Tafuta

Dominika ya 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Mababa wa Kanisa tangu mwanzo katika sehemu hii ya Injili wanaliona Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Dominika ya 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Mababa wa Kanisa tangu mwanzo katika sehemu hii ya Injili wanaliona Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Kumtumainia Mungu

Dominika ya 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Mababa wa Kanisa tangu mwanzo katika sehemu hii ya Injili wanaliona Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Katika maisha na historia yake, Kanisa limekumbana na dhoruba mbalimbali, lakini limeweza kuvuka yote haya na kusonga mbele kwa sababu Kristo Yesu ndiye nahodha wa chombo hiki na kamwe hajawahi kulala na kukiacha chombo kizame! Jambo la msingi ni kumtumainia Mwenyezi Mungu!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji wetu karibu katika tafakari ya Dominika ya 12 ya Mwaka B wa Kanisa. Mababa wa Kanisa tangu mwanzo katika sehemu hii ya Injili wanaliona Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Katika maisha na historia yake, Kanisa limekumbana na dhoruba mbalimbali, lakini limeweza kuvuka yote haya na kusonga mbele kwa sababu Kristo Yesu ndiye nahodha wa chombo hiki na kamwe hajawahi kulala na kukiacha chombo kizame! Tutamsikia Kristo baada ya kuwafundisha makutano siku nzima Kristo alihitaji kupumzika akaamua kuvuka ng’ambo, safari ikiendelea akalala usingizi. Jioni ikaingia jua likazama na upepo kuanza kidogo kidogo na mawimbi madogo madogo na kuongezeka kadiri muda ulivyopita. Mitume waliijua hali hii hivi walishusha ‘tanga’ na kupiga kasia kwa nguvu zaidi ili wawahi lakini upepo ulizidi na mawimbi ya bahari yakawa makubwa, maji yalipoanza kuingia ndani ya boti yao na kutishia kuvunjika wakaona hapa ‘hatuwezi pekee yetu, wakashuka chini alikolala na kwa sauti tetemeshi, ikibeba kwa mbali ‘tone’ ya ukali, mkandamizo, kukosa uvumilivu na kukata tamaa, jasho likiwatoka kwa kupiga kasia, “Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?’… ni aina fulani ya ‘sala’ ya lalamiko iliyofungasha hofu kuu… akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari ‘nyamaza utulie’, kukawa shwari kuu (Mk 4:39).

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu
Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu

UFAFANUZI: Katika somo la kwanza majaribu ya Ayubu (38:1, 8-11) anajibiwa na Mungu baada kutoelewa sababu ya mawimbi, upepo na dhoruba alizozipitia kwa miaka mingi. Kadiri ya Injili hii Bahari ni ulimwengu na mawimbi, dhoruba na upepo ni changamoto za maisha. Kuna muda roho zetu zinapaa juu kama tai hadi kilele cha mafanikio na ghafla dhoruba huja na kutuvuruga na kutudondosha chini katika malengo yetu. Katika nyakati hizi tunamwona Kristo ‘amelala’ sisi tunapohangaika, tunasali na hatuoni matokeo, ni kama vile Mungu ametuacha, hatutazami, haguswi, hatuhurumii tena. Ni kama vile Mungu wa leo ni tofauti na wa zamani. Laiti wangemuacha Yesu apumzike upepo na mawimbi vingeisha tu vyenyewe, hata hivyo Yesu hakatai kuamka, hatufukuzi tunapomlilia… Je, unapopatwa na tatizo unalipokea kwa pupa na paniki kama mitume hawa? Au unapokea kwa ukomavu, utulivu, kujiamini na matumaini ya ushindi? Maisha yetu ni mafupi sana hivi sio hekima kutawaliwa na hofu tena hofu nyingine ya vitu vidogo kabisa. Hata kama Kristo anaonekana ‘kulala’ maishani mwako mruhusu apumzike, anajua hitaji lako na anajua analolitenda, hatakuacha upite njia ngumu kupita uwezo wako wa kustahimili. Mtumbwi ni Kanisa la Mungu, wanafunzi ndani ya mtumbwi ni mimi na wewe tukisafiri kuvuka ng’ambo ya pili, mbinguni kwa Baba... Kwa wayahudi bahari ni makao ya mashetani, ishara ya nguvu za giza.

