Jubilei ya Miaka 50 ya Shirika la Umoja Mtakatifu wa Mioyo ya Yesu na Maria Tanzania
Na Lilian Lihame na Sr. Jesca Ndege, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Waamini Wakatoliki nchini Tanzania wametakiwa kuishi kwa kadiri ya mpango wa Mungu ili kusudio la Kristo Yesu kuzaliwa duniani liweze kutimia kikamilifu. Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, nchini Tanzania kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Shirika la Masista wa Umoja Mtakatifu wa Moyo wa Yesu na Maria (Holy Union Sisters) lilipofika nchini Tanzania; Jubilei ya Miaka 25 ya Kitawa sanjari na Uwekaji wa nadhiri za kwanza. Ibada ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Antony wa Padua Mbagala Zakhiem, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jumatatu tarehe 24 Juni 2024, Sherehe ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Kumbe, kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji kuwafanye wapya kiroho kwa kubadilika kimatendo na kwa kuwa ni watu wema na waadilifu “Tunaona katika somo letu la leo kuwa Mungu anayeumba ndiye anayeita watu wake mbalimbali kwa kadiri ya utashi wake, ili watende kazi yake. Kristo Yesu alipenda Yohane Mbatizaji awe mtangulizi wake; azaliwe kabla yake, ili ampokee hivyo anatakiwa azaliwe pia nyoyoni mwetu kwa kuwa watu wasafi kimoyo, ndipo aweze kuzaliwa kwetu hapo kusudio la kuja kwake duniani litakuwa limekamilika kikamilifu” amesema Askofu mkuu Ruwai’chi. Kila mwamini anatakiwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya kumleta Yohane Mbatizaji kama mtangulizi wa Kristo Yesu kwani kupitia mtumishi huyo wa Mungu yapo ya kujifunza hasa kuishi kwa kadiri ya mpango wa Mungu. Amesema Yohane Mbatizaji ni kioo ambacho kila mwamini anapaswa kukiiga ama kukifuata kama nyenzo ya kujifunza katika kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na kuishi kimatendo kuitangaza na kuishuhudia Injili ambayo ndiyo kusudio la kila binadamu kuwepo hapa duniani.
Askofu mkuu Ruwai’chi aliyetimiza miaka 25 ya uaskofu wake hivi karibuni amesema, wanapokumbuka adhimisho hilo la Misa Takatifu ya kumbukizi ya ujio wa Yohane, Wakristo wamwombe Yohane Mbatizaji huyo awafundishe namna ya kumtumikia Kristo Yesu kwa matendo mema na adili; namna bora zaidi ya kumpenda Yesu, ili aweze kuketi nyoyoni mwa waamini na aweze kuzaliwa upya katika Jumuiya, nyumba zao na katika Kanisa na ulimwengu mzima. Akizungumzia kuhusu Shirika hilo Askofu Ruwai’chi amesema masista wa Holy Union wamekuwa mstari wa mbele katika kustawisha Kanisa Katoliki tangu Utume wao uanzishwe nchini Tanzania. Amesema Masista wa Shirika hilo wamefanya kazi kubwa ya kutoa elimu tangu utume wao ulipoanza na mchango wao unaonekana kupitia watu wengi waliopata elimu na kutimiza ndoto zao za kielimu. “Leo tunapoadhimisha Jubilei ya Masista wetu hawa tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Shirika hili walianzia kule Maua Jimbo Katoliki la Moshi na wamekuwa mstari wa mbele katika ukuaji wa Kanisa hata baadhi ya Mapadre wanaonisikiliza hapa walifundishwa na hao masista kule Seminari Ndogo ya Maua Moshi hata ndugu zetu na marafiki zetu walifundishwa na masista hawa, kumbe tuna kila sababu ya kushukuru zawadi hii ya maisha na utume wao kwa Kanisa la Tanzania. Uwepo wa Shirika hili umesaidia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Injili ya Kristo hivyo kila mmoja ana sababu ya kumshukuru Mungu na katika hilo amewataka masista hao kudumu katika utume huo. “Tunamwomba Mungu aendelee kuwaita Mabinti wengi wema, wenye Afya, na watakatifu ili waweze kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyetwaa Mwili akakaa kwetu; waweze kulijenga Kanisa la Mungu na tunawapongeza wale wanaokumbuka siku walipofunga Nadhiri zao Miaka 25 iliyopita, ili Mungu aliyewawezesha kudumu katika wito wenu aendelee kuwaimarisha, kuwatia nguvu muweze kudumu katika wito huo, amesema, Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam.
