Ask.Sorrentino,Acutis:tarehe ya kutangazwa mtakatifu itaamuliwa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
“Tuna furaha kwamba Papa ametangaza, pamoja na watakatifu wengine wengi, kutangazwa mtakatifu kwa Mwenyeheri Carlo Acutis, ambaye masalia yake yamehifadhiwa katika mahali Madhabahu ya kujivua nguo kwa Mtakatifu Francis huko Assisi. Tarehe bado haijaamuliwa, lakini tuna hakika kwamba Baba Mtakatifu atataka kuchagua tukio muhimu, tufikirie labda katika mwaka ujao wa Jubilei, ili ushuhuda wa Carlo wetu uendelee kugusa dhamiri, hasa za vijana na barubaru lakini pia kuweza kuamsha upendo mkuu kwa Yesu wa Ekaristi na shauku kuu ya utakatifu katika nyayo zake na za watakatifu waliomtia moyo, katika njia maalum ya Francis wa Assisi”. Haya yalisemwa na Askofu wa majimbo ya Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino na Foligno, Askofu Domenico Sorrentino kuhusiana na Baraza la Makardinali lililofanyika Jumatatu tarehe 1 Julai 2024 ambapo Papa aliamuru kwamba mwenyeheri Manuel Ruiz López akiwa na wenzake saba, Francesco Mooti na Raffaele Massabki, Giuseppe Allamano, Marie-Léonie Paradis na Elena Guerra wataandikishwa kwenye Kitabu cha Watakatifu Dominika tarehe 20 Oktoba 2024, wakati Mwenyeheri Carlo Acutis atakuwa kwenye tarehe itakayoamuliwa.
Kanisa la Assisi linafanya kukaribisha mahujaji wanaozidi kuongezeka
Kupitia habari za kidini za Baraza la Maaskofu Italia ( SIR) zinabainisha kuwa Askofu wa Assisi amesema kuwa “Katika miezi hii Kanisa letu la Assisi litafanya kila liwezalo kuwakaribisha mahujaji na wamini wengi wanaoongezeka ulimwenguni. Francis na Carlo kwa pamoja ni timu ya kipekee ya kutangaza Injili, wakionesha ukweli wa kile ambacho Mwenyeheri Carlo alipenda kuwaambia vijana: 'Ni Yesu pekee ndiye anayeweza kutengeneza nakala asili na sio fotokopi, akijaza maisha yetu kwa furaha. Askofu Sorrento aliongeza kusema: “Kitabu ninachochapisha upya (Chanzo cha asili si nakala, Carlo Acutis na Francis wa Assisi, Matoleo ya Wafransiskani wa Kiitaliano) kilichounganishwa na kuongezwa itaoneshwa kwa uthabiti, lakini hata zaidi inaoneshwa na nyuso za vijana na mahujaji wanaotazama ndani ya mahali patakatifu petu na kutoka katika kuwasiliana na Masalia ya Carlo kwa kuvuka mlango wa Fransis wanahisi kusukumwa kukagua uwepo wao katika mwelekeo wa Injili. Mahali hapa haraka pamekuwa volkano ya kweli inayolipuka kwa neema na utakatifu.” Alihitimisha Askofu.
Muujiza uliopelekea Acutis awe Mtakatifu ni wa kijana Valeria
Ikumbukwe mwishoni mwa mwa Mei, Papa Francisko alitambua muujiza mpya wa Carlo Acutis, akiidhinisha Baraza la Kipapa la Mchakato wa kuwatangaza Watakatifu kuchapisha amri inayohusiana na muujiza huo. Muujiza wenyewe ulimfikia Valeria, mwanamke kijana kutoka Costa Rika na mwanafunzi wa chuo kikuu huko Firenze, Italia , ambaye mnamo Julai 2022 alianguka kutoka katika baiskeli yake na kuishia kukosa fahamu. Huko Careggi walimgundua na jeraha mbaya sana la kichwani, muda wake wa kuishi ulikuwa mbali sana. Siku sita baadaye, mama yake Liliana alikwenda Assisi ili kumpendekeza binti yake kwa Mwenyeheri Carlo na akatumia siku nzima kupiga magoti mbele ya kaburi lake. Jioni alipokea simu kutoka hospitalini ikimjulisha juu ya uboreshaji wa ghafla na usioelezeka wa binti yake: Valeria alikuwa ameanza kupumua tena peke yake, siku iliyofuata alianza kupata nafuu na kuzungumza kidogo.
Muujiza wa kutangazwa mwenyeheri ni kupona kwa mtoto wa miaka 6
Mnamo Septemba, pamoja na mama yake, Valeria alifika Assisi kusali kwenye kaburi la Carlo na kutoa shukrani kwa muujiza aliopokea. Mnamo 2020, Carlo Acutis alikuwa tayari ametangazwa kuwa Mwenyeheri na Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu ambalo lilikuwa limechunguza muujiza wake mwingine, ambao ulifanyika mnamo Oktoba 2013 katika Kanisa la Mtakatifu Sebastiani huko Campo Grande, nchini Brazili hasa baada ya kugusa masalio ya kijana, kipande cha shati juu ya mwili wake, mtoto mwenye umri wa miaka sita aitwaye Matheus, ambaye alikuwa na matatizo makubwa ya kongosho, alikuwa mzima kabisa na kupona.