Tafuta

Safari ya Mama Bikira Maria Kwenda kumtembelea binamu yake Elizabeti, ni safari ya matumaini na  safari ya ukombozi. Safari ya Mama Bikira Maria Kwenda kumtembelea binamu yake Elizabeti, ni safari ya matumaini na safari ya ukombozi.  

Bikira Maria Chombo cha Imani, Matumaini na Mapendo Thabiti

Bikira Maria kumtembelea Elizabeti ni tukio la imani na huduma ya upendo na ambao unatangaza utimilifu wa nyakati, kwa kuzaliwa Mkombozi wa ulimwengu anayetanguliwa na Yohane Mbatizaji. Hii ni sikukuu ya kujenga na kudumisha upendo kwa Mungu na kwa jirani! Bikira Maria aliondoka kwa haraka bila hata kujifikiria Mwenyewe hata kidogo, anavuka milima na mabondo ambayo yanageuzwa kuwa ni kikolezo cha ari ya kumwangalia binamu yake Elizabeti! Upendo!

Mama Evaline Malisa Ntenga, - Vatican

Sikukuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti ni ishara ya huduma ya upendo. Elizabeti anampokea Bikira Maria kama Mama wa Bwana wake. Rej. Lk 1:39-56. Hii ni Sikukuu ya utenzi wa Bikira Maria unaojikita katika fadhila ya kusikiliza kwa makini, kutafakari na kutenda kwa imani, mapendo na matumaini. Bikira Maria kumtembelea Elizabeti ni tukio la imani na upendo na ambalo linatangaza utimilifu wa nyakati, kwa kuzaliwa Mkombozi wa ulimwengu anayetanguliwa na Yohane Mbatizaji. Hii ni sikukuu ya kujenga na kudumisha upendo kwa Mungu na kwa jirani! Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, ana haya ya kusema! Tunapohitimisha Mwezi pendwa wa Mama Bikira Maria 31 Mei 2024, hebu tutazame safari ya Mama Bikira Maria Kwenda kumtembelea binamu yake Elizabeti, safari ya matumaini, safari ya ukombozi. Mama Bikira Maria, anaondoka kwa haraka, kwa unyenyekevu, bila kujijali yeye mwenyewe, akisukumwa na upendo na utumishi. Anaamini, anashinda hofu. Hofu au kukata tamaa mara nyingi hutulazimisha kuahirisha mambo, ama kutuzuia kusonga mbele. Kwa upande mwingine, tumaini hutupa ari ya kusonga mbele, hutuongezea uhai. Injili ya leo kutoka Mwinjili Luka 1:39-56 inaweka mbele yetu wanawake wawili ambao hawakujiruhusu wazuiliwe na hofu na kukata tamaa, ambayo wangeweza kuikumbatia kwa kuzingatia uzoefu katika maisha yao: Maria alitii na kukubali mapenzi ya Mungu, anaamka na kuacha vyote, hakukaa kufikiria nini kinaweza kutokea atakapopatikana na ujauzito, hakujali atamwambia nini mchumba wake Yosefu. Kwamba mimi ni mama wa Mungu? Maisha yake yalikuwa hatarini.

Bikira Maria ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo thabiti
Bikira Maria ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo thabiti

