Mkutano Mkuu wa 45 wa WAWATA: Uchaguzi Mkuu na Vipaumbele 2024-2026
Na Mama Evaline Malisa Ntenga, na Agatha Kisimba, Dar es Salaam.
Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika.” Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, jamii na Taifa kwa ujumla, pia wanawake wanakuwa na maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii kwa ujumla, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa ni taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wa Kristo Yesu. Kuanzia tarehe 6 Juni hadi tarehe 9 Juni 2024 Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Taifa imeadhimisha mkutano wake mkuu wa 45 wa WAWATA, Taifa, uliofunguliwa na kufungwa na Padre Beno Kikudo, Mkurugenzi wa Idara ya Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Mkutano huu ulianza kwa: Ibada ya Misa Takatifu, Semina kwa viongozi ili kujiweka imara katika maisha ya kiroho pamoja na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoza vyema katika mkutano wao na hatimaye uchaguzi mkuu. Padre Benno Kikudo amekazia umuhimu wa Wanawake Wakatoliki Tanzania kujikita katika uadilifu, kanuni maadili na utu wema. Wawe wanyenyekevu na wenye ari na moyo wa huduma; wepesi katika kufuata Mafundisho na maelekezo ya Mama Kanisa, kama sehemu ya mchakato wa kuyaendea matakatifu. Wanawake watambue kwamba, wao ni wainjilishaji wakuu, dhamana wanayopaswa kuitekeleza kwa matendo adili, manyofu na matakatifu. Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, amewakumbusha wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 45 wa WAWATA, Taifa kwamba, wanaadhimisha mkutano huu wakati Kanisa katika nchi za AMECEA zinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo; Ujenzi wa Kanisa kama familia ya Mungu. Amekumbushia mafanikio na changamoto walizokumbana nazo katika uongozi wao na wakati wa kufunga amebainisha vipaumbele vya WAWATA kwa mwaka 2024-2026.
Ifuatayo ni hotuba ya Mama Evaline Malisa Ntenga wakati wa kufunga mkutano mkuu wa 45 wa WAWATA Taifa.
Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. 1 Korintho 15: 10. Mpendwa sana Baba Beno Kikudo, mlezi wa WAWATA ulieambatana nasi, wapendwa wakurugenzi wetu wote wa majimbo, masista, wapendwa viongozi, chipukizi wetu na taifa lote la Mungu, kwe upendo wa Kristo. Naomba kuanza kwa kutoa utambulisho mfupi: Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA Taifa. Paschasia Rugumilla, Makamu Mwenyekiti – Jimbo Bukoba. Stella Kahwa, Katibu – Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Faraja Mbena - Katibu Msaidizi, Jimbo Tunduru-Masasi. Dorah Chikongoe; Mtunza Hazina, Jumbo kuu Dar es Salaam. WAWATA Chipukizi kutoka: Kanda ya Jimbo kuu Arusha; Kanda ya Jimbo kuu Dar es Salaam; Kanda ya Jimbo Kuu Dodoma; Kanda ya Jimbo kuu Mbeya; Kanda ya Jimbo kuu Mwanza; Kanda ya Jimbo kuu Songea na hatimaye, Kanda ya Jimbo kuu Tabora. Tumekuwa hapa “Bunju Consolata Mission Centre” kwa siku ya 4 leo. Tulianza na tafakari nzuri ya kutuimarisha na kuganga mioyo iliyopondeka, kuvunjika na iliyokata tamaa. Tumepata elimu ya afya. Tumepata nafasi ya kushrikishana utume tunaofanya katika majimbo yetu na mwisho tukahitimisha kwa uchaguzi. Ni vyema kila mmoja akamshukuru Mungu lakini katika kushukuru akatafakari, amevuna nini na anapeleka nini kwa waliomchagua. Tunahitimisha mkutano wetu leo, tunaanza safari ya miaka miwili (2) iliyojaa changamoto, majukumu, miradi na matarajio mengi kwa waliotuchagua na Kanisa kwa ujumla wake. Yote haya lazima yajumuishwe katika misa tuliyosherehekea: Kuchagua kati ya Mungu na uovu. Papa Francisko amesema mara nyingi kuwa, hofu, mashaka, ukosefu wa ujasiri unaweza kuzuia njia ya kujenga upya Kanisa/utume tunaohitaji leo. Katika Waraka wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anaenda mbali na kusema kwamba, ikiwa tutabaki kudhoofishwa ama kupooza kwa hofu, tunaweza tena kubaki "watazamaji wa anguko lisilo na matunda yoyote katika Kanisa.’
