo. Biblia inasema katika Mika 6:8, “Mungu amekuonyesha yaliyo mema, ewe mwanadamu; anachotaka Mwenyezi-Mungu kwako ni hiki: Kutenda mambo ya haki, kupenda kuwa na huruma, na kuishi kwa unyenyekevu na Mungu wako.” Kama vijana Wakristo, matendo yetu yanapaswa kuakisi maadili yaliyo fundishwa na Kristo—huruma, unyenyekevu, na haki. Fikiria juu ya Msamaria Mwema katika Luka 10:25-37. Matendo ya Msamaria yalivuka mipaka ya kitamaduni na kikabila ili kutoa msaada kwa mtu aliyejeruhiwa. Hadithi hii inatufundisha kwamba maadili sio tu kuepuka mabaya bali pia kutafuta kufanya mema. Inatuhamasisha kujiuliza kila siku: Ninawezaje kutenda haki? Ninawezaje kuonyesha rehema leo? Nautumije muda wangu? Uadilifu unamaanisha kuishi kwa ukweli na uaminifu. Mithali 10:9 inatuambia, "Aendaye kwa unyofu huenda salama, bali aipotoshaye njia zake atajulikana." Uadilifu sio tu kuepuka uongo, wizi, udanganyifu; ni kuonyesha ukweli katika kila sehemu ya maisha yetu. Mwandishi maarufu C.S. Lewis aliwahi kusema, "Uadilifu ni kufanya jambo sahihi, hata kama hakuna anayekuona." Tujitahidi kuishi kwa ukweli, kuhakikisha matendo yetu yanalingana na imani yetu. Fikiria juu ya hadithi ya Danieli kwenye tundu la Simba (Danieli 6). Uadilifu na uaminifu wa Danieli kwa Mungu, hata katika uso wa kifo, ni kumbusho lenye nguvu la umuhimu wa kubaki wa kweli kwa kanuni zetu. Hadithi yake inatuhimiza kuishi kwa uwazi na uaminifu, bila kujali hali.
Kutochagua kazi: Kama wafuasi wa Kristo, tunaitwa kuhudumu kwa namna yoyote inayomheshimu Yeye. Wakolosai 3:23 inatuhimiza, "Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo wenu wote, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu." Hatupaswi kuchagua au kujivuna kuhusu kazi tunazofanya. Iwe ni kazi yenye hadhi au kazi ya unyenyekevu, kila kazi inaweza kumtukuza Mungu ikiwa imefanywa kwa moyo wa dhati. Mama Teresa aliwahi kusema, "Sio sisi sote tunaweza kufanya mambo makubwa. Lakini tunaweza kufanya mambo madogo kwa upendo mkubwa. “I am a little pencil in God's hands. He does the thinking. He does the writing.” Haya yatupe kuona tukitoka hapa, tuangalie ni nini tunachoweza kuanza nacho, bila kujali udogo au hadhi ya shughuli husika - la msingi kuangalia, ni shughuli halali, inanipa hatua ya kutokuwa tegemezi, inaniwezesha kuchangia katika familia, Kanisa, jamii na nchi yangu. Tafakari juu ya mfano wa talanta katika Mathayo 25:14-30. Kila mtumishi alipewa kiasi tofauti cha kusimamia, lakini kilicho muhimu si kiasi, bali uaminifu na jitihada zilizowekwa katika kazi zao. Hii inatufundisha kwamba kila jukumu tunalochukua ni muhimu ikiwa linashughulikiwa kwa kujitolea na moyo wa huduma. Uvumilivu ni fadhila inayoturuhusu kuamini muda wa Mungu badala ya wetu. Yakobo 5:7-8 inatuhimiza, "Basi, vumilieni, ndugu, mpaka kuja kwake Bwana. Tazameni, mkulima hungoja mazao ya thamani ya nchi, naye huvumilia kwa ajili yake mpaka yapate mvua ya masika na vuli." Uvumilivu ni kuvumilia magumu na kusubiri ahadi za Mungu bila kupoteza imani. Hadithi ya Abrahamu katika Mwanzo 12-21, akisubiri ahadi ya mwana, inaonyesha uvumilivu na imani. Licha ya miaka mingi ya kungoja, Abrahamu aliendelea kuamini ahadi ya Mungu, na mwishowe, Isaka alizaliwa. Hii inatukumbusha kwamba mipango ya Mungu hutimia kwa wakati wake mkamilifu, mara nyingi ikihitaji uvumilivu wetu thabiti.
