Tafuta

Kumbukumbu ya miaka 74 ya vita vya Korea:tarehe 25 Juni Kumbukumbu ya miaka 74 ya vita vya Korea:tarehe 25 Juni  (ANSA)

Kumbukizi Vita vya Korea:Wito wa Askofu wa Seoul kwa amani

Askofu mkuu Peter Soon-taick Chung wa Jimbo kuu Katoliki la Seoul nchini Korea Kusini alitoa wito wa kujitolea upya kwa ajili ya amani na upatanisho akisisitiza kwamba ni jambo la msingi kutopitisha urithi wa chuki kwa vizazi vijavyo.Alisema hayo katika mkeshi wa maadhimisho ya miaka 74 tangu kufanyika vita vya Korea

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika mkesha wa maadhimisho ya miaka 74 ya Vita vya Korea, Askofu mkuu Peter Soon-taick Chung wa Jimbo kuu Katoliki la Seoul alitoa wito wa kujitolea upya kwa ajili ya amani na upatanisho akisisitiza kwamba ni jambo la msingi kutopitisha urithi wa chuki kwa vizazi vijavyo.  Wakati wa mahubiri yake kwenye Misa Takatifu kwa ajili ya 'Siku ya Sala kwa ajili ya Upatanisho na Umoja wa Watu wa Korea' iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Myeongdong, Askofu Mkuu Chung alisema, “Ingawa hali kati ya Korea mbili inaweza kuonekana kuwa mbaya, sisi Wakristo hatuwezi kubaki ndani, kukata tamaa. Badala yake, ni katika enzi hii ya chuki inayoongezeka ndipo maombi yetu yanaweza kuangazia wakati huu kwa nuru kubwa zaidi.”

Aliendelea kwa kusisitiza mafundisho ya Yesu akisema, “Yesu Mwenyewe alionesha kwamba amani haiwezi kupatikana kupitia jicho kwa jicho. Amani inaweza kupatikana kwa mazungumzo tu. Askofu Mkuu aidha aliwataka waamini kusali si kwa ajili ya mabadiliko ya mwingine bali azma ya kuiga huruma na subira ya Mungu isiyo na mipaka kwa kuchagua njia ya amani. Akitafakari juu ya ustahimilivu wa watu wa Korea, Askofu Mkuu alisema, “Watu wetu walishikilia matumaini kwamba tunaweza kuondokana na umaskini, ambao ulituletea maendeleo ya kiuchumi, na matumaini ya kushinda udikteta, ambao ulisababisha kupatikana kwa demokrasia. Sasa, lazima tuwe na tumaini jipya kwamba tunaweza kushinda mgawanyiko. Tumaini hilo litaleta amani ya kweli katika Rasi ya Korea.” Akihitimisha mahubiri yake, Askofu Mkuu Chung alitoa wito kwa kila mtu anayeishi kwenye Peninsula ya Korea “kuchagua njia ya msamaha na upatanisho badala ya ile ya chuki na kinyongo.”

Tangu 1965, Baraza la Maaskofu Katoliki Korea limeadhimisha Juni 25 kuwa ‘Siku ya Sala kwa ajili ya Kanisa katika Kimya.’ Katika 1992, jina lake lilibadilishwa kuwa ‘Siku ya Sala kwa ajili ya Upatanisho na Umoja wa Watu wa Korea.’ Jimbo kuu la Seoul lilianzisha Kamati ya Upatanisho wa Watu wa Korea mnamo 1995, kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 50 ya Ukombozi. Kamati hiyo hufanya mikutano ya maombi ya Misa na kugawana amani kila Jumanne saa 1.00, jioni katika Kanisa Kuu la Myeongdong. Hadi leo, Misa 1413 zimefanyika, zikisisitiza kujitolea kwa kudumu kwa kamati katika kukuza amani na umoja kwa sala na tafakari. Kamati pia inasimamia miradi mbalimbali ya elimu na utafiti, inasaidia programu kwa ajili ya Wakorea Kaskazini na walioasi, na kupanga safari za kwenda katika maeneo ya mpakani chini ya mpango wa ‘Pepo za Amani.’

24 June 2024, 14:42