Ili kufanikiwa, tunamhitaji Roho Mtakatifu, tunahitaji umoja na mshikamano, tunamhitaji kila mmoja, tunahitaji mahusiano sahihi. Kuna uhusiano wa kijuujuu, ambao tunahisi hakuna wajibu, unaweza kudumu au kumalizika bila tatizo, lakini kuna uhusiano ambao tumedhamiria, ambapo tunaweza kuhisi thamani yake, lakini ambao pia wakati mwingine kunaweza kuwa na uzito, labda kwa sababu hatujachagua kwa dhati dhamana hiyo tumejikuta tunalazimika kuhusiana wenyewe, au kwa sababu hatukufikiria kuwa ushiriki unahitaji kujisadaka bila kujibakiza. Tunahitaji agano. Agano la mahusiano sahihi tunaweza kulipata kwa kusoma na kuelewa Liturujia ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo tuliyoiadhimisha Dominika tarehe 02/06/2024. Tusome pia kitabu cha Kutoka sura ya thelasini na nne (34) ambapo, sifa za agano lililozaa mahusiano kati ya Mungu na watu wake zinafafanuliwa. Tufanye nini? Anza kwa kumshukuru Mungu aliekuteua, baina ya wengi na kukustahilisha kwani sisi sio bora zaidi bali Mungu amependa kututumia kwa wakati huu. Kila mmoja atafakari wito wake, ameitwa na nani? Mienendo yetu isitiliwe shaka, mavazi yawe na staha jina la Mungu lisitukanwe. Viongozi tujenge tabia kusali, kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu na mapoko ya Kanisa Katoliki ili kuweza kuwamegea wale tunaowaongoza. Tumwombe Mungu atujalie japo fadhila moja ya Mama Bikira Maria hasa ya unyenyekevu, msamaha na usafi wa moyo. Tuombe Mungu Roho Mtakatifu atupe mshikamano sisi watano katika parokia/jimbo/taifa. Mwenyekiti nisiwe mungu mtu. Tunaporejea majimboni, tukawatumikie wale tuliokabidhiwa na Mungu. Tusimtazame mwanadamu.
Vipaumbele vya mwaka 2024/25 – 2025/26 ni pamoja na: Malezi ya Familia – watoto na wenza wao wa ndoa. Wongofu na uadilifu wa kiilolojia – kulinda na kutetea uhai tangu mimba inapotungwa hadi mauti yanapomfika mtu. Kuwa sauti ya wasio na sauti kupitia mradi wa World Women Observatory (WWO). Elimu juu ya kuboresha uchumi wa familia bila kuathiri malezi na makuzi ya watoto. Kujitakatifuza kupitia hija mbalimbali. Kitegauchumi cha Ilala. Mwisho ninapenda kuwashukuru walezi wetu wote katika ngazi zote; viongozi wa Taifa uliotumikia WAWATA kwa kipindi cha 2020-2024, Napenda pia kuwashukuru kwa moyo wa dhati watumishi wote wa ofisi kwa utendaji wao, nawashukuru ninyi nyote viongozi wa majimbo kwani utume ndiko unakofanyika. Napenda kuwashukuru sana wenyeji wetu kwa kutuhudumia vizuri, tunaomba radhi kwa mapungufu yoyote yaliyojitokeza. Napenda kuvishukuru vyombo vyetu vya Habari vya Kanisa – Radio Vatican, Tumaini Media, Radio Maria, Jugo Media, Muphilipi na wote wanaoshiriki kupeleka Habari njema za kumtangaza Kristo. Napenda kuwashukuru wanawake wakatoliki kote Tanzania kwa sadaka zao – fedha/mali na sala. Tunawahitaji nyote. Tuendelee kumwomba Mama Bikira Maria somo wetu atuombee kwa mwanae ili tuwe na hisia na mitazamo sawa nae na mwanae (same feelings & attitudes as Jesus and Mother Mary.) Wanawake Wakatoliki, wajenzi stadi wa mafungamano ya udugu wa kibinadamu kwa amani ya ulimwengu.
