Ujumbe wa masomo ya domenika hii unatuhimiza kuwa kamwe tusikate tamaa katika maisha kwa sababu ya changamoto na majaribu. Ujumbe wa masomo ya domenika hii unatuhimiza kuwa kamwe tusikate tamaa katika maisha kwa sababu ya changamoto na majaribu. 

Tafakari Dominika ya 11 ya Mwaka B wa Kanisa: Kujiaminisha Kwa Mungu

Ujumbe wa masomo ya dominika hii unatuhimiza kuwa kamwe tusikate tamaa katika maisha kwa sababu ya changamoto, majaribu, magonjwa, shida taabu, na mateso. Daima kwa moyo wa imani, tujikabidhi mikononi mwa Mungu kwa sala na maombi, Yeye daima atatusikiliza na kutuokoa. Hii ni changamoto kwa waamini kujiaminisha na kujikabidhi kwa Mwenyezi Mungu kwani bila Yeye mwanadamu hawezi kufua dafu mbele ya matatizo na changamoto za maisha.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 11 ya mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya dominika hii unatuhimiza kuwa kamwe tusikate tamaa katika maisha kwa sababu ya changamoto, majaribu, magonjwa, shida taabu, na mateso. Daima kwa moyo wa imani, tujikabidhi mikononi mwa Mungu kwa sala na maombi, Yeye daima atatusikiliza na kutuokoa. Ndiyo maana zaburi ya wimbo wa mwanzo inayofungua maadhimisho ya kiliturujia katika dominika hii inaimba hivi; “Ee Bwana, usikie, sauti yangu ninalia, umekuwa msaada wangu, usinitupe, wala usiniache, ee Mungu wa wokovu wangu (Zab. 27:7, 9). Tukumbuke kuwa bila Mungu sisi hatuwezi lolote na tukiwa na Mungu yote yanawezekana. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisali; “Ee Mungu uliye nguvu yao wanaokutumaini, uwe radhi kusikiliza dua zetu. Na kwa kuwa pasipo wewe hatuwezi kitu sisi wanadamu dhaifu, utujalie daima msaada wa neema yako, tupate kukupendeza kwa moyo na matendo katika kutimiza amri zako.”

Sala ni kujiaminisha mbele ya Mungu
Sala ni kujiaminisha mbele ya Mungu

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Ezekieli (Eze. 17: 22-24). Jina Ezekieli maana yake ni hii; “Mungu ni mwenye Nguvu”. Somo hili ni tangazo la mpango wa Mungu wa kuwarudisha waisraeli katika nchi ya ahadi kutoka uhamisho wa Babeli, ili kuwafanya taifa kubwa ambalo kwalo mataifa yote watakombolewa nalo kutoka utumwa wa dhambi. Itakumbukwa kuwa baada ya Mfalme Sulemani kufariki, ufalme wa Israeli uligawanyika katika Falme mbili: Ufalme wa Israeli upande Kaskazini ukiwa na makabila 10, mji wake mkuu ukiwa Samaria, na ufalme wa Yuda upande wa kusini, ukiwa na makabila 2, mji wake mkuu ukiwa Yerusalemu. Ezekieli, mtoto wa Kuhani, alizaliwa Yerusalemu wakati ufalme wa Israeli upande wa Kaskazini, ulishavamiwa na kubomolewa na Waashuru. Wakati huo, Ufalme wa Yuda upande wa kusini makao makuu yakiwa Yerusalemu ulikuwa chini ya Yohoakimu, haukuvamiwa maana ulilindwa na Nebukadneza, mfalme wa Babeli kwa kuwa walilipa kodi kwake. Baadae Yohoakimu alikataa kulipa kodi. Mfalme Nebukadineza alituma jeshi likaivamia Yerusalemu, na kuwachukua watu wake wengi mateka na kuwapeleka Babeli katika awamu tatu: Mwaka 605 K.K. waliochukuliwa vijana wengi miongoni mwao akiwa Danieli. Mwaka 597 K.K. watu wengine walichukuliwa mateka, Ezekieli alikuwa mmoja wao. Nebukadineza alimteua Zedekia kuwa mfalme atawale mahali pa Yohoakimu, kwa masharti kulipa kodi. Mwaka 593 K.K Mungu alimchagua Ezekieli kuwa nabii. Na ujumbe alioutoa ni ule ule alioutoa Yeremia kwamba mji wa Yerusalemu na hekalu lake vitaangamizwa kwa sababu ya wingi wa dhambi na kuabudu sanamu kulikokuwa kunaendelea huko Yerusalemu.