Kutafuta fursa za kuhudumia – kujisadaka kwa ajili ya wengine: Tunaitwa kuwa watumishi, tukifuata mfano wa Kristo Yesu aliyesema, "Aliye mkubwa kwenu atakuwa mtumishi wenu" (Mathayo 23:11). Tafuta kila fursa ya kuhudumia wengine, iwe ndani ya chuo chako, jamii, au Kanisa. Mtakatifu Francisko wa Assisi anatukumbusha, "Kwa maana ni katika kutoa ambapo tunapokea." Huduma inabadilisha mtoaji na mpokeaji, ikikuza roho ya upendo na unyenyekevu. Fikiria juu ya Yesu akiosha miguu ya wanafunzi wake katika Yohana 13:1-17. Kitendo hiki cha huduma kilionyesha unyenyekevu na upendo wa kina. Yesu alitoa mfano wa kufuata—hakuna kitendo cha huduma kilicho kidogo sana, na kupitia kuhudumia wengine, tunaakisi upendo wake. Kupanda Mbegu Nzuri: Kila tendo tunalofanya ni mbegu inayopandwa katika ulimwengu. Wagalatia 6:7-9 inatuambia, "Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa lolote apandalo mtu, ndilo atakalovuna. Apendaye kupanda katika mwili wake, katika mwili atavuna uharibifu; bali yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Tusiache kutenda mema, maana tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa." Andiko hili liwe himizo kwetu/kwetu sote kupanda mbegu za wema, upendo, na imani, tukiamini kwamba Mungu atazikuza na kutoa mavuno yenye matunda Mfano wa mpanzi katika Mathayo 13:1-23 unaonyesha jinsi aina tofauti za udongo zinavyoathiri ukuaji wa mbegu. Mioyo yetu na matendo yetu ni kama udongo huo. Kwa kutunza na kukuza matendo mema na mitazamo chanya, tutatengeneza mazingira ambayo neno la Mungu linaweza kustawi na kutoa mavuno mengi. Ninapohitimisha eneo hili, ningependa kusema kuwa, Kama wanajamii inayokua ya Wakristo, tujitoe kuishi kwa kuzingatia maadili haya katika maisha yetu ya kila siku. Tujitahidi kwa ubora wa kimaadili, kudumisha uadilifu, kukumbatia kila aina ya kazi, kuwa na uvumilivu, kutafuta fursa za kuhudumia, na kupanda mbegu nzuri popote tunapokwenda. Kumbuka, sisi ni nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia (Mathayo 5:13-16). Maisha yetu yaangaze, yakiakisi upendo na mafundisho ya Yesu Kristo.
Majibu kwa changamoto zilizoainishwa kwenye risala:Nikirejea kwenye risala yenu, hasa kuhusu changamoto, ni wazi kwamba, kama jamii yoyote inayokua, mnazo changamoto mbalimbali. Changamoto ya vitendea kazi kwa makatekista, uhaba wa seti ya MIC, na mahudhurio hafifu ya waamini katika vipindi vya sala ni mambo muhimu yanayohitaji kutatuliwa. Pia, mwingiliano wa ratiba za masomo na Kanisa ni jambo linalohitaji mikakati madhubuti ili kuhakikisha kwamba waamini wanaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za Kanisa bila kuathiri ratiba za masomo ambazo zina umuhimu mkubwa. Mapendekezo: Napokea kwa mikono miwili mapendekezo yenu ya kusaidia kupata vitendea kazi vya Makatekista. Ni muhimu sana kwa Makatekista kuwa na vifaa vinavyohitajika ili waweze kutoa huduma bora za kiroho. Pia, napenda kutoa wito kwa waamini wote, hasa wale wanaomaliza masomo yao, kuwa wadau wakubwa wa kusaidiana na wanaobaki katika kulitegemeza kanisa. Katika kuchangia katika kutatua changamoto hizo, binafsi nitanununua kanzu zote 6, fedha nitakabidhi kwa uongozi unaoratibu, nimenunua pia vitabu – Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Katekisimu ya Kanisa Katoliki ambavyo nitawakabidhi leo. Hitimisho. Ndugu zangu, ninapohitimisha, napenda kuwashukuru kwa kunialika na kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika sherehe hii. Ni heshima kubwa kwangu na nimefurahia sana kuwa nanyi. Kwa mara nyingine tena, naomba kuwapongeza wahitimu wote kwa juhudi zenu katika masomo yenu na katika shughuli za kigango hicho. Jitahidini kuendelea na moyo huo huo wa kujituma na kujitoa kwa ajili ya imani na jamii yetu. Nawatakia safari njema na yenye baraka nyingi mnapojiandaa na mitihani ya mwisho, na mnaporejea makwenu na kuendelea na utume wenu. Nipende kuwashauri, mnapomaliza mitihani, rejeeni nyumbani kushukuru na kuomba baraka za wazazi. Mungu awabariki sana. Asanteni sana na Mungu awabariki nyote. Tumsifu Yesu Kristo.