Kardinali Rugambwa atunuku astashahada kwa wanaseminari 40 waliomaliza masomo yao ya Taalimungu,Tabora-Tanzania Kardinali Rugambwa atunuku astashahada kwa wanaseminari 40 waliomaliza masomo yao ya Taalimungu,Tabora-Tanzania 

Tanzania,Kard.Rugambwa:Shukrani kwa miaka 100 ya Seminari Kuu,Kipalapala!

Kardinali Rugambwa,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora Tanzania amefanya matembezi katika Seminari Kuu ya Tabora na kutunuku astashahada kwa wanaseminari 40 waliomaliza masomo yao ya Taalimungu na masomo mengine ya maagizo matakatifu.Anamshukuru Mungu kwa maahimisho ya miaka 100 ambayo yameanza maandalizi.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu Mkuu wa jimbo Kuu katoliki la Tabora, Nchini Tanzania, akiwa katika hafla ya kutunuku astashahada kwa wanaseminari 40 waliomaliza masomo yao ya Taalimungu na mafunzo kwa ajili ya maagizo matakatifu alimshukuru Mungu kutokana na  kukua kwa miito ya Kanisa. Kardinali  Rugambwa alisema kuwa: “Tunamshukuru Mungu kwa kuendelea kukua kwa miito katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo iliyopo Kipalapala ambapo kwa sasa tuna takriban wanaseminari 290 wanaomaliza masomo yao ya Kitaalimungu. Pamoja na wakufunzi wao, walimu na wafanyakazi wasio walimu, ni heshima kwetu kuupata mwaka huu ambao tunajiandaa kuadhimisha miaka mia moja.”

Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala Tanzania
Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala Tanzania

Kardinali Rugambwa aidha aliendelea kusema kwamba: “Kipalapala ni mojawapo ya seminari tatu za taalimungu zinazosimamiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC).” Seminari Kuu hiyo, ipo Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, iliyoanzishwa na Wamisionari wa Afrika wakati Tabora ilipokuwa Vikarieti ya Kitume ya Unyanyembe katika mji wa Ushirombo ambako ndiko kulikuwa na makao makuu ya Vikarieti. Kwa hakika  ilikuwa ni mnamo mwaka wa 1918 ambapo baadaye Seminari hiyo ilihamia mahali panapojulikana kama Utinta, katika Jimbo la  sasa la Mpanda na tangu mnamo mwaka 1925 ikawa Kipalapala kilomita chache kutoka Tabora mjini.

Kanisa la Seminari Kuu la Kipalapala, Tabora Tanzania
Kanisa la Seminari Kuu la Kipalapala, Tabora Tanzania

Akizungumza na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari,(FIDES) mahali ambapo Yeye mwenyewe alikuwa na  utume wake kama Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji  wa Watu hadi miaka ya hivi karibuni alipochaguliwa kuwa Askofu Mkuu wa Tabora na hatimaye kuchaguliwa kuwa Kardinali, alisisitiza kwamba: “Kama nilivyoeleza, Seminari inahudumia maeneo yote ya kikanisa ndani ya Tanzania na wakati mwingine pia kuna waseminari kutoka nchi jirani, pamoja na washiriki wa taasisi za kitawa na jumuiya za maisha ya kitume. Kwa njia hiyo Jimbo kuu la Tabora limekuwa na mchango mkubwa katika uwepo na ukuaji wa Seminari hii.”

Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Tabora Tanzania
Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Tabora Tanzania

Askofu Mkuu wa Tabora kwa namna fulani ni mlezi wake kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania,(TEC) pamoja na kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi. Kwa hiyo alisema kuwa:  “Kiukweli mimi binafsi ninashirikiana na washirika wangu na waamini katika shughuli na matukio mbalimbali kwa kuzingatia maandalizi ya Maadhimisho ya Miaka 100 ambayo yatafanyika katika nusu ya pili ya mwaka ujao (2025) na ambayo tayari yanaendelea.” Kwa kuongezea zaidi alisema: “Tunamwomba Mungu mwema abariki juhudi zetu ili Maadhimisho ya Miaka mia moja yawe chemchemi ya maisha mapya na ukuaji wa ufundi unaolenga kupata watumishi bora na wajao wa Kanisa kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania na mahali pengine.”