Itakumbukwa kwamba, Shirika la Umoja Mtakatifu wa Mioyo ya Yesu na Maria, “Sancta Unio” limechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania katika ujumla wao. Wengi wanawakumbuka Watawa hawa kwa mchango wao katika sekta ya elimu nchini Tanzania. Huu ni mchango wa Sr Eleanor McNally na akina Sr. Adriana Van Berg, tangu Chuo cha Maarifa ya Nyumbani Msimbazi Center hadi Idara ya Computer, Chuo Cha Ufundi cha Mtakatifu Gaspar, Mtongani Kunduchi. Akina Sr Margaret Barry na Sr. Aquinas, toka Seminari ya Maua hadi kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Vijana wengi hawawezi kumsahau kamwe Sr. Annette Farrell kwa utume wake Chuo cha Ufundi Mtongani, Kunduchi. Uru Seminari na Maua, walikuwa wanashindana kwa ushindi kitaaluma, lakini nyuma yake, walikuwepo Watawa wa Ushirika Mtakatifu, “Sancta Unio.” Shirika la Umoja Mtakatifu wa Mioyo ya Yesu na Maria, “Sancta Unio” ni Shirika la Kitume lililoanzishwa rasmi huko Ufaransa mwaka 1826 na Padre John Baptist Debrabant, ambaye Mungu alimtumia kama chombo madhubuti ndani ya Kanisa. Padre John Baptist Debrabant, alizaliwa tarehe 13 Oktoba 1801 katika Kijiji cha Licelle nchini Ufaransa. Padre John Baptist Debrabant, alikuwa ni mtoto wa nne kwenye familia ya Bw. Michel Debrabant na Bi. Maria Augustine. Wakati wa mwanzilishi Padre John Baptist Debrabant, huko Ufaransa hali ilikuwa ngumu sana kutokana na Mapinduzi ya Ufaransa yaliyosababisha machafuko ya kisiasa, vita ikapelekea umwagaji wa damu, watu wakapondeka na kuvunjika nyoyo na Serikali ilikuwa katika hali ya kusambaratika, njaa, maradhi na ujinga vilishamiri nchini Ufaransa kwa wakati huo. Mwanzilishi wetu aliishi katika maisha ya kawaida kabisa katika utume wake, parokiani Padre John Baptist Debrabant, alitambua mahitaji msingi ya jamii, alijitoa kiaminifu kwa moyo wake bila kujibakiza katika kuleta matumaini kwenye jamii. Zaidi sana alilenga kuwasaidia vijana kutambua na kuishi maisha adilifu ya Kikristo katika kipindi hiki cha kumong’onyoka kwa maadili na utu wema.
Padre John Baptist Debrabant akiwa katika hali hii ngumu alikutana na wanawake wanne ambao walikuwa wakifanya kazi pamoja; ushirikiano wao ulionesha uwepo angavu wa Mungu kati yao. Walijifunza kushona, kufundisha dini na huduma nyingine za kijamii. Mwanzilishi alikuwa na upendo wa pekee kwa Bwana wetu Yesu Kristo, kutokana na upendo huo aliweza kutambua hitaji muhimu la elimu ya Kikristo katika jamii, kupitia maongozi ya Roho Mtakatifu, Padre John Baptist Debrabant aliweza kuwateuwa wanawake hao wanne ambao walikuwa wakiongozwa na Roho wa Mungu, na kuwasaidia kuimarika zaidi na zaidi katika kazi yao ya kuelimisha na huo ndio ukawa mwanzo wa Shirika la Kitume la Umoja Mtakatifu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu na Maria kwa lugha ya Kilatini “Sancta Unio” na Kwa Lugha ya Kiingereza “Holy Union.” Maana ya Jina la Shirika: Ushirika Mtakatifu tafakari yake kuu inapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Umwilisho yaani, Neno wa Mungu alipoutwaa mwili na kukaa kwake Bikira Maria; huo ukawa ni Ushirika wa Yesu na Maria. Hapo ndipo Mwanzilishi alipopata jina la Shirika letu, kutokana na jina hilo tuliweza kupata Karama ya Shirika letu yaani Ushirika na Upatanisho. Ushirika na Upatanisho, ni roho yetu ya pekee ndiyo inayotutambulisha, ni nguvu inayoendelea kukua na kuwa halisi mara inapofanyiwa kazi na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu.
