Tafuta

Yesu baada ya kuwapa katekesi ya kina jinsi nguvu za Mungu zinavyopingana na za Shetani na kuwa Mungu ana nguvu kuliko Shetani. Alitoa tamko la dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu! Yesu baada ya kuwapa katekesi ya kina jinsi nguvu za Mungu zinavyopingana na za Shetani na kuwa Mungu ana nguvu kuliko Shetani. Alitoa tamko la dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu! 

Tafakari Dominika ya 10 ya Mwaka B wa Kanisa: Kufuru Dhidi ya Roho Mtakatifu

Kristo Yesu baada ya kuwapa katekesi ya kina jinsi nguvu za Mungu zinavyopingana na za Shetani na kuwa Mungu ana nguvu kuliko Shetani. Alitoa tamko la dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu akisema; “Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele.” Kufuru ya Roho Mtakatifu: Kuidhihaki na kuikashfu imani.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 10 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanahusu mapambano ya vita vya kiroho kati ya wema na ubaya, dhambi katika maisha yetu ya kila siku. Lakini hatupaswi kuwa na mashaka daima tutaibuka washindi tukimtumaini Mungu. Ndivyo wimbo wa mwanzo unavyotupa matumaini na ujasiri wa kutokuogopa chochote kwa kuwa Mungu daima yuko upande wetu ukisema; “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Watesi wangu na adui zangu, walijikwaa wakaanguka” (Zab. 27:1-2). Mungu ni asili ya wema wote ndiyo maana katika sala ya mwanzo mama kanisa anasali na kuomba hivi; “Ee Mungu, uliye asili ya mema yote, uziangaze nia zetu sisi tunaokusihi tupate kuwaza yaliyo mema; tena utuongoze tuyatimize kwa matendo.” Somo la kwanza ni la Kitabu cha Mwanzo (Mwa. 3:9-15). Somo hili linatueleza kuwa dhambi ya watu wa kwanza ilikuwa ni kiburi. Matokea ya dhambi hii ni kujitenga na Mungu na kuingia katika maisha ya taabu na mahangaiko. Tunasoma hivi; “Bwana Mungu alimwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema; Nalisikia sauti yako bustanini, naliogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani alikuambia ya kuwa u uchi? Je! umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema; Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke; Nini hili ulilolifanya?

Roho Mtakatifu ni mhimili wa uinjilishaji, maisha na utume wa Kanisa.
Roho Mtakatifu ni mhimili wa uinjilishaji, maisha na utume wa Kanisa.

Mwanamke akasema; Nyoka alinidanganya, nikala. Bwana Mungu akamwambia nyoka; Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” Katika majadiliano hayo kati ya Mungu na Adamu, Mungu na Eva, na mwisho Mungu na Nyoka, Ibilisi. Tunaona kuwa anayelaaniwa ni Nyoka. Adamu na Eva hawalaaniwi. Ila matokeo ya dhambi yao, kukosa utii kwa Mungu, kuchagua kufuata njia yao wenyewe badala ya kufuata mipango ya Mungu yalikuwa mabaya mno. Kwanza ni kutambua kuwa wako uchi, sio uchi wa kukaa bila nguo bali kuwa mbali na Mungu, kukosa hadhi ya kuwa wana wa Mungu. Mbaya zaidi hakuna aliyekuwa tayari kukiri kosa na kuomba msamaha. Adamu alimlaumu Eva na Mungu kwa kumpa Eva. Kuna tofauti kubwa sana katika maneno ya Adamu akimshutumu Eva na Mungu na yale aliyotamka kwa furaha alipomwona Eva Mungu alipomleta mbele yake akisema; “huu ni mfupa katika mifupa yangu na na nyama katika nyama yangu” (Mw 2:23). Lakini sasa anamlaumu Eva na Mungu ili kukana kosa lake; “ni huyu mwanamke uliyenipa, ndiye aniyenipa tunda nikala” (Mw. 3:12). Dhambi inaleta mafarakano kati ya watu walio karibu. Eva naye anamlaumu nyoka na Mungu kwa kumuumba nyoka. Nyoka hamlaumu yeyote; Yeye anafurahia ushindi, kufanikiwa kuwafanya watu wamwasi Mungu.

Roho Mtakatifu ni zawadi maalum kwa maondoleo ya dhambi
Roho Mtakatifu ni zawadi maalum kwa maondoleo ya dhambi

Mungu hawalaani Adamu na Eva; wao ni watoto wake na anawapenda pamoja na kutotii kwao. Kazi ambayo ingekuwa raha kama wangebaki waaminifu, sasa inakuwa adhabu na jambo la kuhenyeka. Katika mpango wa Mungu, ingekuwa furaha tupu kwa mwanamke kujifungua. Lakini sasa baada ya kuanguka jambo hili limekuwa mateso makuu. Zaidi ya hayo kutakuwa na uadui wa moja kwa moja kati ya mwanadamu na shetani. Shetani atajaribu wakati wote kueneza sumu ya dhambi katika moyo wa mwanadamu ili kuleta mahangaiko na mateso katika maisha yake kama ya nyoka anapomuuma mtu kisigino. Lakini Mungu kwa upendo wake anatangaza kushindwa kwa shetani kuwa kutoka katika uzao wa mwamamke shetani atashindwa kwa kuponda kichwa chake kama kichwa cha nyoka. Mzaburi alipotafakari wema na upendo huu wa Mungu kwa mwanadamu aliimba hii zaburi ya wimbo wa katikati kuwa ni vyema kujikabidhi mikononi mwa Mungu akisema; “Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia. Bwana, uisikie sauti yangu, masikio yako na yaisikilize sauti ya dua zangu. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, ili Wewe uogopwe. Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja, na neno lake nimelitumainia. Nafsi yangu inamngoja Bwana, kuliko walinzi waingojavyo asubuhi. Ee Israeli, umtarajie Bwana; Maana kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi mwingi. Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake yote” (Zab. 129).

