Tafuta

Kila mwaka ifikia tarehe 3 Juni ni kumbukizi la Mashahidi wa Uganda.Mahujaji kutoka ndani na nje ya Nchi wanafika katika madhabahu ya Namugongo. Kila mwaka ifikia tarehe 3 Juni ni kumbukizi la Mashahidi wa Uganda.Mahujaji kutoka ndani na nje ya Nchi wanafika katika madhabahu ya Namugongo. 

Mashahidi wa Uganda:Takriban waamini milioni 4 walishiriki sherehe za Wafiadini wa Uganda

Jimbo la Nebbi liliongoza maadhimisho ya Siku ya Mashahidi wa Uganda ambapo Askofu Wokorach,anayemaliza muda wake Jimbo Nebbi kwa kuwa alichaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuula Gulu aliongoza Misa Takatifu na kuonya waamini kutoshawishiwa na aina yoyote ya ibada ya sanamu na matendo yasiyoendana na imani ya Kikristo na kukumbusha mashahidi walivyopendelea kuuawa,badala ya kukata tamaa.

Na Angella Rwezaula - Vatican

Katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashahidi wa Uganda, katika Madhabahu yaliyojengwa kwa ajili yao huko Namugongo, takriban kilomita ishirini kutoka mjini Kampala kwa mara nyingine  tarehe 3 Juni 2024, imeona bahari ya washiriki takribani waamini milioni 4. Maadhimisho ya mwaka 2024 yamekuwa  na umuhimu wa kipekee kwa sababu yamefanya kumbukumbu ya miaka 60 tangu Papa Paulo VI alipowatangaza kuwa watakatifu Wakatoliki 22 na Waanglikani 23 waliouawa kishahidi kati ya mwa 1885 na 1887 kwa amri ya Mfalme Mwanga II, katika ufalme wa Buganda wa wakati huo. Kwa mjia hiyo Mama Kanisa kila ifikapo tarehe 3 Juni  ya kila mwaka inafanya kumbukumbizi  ya kifo cha imani cha Mtakatifu Karoli  Lwanga na wenzake wakatoliki 22 waliouawa.

Wanahija kutoka Jimbo la Lira nchini Uganda wakitembea kwa mguu kuelekea Namugongo
Wanahija kutoka Jimbo la Lira nchini Uganda wakitembea kwa mguu kuelekea Namugongo

Sherehe za mwaka huu ziliongozwa na Jimbo Katoliki la Nebbi nchini Uganda ya kama utamaduni wa kila Jimbo kuandaa na kuongoza maadhimisho hayo. Hata hivyo mnamo tarehe 15 Mei 2024, ujumbe wa mahujaji wapatao 700 kutoka Nebbi walitembea kwa miguu kwenye mvua kwenda kuhiji Namugongo, iliyochukua umbali wa karibu kilomita 500 katika majuma mawili huku, wakivuka kanda ndogo mbili (Bunyoro na West Nile) na Wilaya tano (Pakwach, Kiryandongo, Nakasongola, Luwero na Kampala) kabla ya kufika Mahali Patakatifu Namugongo.

Eneo lililotengenezwa muhimu kwa ajili ya Misa ya Kila Mwaka
Eneo lililotengenezwa muhimu kwa ajili ya Misa ya Kila Mwaka

Kwa njia hiyo katika Siku kuu hii kubwa, Maadhimisho ya Misa Takatifu yaliongozwa  Askofu Raphael p'Mony Wokorach, Askofu anayemaliza muda wake wa kichungaji wa Jimbo katoliki la Nebbi kwa kuwa  alichaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la  Gulu. Askofu Wokorach kama kiongozi wa  Ibada ya Misa Takatifu, aliyoadhimishwa alikuwa na Maaskofu wengine 20, katika banda lililo katikati ya ziwa la bandia lililopo mita mia chache kutoka kwenye Madhabahu ya mahali alipouawa Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake. Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu Mteule aliwaonya waamini kutoshawishiwa na aina yoyote ya ibada ya sanamu na matendo yasiyoendana na imani ya Kikristo kama vile kuoa wake wengi, uchawi na ukeketaji, akikumbuka jinsi ambavyo mashahidi wa Uganda walivyopendelea kuuawa, badala ya kukata tamaa kwa kuikana imani yao.