Tunahitaji utambuzi na neema ya Mungu, uaminifu, ujasiri na utayari wa kukubali haraka, akili na uelewa wa kupanga na kuwa wazi kwa wengine wenye malengo kama yako. Zaidi sana kuwa na imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kupandikiza kitu kipya ndani ya kila mmoja wetu na jamii katika ujumla wake. Karama hii hujionesha kwa Masista wetu kwa kushuhudia: ushirika na upatanisho ndani ya jumuiya na katika utume wetu bila kuzingatia ukabila, lugha, rangi au udini kwa watu wanaotuzunguka, kwani tunaalikwa kuleta umoja na mapatano. Kuenea kwa Shirika, Masista wa Umoja Mtakatifu {Holy Union} tunapatikana katika Bara la Ulaya, Asia na Afrika. Kunako mwaka 1973 Masista walifika nchini Tanzania na kuanza kufanya utume katika Seminari Ndogo ya Maua iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi. Baadaye walielekea Jimboni Morogoro na hatimaye Jimbo kuu la Dar-es-Salaam, Msimbazi Centre na hatimaye kwenye Chuo cha Ufundi cha Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Mtongani, Kunduchi. Hapa Masista waliwekeza matumaini kwa vijana wa kizazi kipya kwa kuhakikisha kwamba, wanawajengea imani na matumaini kwa maisha, ili wanapohitimu mafunzo ya ufundi waweze kujitegemea pamoja na kuzitegemeza familia zao.
Historia ya Shirika la Masista wa Umoja Mtakatifu wa Mioyo ya Yesu na Maria Tanzania imegawanyika katika awamu mbili; yaani, historia ya awali 1973 – 2000 pale Masista wamisionari walipoanzisha shirika hili nchini Tanzania; na historia ya mwisho 2001 – 2024 ambayo inasimulia kuhusu masista wamisionari wanaofanya kazi na masista wazalendo. Awamu ya kwanza kutoka 1973 hadi 2000 ni kama ifuatavyo. Masista wa kwanza waliokuja Tanzania mkoani Kilimanjaro Jimbo Katoliki la Moshi walikuwa Aquinas Botting na Adriana van den Berg kulingana na mwaliko wa mapadri Wakapuchini. Walitoa huduma yao katika seminari ya Maua. Baada ya miaka mitatu Sr Adriana van den Berg alirejea Uingereza na Sr Aquinas Botting aliendelea na huduma kwa miaka 33. Sr Annette Farrell alikuja kujiunga na Sr.Aquinas, akifundisha katika Seminari ya Maua. Pia alifundisha katika shule ya sekondari ya Lombeta, ambapo alianzisha maktaba kwa ajili ya kuazimisha vitabu na kufanya maboresho kadhaa ya majengo ikiwa ni pamoja na ukumbi mpya wa kulia chakula, mabweni na madarasa. Sr. Aquinas alianza kampeni yake ya kuanzisha Chuo cha Ualimu mjini Moshi. Alifanya kampeni na kuchangisha pesa bila kuchoka kwa miaka 20. Chuo hicho kinachoitwa Chuo cha Mtakatifu Joseph sasa ni Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge cha Moshi kilichoko mkoani Kilimanjaro (MWECAU).Alihakikisha kuwa mambo ya Sayansi na Teknolojia yanapewa kipaumbele hasa kuhakikisha kuna nyenzo za kutendea kazi kama vile Maktaba nzuri na ya Kisasa, programu ya kompyuta na maabara za mambo ya sayansi. Hapa pia ndipo wito wa Sr. Agatha uliweza kutunzwa pale alipobisha hodi na kufanya kazi na Sr. Aquinas hasa katika Maktaba ya Chuo na Kompyuta. Ili kuenzi kazi nzuri hii ya Sr. Aquinas mwaka 2015 Sr. Eugenia alienda kufanya mafunzo yake kwa muda wa miezi mitatu pale chuoni hasa kwenye maktaba hii ya kisasa. Sr. Glory anasoma pale masomo yake ya sayansi. Tunatamani sana kuendelea kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa Chuo Kikuu cha Mwenge ili tuweze kuendelea kuipyaisha historia na utume wetu.