Mama Evaline Malisa Ntenga, HOTUBA YA UFUNGUZI: Kwa Upendo Wa Kristo… Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo - Miaka 50 ya kujenga Kanisa kama familia ya Mungu! Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Uhai na kwa zawadi ya Utume wa Wanawake Wakatoliki Tanzania. Kwa namna ya pekee na kwa moyo wa unyenyekevu niwashukuru sana wenyeji wetu Bunju Consolata Mission Centre kwa mapokezi - Ahsanteni sana. Nawashukuru kwa dhati viongozi wa WAWATA Majimboni ambao bila wao WAWATA hakuna. Natambua sadaka zenu, sina shaka Mungu anawalipa na ndio maana mpaka sasa mnang’ara kama mnavyooneka – Tumshangilie Mungu. Wapendwa Baba zetu walezi, Idara ya Kichungaji na Idara ya Walei, kwa Pamoja mkimwakilisha pia Mhashamu Baba Askofu Edward E Mapunda (Mkiti Idara ya Walei) tunaomba mpokee Shukrani zetu kwa kuendelea kutulea, kutushauri, kutuelekeza lakini Zaidi kuendelea kututuma kumtumikia Mungu kwani hii ni nafasi adhimu na njia ya kuuchuchumilia utakatifu. Mungu alituumba ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake mbinguni. Tunaomba mwendelee kutuombea ili tumruhusu Roho Mtakatifu aendelee kutenda kazi ndani yetu na kwa namna hiyo tuiishi kauli mbiu yetu na kwa Upendo wa Kristo tuwatumikie wengine na kuwajibika ipasavyo na kuwa sababu ya furaha kwa wengine na kwa Kanisa zima kwa ujumla.
Wapendwa viongozi, tunaanza mkutano wetu kwa mafungo na tafakari. Nipende kunukuu Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 12:2-8. ‘Wala msiifuatishe namna ya dunia hii, bali mgeuzwe na kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza na ukamilifu’.) Anayetualika kumshukuru Mungu kwa vipawa alivyotujalia na kumshukuru Mungu kwa vipawa vya wengine huku tukimruhusu Mungu Roho Mtakatifu kutukumbuha, kutushauri na kutuongoza. Hebu tupate nafasi ya kumualika Roho Mtakatifu atupatie mang’amuzi nasi tupokee kwa moyo wa unyenyekevu kama Mama Bikira Maria alivyotii mapenzi ya Mungu. Tuko katika safari ya Sinodi na Pia Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo: Wapendwa mama, dada zangu, kama viongozi wa Wanawake Wakatoliki hapa Tanzania mmekuwa chachu katika kushiriki juhudi na kazi za kitume kwa njia ya misaada ya kifedha, hali na mali katika kuwezesha Parokia zetu, majimbo yetu na bila kusahau seminari na nyumba za watawa. Kwa miaka 50 ya WAWATA na miaka 50 ya JNNK mmewekeza kujenga umoja ambao pamoja na changamoto umebaki imara. Katika Homilia ya leo, Baba mlezi ametukumbusha tumeitwa kutumika, kanisa lina matazamio makubwa katika uinjilishaji wetu, ametukumbusha wanawake wa shoka waliojisadaka wakajitoa kwa mali na sadaka wakiambata na Yesu Kristo na kuwahudumia makutano... Joana mke wa Kuza, Maria Magdalena aliyeponywa pepo saba na Susana.
