Tafuta

Masomo ya dominika hii yanatuasa kumtumainia Mungu katika kukabiliana na matatizo na mahangaiko katika maisha. Masomo ya dominika hii yanatuasa kumtumainia Mungu katika kukabiliana na matatizo na mahangaiko katika maisha.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Fumbo la Mateso Katika Maisha ya Mwanadamu

Fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu linabaki kuwa ni swali linaloumiza na hasa tunapojaribu kujiuliza kwa nini Mungu aliye Baba yetu mwema, mwingi wa huruma na mapendo, bado anaruhusu mateso katika maisha ya mwanadamu, na hasa kwa wale wanaojitanabaisha kuwa ni wachamungu na marafiki zake Mungu. Kuna mateso na maovu mengi, swali la msingi, Je, ni kwanini Mwenyezi Mungu anaruhusu mateso na mahangaiko yote haya? Kimya kikuu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 12 ya mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuasa kumtumainia Mungu katika kukabiliana na matatizo na mahangaiko katika maisha. Fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu linabaki kuwa ni swali linaloumiza na hasa tunapojaribu kujiuliza kwa nini Mungu aliye Baba yetu mwema, mwingi wa huruma na mapendo, bado anaruhusu mateso katika maisha ya mwanadamu, na hasa kwa wale wanaojitanabaisha kuwa ni wachamungu na marafiki zake Mungu. Kuna mateso au uovu unasababishwa na mwanadamu, ukatili, uchoyo na ubinafsi wa mwanadamu dhidi ya mwanadamu mwingine, lakini juu ya yote swali linabaki hasa pale tunapojiuliza Je, ni kwa nini Mwenyezi Mungu anaruhusu mateso katika maisha yetu mathalani magonjwa na hata majanga mbalimbali? Ashirio la majibu ya ujumbe huu ni wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya kiliturujia katika dominika hii ukisema: “Bwana ni nguvu za watu wake, naye ni ngome ya wokovu kwa Kristu wake. Uwaokoe watu wako, uwabariki urithi wako, uwachunge, uwachukue milele (Zab.26:8-9). Ni katika muktadha huu, mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali akiwaombea wanae akisema; “Ee Bwana, utujalie kuliheshimu na kulipenda daima jina lako takatifu; kwa maana huachi kamwe kuwaongoza wale uliowaimarisha katika upendo wako.”

Mateso ya Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu
Mateso ya Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu

Somo la kwanza ni la kitabu cha Ayubu (38:1,8-11). Somo hili linahusu jawabu la Ayubu ya kwanini anateseka licha ya kumwamini na kumtumaini Mungu. Ayubu, licha ya kuwa aliishi kitakatifu, aliteseka mateso mengi mno. Hivyo alishindwa kufahamu kisa cha mateso yake. Hii ni kwa sababu, kadiri ya mawazo na fikra za kiyahudi, Mungu hulipa haki juu ya matendo ya mtu hapa duniani kabla hajafa. Ayubu mtu tajiri na mcha Mungu, daima alibaki mwaminifu kwa Mungu licha ya majaribu mengi aliyoyapata. Ayubu alipoteza watoto wake na mali zake zote kwa ghafla, akapata ugonjwa wa ngozi ulioambatana na majipu mwili mzima. Katika hali hiyo, Ayubu alimlalamikia Mungu akimuuliza; Je, ni haki kumwacha mtu mwenyehaki na mwaminifu kwako kama mimi niteseke namna hii? Mungu katika sehemu ya jibu lake kwa Ayubu anamuuliza maswali yanayoashiri ukuu wake, jinsi radi na ngurumo vinavyotokea, jinsi bahari inavyojaa na kupwa na namna nyota zinavyozunguka angani. Katika maswali aliyoulizwa na Mungu, Ayubu hakuweza kutoa jibu lolote. Ndiyo kusema akili ya mwanadamu haiwezi kutambua mipango ya Mungu. Basi Ayubu akayakubali yote na kujikabidhi zaidi kwa Mungu, Naye akamponya na ugonjwa wake, akamrudishia maradufu vyo alivyovipoteza. Kumbe somo hili linatufundisha kuwa tukikumbwa na matatizo, mahangaiko, mateso, na magonjwa njia ya kujikwamua nayo si kumuuliza Mungu maswali kwanini yametokea. Bali ni kujikabidhi kwake, tukitumainia hekima, uwezo na upendo wake. Tukumbuke kuwa kila tulichonacho ni zawadi kutoka kwa Mungu na hakuna mtu anayeweka matumaini yake kwake wakati wa mateso, akamwacha.

Mitume wakamwambia Yesu: Hujali kwamba, tunaangamia?
Mitume wakamwambia Yesu: Hujali kwamba, tunaangamia?