Sr. Adriana alirejea Tanzania ambako alichukua wadhifa katika Kituo cha Elimu ya Watu Wazima kilichopo Msimbazi jijini Dar es Salaam (Msimbazi Centre). Aliendesha madarasa ya ufundi wa kazi za mikono kwa wanawake na kufundisha programu ya mafunzo ya kompyuta kwa watu wazima. Sr. Annemarie Egan alijiunga na Sr. Adriana Chuoni hapo. Alifundisha Kiingereza na muziki katika Kozi ya Ukatibu Kamili pale Msimbazi na pia muziki kwa wanafunzi wa ufundi wa kazi za mikono. Aidha, alifundisha Kiingereza na muziki kwa Masista wa Dada Wadogo wa Mtakatifu Francisko na alitoa msaada mkubwa kwa Liturujia katika kanisa la Mtakatifu Petro huko Oysterbay. Sr. Eleanor McNally alikuja Tanzania kutokea Marekani. Alifanya kazi Jimbo Kuu la Dar es Salaam akianzisha na kuendesha ofisi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Idara ya Caritas. Alisaidia kutoa mafunzo kwa wenyeji akishirikiana na wafanyakazi 20 ambao ni Watanzania. Mipango iliyoanzishwa ni pamoja na mikopo midogo midogo kwa wanawake, msaada kwa akina mama wajane katika maeneo ya makazi duni, kilimo katika vijiji 20 kikiwemo kisiwa cha Mafia. Kuwa na uelewa wa jinsia na elimu ya kusoma na kuandika katika maeneo ya vijijini pamoja na kutengeneza matofali ya kujenga , upandaji miti, ustawi wa jamii na kujihusisha na jamii ya wavuvi wa Pwani. Alifanya kazi na Sr. Marilyn Spellman. Kazi iliendelea kwa uaminifu chini ya uongozi wa Christian Shembilu. Alikuwa mwaminifu kwa utume huu mpaka pale alipostafu na kazi hiyo inaendelea chini ya uongozi wa Sr. Mary Lou Simcoe.Sr Mary Lou Simcoe alikuja Tanzania ambapo alijiunga na Sr. Eleanor na Sr. Denise katika jumuiya yao katika Mtaa wa Mindu. Alifundisha Shule ya Sekondari ya Jangwani.
Sr. Rita Hannon alikuja Tanzania akitokea Burundi. Alifundisha kwa muda katika seminari ya Maua na katika shule ya Sekondari ya Lombeta. Sr. Rita alihamia shule ya Sekondari Bigwa huko Morogoro ambako walihitaji mwalimu wa Kiingereza kwa ajili ya shule ya sekondari ambayo ilianzishwa kufundisha masista kutoka katika masharika mbalimbali. Akiwa huko alikutana na Dostea Msenga na kumtia moyo katika kutambua wito wake kwa Masista wa Umoja Mtakatifu wa Mioyo ya Yesu na Maria. Sr. Denise O'Brien alikuja Tanzania na kwa mwaka mmoja alifundisha katika shule ya Bigwa Sisters na Sr.Rita lakini alihamia Dar ambapo alijiunga na Sr. Eleanor McNally na kufundisha katika shule ya Sekondari ya wasichana ya Jangwani jijini Dar es Salaam kwa miaka minne kabla ya kurejea tena Ulaya. Kwa ombi la Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S Sr. Annette alichukua jukumu la kusimamia Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Mtakatifu Gaspar del bufalo, Mtongani, Kunduchi, Jimbo kuu la Dar es Salaam ambapo wanafunzi waliweza kujichotea ujuzi na maarifa ya: Useremala, ufundi Umeme, ushonaji na uchomeleaji. Hapa alianzisha madarasa ya Kiingereza na hisabati Sr.Adriana alianzisha programu tofauti ya mafunzo ya kompyuta. Sr. Eileen Morrissey alikuja Tanzania na kufundisha Kiingereza katika shule ya Msingi ya Mtakuja pamoja na shule ya ufundi ya St. Gaspar. Ili kutimiza matakwa ya shirika kabla ya kuwaalika vijana wakike wa Kitanzania kujiunge nasi kwa misingi ya ‘njoo uone’.Sr.Adriana, Annemarie na Annette walihamia Mtongani kaskazini mwa Dar es Salaam ili kuunda jumuiya ambayo vijana wa kike wa Kitanzania wangeweza kushiriki maisha yao na kutambua wito wao. Dostea alijiunga na jumuiya katika safari yake ya wito provensia ya Anglo-Hibernia ilikubali Tanzania kama sehemu muhimu ya provensia na kuanzia hapo iliitwa AHT. Kwa wakati huu, ombi la ujenzi wa nyumba lilikubaliwa na shirika kwani hatukua na nyumba yetu wenyewe, ambapo malezi yangeweza kufanyika. Kufuatia mafanikio hayo Sr. Annette akaenda Afrika Kusini kufanya kozi ya mafunzo ya kuwalea vijana wapya wakitanzania watakaojiunga na shirika. wakati huu tulianza kuwasiliana zaidi na Cameroon ambao tayari walikuwa na uzoefu mkubwa katika kazi ya Malezi. Mnamo 1998 Dostea alijiunga na Pre-Novisiate nchini Cameroon.Nyumba mama ilijengwakwa kufadhiliwa na Provensia ya AHT kama mradi wao wa mileniam na ilijengwa mwaka wa 2000 Majimatitu Mbagala,Dar es Salaam, Sr. Eleanor alichukua jukumu la kusimamia ujenzi wa nyumba hiyo.