Katika mkutano wetu wa Bodi ya Wanawake Wakatoliki Duniani WUCWO, hivi karibuni tulipata nafasi ya kufanya mkutano na mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha: Kardinali Kevin Joseph Farrell ambapo Kardinali Farrell aliwapongoeza Wanawake na kuwasihi kutokatishwa tamaa na changamoto wanazokumbana nazo katika utume badala yake wadumu katika kusali kwani kazi wanayoifanya ni wito wa Mwenyezi Mungu. Alisisitiza hakuna parokia inayoweza kusimama bila Wanawake. Leo tukitazama nyuma, tunaweza kuhesabu na kuandika mafanikio mengi na makubwa yaliyozaa matunda hasa kwa kufanyia kazi maazimio yenye lengo la kutafuta amani, ulinzi na utunzaji bora wa mazingira yetu, kuboresha maisha ya wanawake na watoto, majadiliano ya kidini na kiekumene, ulinzi wa mtoto, Shule ya Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na kazi za WWO za utafiti dhidi ya kilio cha moyoni cha mwanamke wa Kiafrika ambazo zinaendelea kwa mafanikio makubwa.
Mtakubaliana nami kuwa juhudi kubwa sana zimekwisha kufanyika lakini bado yapo mengi ya kuendelea kufanya na kuwa kikao hiku ni mwanzo mpya wa kufanya kwa juhudi zaidi kuwaalika wanawake wote wa kushiriki Utume wa WAWATA na WUCWO. Katika kipindi hiki cha Sinodi, Wanawake wote wa WUCWO wanashiriki katika kutafuta kanisa linaloishi ambalo Mungu alikusudia kwa watoto wake – familia ya Mungu. Huu ni uzoefu wa maisha ya ushiriki, kuheshimiana, kusikilizana na kushirikiana. Katibu msaidizi atatushirikisha namna ambavyo Wanawake ulimwenguni wameshiriki kujadili ripoti ya awali ya mababa wa Sinodi (Synthesis report) na namna ambavyo nasi tunaweza kuendelea kushiriki katika safari hii. Tutambue kwamba, pamoja na yote haya, jambo la kwanza na la muhimu zaidi ni wajibu wetu wa malei ya familia kwa kutoa elimu kwa watoto wetu katika ngazi zote kwani wao ni kanisa la leo na kesho na ndio jamii yenyewe. Leo, wanawake lazima tutembee pamoja, tuwaze/kunia mamoja, kusali pamoja kama watendaji wa neno ili kuweza kufanikiwa. Mababa wa Kanisa wanatuhimiza kutekeleza wajibu wetu msingi wa malezi ya familia, kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia tusipuuzie wito huu na sauti hii.
"Kupitia Sakramenti, hasa ya Ubatizo, Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa, Je, sisi si dada na ndugu katika Kristo, tumeungana katika ushirika ambao bado haujakamilika lakini hata hivyo ni halisi? Je, si Kristo anayetuita na kutufungulia njia ya kwenda mbele pamoja naye kama wasafiri wenzetu, pamoja na wale wanaoishi pembezoni mwa jamii zetu? Katika safari hii, katika mazungumzo ambayo yanapatanisha, tunataka kukumbuka kwamba tunahitaji kila mmoja, sio ili tuweze kuwa na nguvu pamoja lakini kama mchango wa amani katika familia ya binadamu. Tuendelee kumshukuru Mungu na kuombea kuongezeka kwa ushirika, tuweze kukabiliana na kasi ya matabaka inayokithiri na ambazo zinavunja familia ya binadamu na kilio cha dunia. Kwa kukutana na kusikilizana, tutembee pamoja kama watu wa Mungu." Kwa kuwa tutafanya uchaguzi katika mkutano huu, naomba tujikumbushe leo zamani: Mkutano wetu wa uchaguzi 2020 ulifunguliwa kwa Misa takatifu iliyoadhimishwa na Askofu Deusiderius Rwoma – Askofu Mwenyekiti, Idara ya Utume wa Walei Katoliki Tanzania na Askofu wa Jimbo la Bukoba. Ilikuwa ni sikukuu ya Yohana Mbatizaji ambae aliuwawa kikatili na Herode kufuatia ombi la binti yake alieshawishiwa na mamae kuomba kichwa cha Yohana Mbatizaji baada ya kucheza vizuri mbele ya Babae alieahidi kumzawadia chochote atakachoomba. Mama huyo kwa jina la Herodia hakuwa mke wa ndoa, Herode alimnyang’anya mdogo wake. Kutokana na dhuluma hiyo na utovu wa maadili Yohani mbatizaji alimkanya Herode kuwa alichofanya si haki na si maadili mema katika jamii. Ndipo Herode kwa ukatili wake akamweka gerezani. Somo la kwanza – Yeremia 1:17-19, Zaburi 71:1-6,15,17 na Injili: Marko 6:17-29.