Kwa upande mwingine Binamu yake Elizabeti ni dhahiri alishajihesabia kukosa, hatarajii tena chochote chema katika maisha; pengine alishabatizwa kuwa binadamu tasa, binadamu asie na tumaini, akiaminishwa kwamba yeye ni mti usioweza kuzaa matunda. Pengine alifikiri Mungu tayari yupo mbali nae. Hata mume wake Zakaria, licha ya muda anaotumia hekaluni kuwasiliana na watakatifu, haamini tena kama Mungu anaweza kutenda katika maisha yao. Mama Bikira Maria na Binamu yake Elisabeti wanatufundisha kwanza kabisa kutulia tunapokuwa na kikwazo chochote katika maisha. Mama Bikira Maria anapewa taarifa ya kuwa atachukua mimba, atamzaa Mkombozi. Katika umri wake mdogo, hana mume, kwa mila za kiyahudi malipo ni kifo. Anahitaji mtu wa kusema nae Kwa haraka Mama Bikira Maria anaanza safari kuelekea milimani. Mara nyingi tunaitazama milima kama kikwazo/kizuizi. Maria haruhusu hofu itangulie lengo lake akisukumwa na upendo. Bikira Maria anashinda mlima – kikwazo cha kutembea mbali. Kikwazo ambacho kingeweza kuzuia kuona lengo. Bila shaka Bikira Maria anatiwa moyo na hamu ya kushiriki na Elizabeti kile wanachopitia wote wawili: Mungu anafanya kazi katika maisha yao. Kwa hiyo, Maria anatafuta mtu ambaye anaweza kumwelewa, mtu ambaye anapitia uzoefu kama anaopitia yeye. Kwa upande mwingine. Bikira Maria pia anasukumwa na hamu ya kutumikia. Kwa sababu ametambua kwamba kuna mtu anayemhitaji: kushiriki na kutumikia ni msukumo ambao unaturuhusu kuona mbali ya changamoto zetu binafsi. Kabla ya kujilaumu, kukata tamaa, tutambue kuna wengine wanauhitaji zaidi yetu. Kuna wengine wanatuhitaji.

Bikira Maria ni Kimbilio la wakosefu
Bikira Maria ni Kimbilio la wakosefu

Elizabeti, kwa upande wake, hakubaki amefungwa katika kukatishwa tamaa ya maisha ambayo hupita bila kuzaa matunda. Yeye anatupa mfano wa binadamu ambae katika hali ya ubinadamu anaonekana amekata tamaa lakini aliendelea kusubiri kwa kimya kwamba Bwana atafanya. Hakupoteza tumaini. Ni kwa ubinadamu huu kwamba Bikira Maria anamleta Mkombozi.  Bikira Maria ni mfano wa Kanisa, aliyeitwa na kukubai kujisadaka akamleta Yesu mahali ambapo ubinadamu umevunjika moyo na kukata tamaa. Elizabeti anatukumbusha Mungu anatimiza ahadi yake ya mema kwa kila kiumbe, mwanamume na mwanamke hata kama ni baada ya miaka mingi.  Ni wazi kuwa Elizabeti alishinda majaribu ya kuvunjika moyo kwa kuhisi Mungu yupo mbali. Aliendelea kuingoja ahadi. Daima kuna wakati ambapo Mungu anakuja karibu na kujibu maombi yetu kwa namna ya ajabu. Elizabeti anatufundisha kamwe kutopoteza matumaini. Elizabeti ni mwanamke anayesikiliza kwa makini. Ni katika kusikiliza kwa makini tunamsikia Roho Mtakatifu. Elizabeth anatajwa hapa kama mwanamke wa utambuzi. Ni baada ya kumsikiliza Mama Bikira Maria anajihoji, imekuwaje mama wa Mkombozi kunitembelea? Elizabeti na Mama Bikira Maria hawakuwa watu mashuhuri ama wenye mamlaka. Ni wanawake wa kawaida kabisa wanaandika historia. Huu ni mwaliko wa kubadilisha mitazamo yetu juu ya wengine, mwaliko wa kugundua jinsi Mungu anavyoweza kuingilia kati hali za watu na kuandika historia. Kila jambo, lina majira. Hata Mungu mwenyewe ana majira na wakati mwingine majira ya Mungu hutimia katika namna ambazo hatuzitarajii. Huu ni mwaliko kwetu sisi pia, kuna wakati inabidi tusimame ama tunasema kuweka break, kufanya tafakari na kuanza tena safari. Mama Bikira Maria ni mwombezi wetu. Mama Bikira Maria ni kimbilio letu. Daima tumkimbilie yeye. Mwisho wa mwezi wa Rozari Takatifu usiwe mwisho wa kusali rozari, bali mwanzo wa safari ya kuendelea kumsihi Mama Bikira Maria atusindikize katika changamoto zetu, katika madhaifu yetu.

Bikira Maria
07 June 2024, 14:30