Shughuli za Seminari Kuu Kipalapala

Hata hivyo hivi karibuni, mwandishi wa Vatican News akitembelea maeneo ya Seminari Kuu Tabora aliweza kuona maandalizi ya kiroho  kwa ajili ya Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari Kuu hiyo, ambapo kwa hakika ni waseminari walioko katika  maandalizi ya Ukuhani, na waamini wanaozunguka maeno hayo. Maisha yao katika seminari, yanajikita katika shughuli mbali mbali kuanzia na sala, misa, masomo, tafakari, binafasi, kuabudi na vile vile katika shughuli za nje ambazo ni za kawaida kwa kila aliye katika seminari za kiafrika mbali na seminari za kiulaya au labda kwingineko.

Miti ya maembe iliyopandwa na wamisionari wa kwanza huko Tabora
Miti ya maembe iliyopandwa na wamisionari wa kwanza huko Tabora

Seminari kuu ya Tabora, ina mashamba makubwa ya kilimo, bustani za mboga mboga, na zaidi, cha kufurahisha ni mifungo mingi kama vile: Ng’ombe, kuku, na nguruwe! Pamoja na waseminari hao , Mapadre walezi wao, pia wapo Masista wanaotoa huduma hapo na wafanyakazi ambao wanashirikiana bega kwa bega katika kuhakikisha utume huo wa Kanisa, hasa katika malezi na makuzi ya  kiroho na kimwili ya vijana yanakwenda vizuri ili wapate kuwa hodari wa kulitangaza Neno la Bwana kwa watu ambao walitoka huko na  watarudi huko huko kwa namna fulani wamebadilika, lakini bado wakiwa ni watu watakatifu wa Mungu waliowekwa wakfu na kwenda kuwatumikia  watu watakatifu wa Mungu.

Seminari Kuu Nchini Tanzania  

Ikumbukwe kwamba mnamo 2021  Kanisa Katoliki nchini  Tanzania lilianza mchakakato wa kufanya mabadiliko ya utoaji Elimu katika Seminari Kuu za Kanisa Katoliki za Falsafa na Taalimungu, wengi wanatambua kama (Teolojia), kwa kuziingiza kwenye mfumo wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na mfumo wa Elimu ya Ngazi za Juu duniani. Hayo yalithibitishwa na Makamu  Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Flavian Kasala,  wa Jimbo Katoliki la Geita, wakati wa mahojiano na kurugenzi ya mawasiliano ya  Baraza la Maaskofu TEC, jijini  Dar es Salaam.  Sababu za mabadiliko hayo yalikuwa ni kutii maombi Baba Mtakatifu, Francisko; ambaye  aliomba kubadili mfumo wa Seminari zote kuu katika ngazi zote za Falsafa na Taalimungu, ili kuingia katika mfumo wa Vyuo vya Elimu ya juu, tofauti na mfumo wa awali ambapo seminari hizo zilizokuwa ni taasisi za kidini, zikijihusisha zaidi na malezi ya Mapadre, katika hatua ya Falsafa na Taalimungu. (Rej.Costituzione Apostolica Veritatis gaudium yaani Katiba ya Kitume ya Papa Francisko ya Furaha ya Ukweli iliyochapishwa mnamo tarehe 29 Januari 2018.

