2024.06.01 Mkutano wa Mpango wa Watawa huko Afrika miongoni akiwemo Dk.Ruffini Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. 2024.06.01 Mkutano wa Mpango wa Watawa huko Afrika miongoni akiwemo Dk.Ruffini Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. 

Mpango wa Masista Wakatoliki:Ushirikiano katika huduma ya manufaa ya wote

Masista wa Kikatoliki kutoka zaidi ya nchi 15 walikusanyikanchini Zambia na Mfuko wa Conrad N.Hilton.Walijikita na maono ya pamoja,kujifunzana ushirikiano katika huduma ya manufaa ya wote.Miongoni mwa washiriki ni pamoja na Dk Ruffini,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano,Sr.Becquart,Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Sinodi, Sr.Smerilli,Katibu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani.

Na Sr. Michelle Njeri – Lusaka na Angella Rwezaula – Vatican.

Zaidi ya watawa  100 kutoka nchi zaidi ya 15 walikusanyika jijini Lusaka, nchini Zambia, kuanzia tarehe 29 hadi 31 Mei  2024, kwa ajili ya Mkutano uliandaliwa na Mfuko wa Conrad N. Hilton  wa Mpango kwa ajili ya Watawa.  Lengo la tukio hilo lilikuwa kutoa fursa za kuimarisha uelewa na utendaji wa sinodi na kubadilishana mawazo ili kuendeleza maono ya pamoja ya kujifunza kwa pamoja juu ya  athari za kimkakati na ukuaji, na kuendelea kushirikiana kwa manufaa ya wote. Sr. Jane Wakahiu, Makamu wa Rais Mshiriki wa Operesheni za Programu na Mkuu wa Mpango wa Masista wa Kikatoliki katika Mfuko wa Conrad N. Hilton katika mkusanyiko huo alisema kuwa “Kuwa  pamoja ni fursa ya kuruhusu nafasi kwa miunganisho mipya kufanywa na ile iliyopo kuongezwa kwa kina, tunapotamani kuimarisha ubora na uendelevu wa juhudi zetu za pamoja.”

Mada za kuinua sauti za watu duni zilisikika

Wakati wa Mkutano huo  walijadili mada zilizojumuisha kuinua sauti za watu wanaoishi katika hali duni, kukumbatia mbinu zenye ushuhuda ili kukuza jumuiya za kitawa zinazostawi, na kubadilisha desturi zilizokita mizizi ili kutumikia manufaa ya wote. Kiini kikuu hasa kilichounganisha mada kilikuwa sinodi. Kwa njia hiyo watawa kama wahusika wakuu wa mawasiliano katika Kanisa.  Wakati wa kuzungumzia juu ya  sinodi, wawakilishi kutoka Vatican walishiriki katika mazungumzo kuhusu utume na wajibu wa kichungaji wa Mabaraza yao, ikiwa ni pamoja na mchakato wa kujihusisha na Makanisa mahalia. Jopo hilo liliongozwa na Sr. Mumbi Kigutha, Rais wa Marafiki katika Mshikamano, ambaye alijikita kueleza himizo la Baba Mtakatifu Francisko kuwatia moyo wa kusikiliza, kushirikiana na umoja.

Dk.Ruffini:Masisita lazima wawe wahusika wakuu wa mawasiliano katika Kanisa

Katika mkutano huo pia alishiriki Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano Dk. Paulo Ruffini ambaye akitoa maoni yake alisisitizia umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja ili kutoa muonekano wa kazi za masista wakatoliki duniani. Kwa upande wake alisema “Masista wawasilianaji wanapaswa kuwa wahusika wakuu wa mawasiliano katika Kanisa kwa kutoa mtazamo wa Kikristo.” Na  aliongeza kuwa wanapaswa kuwa wazi katika kusimulia historia kwa njia ya ukombozi, kuunda njia mpya ya mawasiliano ambayo inazingatia uzuri wa jamii. Mkuu huyo alisisitiza haja ya mawasiliano kutiririka kutoka viunga vya Vatican kwakuwa Baraza la Mawasiliano liko kwenye huduma ya Kanisa mahalia. “Ni juu ya ushirikiano na mitandao kwa manufaa ya wote katika roho ya sinodi”.

