Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 aliitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 aliitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre.  (Vatican Media)

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Chemchemi: Huruma, Upendo na Matumaini

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 aliitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ibada ya Moyo Mtakatifu ni chemchemi ya neema!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican leo Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, sanjari na Siku ya kuombea: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha ya Mapadre. Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kuandika Waraka wa Kitume kuhusu Moyo Mtakatifu wa Yesu, unaotarajiwa kutolewa Mwezi Septemba 2024. Huu ni waraka unaochota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu; Tafakari za Mababa wa Kanisa kuhusu Upendo wa Kristo Yesu, ili kulipyaisha Kanisa na ujumbe mahususi kwa walimwengu, kwani ulimwengu mamboleo unaonekana kukosa moyo! Itakumbukwa kwamba, Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya: imani, upendo, huruma, msamaha, uvumilivu, uaminifu na unyenyekevu wa Mungu, aliyejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta maisha na uzima wa milele!

Moyo Mtakatifu wa Yesu
Moyo Mtakatifu wa Yesu

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 aliitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu. Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Utakatifu wa Mapadre ni hitaji muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ukweli huu wa imani katika maisha na utume wa Mama Kanisa, unagusa hata maisha ya waamini walei ambao usiku na mchana wanatafuta utakatifu wao, kwa kutambua au kwa kutokujua kutoka kwa mtu wa Mungu. Waamini wanamwona Padre kuwa ni mshauri wa maisha ya kiroho, mpatanishi wa amani; mtu mwenye hekima na busara. Ni kiongozi salama ambaye watu wa Mungu wanaweza kujiaminisha kwake nyakati ngumu na wakati wa majaribu ya maisha, ili kuonja na hatimaye, kupata faraja na usalama wao! Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre kuendelea kukesha kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Upatanisho mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha wongofu wa shughuli za kichungaji. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu ni dalili kwamba, wito na utume huu mtakatifu, umehifadhiwa katika chombo cha udongo. Mapadre wanaopitia vipindi vigumu vya maisha na utume wao, wanapaswa kusindikizwa kwa huruma na upole; wasikilizwe kwa makini; wasaidiwe kufikia mang’amuzi na ukomavu katika maisha. Huu ni wajibu wa kwanza kwa Maaskofu mahalia, lakini hata kwa Jumuiya nzima ya waamini pamoja na familia zao, ambazo mara nyingi zinabeba Msalaba mzito! Wakleri ni watu ambao wanapaswa pia kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha na utume wao!

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Siku pia ya kuombea Utakatifu wa Mapadre
Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Siku pia ya kuombea Utakatifu wa Mapadre

UFAFANUZI: Moyo huonesha kiini cha jambo mfano ‘Moyo wa nchi’. Huweza pia kuashiria hali ya kujitahidi bila kukata tamaa mf. moyo wa kazi, majitoleo, uvumilivu nk. Kidini, ‘kuwa na moyo ni kuwa mtu laini, mwepesi, msikivu, muelewa, mtaratibu, mwenye huruma na ubinadamu. Manabii hutumia taswira ya ‘moyo wa nyama au wa jiwe’ kuonesha ugumu au usikivu wa watu. Moyo hudhihirisha furaha au huzuni, hasira au amani, kuridhika, kupenda na kuchukia. Moyo wa Yesu ni ufupisho wa ubinadamu wa Kristo, ulijengeka mwilini mwa Mama Bikira, ukadundadunda alipotembea Galilaya na Yerusalemu, ukapigapiga alipofundisha na kusimama alipokufa, ukashika kasi alipofufuka na sasa una ‘show love’ kwa wote wanaojizamisha humo ili kuogelea katika bahari ya huruma yake. Moyo wa Yesu huoneshwa ukivuja damu, umezungukwa na miiba, alama ya upendo na huruma... amani na upatanisho wetu, uzima na ufufuo wetu, naam, Moyo wa Yesu ni furaha ya watakatifu wote... tuuabudu, tuusifu na tuuombe Moyo huu wa Mwana pekee wa Mungu. Leo upendo na huruma ya Mungu vimefunuliwa. Mungu Baba alionesha tangu awali kabisa upendo huo kwa kulitendea taifa la Israeli kama Baba amtendeavyo mwanawe. Somo I (Hos 11:1b,3-4,8c-9) laeleza “lakini nalimfundisha Efraim kwenda kwa miguu, naliwachukua mikononi mwangu... nikaandika chakula mbele yao.” Mungu ndiye amfundishaye binadamu kwenda kwa miguu yaani kujitegemea katika fikra na maamuzi kuhusu maisha yake kwa akili, utashi na hekima... anatufundishaa kutembea katika njia ya haki na uadilifu, njia ya ukweli na matumaini. Humfundisha mwanadamu sheria, kanuni na amri ili azishike na kupata uzima. Ni pendo hilo ndilo lililopelekea Moyo wa Yesu ufunguliwe kwa mkuki juu ya Msalaba tulivyosimuliwa leo na Yohane 19:31-37, damu na maji vikabubujika nasi tukaona hazina zote zilizositirika humo, hazina za hekima na za elimu, tukajichotea neema na kuimarishwa (maji yale ni kielelezo cha uneemevu, usafi na utakaso katika ubatizo… na damu ya Mwanakondoo wa Agano Jipya imwagikayo, ishara safi ya Ekaristi Takatifu) naam, “basi kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu” (Isa 12:3-4).

