Tafuta

Tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atuangaze tuweze kuutafakari na kuuishi vizuri upendo mkamilifu. Tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atuangaze tuweze kuutafakari na kuuishi vizuri upendo mkamilifu.  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika ya Sita Kipindi Cha Pasaka Mwaka B wa Kanisa: Pendaneni Kama Nilivyowapenda!

Mapendo ni fadhila ya Kimungu inayomwezesha mwamini kumpenda Mwenyezi Mungu kuliko vitu vyote, kwa ajili yake Mwenyewe; jirani kama wanavyojipenda wenyewe, kwa ajili ya mapendo ya Mungu. Yesu aliyafanya mapendo kuwa ni Amri mpya. Upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake umejionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Pasaka. Mtume Paulo katika utenzi wake kuhusu upendo anasema: “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo...!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI, Karibu mpendwa msikilizaji na msomaji, tukiwa bado katika shangwe ya Pasaka leo ni dominika ya sita, tunaelekea kuhitimisha kipindi hiki cha pasaka, na wazo kuu katika masomo ya leo ni “UPENDO.” Mapendo ni fadhila ya Kimungu inayomwezesha mwamini kumpenda Mwenyezi Mungu kuliko vitu vyote, kwa ajili yake Mwenyewe; jirani kama wanavyojipenda wenyewe, kwa ajili ya mapendo ya Mungu. Yesu aliyafanya mapendo kuwa ni Amri mpya. Upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake umejionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Pasaka. Mtume Paulo katika utenzi wake kuhusu upendo anasema: “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.” 1Kor13:4-8. Matunda ya upendo ni furaha, amani, huruma; upendo unadai ukarimu na kuonyana kidugu; upendo ni wema; hukuza hali ya kupokeana; hubaki huru bila ya kujitafutia faida; ni urafiki na umoja. Utimilifu wa kazi zote ni upendo. Hapo ndipo lilipo lengo. Mwaliko kwa waamini kulikimbilia, ili wapate kitulizo cha ndani. Rej. KKK 1822-1829. Lakini kwa wenzetu Wagiriki wana maneno matatu yanayoeleza maana tofauti za neno upendo. Kwanza kuna eros; hili ni neno linalomaanisha upendo wa kimapenzi. Pili kuna neno “philia”; Haya ni mapendo ya urafiki, yanaweza kuwa upendo kati ya kaka na dada, watoto na wazazi na marafiki wengine. Mwisho kuna neno agape; Haya ni mapendo ya kimungu, ambayo yana subira, huruma na kujitoa kwa ajili ya wengine. Hizo ndizo maana za neno upendo.

Upendo ni fadhila ya Kimungu
Upendo ni fadhila ya Kimungu

Kupenda na kupendwa ni msukumo wa kiasili uliopo ndani ya mioyo ya wanadamu. Kila mmoja wetu hapa ana kiu ya kutaka kupendwa. Na kila mmoja wetu ana msukumo ndani yake unaomfanya ampende mtu fulani kitu au jambo fulani. Masomo ya leo hasa somo la pili na Injili yanaongelea juu ya upendo. Mungu wetu ndio upendo wenyewe. Tulipoanguka dhambini Mungu hakuacha kutupenda. Aliamua kumtuma Mwanaye ili awe kipatanisho kati yetu na Mungu Baba. Huyu mwana wa pekee wa Mungu ili naye kuonyesha kuwa anatupenda, alikubali mwito wa Mungu Baba akautoa uhai wake kwa ajili ya wokovu wetu. Ili tuweze kudumu katika pendo hilo, Kristo anatuagiza tushike amri yake ya kupendana kindugu.  Neno la Mungu linatupa habari njema, habari inayopendwa na kila mwenye mwili, wakubwa, watoto, wake kwa waume, ni habari inayotamaniwa na wazima-wagonjwa, matajiri na fukara, viwete, vipofu, bubu na watu wote. Ni habari ya UPENDO iliyo amri mpya na kuu kabisa. Tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atuangaze tuweze kuutafakari na kuuishi vizuri upendo.  Niwaalikeni tutafakari wazo hili, upendo unatutambulisha na kutukamilisha sisi kwa sisi.