Mzaburi alipotafakari wema, upendo na ukuu wa Mungu akaishia kuimba zaburi hii ya wimbo wa katikati akisema; “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele. Washukao baharini katika merikebu, wafanyao kazi zao katika maji mengi, hao huziona kazi za Bwana, na maajabu yake vilindini. Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba, akayainua juu mawimbi yake. Wapanda mbinguni, watelemka vilindini, nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya. Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, akawaponya na shida zao. Huituliza dhoruba, ikawa shwari, na mawimbi yake yakanyamaza. Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia; Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani. Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, na maajabu yake kwa wanadamu (Zab. 106:1, 23-26, 28-31). Somo la pili ni la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2 Kor. 5:14-17). Katika somo hili mtume Paulo anaongelea vitu vinavyokinza – maisha na kifo, mambo yaliyopita na yajayo, dhambi na wokovu, ukombozi. Kuhusu maisha na kifo, Mtume Paulo anasisitiza kuwa Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, nasi tumekufa na kufufuka pamoja naye katika imani na ubatizo. Kama sasa tu viumbe vipya, basi tuishi kwa ajili ya yule aliyekufa na kufufuka kwa ajili yetu, Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wa maisha yetu aliyekufa na kufufuka ili sisi nasi tufe kuhusu dhambi na kuamkia uzima wa milele. Haya yote yametendeka kwa nguvu ya upendo wa Yesu Kristo kwetu sisi wanadamu. Hivyo ili tuweza kuyafaidi, yatupasa nasi kuishi tukipendana sisi kwa sisi kama Yesu alivyotupenda.

Bwana hujali kwamba tunaangamia?
Bwana hujali kwamba tunaangamia?

Injili ni ilivyoandikwa na Marko (Mk. 4:35-40). Sehemu hii ya Injili inasimulia tukio la Yesu kutuliza dhoruba. Katika tukio hili, tunaweza kusema kuwa kuna wahusika wa aina tatu. Kwanza ni dhoruba kuu ya upepo, iliyosababisha mawimbi kukipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Hapa tunakumbushwa simulizi la Yona ambapo Yesu naye alilala kama Yona (Yona 1:5). Tunaona hali ya bahari kama alivyoiona Ayubu katika somo la kwanza. Wahusika wa aina ya pili ni Mitume ambao wanamuita Yesu mwalimu, nabii mwenye nguvu na mamlaka juu ya maji ya bahari. Mamlaka na nguvu hizi, katika kitabu cha Yona, ni mamlaka na nguvu za Mungu peke yake. Na mhusika wa tatu ni Yesu mwenyewe ambaye ndiye mwenye nguvu na mamlaka juu ya maji ya bahari, na anaiamuru, inyamaze na kutulia. Simulizi hili, linatufundisha kuwa tukiwa katika hali ngumu ya maisha, na mateso, mahangaiko tumkimbilie Mungu nafsi ya pili, Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye alituahidi kuwa pamoja nasi siku zote mpaka ukamilifu wa dahari (Mk 28:20). Mitume walijaribu kwa nguvu zao zote kupambana na dhoruba bila mafanikio. Hofu na mashaka vikazidi kuwaingia. Walipokumbuka kuwa kati yao yupo Mungu nafsi ya pili, muweza wa yote, waliomba msaada kwake lakini kwa malalamiko wakisema; “Bwana haujali kwamba tunaangamia?” Yesu akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari; Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia; Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Fumbo la Mateso na Mahangaiko Katika maisha ya mwanadamu
Fumbo la Mateso na Mahangaiko Katika maisha ya mwanadamu

Hata sisi tunawekuwa na mashaka na kukata tamaa nyakati za matatizo baada ya kujaribu kwa nguvu zetu zote kuyatatua na kushindwa. Tukumbuke kuwa Yesu, nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu yupo nasi daima. Yale yanazidi uwezo wetu tukate rufaa kwake kwa moyo wa imani. Nyakati zingine sala na maombi yetu ni kama malalamiko. Wakati mwingine imani yetu kwa Mungu inapotetereka tunaanza kuona mashaka. Mungu anakaa kimya kwa sala zetu. Nasi tunaanza kumlaumu kwa kutotujali kwake. Tusione shaka bali tuwe na imani kuwa yote yawezekana. Tukumbe daima kuwa ili sala na maombi yetu yasikilizwe na Mungu yatupasa tuwe na muunganike naye, tusiwe katika hali ya dhambi, tujitakase na kujipatanisha naye. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, pokea sadaka hii ya kutupatanisha nawe na kukusifu. Utujalie itutakase tupate kukutolea mapendo safi ya mioyo yetu”. Tukiwa na muunganiko na Kristo daima yeye atasema; “Mimi ndimi mchungaji mwema, nami nautoa uhai kwa ajili ya kondoo wangu” (Yn. 10:11, 15). Ni katika tumaini hili mama Kanisa anapohitimisha maadhimisho ya kiliturujia ya dominika hii anasali hivi akituombea; “Ee Bwana, sisi tuliolishwa Mwili na Damu takatifu, tunaomba rehema yako ili ibada hii tunayofanya mara nyingi ituletee kweli ukombozi”. Hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 12 ya Mwaka B
19 June 2024, 07:37