Awamu ya pili 2001-2024 ni kama ifuatavyo: KUINGIA RASMI MAJI MATITU- MBAGALA: Jimbo kuu la Dar es Salaam. Januari mwishoni mwa mwaka 2001 Sr. Annette, Adriana na Eileen pamoja na Benedicta walihamia Maji Matitu ili kuanza awamu mpya ya utume wetu nchini Tanzania. Masista waliendelea kutoa huduma katika shamba la Mungu. Makundi tofauti tofauti yalihusika katika utume huu kama vile: Kwakuitikia mwito wa sehemu, kulingana na mahitaji hasa katika elimu, mwaka 2001 hakukua na shule ya msingi hapa Maji Matitu viongozi wa serikali za mtaa walikuja kuomba msaada wetu wa kuanzisha hiyo shule na baada ya makubaliano shule ilianzishwa. Tuliungana nao bega kwa bega kama raia wanaowajibika katika kutekeleza azima yao. Hili lilikuwa hitaji kubwa kwani mpka sasa Shule hii inawanafunzi wengi na hata kufikia mahali serikali kuanzisha shule ingine ambayo ni shule ya msingi Martin Lumbango. PASADA Kutokana na tatizo la UKIMWI imetulazimu kusaidia familia ambazo zina tatizo hilo kwa kuwaongoza kufika PASADA, ili watoto na walioathirika wenyewe waweze kupata msaada unaohitajika. Yote yalifanyika kwa msaada wa Sr. Adriana ambaye alikuwa anafanya utume PASADA kitengo cha kompyuta hapa Jimbo kuu la Dar Es Salaam. CHEKECHEA Kutokana na wakati huo Tanzania kutokuwa na shule za Awali kwa watoto wote, sisi pia tuliamua kuanzisha Chekechea katika eneo letu ili hata watoto waweze kufaidika na elimu. Sr. Dostea alifanya utume kama mkuu wa Shule yetu ya watoto ambayo kwa sasa imekuwa na kuitwa "Holy Union Pre and Primary School."
ELIMU YA WATU WAZIMA: Tunapenda, hii nyumba iliyojengwa kwa ajili ya kikundi cha wanawake walemavu ili kuwasaidia kupata mahali pa kuishi na kuendeleza kipaji chao cha ushonaji ili waeze kupata kipato kidogo cha kujikimu. Sr. Adriana alifanya mawasiliano katika vituo vinavyojihusisha na watoto wa Mitaani wa Kinondoni na baadaye na watoto wa Kigamboni. KUWASAIDIA WALIMU. Masista pia walihakikisha walimu wa shule za msingi hasa Maji Matitu wanapata nyumba ambapo kupitia Shirika la “HABITAT FOR HUMANITY TANZANIA” waliojihusisha na programu ya nyumba za gharama nafuu ambapo nyumba takribani 16 za awamu ya kwanza zilijengwa PALMETO eneo la Saku na 23 zilijengwa Chamazi. Jumla ya nyumba 39 zilijengwa na walimu walipata makazi na kufanya kazi zao kwa weledi na ufanisi mkubwa. Tulifanya hivyo kwa kutamabua mchango wa walimu na hali duni ya maisha ya wengi wao! MEMKWA/CHEKECHEA: Kwa upande wa Memkwa tuliitikia wito wa serikali kusaidia kuwapa elimu vijana ambao walikosa elimu kwasababu ya umaskini, kuvunjika kwa familia, yatima kwasababu ya ukimwi na matatizo mengine ya jamii. Watoto ambao walionekana kama mzigo, sasa wamekuwa kioo cha jamii. Sr. Mairead toka Januari 2006 alipofika nchini alichukua jukumu la kusimamia Chekechea ya Montessori na kumruhusu Sr. Dostea kwenda kusomea katekesi huko Sanya juu. Memkwa imekua chini ya uangalizi wa Sr.Annette na utume na vijana katika swala la Bendi ambapo vijana walipiga bendi wakat wa ziara ya Waziri Mkuu Bertie Ahern hapa Tanzania kwenye ubalozi wa Ireland.
