Padre Francis Bartolon, C.PP.S: Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo makini cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni zawadi; na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha ushirika, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa kujikita katika utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao!
Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo! Kumbe, Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu ya Upadre ni chanda na pete na kwamba, Ekaristi Takatifu ni kifungo cha upendo. Padre ni Mhudumu wa Ekaristi Takatifu na ni shuhuda wa Agano Jipya na la Milele. Ni Sadaka ya Kristo Yesu inayotolewa juu ya Altare, kielelezo cha Agano Jipya na la milele. Hii ni sadaka ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! Mwenyezi Mungu anawaita watu katika miito mbalimbali ndani ya Kanisa na kumwamini na kwamba, imani ni msingi wa kila wito ndani ya Kanisa, changamoto ni kwa kila mwamini kujiaminisha mbele ya Mungu kwa kusema, “Ndiyo” ili kutekeleza kwa imani, matumaini na mapendo mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Ekaristi Takatifu inajenga na kudumisha umoja, ushirika, mshikamano na ujirani mwema. Kila siku Mapadre wanaitwa na kuhimizwa kupyaisha ile “Ndiyo” yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Ni katika muktadha huu, Padre Francis Bartolon, C.PP.S. katika mkesha wa Sherehe ya Ekaristi Takatifu “Corpus Domini” tarehe Mosi Juni 2024 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 30 Machi 1974, huko kwenye Kanisa la Abasia ya Mtakatifu Felice, “Giano dell’Umbria” iliyojengwa kunako Karne ya XII. Hapa ni mahali alipozaliwa yaani tarehe 13 Oktoba 1948 na kukulia Padre Francis Bartolon, C.PP.S. Hapa ni mahali ambapo Mtakatifu Gaspari del Bufalo kunako tarehe 15 Agosti 1815 alianzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Padre Francis Bartolon, C.PP.S., akiwa Padre kijana kabisa, baada ya kuhudumia Parokia ya “St. Roch” huko Toronto, Canada tarehe 17 Januari 1975 alifika nchini Tanzania. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa ni Paroko, Mkuu wa Wamisionari wa Damu ya Yesu Vikarieti ya Tanzania, Mkurugenzi wa Miito, Mhazini na Makamu na Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Ulimwenguni na hatimaye, Meneja wa Miradi ya C.PP.S., Water Projects katika kipindi chote cha miaka 38 ya maisha na utume wake kama Padre na mmisionari. Hiki kimekuwa ni kipindi cha uaminifu kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Amejifunza kutumikia na kulipenda Kanisa la Kristo Yesu.
Padre Francis Bartolon, C.PP.S., katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, anamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amemwita kwa: imani, huruma na mapendo yake makuu, kiasi cha kujiaminisha kwake. Miaka 50 ni kielelezo cha uaminifu wa Mungu katika maisha na utume wake. Uaminifu huu umejibiwa kwa imani, upendo na uwepo wa karibu wa Mungu katika maisha yake. Tangu alipowasili nchini Tanzania kunako mwaka 1975 ameonja upendo, urafiki na ujirani mwema na watu wa Mungu nchini Tanzania. Amejitahidi kuwashirikisha maisha na utume wake katika medani mbalimbali za maisha nchini Tanzania. Alikuwa ni muasisi wa malezi na majiundo ya Wamisionari wa Damu Azizi kutoka Tanzania. Kazi hii ilikuwa na changamoto zake, lakini kwa msaada wa Mungu na nguvu za Roho Mtakatifu aliweza kuitekeleza kwa uaminifu mkubwa na leo anakumbukwa na wengi kutokana na malezi na majiundo ya wale wote waliopitia mikononi mwake. Alithamini na kuendeleza vipaji vya Majandokasisi na kwamba, watu wengi wanamheshimu kutokana na mchango wake katika maisha ya vijana wengi.
Padre Francis Bartolon, C.PP.S., anasema, Mungu anapokuamini, jitahidi kujiaminisha kwake na utende kazi yako kwa juhudu na maarifa. Mapadre watambue kwa Kanisa linawahitaji, kumbe wanapaswa kuwa tayari kujituma bila ya kujibakiza kwa ajili ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Tanzania na la Ulimwengu katika ujumla wake. Padre Walter Milandu, C.PP.S., kwa ufupi anasema, Padre Francis Bartolon anakumbukwa na wengi kwa sadaka na majitoleo yake katika malezi, makuzi na majiundo ya Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu tangu: Nyumba ya malezi ya Itigi, Singida; Nyumba ya Malezi ya Yohane Merlin, Jimbo kuu la Dodoma, Chuo cha Mtakatifu Gaspari del Bufalo, Jimbo Katoliki la Morogoro. Alijitahidi kuwasaidia, kuwaongoza na kuwaelekeza Majandokasisi katika maisha na huduma kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Kwa hakika Padre Francis Bartolon, C.PP.S., ni mtu wa watu na kwamba, anaendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Tanzania na Shirika katika ujumla wake. Kwa upande wake Baraka Franco Chibiliti, Mwamini mlei aliyebatizwa na Padre Francisko akiwa na miezi minne, anamkumbukwa kwa huduma na utume wa hasa alipokuwa Itigi, Mayoni, Singida pamoja na Dodoma: Upendo na ukarimu wake kwa watanzania; malezi, majiundo na makuzi makini kwa watanzania ni kati ya mambo ambayo kamwe hayataweza kufutika katika sakafu ya moyo wake.
Kwa upande wake Mheshimiwa Padre Benedetto Labate, C.PP.S., Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia aliyechaguliwa hivi karibuni, amempongeza Padre Francis Bartolon, C.PP.S. kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre sanjari na Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Corpus Christi: Kwani Padre ni Mhudumu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, Ni Mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Padre ni Mhudumu wa haki, amani na upatanisho. Miaka 38 ya maisha na utume wa Kipadre nchini Tanzania "Si haba kama kiatu cha raba." Daima katika maisha na utume wake, amejitahidi kudumisha kifungo cha upendo na mshikamano: "Vinculum Caritatis, Bond of love; Kifungo cha upendo." Hii ni changamoto ya kuendelea kupyaisha kila siku ile "Ndiyo" ya maisha na utume wa Kipadre, ili kuendelea kuwa waaminifu, daima kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na kuendelea kumpenda Kristo Yesu na Kanisa lake.