Sehemu ya Mahubiri: Yohane Mbatizaji anatupatia tafsiri sahihi ya upendo. Yohane Mbatizaji anatumikia na Kuwajibika kwa upendo wa Kristo na zawadi yake ni Kifo. Tuombe Mungu tukijua kuwa kwa kusema ukweli tunatafuta uadui na dunia na mateso yaweza kuwa mengi, lakini thawabu ya kusema ukweli na kutumikia kwa Haki ni kufufuka Pamoja na Kristo na ndivyo alivyofanya Yohane Mbatizaji. ‘Changamoto kubwa ya uongozi katika Utume wa waamini walei ni ushirikina. Ushirikina ni hofu ya kupoteza usalama.’ Pd Leornad Maliva. Kiongozi aogope kutenda uovu ili kupata sifa za watu. Wakati huu wa uchaguzi watu wengine wanarubuniwa kupokea fedha kupindisha haki. Herode anajua lililo ovu lakini kwa nia ya kuwafurahisha watu anamuangamiza Yohane Mbatizaji. Viongozi tunaaswa kuwa watetezi wa haki. Katika uchaguzi tunaoelekea kufanya basi tusimamie haki na ukweli. Tuwafundishe na kuwaelekeza Watoto wetu na Kanisa kusimamia haki na ukweli huku wakiwa wanyenyekevu kwani ni katika upole na unyenyekevu ndivyo mtu anavyobarikiwa/anavyopokea hata kama watu wote wataona tunapotea.
Nimeendelea kuona maneno haya yakiishi na hata sasa yanatuhusu. Mungu wetu atuwezeshe kuyaishi. Utumishi ni zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu, mtu yeyote asije akajisifu. ‘God choses people and qualify them’, ‘Mungu huchagua watu na kuwawezesha.” Mama Bikira Maria aliitika kwa unyenyekevu …’ Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana, nitendewe ulivyonena’ Luka 1:38. Maandiko Mtakatifu yanamtaja Abrahamu kuwa ni mfano bora wa imani katika Agano la Kale. Lakini imani ya Bikira Maria kwa Mungu kilikuwa ni kielelezo cha haki, kwa sababu alimpenda Mungu na kujisadaka kwa furaha bila hata ya kujibakiza! Akawa amemchukua Mtoto Yesu moyoni mwake, hata kabla ya kutungwa kwake mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Bikira Maria alisema “Fiat” badala ya neno “Amina” yaani “na iwe hivyo”. Ikumbukwe kwamba, “Fiat” ni jibu lililokuwa linatumika katika maadhimisho ya Liturujia. “Fiat” yaani “Ndiyo”. Ndiyo ya Bikira Maria inaonesha imani na utii kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu, katika hija ya maisha yake hapa ulimwenguni. Huu ni mwaliko pia kwa sisi viongozi kufufuka na kuiga imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Bikira Maria. Tumkimbilie Mama Bikira Maria mwaminifu “Virgo fidelis” ili aweze kutuombea imani, matumaini na mapendo katika safari yetu ya kumtangaza Krsito mfufuka kupitia uongozi wa WAWATA! Maisha yetu yawe injili kwa wengine.