Kanisa Kuu la Tabora nchini Tanzania
Kanisa Kuu la Tabora nchini Tanzania

Kwa upande wa Kanisa Katoliki nchini  Tanzania, kuna Seminari Kuu saba, ambazo ni Kibosho (Moshi), Ntungamo (Bukoba,) Segerea(Dar es Salaam,) Nazareth Mwendakulima(Kahama), Jordan  (Morogoro), Peramiho (Songea) na Kipalapala (Tabora.) Tangu kufanyika mabadiliko mfumo wa Seminari Kuu uliokuwa ukitumika nchini Tanzania ambao ulikuwa hautambuliwi na Mfumo wa Vyuo Vikuu vya Kipapa vilivyopo Ulaya,  na mbapo  sasa unawezesha tayari hata mwanafunzi anatoka katika mafunzo ya  Taalimungu kutoka Tanzania kuja Vyuo Vikuu vya Ulaya kutambuliwa moja kwa moja bila kurudia masomo.

Je wajua Majiundo ya Kikuhani?

Katika majiundo ya Upadre, tangu kuhitimu kidato Cha VI, Mhusika anapaswa kusoma Falsafa ambayo ni miaka mitatu, halafu Taalimungu ambayo ni miaka minne na mwaka mmoja wa Kichungaji, jumla miaka nane, Utaratibu huo pia unategemea na walezi wakuu kama maaaskofu na wakuu wa Mashirika katika majiundo yao ya mashirika, na hivyo  miaka inaweza kuwa zaidi kabla mseminari hajawa Padre. Hata hivyo kwa  mujibu wa Katiba ya Veritatis Gaudium ya Papa Francisko Vitivo vya Falsafa na Taalimungu mtahiniwa anajifunza hayafuatayo:

Mtaala wa masomo ya Kitivo cha Taalimungu ni pamoja na:

a) mzunguko wa kwanza, wa kitaasisi, ambao hudumu kwa kipindi cha miaka mitano au mihula kumi, au kwa kipindi cha miaka mitatu au mihula sita, ikiwa kipindi cha miaka miwili ya falsafa inahitajika kabla yake. Miaka miwili ya kwanza lazima ijikite zaidi katika elimu dhabiti ya falsafa ambayo ni muhimu kushughulikia ipasavyo somo la taalimungu. Shahada iliyopatikana katika Kitivo cha Falsafa ya kikanisa inachukua nafasi ya kozi za mzunguko wa kwanza wa falsafa katika vitivo vya taalimungu. Shahada  katika Falsafa iliyopatikana katika kitivo kisicho cha kikanisa haijumuishi sababu ya kumfukuza kabisa mwanafunzi kutokana na  kozi za mzunguko wa kwanza wa falsafa katika vitivo vya taalimungu. Taaluma za kitaalimungu lazima zifundishwe kwa namna ya kuwasilisha ufafanuzi wa kiungo cha  mafundisho yote ya Kikatoliki, pamoja na utangulizi wa mbinu ya utafiti wa kisayansi. Mzunguko huo unaisha na shahada ya kitaaluma ya Shahada au nyingine inayofaa, itakayobainishwa katika Kanuni  za Kitivo.

Kardinali Rugambwa akiwa katikati ya watawa wanaoishi jijini Roma
Kardinali Rugambwa akiwa katikati ya watawa wanaoishi jijini Roma

b) Mzunguko wa pili, wa utaalam, ambao hudumu kwa miaka miwili au mihula minne. Ndani yake, taaluma fulani hufundishwa, kulingana na asili tofauti ya utaalamu, na semina na mazoezi hufanyika ili kupata uwezo wa kufanya utafiti wa kisayansi. Mzunguko huo unaisha na shahada ya kitaaluma ya leseni maalum.

c) Mzunguko wa tatu ambapo mafunzo ya kisayansi yanakamilishwa kwa muda unaofaa, hasa kupitia utayarishaji wa tasnifu ya udaktari. Mzunguko huo unaisha na digrii ya kitaaluma ya Udaktari.

Kifungu cha 75. §1. Ili mtu ajiandikishe katika Kitivo cha Taalimungu, ni muhimu kuwa amekamilisha masomo ya masharti, kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha Katiba hiyo. §2. Ambapo mzunguko wa kwanza wa Kitivo ni wa miaka mitatu, mwanafunzi lazima awasilishe cheti cha kipindi cha falsafa cha miaka miwili, kilichokamilishwa ipasavyo katika Kitivo au Taasisi ya falsafa ya kikanisa iliyoidhinishwa.