Mpango wa Pentekoste wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano

Dk. Ruffini vile vile alijikita kuelezea juu ya “Mpango wa Pentecoste” ambao ni wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anaoungwa mkono na Mfuko wa C. Hilton kama mfano! Alisema kuwa “mpango huo unatoa fursa kwa masisita kuanzia na  kozi za malezi mtandaoni na mifumo ya mtandao ili kuboresha ujuzi wa masista katika mawasiliano hadi mafunzo ya ana kwa ana katika vyombo vya habari za Radio  Vatican,” ambayo alisema “inaweza kuleta fursa mpya za ushirikiano. Na hivi sasa tayari kumekuwepo na masista 13 kutoka nchi 12 walio katika mafunzo ya kazi katika  Radio (Vatican News - Radio Vatican), na kwa sasa kundi la masista wa Kikatoliki la 2024 wanahudhuria mikutano 12 ya kila Juma kwa njia ya  Zoom kuanzia mwezi Aprili hadi Juni, kwa lengo la kupokea malezi ya hali ya juu, na mabadilishano  ya pamoja,” alifafanua Mkuu wa Mawasiliano Vatican.

Sr Nortes: Haja ya kusikiliza na kushirikiana

Akijadili kuhusu Sinodi, Sr. Carmen Ros Nortes, Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirikia ya Kitawa na Vyama vya Kitume, alijikita juu ya dhamira ya Kanisa katika maisha ya kuwekwa wakfu. Kwa mujibu wake alibainisha kwamba “Baraza la Kipapa linaweza kuonekana kama maabara ambapo mahusiano yamefumwa kati ya karama na huduma mbalimbali, na uzuri wa Kanisa unaweza kuoneshwa,” alisema.

Sr Becquart Masista wanajukumu la kutekeleza mchakato wa Sinodi

Na wakati huo huo Sr. Nathalie Becquart, Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Sinodi, alisisitiza haja ya kusikiliza na kufanya kazi kwa pamoja, kuthamini watu na mchango wao kwa manufaa ya wote. “ Masisita wana jukumu muhimu sana la kutekeleza katika mchakato wa sinodi, kwa sababu wamehusika tangu mwanzo, na wanahitaji kuwasaidia watu wa Mungu kukumbatia mtindo wa sinodi, ambao ni mtindo wa Yesu," alisema.

Sr Smerilli akizungumza katika mkutano wa Masisita huko Lusaka Zambia
Sr Smerilli akizungumza katika mkutano wa Masisita huko Lusaka Zambia

Kulikuwa na mada pia ua Uhamiaji ambayo ililetwa na Sr. Alessandra Smerilli, Katibu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendelefo Fungamani ya Binadamu, na  ambaye alisema kuwa “ moja ya majukumu ya Baraza  ni kusaidia Makanisa mahalia kuondoa vikwazo ambavyo vinatoa ardhi yenye rutuba ya uhamiaji. Uhamaji wa kulazimishwa ni changamoto tunayoifanyia kazi pamoja na maaskofu na Makanisa mahalia; tunatoa wito kwa maaskofu kushirikiana na serikali zao kushughulikia suala hili.” Aidha Sr. Smerilli pia alisisitiza kwamba, bila kujali safari yao, wahamiaji bado ni wa Kanisa moja na wanapaswa kusaidiwa popote walipo, na Makanisa mahalia yawasindikize kwa uangalizi mzuri wa kichungaji. Aidha alikumbuka juu ya mada ya mwaka huu 2024 wa Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani isemayo: “Mungu anatembea na watu wake” na akasisitiza kwamba “kila mtu ameitwa kutambua uso wa Mungu kwa wale wanaolazimika kuhama.”

Mkutano wa Masista huko Lusaka, Zambia uliofadhiliwa na Mfuko wa C.Hilton
04 June 2024, 15:58