Kristo Yesu alitoa Upendo kuwa ni Amri kuu
Kristo Yesu alitoa Upendo kuwa ni Amri kuu

UFAFANUZI: Kristo Mfufuka leo anatupa amri mpya ya mapendo. Anatupa amri si kwa maneno tu bali hata kwa matendo yake. Yeye mwenyewe anatuambia hakuna aliye na upendo mwingi kuliko wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. (Yn 15:13), Tukitazama somo I (Mdo 10:25-26, 34-35, 44-48) tunaona Mt. Petro anashangilia kuwa “Mungu hana upendeleo” hana ubaguzi, anataka wote kabisa waokoke na kuurithi ufalme wa Mungu. Hii inatokana na uwepo wa ubaguzi katika jamii ya kiyahudi enzi za Yesu. Kulikuwa na madaraja matano ya watu: Daraja la I liliwahusisha wayahudi halisi waliozaliwa kwa baba na mama wa kiyahudi. Hata katika daraja hili wanaume walikuwa juu kuliko wanawake (kila asubuhi wanaume walisali “nakushukuru Ee Mungu kwa sababu umeniumba huru sio mtumwa, myahudi na sio mtu wa mataifa, mwanaume na sio mwanamke”, wanawake hawakutoa huduma za jamii ila za nyumbani tu, kujifunika uso, kutoongea na wanaume mbele za watu, kutotoa ushahidi mahakamani, hawakubanwa na sheria za kidini kama wanaume na hawakushiriki kazi za kiliturjia). Nasikitika kusema bado kuna mila zenye dhana hii ya kuwaona akina mama kama watu duni, watu wa daraja II wasio na chochote cha pekee mbele ya wanaume. Yesu hakuwabagua, aliongea nao, walimuhudumia na walikuwa mashahidi wa ufufuko-tunashukuru leo mapinduzi makubwa Mwanamke au mama anavyotoa mchango mkubwa katika jumuiya ya binadamu katika kila taifa, jamii, kabila, familia nk hata wakovu wetu umeanzia kwa mwanamke (BK Maria) ufufuko watangazaji wa kwanza wanawake.

Watu wapendane kwa vitendo, utimilifu wa Amri ya upendo
Watu wapendane kwa vitendo, utimilifu wa Amri ya upendo

Daraja la II walikuwa Wayahudi wa damu lakini waliojishughulisha na kazi zilizodharauliwa mfano kukusanya kodi na ushuru, uchungaji na kuchuna na kufuma ngozi za wanyama. Hawa walibaguliwa sababu walikuwa wakorofi wasio na muda wa sala, kutafakari torati na kufanya usafi wao binafsi hivi walichukuliwa kama wadhambi. Daraja la III walikuwa watu wasio wayahudi lakini wamejiunga na wayahudi baada ya kukubali sheria ya Musa na kufanya tohara. Hawakuruhusiwa kuoa kwenye ukoo wa kikuhani au kupewa madaraka makubwa ya jamii. Daraja la IV walikuwa Wayahudi watumwa, hawa hawakupigwa viboko na waliachiwa huru kwenye mwaka wa jubilee. Daraja la V ni watumwa wasio wayahudi. Hawa walichapwa viboko, kunyanyaswa na hawakuachiwa huru kwenye mwaka wa jubilei, watu wa mataifa. Ni katika mazingira hayo ndipo Mt. Petro anafurahi kuwa Mungu hana upendeleo, habagui, anawapenda wote. Tukiwa bado katika furaha ya ki-Pasaka inatubidi kuonesha upendo kwa wengine kama Kristo mwenyewe alivyoonesha upendo wake kwetu. Kujiita mfuasi wa Kristo kunamaanisha kuwapenda wenzetu. Hatuwezi kusema tunampenda Mungu wakati hatuna uhusiano mzuri na majirani zetu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume unaoitwa “Mungu ni Upendo” (Deus Caritas es t-kilatin) anasema kwamba kwa kuwasaidia majirani zangu, ndipo na mimi nagundua upendo wa kimungu uliopo ndani yangu. (No. 18).

Kuna watu wanateseka sehemu mbalimbali za dunia; waonjeshwe upendo
Kuna watu wanateseka sehemu mbalimbali za dunia; waonjeshwe upendo