Masalia ya Mashahidi wa Uganda
Masalia ya Mashahidi wa Uganda

Mwanzoni mwa mahubiri, hata hivyo Askofu Mkuu Wokorach alishukuru Baraza la Maaskofu wa Uganda kwa kulipatia Jimbo Katoliki la Nebbi fursa ya kuongoza Siku ya Mashahidi mwaka huu. Alisema maadhimisho ya Siku ya Wafiadini “yana maana kubwa kwa Wakristo nchini Uganda na kanisa kwa ujumla. Kuadhimisha siku hii ni kukiri na kudhihirisha wema wa Mungu kwa Kanisa na kwa Waganda. Ni tendo linaloburudisha namna yetu ya kuwa Wakristo nchini Uganda na kwingineko.” Kiongozi huyo aligusia maadhimisho hayo ya Siku ya Mashahidi wa Uganda kila mwaka, “kama tukio la Pentekoste mpya, mahali ambapo watu kutoka pembe zote za dunia hukusanyika pamoja katika maombi kama familia moja ya Mungu iliyounganishwa katika imani.” Aliendelea Kiongozi hyo kuwaalika “mahujaji kuiga urithi wa Mashahidi wa Uganda walioishi na kuonesha imani thabiti bila kujali hatari kwa maisha yao wenyewe. Wafia imani walilichukulia Neno la Mungu kwa uzito, nalo likatengeneza na kuashiria maisha yao.”

Ibada ya Misa wakati wa Hija ya Papa Francisko 2019 katika eneo lililoandaliwa kwa ajili ya misa za mashahidi
Ibada ya Misa wakati wa Hija ya Papa Francisko 2019 katika eneo lililoandaliwa kwa ajili ya misa za mashahidi

Kwa kufuata mfano wa Mashahidi wa Uganda waliosimama kidete katika misingi thabiti ya imani yao, Askofu Wokorach pia alichukua muda kuwahimiza viongozi wa nchi hiyo, watunga sera na watu wote wenye mamlaka kujifunza kutokana na ujasiri wa mashahidi hao na kukabiliana na janga la ufisadi nchini Uganda. “Ufisadi, sasa umepenya katika sekta nyingi za jamii ya Uganda,”Alisema Askofu. Katika kilele cha mahubiri yake, Askofu mkuu Mteule, Wokorach aliwahimiza “Wakristo kukumbatia Sakramenti ya Ndoa Takatifu ikiwa ni njia mojawapo ya kuimarisha familia na mataifa. Kwa mfano wao, familia zina Familia Takatifu ya Nazareti, kama mfano unaofaa kuigwa” ambapo, askofu wa Jimbo kuu la Gulu alidokeza. Kwa njia hiyo aliomba huruma za  Mungu kwa mahujaji wote na kuwaombea kwa Mungu awaonee huruma kwa maombezi yao yote.

Mahujaji kutoka Jimbo la Lira wakitembea kuelekea Namugongo
Mahujaji kutoka Jimbo la Lira wakitembea kuelekea Namugongo

Ikumbumkwe Jimbo Katoliki ya Nebbi lilihuisha Siku ya Wafiadini kwa mara ya mwisho, huko Namugongo, mnamo mwaka wa 2007.  Vile vile kama tulvyoeleza hapo mwanzo, Mwaka huu, Kanisa Katoliki nchini Uganda linaadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 tangu Papa Paulo VI alipotangaza kuwa watakatifu  Mashahidi wa Uganda mwaka 1964. Pia linaadhimisha miaka 145 ya imani ya Kikatoliki nchini Uganda iliyoletwa na Wamisionari wa Afrika, wanaojulikana kama Mababa Weupe. Kwa njia hiyo Sherehe hiyo ilivutia waamini sio tu kutoka Uganda, bali kutoka nchi kadhaa za Afrika : Sudan Kusini, Kenya, Rwanda, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Cameroon, Botswana, Afrika Kusini na mabara mengine kama vile kutoka nchini  Argentina, Colombia, Australia na Denmark. Misa hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi muhimu wa serikali akiwemo hata wabunge wa Uganda, viongozi wa kiutamaduni na wakuu wa vyama tofauti vya kisiasa, na madhehebu mbali mbali na zaidi Rais wa Nchi ya Uganda BwanYoweri Kaguta Museveni na ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za mwaka huu za Siku ya Mashahidi

04 June 2024, 19:50