Waamini wanapaswa kujiaminisha na kumtegemea Mungu
Waamini wanapaswa kujiaminisha na kumtegemea Mungu

Tunasahau kuwa ni Yeye ndiye aliyeamuru ‘…NA TUVUKE MPAKA NG’AMBO…’ na kwamba uwepo wake tu kwetu ni salama ya milele sababu ulimwengu na vyote viujazavyo ni mali yake na daima vinamtii, basi tuyashike mausia yake tukidumu katika imani sababu katika dakika ile tunapoona tunaangamia, pale ambapo mang’amuzi yetu yamefika mwisho, kizunguzungu kimetufunika macho ndipo Kristo ‘anapoamka na kuukemea upepo na bahari’ na kila kitu kinakuwa shwari. Ni aibu kiasi fulani kukemewa na kuulizwa ‘mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?’… Haijalishi ni dhoruba kubwa kiasi gani unapitia muda huu, Kristo yu tayari ‘kuamka’ ndani mwako ili kukemea hayo yote, na anapoinuka hakuna kinachosimama tena, iwe bahari, uwe upepo, awe ibilisi, iwe malimwengu, vyote hustaajabu tu na kuambiana, ‘ni nani huyu basi hata upepo na bahari humtii?’ tusimuaibishe kwa hofu zisizo na tija. “… na tuvuke mpaka ng’ambo tupate kupumzika.” Kama wafuasi wa Kristo tunapaswa kuwa na ‘ng’ambo moja tu’ upande wa pili, mbingu. Wewe ng’ambo yako ni ipi, unasafiri kwa mtumbwi upi au kwa usafiri gani kuvuka Bahari hii ya machafuko yaani dunia tunayoishi? Huenda ng’ambo unayoikimbilia sio hii anayotutaka Kristo tuivukie na mbaya zaidi Yesu hayumo kwenye hiyo mashua. Tupo tunaopambana na mawimbi kwa lengo la kupata utajiri mnono, majina makubwa, umaarufu, vyeo au madaraka, nguvu, ushawishi, mvuto, wapenzi, na mambo makubwa kupita uwezo, ndio ng’ambo yetu… Je, ‘itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote akipata hasara ya nafsi yake?’ (Mk 8:36). Wapo wenye hayo yote lakini hawana furaha, amani, afya njema, wamekata tamaa, msongo wa mawazo saa 24, wamedhoofu.

Waamini wajiaminishe kwa Mungu kwa njia ya Sala
Waamini wajiaminishe kwa Mungu kwa njia ya Sala

Katika hali hii inafaa kutafakari si tu mwendo wa mtumbwi wetu katikati ya bahari ngumu ya ulimwengu bali pia uelekeo wa mtumbwi wenyewe. Mtumbwi wa hivi upo hatarini, unavunjika sababu ya dhambi zinazolia mbele ya Mungu, hasira, kisasi, ghadhabu, chuki, ugomvi, kutojali…  Labda tunatumia nguvu kubwa ya akili, mwili na rasilimali nje kabisa ya lengo la Kristo, tunapiga kasia kwa nguvu kubwa tukikimbilia ng’ambo tusiyotumwa kwenda na kuishia kutangatanga. Halafu tunajiuliza ‘tunakwama wapi, mbona hatuoni matokeo mema, hatuna furaha wala utulivu?’ Sababu ni hii kwamba mwendo wetu mkali hauelekei ng’ambo tuliyoamriwa. Ni vema tukiunganika na Kristo ambaye kadiri ya somo II (2Kor 5:14-17) ameunganika na waamini nao wanafanyika viumbe wapya ndani yake. Roho zetu ni kama mtumbwi, moyo ndio kapteni na Kristo ndiye Muongozaji, kwa wema wake na asaidie kusudi mioyo yetu ipate utulivu, amani na usalama katika Yeye, na ni Yeye tu, sasa na siku zote. Nakutakia uamuzi na utashi imara wa kuvuka ngàmbo ya mabadiliko ya kiroho, kimaadili, kiuchumi, na kufanya mabadiliko ya jumla ya binadamu anayemcha na kumtii Mungu katika yote.

Liturujia D 12 Mwaka B wa Kanisa
21 June 2024, 13:51