Katika shida na majaribu ya maisha, sala iwe ni kimbilio la imani na faraja
Katika shida na majaribu ya maisha, sala iwe ni kimbilio la imani na faraja

Ezekieli aliwaonya Waisraeli waliokuwa uhamishoni na wakati huo huo Yeremia akiwaonya waliobaki Yerusalemu. Ujumbe huu ulitimia baada ya Majeshi ya Babeli kuja kwa mara ya tatu yakauharibu kabisa mji wa Yerusalemu na Hekalu lake, mfalme Zedekia alikamatwa, mtoto wake akachinjwa mbele yake kisha yeye mwenyewe akang’olewa macho, na kupeleka uhamishoni Babeli kama mtumwa na kufa huko. Tukiongea kibinadamu, maangamizi haya yalipaswa kuashiria mwisho wa Taifa la Israeli na utawala wake. Lakini mnamo mwaka 586 K.K Ezekieli alitangaza ujumbe mpya wa matumaini, kuwa: Mungu ni Mchungaji Mkuu wa Israeli. Yeye atawakusanya tena kutoka miisho ya dunia na kuwarudisha tena katika nchi yao wenyewe. Ndio ujumbe wa somo la kwanza la dominika hii ya 11 mwaka B. Katika kutoa ujumbe huu, Nabii Ezekieli anatumia lugha ya picha ya miti na ndege. Taifa la Israeli linafananishwa na mti unaonyauka na kukaribia kutoweka katika uso wa dunia. Mungu anaahidi kuuhuisha na kuupa uhai tena, kuliinua na kulifanya kuwa taifa kubwa litakalowavutia watu wa mataifa mengine, nazo falme ziliwagandamiza kwa mabavu zingetokomezwa katika geografia ya ulimwengu. Ingawa ni kweli kuwa miaka 50 baadaye, Wayahudi waliruhusiwa kurudi Yerusalemu na nyakati za kuzaliwa kwake Yesu, falme zilizowakandamiza zilibaki katika historia. Lakini utabiri huu haukuhusu ufalme wa kidunia, bali ufalme wa Mungu uliosimikwa na Yesu Kristo, nao utadumu milele yote.

Mwenyezi Mungu ni kimbilio la waja wake wakati wote.
Mwenyezi Mungu ni kimbilio la waja wake wakati wote.

Somo la pili la ni la Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2Kor. 5:6-10). Somo hili lina mwangwi wa ujumbe wa Nabii Ezekieli juu ya ufalme wa mbinguni. Mtume Paulo anasema kuwa anatarajia maisha ya furaha baada ya taabu ya hapa ulimwenguni. Hivyo anatualika kuwa na matumani tukienenda kwa imani. Licha ya kuwa baada ya kufa, watu wote watahukumiwa na Kristo, Paulo anajipiga moyo konde kwani anajiona hana hatia kwa kuwa anaishi kadiri ya amri na mpango wa Mungu. Hivyo haogopi kumwendea Mungu, hakimu mwenye haki. Nasi tunapaswa kuwa na ujasiri huo huku tukiishi tukiwa na muunganiko na Kristo Bwana na mkombozi wa maisha yetu. Injili ni ilivyoandikwa na Marko (Mk. 4:26-34). Sehemu hii ya Injili inatupa mifano miwili. Mfano wa kwanza unahusu namna mbegu ivyootavyo na kukua hata kutoa mazao yake. Yesu anasema kuwa mkulima hawezi kufanya lolote ili mbegu ziote, zikue na kuzaa matunda katika shamba lake isipokuwa tu kuzipanda kuzisubiri kwa uvumilivu na moyo wa subira, ziote, azipalilie ziweze kutoa mazao yake. Namna ambavyo zinaota na kukua mpaka kufikia ukomavu wake na kutoa matunda, mkulima hawezi kufanya lolote, isipokuwa kutegemea nguvu na hekima ya Mungu inavyofanya kazi katika mbegu alizozipanda. Mfano wa pili ni wa punje ya haradali, licha ya kuwa ni ndogo sana, ikimea inakuwa na kuwa mti mkubwa. Ndivyo alivyopenda na kupanga Mungu.

Pasipo Mungu Mwanadamu hawezi lolote lile.
Pasipo Mungu Mwanadamu hawezi lolote lile.

Mifano hii inatupa ujasiri na kututia moyo kuwa tukimtegemea Mungu maisha yetu yatashamiri na kuendelea kuwa ya furaha na amani. Huu ni ukweli wa wazi. Ndiyo maana maneno ya Nabii Ezekieli ya kuwafariji waisraeli kuwa Mungu hushusha chini mti mrefu na kuuinua mfupi, huukausha mti mbichi na kuustawisha mkavu. Bikira Maria aliyaimba akisema; “Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi akawapandisha wanyenyekevu, wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.” Kumbe basi katika maisha yetu tusikate tamaa kamwe, maana Mungu akiwa upande wetu, hakuna wa kutushinda. Nasi hatuna cha kumlipa zaidi ya kumshukuru kwa wema wake kwetu tukiimba pamoja na mzaburi wimbo wa katikati tukisema; “Ni neno jema kumshukuru Bwana, na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu. Kuzitangaza rehema zako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku. Mwenye haki atasitawi kama mtende, atakuwa kama mwerezi wa Lebanoni. Waliopandwa katika nyumba ya Bwana, watasitawi katika nyua za Mungu wetu. Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, watajaa utomvu, watakuwa na ubichi. Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili. Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu” (Zab. 91:1-2, 12-15). Naye mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasisitiza akisema; “Ee Mungu, umetujalia mazao haya ya nchi yawe chakula cha kulisha miili yetu na Sakramenti ya kutufanya wapya rohoni. Tunakuomba utujalie tusitindikiwe fadhili hiyo kwa ajili ya miili na roho zetu.”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika ya 11 Mwaka B wa Kanisa
13 June 2024, 07:34