Kardinali Rugabwa siku ya kukabidhiwa hati ya utambulisho wa kuwa Kardinali
Kardinali Rugabwa siku ya kukabidhiwa hati ya utambulisho wa kuwa Kardinali

Kifungu cha 76. §1. Ni kazi ya pekee ya Kitivo cha Taalimungu kutunza mafunzo ya kitaalimungu ya kisayansi kwa wale wanaoelekea kwenye upadre na wale wanaojiandaa kutekeleza majukumu maalum ya kikanisa; kwa sababu hiyo ni lazima kuwe na idadi inayofaa ya walimu wa makuhani. §2. Kwa ajili hiyo pia kuna taaluma maalum zinazofaa kwa waseminari; Hakika, "Mwaka wa Kichungaji" unaweza kuanzishwa ipasavyo na Kitivo chenyewe ili kukamilisha mafunzo ya kichungaji, ambayo yanahitajika, baada ya kukamilika kwa kipindi cha kitaasisi cha miaka mitano, kwa upadre, na inaweza kuhitimishwa kwa kutoa Diploma maalum.

Kitivo cha Kifalsafa

Kifungu cha 81. §1. Kitivo cha kikanisa cha Falsafa kina lengo la kuchunguza kwa kina matatizo ya kifalsafa na, kwa kuzingatia urithi halali wa kudumu wa kifalsafa (rej. Optatam totius, 15: AAS 58 [1966], 722), ya kutafuta suluhisho lake katika nuru ya kawaida ya sababu, na zaidi ya hayo, kuonesha mshikamano wao na maono ya Kikristo ya ulimwengu, ya mwanadamu na ya Mungu, yakionesha uhusiano kati ya falsafa na taalimungu. §2. Kisha inalenga kuwaelimisha wanafunzi, ili kuwafanya kufaa kwa kufundisha na kufanya shughuli nyingine zinazofaa za kiakili, pamoja na kukuza utamaduni wa Kikristo na kuanzisha mazungumzo yenye matunda na Watu  wa wakati wao.

Kifungu  cha 82. Mtaala wa masomo wa Kitivo cha Falsafa ni pamoja na: a) mzunguko wa kwanza wa kitaasisi, ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu au mihula sita, kuna udhihirisho wa kiungo cha  sehemu mbali mbali za falsafa, ambazo zinahusika na ulimwengu, mwanadamu na Mungu, na vile vile historia ya falsafa, kwa kuanzisha mbinu za kazi ya kisayansi; b) Mzunguko wa pili, au utaalam wa awali, ambapo, kwa miaka miwili au mihula minne, kupitia taaluma maalum na semina, tafakari ya kina ya falsafa imeanzishwa katika sekta fulani ya falsafa; c) mzunguko wa tatu ambao, kwa kipindi cha angalau miaka mitatu, mafunzo ya kisayansi yanakamilika, hasa kupitia maandalizi ya tasnifu ya udaktari.

Kifungu cha 83. Mzunguko wa kwanza unaishia na shahada ya  pili na Leseni maalum, na tatu ni Shahada ya Uzamivu.

Kifungu cha 84. Kujiandikisha katika mzunguko wa kwanza wa Kitivo cha Falsafa ni muhimu kukamilisha masomo ya masharti, kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha  Katiba hiyo  ya Kitume. Ikiwa mwanafunzi, ambaye amemaliza kwa mafanikio kozi za kawaida za falsafa katika mzunguko wa kwanza wa kitivo cha taalimungu, basi anataka kuendelea na masomo yake ya falsafa ili kupata Shahada katika kitivo cha kikanisa cha falsafa, kozi zinazohudhuriwa wakati wa njia iliyotajwa hapo juu lazima zizingatiwe kwa makini.

Kardinali Rugambwa katika Seminari Kuu ya Kipalapala Tabora Nchini Tanzania
11 June 2024, 16:11