Ujumbe wa Pentekoste Kutoka Halmashauri Walei Katoliki Tanzania
Na Kamati Tendaji Halmashauri Walei Katoliki Taifa, Dar es Salaam, Tanzania.
Leo ni siku maalum ambapo tunaadhimisha Sherehe ya ujio wa Roho Mtakatifu katika Kanisa. Roho Mtakatifu ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake. Katika Maandiko Matakatifu, tunasoma; Mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo Mfufuka ndio waliokuwa wa kwanza kushukiwa na Roho Mtakatifu (Taz. Mdo 2:1-4). Mitume waliendelea kuirithisha Imani Katoliki kwa vizazi vilivyofuata; hata nasi tukaipokea imani hiyo, kama alivyoagiza Bwana Wetu Yesu Kristo Mfufuka kwenda katika ulimwengu wote na kuihubiri Injili kwa Kila Kiumbe (Mk 16:15). Sisi kama walei tuna wajibu mkubwa wa kujitafakari ni kwa jinsi gani tunaukumbuka wajibu wetu kama wabatizwa. Aidha, wito huu ni wa msingi hasa tukizingatia tupo kwenye kipindi cha kuhitimisha matukio makubwa matatu ambayo ni: (i) Sinodi ya 16 ya Maaskofu (Kanisa la Kisinodi) (2021-2024); (ii) Kongamano la Ekaristi Takatifu (2023-2024); na (iii) Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo (2023-2024). Mara kwa mara, na kila mwaka Mama Kanisa huwa anatupatia vipindi vya kutafakari na kupeana shime kama vilivyotajwa hapo juu. Kwa kuzingatia uzito na umuhimu wa vipindi hivi; kipindi cha kutafakari Ekaristi Takatifu ambacho kauli mbiu yake ni “Udugu huponya ulimwengu: Nanyi nyote ni ndugu!” (Mt 23:8); kinapewa kipaumbele cha kwanza kwa sababu Ekaristi Takatifu ni kiini na Kilele cha maisha yetu ya Kikristo. Papa Leo XIII anasema: Ekaristi Takatifu ni roho ya Kanisa (Denz.3364). Kimsingi, Ekaristi Takatifu ni kiini kamili cha Kanisa, na Kanisa haliwezi kitu pasipo Ekaristi Takatifu; kwa sababu ni Kristo mwenyewe anayejitoa kweli kama sadaka kwa ajili ya Kanisa lake.
Tukijizamisha zaidi katika matukio ya kipaumbele tunayoendelea nayo ya Sinodi ya Maaskofu, na Jubilei ya miaka 50 ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikirsto (JNNK); tunapata fursa ya kipekee kutafakari Hija yetu ya hapa ulimwenguni. Tukikumbuka kwamba hapa duniani sisi ni wasafiri kwa hiyo tunao wajibu wa kuhakikisha kwamba tunajitahidi kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Kristo Mfufuka, tukitambua uwepo wake katika maumbo ya mkate na divai. Kama tulivyogusia hapo juu, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; na ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: Kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha Imani hai. Fumbo hili linahitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kutafakari nguvu yake katika maisha yetu. Kila mwamini anaalikwa kuguswa na kuongozwa na Neno la Mungu kila siku ya maisha yake. Ekaristi Takatifu ni chakula bora cha kiroho kinachositawisha roho zetu ili ziweze kukua kiimani, kiutu na kimadili. Ekaristi Takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ni kielelezo cha huduma kinachowasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Aidha ni chachu ya haki, upatanisho na amani. Katika kauli mbiu ya Ekaristi Takatifu “Ninyi nyote ni ndugu” inatualika sisi waamini kujitahidi kuwa wakamilifu kama Baba Yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu kwa kupinga ukosefu wa haki, kusimama kidete dhidi ya rushwa na ufisadi mambo yanayovuruga amani, umoja na mshikamano wa Kindugu. Katika kila Sadaka ya Misa tunashuhudia Padri ‘akiumega’ mkate, yaani; Bwana wetu Yesu Kristo anakubali kuvunjwa au kumegwa kila inapoadhimishwa Sadaka ya Misa Takatifu akitufundisha kwa unyeyekevu kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Tendo hili linatualika sisi wafuasi wake kuwa tayari kuvunjwa au kumegwa kama yeye; tunaposhiriki ibada kwenye Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo tukisafiri pamoja kama Kanisa la Kisinodi linavyotutaka kwa manufaa ya wokovu wetu na wa wengine.