Tulianza uongozi wetu Agosti 2020 tukiwa bado kwenye janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Hata hivyo kwa pamoja tuliweza kutekeleza mengi pamoja na yafuatayo: Uzinduzi wa Jubilei Julai 11, 2021. Tulipata semina ya uongozi ndani ya kanisa – WHO DO YOU HAVE IN YOUR CYCLES??, Pd Almacheus Rwejuna. Tumeendelea kuwainua WAWATA chipukizi na nipongeze Jimbo kuu la DSM kwa hatua kubwa kiasi cha Askofu mkuu kuagiza Maparoko na viongozi wa Hamlashauri ya walei kuhakikisha kila Parokia ina WAWATA chipukizi. Tulipanda miti ya kutosha +500K kama moja ya malengo ya kilele cha Jubilei. Naomba tuwe waaminifu kuisimamia. Tulizindua Jubilei na kuhitimisha Majimboni – Makofi ya kutosha kwenu. Tulifanya Kilele cha Jubilei kwa kishindo Septemba 11, 2022 mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Tuna kitabu cha historia ya Umoja wetu – WAWATA, naomba tukinunue na tukisome. Tulishiriki utafiti kwa njia ya DODOSO kuhusu changamoto na unyanyasaji kupitia project ya WWO (World Women Observatory) – “Make the invisible woman Visible.” Yapo ambayo hatukuweza kufanikisha kwa kiwango cha kuridhisha hapa naweka machache na ombi kwa uongozi utakaochaguliwa kuendelea kuyafanyia kazi: Unjilishaji wa kina kuwafikia wanawake wote – hasa wa vijijini. Ushirikiano na UWAKA, tulipewa huu wajibu tulipochaguliwa 2020 na wakati wa uzinduzi wa Jubilei Julai 2021 kama moja ya wajibu Msingi. Hatujaweza kuwaibua chipukizi vya kutosha – kuna baadhi ya majimbo hawana chipukizi hata mmoja, ama wapo wanaosinzia. Marejesho ya WASMEP kufikia 31/08/2022 na – Michango ya Jubilei ya miaka 50 kufikia 31/08/2022. Inasikitisha kuona mpaka sasa kuna majimbo hayajachangia hata senti moja.
Naomba sana majimbo yanayodaiwa yalipe. Kufufua kitega uchumi cha Ilala. Kufungua benki /Microfinance ya WAWATA. Tunahitaji kujitoa/kujisadaka zaidi ili tutoke tulipo. Tuondoke kwenye makao makuu ya majimbo “Cathedrali” Jimboni na Makanisa ya Parokia twende walipo WAWATA kwenye vigango na parokia za pembezoni. Twende kule ambako hawawezi hata kutuchangia nauli ya shilingi 1000 ya kupanda basi. Huko ndiko wanakotuhitaji zaidi. Upendo / Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji. Tukunjue mikono yetu kwa ajili ya wanyonge: Kila mmoja wetu – Tenga muda wa Familia yako na baadae jamii. Omba Mungu akusaidie kuwa chombo cha amani – omba fadhila ya msamaha – jisamehe wewe binafsi na wasamehe wengine. Toa elimu kwa Watoto wako / wajukuu kuhusu uhai/mazingira. Watoto wetu wa shule za msingi wanatumia vidhibiti mimba, dawa za dharura za kuzuia mimba katika umri mdogo. Tutasikia leo mchana madhara ya madawa haya. Pata nafasi kuwatembelea waliosukumizwa pembezoni – tunao wengi kwenye malango yetu na ukiweza kwenda na watoto wajukuu hii ni Katekesi tosha. Shiriki na hamasisha wengine kushiriki mchakato wa Sinodi. Kama kauli mbiu ya mkutano mkuu wa WUCWO na kipaumbele cha miaka minne ijayo, tupokee wito tuliopewa na kwa furaha tukatende – UPATANISHO na kujenga amani ndio kiwe kipaumbele chetu. Mwisho, lakini sio kwa umuhimu na kwa namna ya pekee sana, nipende kuishukuru kamati tendaji ya WAWATA Taifa ushirikiano wao katika kutekeleza vipaumbele tulivyojiwekea kwa kipindi cha 2020-2023/ 2023/24, Mungu awabariki sana kwa sadaka zenu na sala zenu. Napenda pia kuwashukuru kwa moyo wa dhati watumishi wote wa ofisi kwa utendaji wao, nawashukuru ninyi nyote viongozi wa majimbo na Baba zangu Wakurugenzi na mwisho niwashukuru Watanzania wote kwa sala na matashi mema. Namwomba Mama yetu Bikira Maria, Malkia wa WAWATA aendelee kuambatana nasi katika utume wetu. Nautakia umoja wetu na wanachama wote wa WAWATA maisha marefu. Mungu ibariki WAWATA, Mungu wabariki Wanawake wote Wakatoliki Tanzania.