Somo II (1Yoh 4:7-10) linasema “wapendwa na tupendane”. Anatuhamasisha tusiwe wabaguzi bali kama Wakristo ni lazima dini yetu idhihirike katika maisha ya kupendana kindugu. Mafundisho haya ya Petro na Yohane hii leo yana msingi wake katika amri ya Kristo anaposema “Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana” tukipendana tutakaa katika pendo lake, na huo ndio ushuhuda halisi wa Pasaka. Kristo mfufuka anaonekana katika upendo wa kweli. Fundisho hili juu ya mapendo ni muhimu kwetu sote katika maisha yetu ya kila siku. Tunapaswa kuonesha upendo kwa kila mtu na kuwahudumia wote bila kujali Changamoto nyingi za familia na jamii kwa ujumla zinatokana na kukosa upendo. Jamii imefunikwa na usasa na ipo hatarini kuacha barabara. Mungu anaondolewa katika maisha ya watu na mambo ya kidunia yanatawala zaidi. Athari zake zinaonekana katika maisha ya kijamii yanayowagusa watu, kuhalalisha sheria zinazopingana na mpango wa Mungu mf. Utoaji wa mimba, ndoa za jinsia moja, dhuluma, ukosefu wa haki, uchu wa madaraka, mali, ufisadi na mengine mfano wa hayo. Tunu bora za asili, mila na desturi zimeachwa na matokeo yake tumekosa utambulisho. Kila mmoja ana njaa ya upendo, hakuna ambaye anaweza kusema sasa nimeshapendwa vya kutosha. Mtakatifu Mama Teresa wa Kalkuta aliwahi kusema ‘Njaa ya upendo ni ngumu kuiondoa kuliko njaa ya mkate.’  Kiukweli watu wanahitaji upendo. Kila mtu anahitaji kupendwa. Kuna watu wanakuwa wagonjwa kwa sababu tu hawajaoneshwa upendo. Vile vile kuna wagonjwa wanachelewa kupona kwa sababu hawajahudumiwa kwa upendo.  Ndoa zinavunjika kwa sababu zinakosa upendo. Changamoto hizi zisingalikuwapo kama kungekuwa na upendo. Upendo hauna kipimo wala masharti, hauchagui, haubagui. Mama Teresa wa Calcutta anasema “umasikini sio tu kukosa chakula, nguo na mahali pa kuishi. Umasikini mkubwa zaidi ni hali ya kujiona hutakiwi, hupendwi, na hakuna anayekujali... Ugonjwa mbaya sio UVIKO-19 Korona, Kisukari UKIMWI, TB,shinikizo la damu nk ila ni kutopendwa na kutothaminiwa” Anatuhamasisha tuanze katika nyumba zetu kupambana na umasikini na ugonjwa huu mbaya. Sote tunatamani kupendwa, upendo ndio njaa kali kuliko hata ya chakula.

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi: upendo
Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi: upendo

Tuwapende wenye shida, tuwape moyo kuwa Bwana amefufuka. Ndugu wengi wana matatizo ya ugonjwa, umasikini, watoto wa mitaani, yatima na wajane. Wamekata tamaa, wanahitaji upendo wetu sababu ni ndugu zetu; kaka, dada na rafiki zetu katika Kristo. Kumbuka unapotabasamu mbele ya mtu mwenye shida unafanya tendo la upendo, kwake tabasamu tu ni kitu adimu, zawadi bora na njema ajabu. Ukimuongezea na maneno mazuri kama ‘Mungu anakupenda, Nakupenda! Amani kwako! Wewe ni wa thamani’ unamuongezea imani kwa Mungu na siku za kuishi. Upendo wetu uwe wa kweli, tusipende kilaghai au kimaslahi. Tukumbuke kuwa upendo hauna kipimo (ukifaulu kupima tambua hupendi). Wengine tunachanganya kupenda na kutamani na hata tumefikia kulinganisha upendo na vitu au vyakula mf. “nakupenda kama chocolate”. Yesu ametupenda hadi kuutoa uhai wake kwa ajili yetu, nasi tumpende Mungu na kupendana sisi kwa sisi. Ubinafsi, choyo, tamaa na ubaguzi visitajwe kwetu na hili linawezekana – kwa imani. Penda hivi kwamba hata wengine wakiita ukichaa wewe uite upendo sababu maisha ni kama ua na upendo ndio asali yake. Tunahitaji upendo kama moyo unavyohitaji mapigo yake na upendo ni kama upepo, hatuuoni kwa macho lakini tunauhisi na kuuonja. Jumuiya au familia yenye watu wanaopendana kama ile jumuiya ya kwanza ya ki-Kristo, itakuwa ni jumuiya ya mfano kwa jumuiya nyingine. Wanajumuiya hata kama watakuwa wanakoseana hapa na pale kwa sababu ya mapungufu ya kila mmoja wao, itakuwa rahisi kusameheana na kuzidi kusonga mbele. Katika hili Mt. Vinsenti wa Paulo anatuambia kwamba; “Upendo unaweza kugeuza dhiki inayosababishwa na wengine ipokelewe kwa hiyari na iwe fadhila”. Basi wapendwa katika Kristu tukipendana kwa dhati, hakika jumuiya na familia zetu zitakuwa sehemu salama za kuishi na kujiletea maendeleo. Dominika ya leo tumwombe atujalie nguvu ya Roho Mtakatifu ili kweli tuweze kuishi kwa upendo tukikumbuka kila wakati maneno ya Kristo mwenyewe akituamuru “Mpendane kama nilivyowapenda ninyi.”

Liturujia D 6 Pasaka
04 May 2024, 09:07