Taifa la Mungu tunapoelekea maadhimisho ya kilele cha Jubilei ya miaka 50 ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo; yenye kauli mbiu ya “Kujenga Kanisa kama Familia ya Mungu” sisi Wakristo Wakatoliki Walei, tunaendelea kutafakari wajibu wetu wa kueneza Habari Njema kwa wahitaji. Je, tumewahi kujiuliza tunatimizaje wajibu mkubwa wa kueneza Injili tuliyoachiwa na Bwana wetu Yesu Kristo Mfufuka kupitia kwa Mitume wake? Tujikumbushe kuwa mwaka 1976 Maaskofu wa AMECEA waliazimia kwamba Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ndio mpango maalumu wa kichungaji katika nchi hizo. Msimamo huo ulitiliwa mkazo na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) katika kikao cha Juni 1977 - kwamba juhudi za kichungaji zielekezwe katika utume huo kwa sababu zifuatazo: Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ni Kanisa la mwanzo linaloundwa na kaya/familia zinazokutana pamoja kwa misingi ya ujirani ili kushuhudia Imani yao pamoja wakiongozwa na mwanga wa Neno la Mungu ambapo jumuiya ya kwanza na ya mfano ni ile ya Yesu na Mitume wake (Mdo 2:44-47). Hata hivyo, jumuiya hii ilitawanyika baada ya mitume kutumwa sehemu mbali mbali kwa ajili ya kueneza Injili. Baada ya Mitume kusambaa sehemu mbalimbali, Kanisa lilianza kutafuta njia bora ya kueneza utume na huduma yake ambapo kwa maongozi ya Roho Mtakatifu Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ziliasisiwa kuwa njia mpya ya Kanisa katika kujenga na kuimarisha familia bora ya Mungu. Kwa hiyo, Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ni kitovu na ishara ya uhai ndani ya Kanisa na chombo bora cha malezi na uinjilishaji.
Wapendwa Taifa la Mungu; maisha ya kiroho ya wabatizwa ni safari endelevu ndio maana tunakumbushwa ukweli huo na Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Wafilipi ili tujitahidi kulielekea lengo la imani yetu: “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo, kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu” (Fil 3:12-14). Daima tunategemea neema ya Mungu ili tuweze kukua na kustawi kiroho. Sisi wenyewe tuweke bidii isiyokoma ili kuweza kuishi katika muungano na Mungu. Moja ya nyenzo za kutuwezesha kuishi tukiungana na Mungu ni Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo. Tunaposhiriki kwenye ibada ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo tunakutana na Mungu na jirani zetu (Mt 18:20). Jumuiya Ndogo Ndogo ni chombo kizuri cha kuiunganisha parokia, chachu ya uwajibikaji na mahala pazuri pa kusoma na kutafakari Neno la Mungu, kusali pamoja na kushirikishana upendo katika maisha ya kila siku ya mitaani na katika kukabili changamoto za kiimani na kifamilia. Maisha yetu ya utume ni kama harufu nzuri ambayo shetani akiisikia anatuwinda kama ayala anavyowindwa na wanyama akikosa maji. Je nitawezaje kuelewa ni njia ipi ya kutusaidia ili tuweze kukaa na Yesu Kristo Mfufuka katika Neno la Mungu? “Je nitawezaje kuelewa mtu asiponiongoza?” (Mdo 8:31). Katika tafakari ya kipindi cha Kwaresima tuling’amua athari za kutofahamu Neno la Mungu kiimani, kimaadili, kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na uharibifu wa mazingira. Jibu la swali hapo juu na kwa ajili ya kutatua hizo changamoto ni kujiunga katika Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo na kushiriki kiaminifu kwenye mikutano ya sala na tafakari hatimaye kila mmoja wetu atajikuta anaweza kuwaongoza