Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu.   (ANSA)

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Shule ya Imani, Upendo, Matumaini na Ukarimu

Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo makini cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya imani

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Mpendwa msikilizaji na msomaji, Leo Mama Kanisa anasherehekea sikukuu nyingine kubwa ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Sadaka ya Mkate na Divai inayotolewa katika Misa Takatifu inageuzwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kuwa Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kweli Rangi haibadiliki, saizi haibadiliki, harufu haibadiliki ila si Mkate wala Divai tena bali ni Mwili na Damu ya Kristo Mwenyewe.  Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo makini cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni zawadi, na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani, kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa maskini ndani ya jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Naomba nitoe mfano wa nyaya za umeme. Nyaya zinazo pitisha umeme hazibadiliki rangi wala saizi, ila zimebeba nguvu kubwa sana ya umeme na bahati nzuri saivi tupo katika digital vitu vingi vinafanyika bila kutumia nguvu kubwa. Ndivyo ilivyo katika Sakramenti ya Ekaristi.  Mtakatifu Thomas wa Akwino alisema yamefichika machoni ila imani huyaona. Machoni unaweza ukaona ni Mkate au Divai, ila maumbo haya yamebeba siri kubwa, yaani kristo mwenyewe. Tutafakari Pamoja wazo hili Ekarist takatifu ishara wazi ya uwepo wa Kristo Yesu kati yetu wakati wote!

Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani, matumaini na mapendo
Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani, matumaini na mapendo

UFAFANUZI : Katika Injili tukianza na Taalimungu, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unasema “Ekaristi takatifu ni kiini na kilele cha maisha ya mkristo” LG 11. Kwanini? Kwa sababu inatusaidia kushiriki katika sadaka ya Yesu sasa, na kufaidika na matunda yake katika maisha yetu. Inatusaidia kumwabudu Mungu baba, Mwana na Roho Mtakatifu katika njia sahihi zaidi. Inatuimarisha katika umoja na upendo wetu na Yesu na kati yetu katika kufanya sadaka pamoja ya Mwili na Damu kwa Baba. Inatukumbusha mateso ya Yesu, kifo na ufufuko na kutukumbusha kufanya sadaka ya upendo kwa wengine. Ekaristi takatifu ni fumbo la imani, matumaini yetu, na mapendo yetu. Tujiulize kwa nini kusheherekea Ekaristi sasa zaidi ya miaka 2024 imepita? Jibu tunafanya hivi kwa sababu Yesu ametuambia “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” Yesu amekamilisha Agano la kale kwa kuweka agano jipya. Yesu ameweka Ekaristi takatifu kukamilisha kile kilichofanywa katika agano la mlima Sinai. Amembadili Musa kama mteule kiunganishi cha Mungu na kuweka agano jipya lililotabiriwa na Nabii Yeremia 31:31-34, kwa kutumia damu yake badala ya damu ya wanyama. Katika sakaramenti kula na kunywa mwili na damu ya Yesu sisi tunaunganishwa na Mungu zaidi. Hivyo Yesu alitengeneza kizazi aminifu kinachoungana na Mungu zaidi kwa njia ya damu ya sakaramenti. Yesu ameweka Sakaramenti ya Ekaristi takatifu katika karamu ya mwisho kama mlo wa kisakramenti na kisadaka. Kama sakramenti Ekaristi ni alama ya nje katika huo tunakutana na Yesu ambaye anatushirikisha maisha yake ya neema. Katika sakaramenti takatifu ya ekaristi mwili na damu ya Yesu, pamoja na Roho na Umungu wa Yesu Kristo na hivyo Yesu mzima yupo. KKK 1374.

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Katika Sakaramenti ya Ekaristi tunakutana na Yesu mfufuka ambaye anakuja kwetu katika maumbo ya mkate na divai ambaye anatuimarisha katika safari yetu ya maisha. Katika mlo wa Ekaristi ni fumbo kubwa kwasababu katika maadhimisho hayo maumbo ya mkate na divai yanageuzwa kuwa Mwili na Damu ya Yesu mfufuka wakati mwonekano na ladha yake vinabaki vilevile. Ekaristi ni Sakramenti ya sisi kuungana na Yesu. Katika sakramenti hii Yesu anatupa sisi mwili wake uliotolewa pale msalabani na damu yake azizi iliyomwagika kwa ajili yetu ili dhambi zetu zisamehewe. Sisi tunahitajika kupokea ujumbe huu wa umoja na sadaka ya mapendo. Ekaristi takatifu inatufundisha umuhimu wa jumuia tunayounganishwa na sadaka hii. Baba wa Kanisa Yohane Chrisotom alisema, “Mkate hasa ni nini? Mwili wa Yesu, Wale wanaopokea wanakuwaje? Mwili wa Yesu, kama vile mkate unavyotokana na muunganiko wa punje za ngano, ambapo hata huwezi kuzitofautisha tena kwa sababu ngano hizi zimeungana, hivyo tumeungana na Yesu. Kama ilivyo punje nyingi za ngano zilivyounganisha kutengeneza mkate, na zabibu nyingi zimetengeneza divai hivyo nasi tunakuwa tumeungana katika sadaka hii. Yesu Kristo alichagua kutumia maumbo haya ili kutuonyesha kwamba tunatakiwa kila wakati kutafuta kuungana, kumruhusu Roho mtakatifu atubadilishe kuelekea kwa Yesu na kufanya kazi naye, Kristo akiwa yeye ni kichwa na sisi ni mwili wake. Pamoja ni wamoja kinachotuunganisha ni utayari wetu kutolea muda wetu, vipaji vyetu kwa Mungu katika wanajumuia wenzetu. Hivyo Ekaristi takatifu iimarishe umoja na upendo.

