Tafuta

Ujumbe wa masomo ya dominika hii umejikita katika ukweli huu; “asili na chanzo cha uhai ni Mungu.“ Ujumbe wa masomo ya dominika hii umejikita katika ukweli huu; “asili na chanzo cha uhai ni Mungu.“  

Tafakari Dominika 13 ya Mwaka B wa Kanisa: Imani Inayorutubishwa Kwa Matumaini

Ujumbe wa masomo ya dominika hii umejikita katika ukweli huu; “asili na chanzo cha uhai ni Mungu.“ Uhai ni zawadi na tunu ya Mungu kwetu sisi wanadamu. Mungu anapenda tuishi, tena tuishi kwa furaha na amani. Magonjwa, mahangaiko, mateso na kifo havitoki kwa Mungu bali kwa yule mwovu, shetani, mkuu wa giza, dhambi na mauti. Mungu ni Bwana wa uhai. Yeye daima yupo upande wa maisha, upande wa nuru. Imani inayorutubishwa kwa matumaini!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 13 ya mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya dominika hii umejikita katika ukweli huu; “asili na chanzo cha uhai ni Mungu.“ Uhai ni zawadi na tunu ya Mungu kwetu sisi wanadamu. Mungu anapenda tuishi, tena tuishi kwa furaha na amani. Magonjwa, mahangaiko, mateso na kifo havitoki kwa Mungu bali kwa yule mwovu, shetani, mkuu wa giza, dhambi na mauti. Mungu ni Bwana wa uhai. Yeye daima yupo upande wa maisha, upande wa nuru. Nasi hatuna budi kumshukuru kwa nyimbo za shangwe kwa zawadi ya uhai kama mzaburi katika wimbo wa mwanzo anavyosema; “Enyi watu wote, pigeni makofi, mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe” (Zab. 47:2). Naye mama kanisa katika sala ya mwanzo anasali akituombea hivi sisi wanae; “Ee Mungu, umependa kutufanya sisi tuwe wana wa nuru kwa neema uliyotufadhili. Tunakuomba utujalie tusifunikwe na giza la udanganyifu, bali tukae daima peupe katika nuru ya ukweli.” Somo la kwanza ni la kitabu cha Hekima ya Sulemani (1:13-15; 2:23-24). Somo hili linatueleza kuwa Mungu alikusudia heri kwa mwanadamu alipomuumba. Mungu aliyetuumba na kutujalia zawadi ya uhai anapenda tuishi kwa furaha na amani. Hivyo chochote kinachoangamiza maisha na uhai hakitoki kwa Mungu bali ni matokeo ya kukiuka misingi ya uhai na maisha aliyotujalia Mungu. Mateso, mahangaiko na kifo ni matokeo ya dhambi. Biblia yafundisha kwamba taabu zote tupatazo ni mapato ya dhambi, kumtii na kumsikiliza shetani, kumkaidi na kutokumtii Mungu. Ni wazi Mungu hakuifanyiza mauti, wala hafurahii kifo cha mwenye dhambi, licha ya kuwa kwa kifo na ufufuko wa Yesu, kifo chetu kimekuwa njia na namna ya kufika kwa Mungu.

Imani inayoboreshwa kwa matumaini.
Imani inayoboreshwa kwa matumaini.

Maandiko Matakatifu yanasema wazi kuwa matokeo ya kwanza ya dhambi ni kifo cha kiroho. Dhambi inaharibu na kuua uzima wa kimungu ndani mwetu. Madhara yake ni mahangaiko ya kimwili, kiakili, na kisaikolojia yanayopelkea kifo cha mwili. Kifo cha roho kikishatokea, kifo cha mwili ni dhahiri. Kumbe kifo ni adhabu kwa sababu ya dhambi; “Kwa maana u-mavumbi wewe na mavumbini utarudi” (Mwa 3:19). Hili lilikuwa tangazo la huzuni, matokeo na madhara ya dhambi. Dhambi inatuondolea uzima wa kimungu ndani yetu. Dhambi ni sumu dhidi ya mwili, iingiapo mwilini, kifo hakiepukiki. Kumbe, basi kama hali ndivyo ilivyo, ili tuweze kuwa salama yatupasa kujikabidhi mikononi mwa Mungu. Mzaburi alipotafakari na kutambua ukweli huu, aliimba hii zaburi ya wimbo wa katikati akisema; “Ee Bwana nitakutukuza, kwa maana umeniinua, wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu. Umeniinua nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka kuzimu. Umenihuisha na kunitoa, miongoni mwao washukao shimoni. Mwimbieni Bwana zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani, kwa kumbukumbu la utakatifu wake. Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, katika radhi yake mna uhai. Huenda kuliko kuja kukaa usiku, lakini asubuhi huwa furaha. Ee Bwana, usikie, unirehemu, Bwana, uwe msaidizi wangu. Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ee Bwana, Mungu wangu, mitakushukuru milele yote” (Zab. 29:1, 3-5, 10-12).