SEKONDARI: Katika sekta ya elimu ya Sekondari tuliitikia pia wito wa Serikali kusaidia kupanua idadi ya Shule za Sekondari. Kwahiyo Mnamo Januari 2008 shule ya Sekondari ya Debrabant ilifunguliwa rasmi iIlikuwa imechukua miaka 4 kujenga chini ya usimamizi wa Sr. Annette. Lengo letu ni kuifanya kuwa mfano wa shule nyingine na vilevile kujenga uhusiano na ushirikiano bora kati ya shule zote mpya za jirani zikiwemo shule za kata. Sr.Dostea na Eugenia walitumwa na kusimikwa rasmi katika jumuiya mpya ya Betania Saku. Sr. Dostea alifundisha somo la Dini na Malezi kwa vijana na hasa katika shule yetu ya Debrabant. KUWASAIDIA WATOTO WALEMAVU: Huu pia ulikua mwaliko mpya kutoka kwa jamii kuwasaidia watoto walemavu wa mahali. Tumefanya utafiti na tumeona kuwa ni kweli inahitajika sana. Kwa Sala na Imani tunajitahidi kutafuta njia ya kuwawekea kituo ambapo watoto na wanaowatunza waweze kupata misaada inayohitajika hasa katika kuwafanyia mazoezi watoto hawa. Pia wazazi wao kupata elimu ya ufundi wa kushona ili waweze kujikimu na kupata mahitaji yakuendelea kuwalea watoto wao. Kituo cha Matumaini kilifunguliwa ili kusaidia watoto walemavu na kusaidia familia zao. Kituo hiki ambacho kimsingi kumefuta machozi ya wanawake na watoto wengi ambao walionekana kama mzigo katika familia zao. Na katika kituo hiki tunatengeneza mazingira ya kuwasaidia watoto ambao wanashida ya autism( hili ni tatizo la kihisia linalotokea kwa watu tangu utotoni na kuathiri uwezo wao wa kuwasiliana na watu wengine) haya yote ni ndoto ya aliyekuwa msimamizi mkuu Sr. Adriana.
KIBALI CHA NYUMBA YA MALEZI TANZANIA: Baada ya muda wote toka 1998 kuwatuma walelewa wetu Cameroon mwaka 2015 tulipewa kibali cha kuanza nyumba ya malezi hapa nchini Tanzania na Sr. Dostea na Alice wakaenda Zambia kuanza kozi yao ya Malezi katika Kituo cha Mafunzo cha Kalundu. Halafu malezi ya Wanovisi yakaanza rasmi chini ya mama mlezi Sr. Dostea. Kwa muda walianzia katika nyumba yetu ndogo “Amani House” na Ufunguzi rasmi wa nyumba ya Wanovisi huko Dundani Mkuranga ulifanyika ambako sasa ndio nyumba ya malezi. Tunamshukuru Mungu kwa jambo hili. UTUME KISIJU- PWANI: Tumeweza pia kufungua nyumba yetu huko Kisiju ambapo tunatoa utume wetu hasa katika nyanja ya malezi kwa vijana na pia kufundisha somo la Dini msingi na sekondari. Katika Parokia ya Kisiju tunaweza kutoa katekesi na pia Sunday School. Hii inafanya tuwe na nyumba au jumuiya nne hapa jimbo kuu la Dar Es Salaam. Tunamshukuru Mungu kwa utume huu hasa katika kuitenda kazi ya mungu katika shamba lake majimbo matatu Jimbo Katoliki la Moshi, Dar Es Salaam na Morogoro. Kote huku tumejihusisha zaidi na Elimu katika nyanja zote na hasa elimu ya dini na malezi kwa vijana na familia zao.