Maandamano ya Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wa imani kwa Yesu wa Ekaristi
Maandamano ya Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wa imani kwa Yesu wa Ekaristi

Ekaristi takatifu ni ishara ya agano na sisi ndio wadau wenyewe wa Agano hivyo, tunahitajika kujiandaa vizuri kupokea Ekaristi takatifu. Hivyo kunahitaji la kufanya toba kabla ya kupokea ekaristi takatifu. Tukumbuke onyo alilolitoa Mtume Paulo 1Kor 12:27 na ile Sala ya Ekaristi yanayosema anayekula mwili na damu ya Yesu pasipo kustahili anakula hukumu yake mwenyewe. Tupokee ekaristi takatifu kwa mapendo makuu na unyenyekevu, na sio kutimiza ratiba tu na hapo Ekaristi takatifui ishara ya agano italeta umaana kwetu na kutufaidia sisi. Kama washiriki katika Agano kwa kupokea ekaristi takatifu tunambeba Yesu kma Bikira Maria na hivyo tunapewa jukumu la kumtangaza Yesu kwa wengine katika majumba yetu, vyumbani mwetu na mwa wenzetu, sehemu za kazi kwa kuonyesha upendo, huruma, msamaha, utii na kujisadaka na hapo tutatimiza hili kuwa Ekaristi takatifu ni ishara ya agano Tunaposheherekea sherehe hii kubwa ya imani yetu, tuabudu kile Mtakatifu Thomas wa Akwino hakusita kukiita “Muujiza mkuu ambao Yesu hakuwahi kuufanya duniani.” Ekaristi takatifu ni ishara ya agano kwa kutaka hilo liwe endelevu Yesu akatuamuru kwa kusema “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” agizo hili hakuwapa mitume na waandamizi wao tu kama waadhimishaji wa ekaristi takatifu, bali hata sisi washiriki katika mlo huo tutoe heshima kwa ekaristi takatifu kama yeye mwenyewe katika mlo ule na wafuasi wake walivyoshiriki ule mlo kwa heshima, anatutaka tushiriki kwa upendo na amani, anatutaka kila mmoja wetu awe mshiriki katika mlo huu, anatutaka tujistahilishe kuingia katika mlo, kujiandaa na kuandaana kuingia katika mlo, tuuheshimu mlo huo.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano

Leo tunapofanya sherehe ya Fumbo la Mwili na Damu Azizi ya Yesu, tukumbuke kuwa katika mkate na divai vinageuzwa kuwa mwili na damu ya Yesu kweli hata kama maumbo na ladha hubaki ileile, hivyo tunatakiwa tuiheshimu ekaristi takatifu na tukifanya hivyo tunatimiza hili agizo la Yesu “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Kwetu waamini suala la kuja kupokea Ekaristi takatifu si suala la hiari ni la lazima kadiri tulivyosikia katika injili ya leo, hivyo sisi ambao hatushiriki kwa sababu ya vikwazo tunafanya mgomo, tunamgomea Yesu kama alivyotuagiza “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” Leo tunapoadhimisha hii sherehe ya mwili na Damu ya Yesu, tukumbuke Maneno ya Mtume Paulo 1Kor 12:27 na ile Sala ya Ekaristi yanayosema anayekula mwili na damu ya Yesu pasipo kustahili anakula hukumu yake mwenyewe na anajiweka yeye mwenyewe nje ya Agano. Wazazi tukijua wazi Ekaristi takatifu ni ishara ya agano, Kanisa mahalia liweka utaratibu wa watoto kati ya miaka 7-10 au wa darasa la 3 waandaliwe ili kupokea komunio ya kwanza, ambapo tumepewa agizo “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”. Tunawajibike sawasawa kuwaandaa watoto wenu kupokea komunio ya kwanza. Tunawasisitiza wahudhurie mafundisho wakati wa mafundisho na sio kuwapeleka kwenye masomo ya ziada. Leo tunapofanya sherehe hii ya Mwili na Damu ya Yesu ambapo tunakumbushwa kuwa Ekaristi takatifu ni ishara ya agano na pia tunatimiza lile agizo la Yesu, “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” tutafakari kila mmoja wetu kiwango chake cha kuiheshimu ekaristi takatifu kipo asilimia ngapi, kila mmoja aweke malengo ya kuheshimu ekaristi takatifu kwa asilimia miamoja. Wahudumu wa Ekaristi takatifu tuhudumie kwa umakini, ibada na uchaji na sio kutimiza wajibu tu. Historia inaonesha wengi walioidharau ekaristi takatifu wamepata madhara. Pia tukumbuke hakuna tatizo linalompata binadamu likashindwa kutatuliwa mbele ya Ekaristi takatifu ukisali kwa imani na uthabiti. EkaristiTakatifu ni urithi wetu Ekaristi Takatifu lishe yetu isiyoisha kamwe.

Ekaristi Takatifu

 

01 June 2024, 08:37