Mwenyezi Mungu anapenda waja wake waishi kwa furaha na amani.
Mwenyezi Mungu anapenda waja wake waishi kwa furaha na amani.

Somo la pili ni la Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (8:7, 9:13-15). Somo hili linahusu mausia ya Mtume Paulo kwa wakorinto kuhusu kushika ahadi walizoziweka mbele za Mungu. Wakorinto waliahidi kuwasaidia fukara wa Yerusalemu. Hivi Mtume Paulo anawajulisha kuwa kuwasaidia fukara ni neema si hasara. Neema ya Yesu na iwabidishe kwa ajili ya manufaa ya walio wahitaji kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na kwa ajili ya wao kujipatia zaidi neema na baraka za Mungu kwa matendo yao ya huruma yanayoongozwa na upendo. Neema na baraka hizi wazipatazo zinazowawezesha kuurithi uzima wa milele. Nasi daima tujitahidi kutenda matendo ya huruma ya kimwili na kiroho kwa upendo, kwani ni kwa ajili ya hayo, baada ya kifo, Yesu atatuambia hivi; “Vyema, mtumishi mwema na mwaminifu! ... Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!” (Mt. 25:21). Akaendelea kusisitiza akisema; “Njoni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea … Amin, amin ninawaambia, kwa jinsi mlimvyotendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea Mimi” (Mt. 25:35-36, 41).

Papa Francisko akiwafariji waamini waliofikwa na msiba wa mtoto wao
Papa Francisko akiwafariji waamini waliofikwa na msiba wa mtoto wao

Injili ni ilivyoandikwa na Marko (5:21-43). Sehemu hii ya Injili inasimulia miujiza miwili aliyoifanya Yesu. Muujiza wa kwanza, ni wa kuponywa mwanamke aliyetoka damu, kwa miaka 12, ambapo juhudi zake za kutafuta tiba kwa waganga wengi na kupoteza mali zake, hazikufua dafu. Lakini kwa kugusa tu upinde wa vazi la Yesu kwa imani kuu, alipona saa ile ile. Muujiza wa pili ni wa kumfufua binti Yairo. Miujiza hii miwili inatufundisha kuwa katika taabu, mahangaiko, magonjwa, mateso na mbele ya kifo, Yesu ndiye kimbilio letu. Na kila anayemkimbilia na kujikabidhi kwake kwa moyo wa imani, daima atakuwa na furaha na amani katika maisha ya sasa na yajayo, katika uzima wa milele mbinguni. Yesu mwenyewe ametuahidi uzima wa milele akisema; “Mimi ni ufufuko na uzima, kila aniamiye, hata akifa, ataishi” (Yn 11:26). Mtume Paulo naye anasisitiza jambo hili akisema; “Ikiwa tunaamini kuwa Kristo alikufa na kufufuka, vivyo hivyo, na hao waliolala katika Yeye, Mungu atawaleta pamoja naye” (1Thes 4:14). Ili tuweze kuurithi wa uzima wa milele yatupasa kumpenda Mungu na jirani. Tukumbuke kuwa dhambi ni sumu ya upendo. “Anayempenda ndugu yake, anaishi ndani ya Mungu, na Mungu anaishi ndani yake” (1Yn 4:16). Yeye asiyependa anaishi katika mauti (1Yn 3:14). Tukiwatendea vyema ndugu zetu wahitaji kwa upendo, tunawaongezea uhai, heshima ya utu wao, na tunashirikiana na Mungu katika kazi ya uumbaji na ukombozi.

Ee Bwana nitakutukuza milele
Ee Bwana nitakutukuza milele

Tuombe neema za Mungu ili kwa kafara ya Yesu ambayo inatolewa katika kila adhimisho la Misa Takatifu iweze kweli kuunganishwa na majitoleo yetu tunayoyafanya katika kuwa hudumia wengine kama anavyotuombea mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu akisema; “Ee Mungu, umependa kutuletea baraka za mafumbo yako. Tunakuomba utujalie ibada zetu ziafikiane na hii sadaka takatifu tunayokutoea. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa ndani na Kristo naye ndani yetu kama Yesu mwenyewe anavyosisitiza katika maneno ya antitofana ya Komunio akisema; “Baba, nawaombea hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kuwa wewe ndiwe uliyenituma” Basi tukifanya hivyo kweli tutakuwa na uzima wa kimungu ndani mwetu hapa duniani na kuungana na Yesu Bwana na mwokozi wa maisha yetu huko mbinguni aliko Yeye. Ndiyo maana mama Kanisa anapohitimisha maadhimisho ya Sadaka ya Misa Takatifu katika dominika hii anatuombea kwa matumaini haya akisema; “Ee Mungu, tunaomba kafara hii takatifu tuliyokutolea na kuila itutie uzima wako. Hivyo tuwe tumeungana nawe siku zote kwa mapendo, tupate kuzaa matunda yenye kudumu daima." Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 13 Mwaka B
27 June 2024, 08:07