wengine katika kuijua Imani yetu. Iwapo tutaizingatia kauli mbiu ya Sinodi ya Maaskofu, na kuhakikisha tunatembea Kisinodi; tutaweza kujenga Kanisa kama familia ya Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake mwanzoni mwa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, alikazia mambo makuu matatu mintarafu Liturujia ya Neno la Mungu: kukutana, kusikiliza na kung’amua. Kwamba ni wakati wa sala, ibada na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu na kwamba ni wakati wa kukutana na kujitajirisha kutokana na karama, miito na utume katika ukweli, uwazi, na uwepo wa ujasiri. Sasa ni muda muafaka wa kujiuliza ikiwa kama jumuiya ya Wakristo inamwilishwa ndani mwake ule mtindo wa maisha wa Mungu wa kusafiri na wengine, au wana mashaka ya kusafiri pamoja na wengine! Huu ni wakati muafaka wa kuvua utu wa kale na kuvaa utu mpya kwa kuondokana na tabia ya kufanya mambo kwa mazoea. Sinodi maana yake ni mwaliko wa kutembea pamoja kama ilivyokuwa kwa Yesu na mitume wake. Baba Mtakatifu Fransisko katika mahubiri yake hayo anatualika sisi waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujizatiti kikamilifu ili tuweze kuwa ni wajenzi wa Sanaa ya watu kukutana. Huu ni wakati wa kukutana na kuzungumza na Kristo kwa njia ya sala, kuabudu Ekaristi Takatifu na kumsikiliza Roho Mtakatifu anataka kulikumbusha nini Kanisa kwa nyakati hizi. Tunaalikwa kuukumbatia mwelekeo mpya unaotutaka sisi waamini kutoka katika ubinafsi na mazoea tunayoyaishi. Baada ya kukutana na kusikiliza Neno la Mungu, kitendo kinachofuata ni mang’ámuzi alisema Baba Mtakatifu. Neno la Mungu ni ufunguo wa mang’amuzi na mwanga wa maisha ya kiroho (Ebr 4:12).
Katika kipindi cha Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Yesu Kristo anatutaka sisi waamini kutokumezwa na malimwengu, kuwa wazi na kuendelea kusoma alama za nyakati ili kuweza kuondokana na tabia ya kutekeleza shughuli za kichungaji kwa mazoea, ili hatimaye tuweze kutambua kile ambacho Mungu anataka kwa ajili ya Kanisa lake na ni wapi anataka kulipeleka. Tukiisha kutafakari hayo tunawaombea waamini wote safari njema ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Kongamano la Ekaristi Takatifu na miaka 50 ya Uwepo na Utume wa Jumuiya Ndogo Ndogo Ndogo za Kikristo tukiongozwa na Roho Mtakatifu katika kulijenga Kanisa kama familia ya Mungu katika nchi za AMECEA. Tudumu kama familia moja huku tukitembea pamoja kama Kanisa la Kisinodi kweli. Kila mwamini aanzie hapo mahali alipo; ashiriki ipasavyo katika kukuza na kuimarisha Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo yake. Kwa umoja wetu tuzijenge na kuziimarisha Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ili ziweze kuwa kweli chombo bora cha kusaidia kuimarisha imani yetu, kukuza maisha yetu ya Kikristo na kujiimarisha kiutume. Kwa njia hiyo tutakuwa kweli chumvi na mwanga katika jamii tunamoishi; huku tukiyatakatifuza malimwengu (Mt. 5:13-16). Mwisho tunawatakia wote Imani thabiti na upendo kwa Kristo Mfufuka ili kweli tuweze kuwa ni wamisionari na wafuasi amini kwa kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa moja Takatifu Katoliki la Mitume; na kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya wengine. “Kwa maana yeye ndiye Amani yetu aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga” (Efe 2:14).
Ni sisi watumishi wenu, Kamati Tendaji ya Halmashauri Walei Taifa. 29 Aprili, 2024.