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo
Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo

Vile alivyomfundisha Efraim kwenda kwa miguu, nasi tunapaswa kuitembea njia hiyo kwa uvumilivu hadi siku ile tukufu ya Bwana itakapofika. Safari yetu kiroho ni lazima iendelee kuelekea nyumbani na huko karamu imeandaliwa kwa ajili ya wote (Isa 25:6-9), tutakaribishwa vyumbani mle kwenye nuru isiyofifia... nitumia lugha ya kitabibu katika kunogesha tafakari yetu ni kwamba kimaumbile moyo una vyumba vinne vinavyopokea na kusukuma damu (auriko 2 na ventriko 2). Heri yao watakaoingia vyumba vya Moyo Mtakatifu sana wa Yesu, humo tabu haisumbui, mapendo yanabubujika kwa furaha isiyokwisha. Auriko ya kulia hupokea damu chafu toka mwilini, ni ishara ya Kristo anayetupokea na madhaifu yetu kutukusanya na kutuingiza ndani zaidi kwenye ventriko ya kulia halafu anafunga mlango tusirudi kwenye auriko ya kulia badala yake anatuongoza kwenye mapafu kuchuja hewa ya sumu na kujipatia Oxygen safi, ni ishara ya utakaso wa dhambi zetu kwa njia ya Sakramenti ya kitubio na msamaha wa Mungu, Baba Mtakatifu katyika kuutfakari upendo na huruma ya Moyo Mtakatifu wa Yesu  anasema Mungu hachoki kutusamehe bali sisi ndio tunachoka kutubu” Kutoka kwenye mapafu damu safi hurudi moyoni kupitia auriko ya kushoto, kwamba tumekuwa safi sharti tuingie chumba kingine kisafi kama hali yetu, tuna hali mpya, wasafi moyoni, rohoni na mwilini. Kisha damu huingia ventriko ya kushoto na hapo kwa nguvu kubwa husukumwa mwilini kupitia mishipa mikubwa. Ventriko ya kushoto ni msukumo wa kutoka nje na kuwapelekea wenzetu hali ya usafi tuliojipatia ndani ya vyumba vya Moyo Mt wa Yesu. Hatupaswi kukumbatia neema na baraka za Moyo wa Yesu peke yetu, ni lazima tuwashirikishe wenzetu tukiwapelekea habari njema, faraja, upatanisho na mapendo yetu. Mishipa ya damu, Aorta na dada zake, ni njia ya usafiri wa mambo yote mema, ni neema ya Mungu inayofanya njia pasipokuwa na njia ili tusafiri salama tunapotembea kwa miguu alivyotufundisha Mwenyewe kama alivyomfundisha Efraim.

Toba, Wongofu wa ndani na Utakatifu wa Mapadre
Toba, Wongofu wa ndani na Utakatifu wa Mapadre

Mbali na moyo msukumo wa damu hupungua, oxygen hupungua na taka za sumu huongezeka kutoka mwilini na nguvu ya kurudi moyoni huwa ndogo. Ni ishara ya dhambi na uchovu katika maisha, kukata tamaa na kuvunjika moyo. Katika hali hii, mazoezi ya viungo hufungua hata vimishipa vidogo kabisa na kuruhusu damu ifike mbali zaidi. Tunahitaji mazoezi ya kiroho kwa njia ya mifungo, retreat, semina, neno la Mungu, sala na kukomunika ili kupata nguvu mpya ya safari... tunapoumia damu huvuja nje ya mfumo wake, katika maisha inawezekana kutoka nje ya mfumo yaani kujitenga na mapendo ya Moyo wa Yesu, kujitenga na Kanisa na wenzetu, tutakufa kwa umasikini na njaa. Neema ya Mungu i ndani ya vyumba vinne vya Moyo wa Kristo, tupambane kubaki humo, tutoke twende wapi?Kwa ajili ya neema hii kubwa, tumshukuru Mungu tukitakiana heri na baraka za Moyo huu Mtakatifu sana tukisema na Mt. Paulo katika somo II (Efe 3:8-12, 14-19), “kwa hiyo nampigia magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani. Kristo akae moyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo...” ‘Usifiwe Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotuletea wokovu wetu, utukuzwe na uheshimiwe milele, Amina.’ 

Liturujia : Moyo Mtakatifu
07 June 2024, 15:05