Kard.Zuppi na wanahija 160 wa Bologna huko Nchi Takatifu na ukaribu kwa wateswa!
Na Roberto Cetera – Yerusalemu na Angella Rwezaula – Vatican.
Kuwa karibu na wale wanaoteseka, ndiyo maneno yaliyosika katika vyombo vya habari vya Vatican, kutoka kwa Kardinali Matteo Maria Zuppi, rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Italia (CEI) na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Bologna nchini Italia, wakati wa kutoa muhtasari wa roho na malengo ya hija iliyoanza tarehe 13 Juni na ambayo itahitimishwa Jumatatu tarehe 16 Juni 2024 katika Nchi Takatifu akiwa na waamini 160 wa Jimbo Kuu la Bologna katika hija ambapo waamini hawa wanatoka katika hali tofauti za harakati na Jumuiya kwa kutaja machache ni kama vile: Pax Christi Italia, Jumuiya ya Papa Yohane XXIII, Agesci, Harakati ya Wafocolari, Acli, Chama cha matendo ya kikatoliki cha vijana na wengine.
Misa na kukutana na familia za mateka
“Amani kwenu ndiyo kauli mbiu inayoongoza mpango uliopendekezwa na Kanisa la Bologna kwa ushirikiano na Upatriaki wa Kilatini ya Yerusalemu. Hata hivyo kwa dhati, alikuwa ni Patriarki, Pierbattista Pizzaballa, ambaye aliwakaribisha mahujaji wakiongozwa na Kardinali Zuppi! Kwa njia hiyo Patriaki Pizzaballa pia aliadhimisha Misa katika Kanisa Kuu la Mataifa huko Gethsemani mara baada ya kuwasili kwa wageni hao. Miongoni mwa walioshiriki katika ibada hiyo alikuwepo hata msimamizi wa Nchi Takatifu, Padre Francesco Patton(OFM). Mwishoni mwa liturujia, kikundi hicho kilielekea kwenye Kanisa Kuu Mtakatifu Mwokozi la Yerusalem, ambapo Walisali pamoja masifu ya jioni ikiwa ni kumbu kumbu ya sikukuu ya Mtakatifu Antoni wa Padua, ambaye pia mlinzi wa Nchi Takatifu. Mara tu baada ya hapo, mkutano ulikuwa umepangwa wa kukutana na baadhi ya wanafamilia wa mateka wa Israel waliotekwa na Hamas huko Gaza tangu tarehe 7 Oktoba. Na Programu ya tarehe 14 Juni 2024 inajumuisha Misa Takatifu kwenye Kaburi Takatifu na kisha kuhama kwenda huko Bethlehemu.
Kardinali Zuppi:Hija hii ni kama kumtembelea rafiki
Akizungumza na Vatican News, kuelezea ziara hiyo Kardinali Zuppi alisema: “Tulianza safari ya Hija na Patriaki Pizzaballa ambaye tumeunganishwa kwake na ushirika wa karibu. Ni kama kwenda kumtembelea rafiki ambaye anateseka na kumwambia 'tunakupenda, tuko karibu na wewe na tunangojea ahueni ambayo tunatarajia itakuja hivi karibuni'. Mwisho wa ghasia ni chaguo muhimu katika njia ya amani." Maneno yake pia yaliyozinduliwa kwa upya na rais wa CEI kwa kikundi cha waandishi wa habari waliokutana naye huko Yerusalemu. Akijibu baadhi: “Ni kitu, ambacho tumekuwa tukiota juu yake, tangu vurugu zilipoanza kutikisa Nchi Takatifu,” Alisema Kardinali Zuppi akimaanisha hija hiyo. “Tunataka kusema kuwa tuko karibu, haitoshi kuifanya kwa mbali au kwa ujumbe … Inabadilisha kila kitu kuwa karibu na wengi wanaoteseka, tunawaombea ambapo ni ukaribu wa kwanza na pamoja nao tunaota kwamba katika giza nuru ya amani itafika hivi karibuni.”
Kardinali Pizzaballa:ukaribu na huruma ndio tunachohitaji
Kwa upande wake Kardinali Pizzaballa, alitoa "shukrani nyingi kwa mpango huu wa ujasiri." Kupitia vyombo vya habari vilivyokuwepo alitaka kusema adharani ile: “asante Kardinali Zuppi kwa sababu katika kipindi ambacho kila mtu anaogopa kufika aliweza kuandaa kikundi cha watu 160 waliokuja hapa kwa hija ya mshikamano, sio tu na Wakristo, bali na watu wote wa Nchi Takatifu, Israeli na Palestina”. Kwa njia hiyo Patriaki Pizzaballa aliongeza: “Natumaini kwamba ishara hii itachukuliwa na wengine, kwa sababu tunahitaji uwepo wa mahujaji ambao huleta utulivu kwa familia nyingi zilizoachwa bila kazi na pia kurejesha uhai.” Kwa mujibu wa Kardinali Pizzaballa “ni wazi kuwa amani haitazuka katika wakati huu ambao ishara pekee tulizonazo ni vurugu na migogoro. Kuja hapa kutoa uaminifu, ukaribu na huruma ndio tunachohitaji hivi sasa. Inatuonesha kwamba tunaweza kutegemea marafiki wengine, tunashukuru.”
Balozi wa Vatican,Yllana: mahali patakatifu huwa wazi kwa mahujaji wote
Ni shukrani vile vile ambayo ilioneshwa pia Askofu mkuu Adolfo Tito Yllana, Balozi wa Vatican nchini Israeli na Mwakilishi wa kitume wa Yerusalemu. Kwa vyombo vya habari vya Vatican, kiongozi huyo alisisitiza jinsi ambavyo uwepo wa rais wa Baraza la Maaskofu Italia pamoja na kundi la jimbo lake kuu umekuwa muhimu. Na kwamba: “unaonesha ukaribu na ushirikiano na jumuiya ya Kikristo ya mahali patakatifu. Zaidi ya hayo, ni muhimu sana kwa sababu inaonesha kila mtu kwamba, licha ya hali ilivyo hapa, mahali patakatifu huwa wazi kila wakati kwa ajili ya mahujaji. Ni uthibitisho tena unaoimarisha imani katika nchi hii, Yerusalemu, Mama wa Makanisa yote.”Alisisitiza Balozi wa Vatican nchini Israel na Mwakilishi wa Kitume wa Yerusalemu.