Roho Mtakatifu anawakirimia waamini ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Yesu
Roho Mtakatifu anawakirimia waamini ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Yesu

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2 Kor. 4:13-15:1). Katika somo hili Mtume Paulo anatufariji na kututia moyo kuwa taabu za maisha ya sasa si kitu tukitazamia heri na furaha tutakazozipata baada ya ufufuko wetu ambao chanzo chake ni Kristo mfufuka. Hivyo basi tujitahidi daima kujikabidhi kwa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo nyakati zote za maisha yetu na tukianguka dhambini tuamke mara, tuikimbilie sakramenti ya kitubio, tujipatanishe na Mungu Baba yetu. Injili ni ilivyoandikwa na Marko (Mk. 3:20-35). Sehemu hii ya Injili inasimulia jinsi ndugu zake Yesu walivyomkashfu wakisema; “Amerukwa na akili.” Waandishi nao wakamkufuru kwa kumsingizia kuwa anafanya miujiza ya uponyaji kwa kushirikiana na shetani wakisema, “ana Beelzebuli, na, kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo.” Yesu baada ya kuwapa katekesi ya kina jinsi nguvu za Mungu zinavyopingana na za Shetani na kuwa Mungu ana nguvu kuliko Shetani. Alitoa tamko la dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu akisema; “Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele.” Lakini hii dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi? Kwanza kabisa neno “kukufuru” kwa kiyunani “Blasphemia” maana yake ni kutukana, kuzungumza vibaya, kudharau, kudhihaki na kukashifu imani au kitu ulichokijua mwanzoni na kukiamini au kukikubali na ni cha kweli. Hivyo “kumkufuru Mungu” maana yake ni kumtukana Mungu au kumdharau na kuzungumza vibaya juu ya Mungu. Na adhabu ya ki-biblia kwa mtu aliyethibitika kumkufuru Mungu ilikuwa ni kupigwa mawe mpaka kufa (Walawi 24:10-160.)

Roho Mtakatifu ni mhimili wa uinjilishaji, maisha na utume wa Kanisa.
Roho Mtakatifu ni mhimili wa uinjilishaji, maisha na utume wa Kanisa.

Sasa kumkufuru Roho Mtakatifu ni kumuasi Roho Mtakatifu, ni kuwa kinyume naye, kuzikana, kuzikataa na kuzisema vibaya kazi zake. Kumkufuru Roho Mtakatifu ni kuzihusianisha kazi za kweli za Roho Mtakatifu na nguvu za shetani. Mafarisayo kwa maneno yao walikana kazi ya kweli ya Roho Mtakatifu, walitoa sifa kwa kazi yake kwa Beelzebuli, Shetani. Kwa namna hii walimkufuru Roho Mtakatifu. Kumkufuru Roho Mtakatifu ni kitendo cha ukaidi wa hiari ni kukataa kazi ya Roho Mtakatifu kwa makusudi kabisa. Mafarisayo waliona nguvu za Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu zikifanya miujiza, wakazikataa kwa makusudi kabisa na kwa makusudi hayo hayo wakazinasibisha kwa Shetani. Lakini kwanini hii dhambi haina msamaha? Hii ni kwa sababu moja ya kazi kuu ya Roho Mtakatifu ni kutusaidia kutambua dhambi na makosa yetu, kutuelekeza katika ukweli (Yn 16: 8-9), na kutuongza mpaka kwa Kristo aliye chanzo cha wokovu wetu (Yn 6:44). Zaidi sana ufunguo wa msamaha ni toba. Ufunguo wa toba ni imani. Chanzo cha imani ni Roho Mtakatifu. Kwa hiyo kukataa kazi ya kweli ya Roho Mtakatifu, ni kukataa chanzo cha imani. Na kukataa chanzo cha imani ni kunaziba njia zote za kutusaidia kufanya toba na hivyo hakuna msamaha. Hivyo sababu ya kutosamehewa kwa dhambi ya kumkufuru Roho Mtaktifu ni kutokuomba msamaha, kuwa nje ya mpango wa Mungu, kuyakataa mapenzi ya Mungu. Ndiyo maana baada ya hapo Yesu alitoa sharti la kuwa ndugu zake, kuwa mshirika katika familia ya Mungu akisema; “Kwa maana mtu ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.” Basi tujitahidi kuishi kwa upendo maana upendo hushinda ubaya wote ndiyo maana katika sala kuombea dhabihu mama Kanisa anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba utazame kwa wema ibada yetu, na hii sadaka tunayokutolea ikupendeze na kutuongezea mapendo”. Nayo antifona ya komunyo inatilia mkazo ikisema “Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake” (1Yoh. 4:16). Tukiwa ndani ya Mungu, Yeye atatuponya kwa huruma yake. Ndiyo maana katika sala baada ya Komunyo Mama Kanisa kwa matumaini makubwa anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, kazi yako ya huruma ituponye maovu yetu na kutuelekeza tutende yaliyo adili."

09 June 2024, 14:46