Tafakari Dominika ya Sita ya Pasaka Mwaka B wa Kanisa: Upendo Ni Utambulisho wa Mkristo
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu dominika ya sita ya Pasaka mwaka B. Kwa kuwa dominika hii ni ya mwisho katika kumtafakari Kristo Mfufuka na kuanzia dominika ijayo tunaanza kudhimisha sherehe zinazohitimisha kipindi cha Pasaka na kutuingiza tena katika kipindi cha kawaida ambazo ni; Sherehe ya Kupaa Bwana, Sherehe ya Pentekoste, Sherehe ya Utatu Mtakatifu, Sherehe ya Mwili na Damu Ya Kristo - Ekaristi Takatifu na Sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ni vyema tujikumbushe japo kwa kifupi tuliyotafakari katika Dominika za kipindi hiki cha tutafakari Fumbo la wokovu wetu. Dominika ya Pasaka tulitafakari juu ya uwepo wa Kristo mfufuka kati yetu na namna anavyojidhihirisha katika maisha yetu ya kila siku; Dominika ya 2, dominika ya huruma ya Mungu Yesu Mfufuka alitutakia Amani tunda la msamaha wa dhambi, kazi ya Roho Mtakatifu akisema; “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Dominika ya tatu ya Kipindi cha Pasaka tukatafakari namna ya kumtambua Yesu mfufuka kwanza kwa kuyasoma na kuyaelewa Maandiko Matakatifu kama walivyoagua Manabii na katika kuumega mkate; Dominika ya 4 tukamtafakari Yesu Kristo mchungaji wetu mwema; na Dominika ya 5 Yesu Kristo mzabibu wa kweli nasi tu matawi na uzima wetu unategemea kushikamana naye na pasipo yeye hatuwezi kitu. Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka tunatafakari juu ya upendo ambao ni dira na utambulisho wetu wakristo, kuishi kwa ukarimu, wema, huruma, amani na uaminifu, kupokeana na kuonyana kindugu. Haya ndiyo ambayo tunayaagizwa na wimbo wa mwanzo kuyafanya ukisema; “Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazane haya yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amelikomboa taifa lake, aleluya” (Isa. 48:20). Naye Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea ili tuweze kuyaishi vyema akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, utuwezeshe kuadhimisha kwa bidii siku hizi za furaha, tunazozitumaini kwa heshima ya Bwana aliyefufuka. Na hayo tunayoyakumbuka sasa, tuyazingatie daima kwa matendo.”
Somo la kwanza ni la Matendo ya Mitume (Mdo 10:25-27, 34-35, 44-48). Somo hili linatufunulia maongozi ya Mungu kwa wokovu wa wapagani kupitia Kornelio na watu wa nyumbani kwake walipohubiriwa na Petro na kumpokea Roho mtakatifu huko Jaffa. Kornelio alitokewa na Malaika akimwagiza atume ujumbe wa kumwita Petro aje kuwahubiria. Petro alipofika, Kornelio akatoka kumlaki akamwangukia miguu, kumsujudia. Lakini Petro akamwinua akisema; “simama, mimi nami ni mwanadamu. Anayestahili kuabudiwa ni Mungu peke yake.” Petro aliwahubiria habari za kufufuka kwake Kristo na ondoleo la dhambi. Nao waliposikia habari hizi waliamini, Roho Mtakatifu akawashukia, wakaanza kunena kwa lugha. Akiongozwa na mwanga wa Roho Mtakatifu, Mtume Petro alitambua kuwa wapagani sio lazima watahiriwe ili waweze kukombolewa kama Sheria ya Kiyahudi ilivyodai. Inatosha tu wao kusadiki mafundisho ya Yesu na kupokea ubatizo. Ndiyo maana Petro anauliza; Nani awezaye kukataza maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vilevile kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo. Haya ndiyo maajabu ya Mungu ambayo zaburi ya wimbo wa katikati inayaimba ikisema; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. Bwana ameufunua wokovu wake, machoni pa mataifa, ameidhihirisha haki yake. Amezikumbuka rehema zake, na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu. Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi” (Zab. 98:1-4). Nasi hatuna budi kumshukuru Mungu kwa ajili ya makuu haya.
Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Yohane kwa Watu Wote (1Yn 4:9-17). Somo hili linatueleza juu ya asili ya Mungu kuwa ni Upendo. Ingawa tulimkashifu kwa dhambi, Yeye hakuacha kutupenda. Alimtuma Mwanae wa pekee kama kipatanisho ili sisi tumrudie Yeye Mungu Baba. Kwa hiyo, kama vile Mungu asivyokoma kutupenda, nasi tusikome kupendana. Ni vyema na haki kabisa kuyasikiliza maneno ya Yohane. Anasema hivi: “Wapenzi, na tupendane; kwa kuwa pendo la toka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili, pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba, Mungu amemtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.” Basi tujitahidi kuishi kwa upendo. Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 15:9-15). Sehemu hii ya Injili inaelezea ukuu wa upendo wake Kristo kwetu sisi wanadamu, upendo unaojidhihirisha kwa Yeye kuutoa uhai wake kwa ajili ya wokovu wetu. Ili tuweze kudumu katika pendo hilo, Kristo anatuagiza tushike amri yake ya kupendana kindugu. Upendo ambao Bwana wetu Yesu Kristo anatuasa sisi wafuasi wake tuuishi na kudumu nao ni upendo usiojitafuta wenyewe.
Upendo huu ni fadhila ya kimungu ndani mwetu na ni msingi wa fadhila zingine zote ambazo kwayo zahuishwa na kuangazwa na Mungu mwenyewe ndani mwetu. Asili ya upendo huu ni Mungu mwenyewe, “aliyeupenda ulimwengu hivi hata akamtoa mwanae wa pekee ili kila amwaminie asipotee bali awe na uzima wa milele” (Yn 3:16). Huu ndio upendo ambao Kristo anatutaka tuuishi akisema; “pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.” (Yn 13:34). Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika barua yake kwa Mapadre ya tarehe 06/04/1979 anasema kuwa upendo ni wito na ni wajibu. Kumbe tunawajibika kuonesha upendo na kuudhihirisha “kwa kupendana kindugu. Kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa hekima” (Rom 12:10). Upendo huu ni amri. Yesu mwenyewe anasema; “Kama mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake vivyo hivyo nanyi mfanye hivyo”. “Nawaamuru, mpendane (Yn 15:17). Basi tuombe daima neema za Mungu tuweze kuishi kwa upendo sisi kwa sisi ili siku ya Pentekoste tuweze kumpokea Roho Mtakatifu anayetuahidi Yesu mwenyewe akisema; “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele” (Yn. 14:15-16). Tumsifu Yesu Kristo.