Tafuta

Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo: “Masista wa Vyombo vya Upashanaji Habari” kwa mwaka 2024 wanasherehekea miaka 109 ya maisha na utume wao katika mchakato wa uinjilishaji Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo: “Masista wa Vyombo vya Upashanaji Habari” kwa mwaka 2024 wanasherehekea miaka 109 ya maisha na utume wao katika mchakato wa uinjilishaji  

Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo: Miaka 109 ya Uinjilishaji

Tarehe 29 Juni 2024 Mabinti wa Mtakatifu Paulo, Jimbo kuu la Dar es Salaam waliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kumshukuru Mungu kwa kupandishwa hadhi na kuwa sasa Kanda ya Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo, sanjari na uzinduzi wa Nembo ya Shirika na Utume wa Shirika. Ibada iliongozwa na Padre Patrick Musumba akisaidiana na Padre Dennis Wigira, Dekano wa Dekania ya Mtakatifu Yosefu na Padre Dominic Mavula, C.PP.S, Mkurugenzi, Matangazo: RM.

Na Daniel A. Ling’wentu, - Dar Es Salaam & Sr. Roselyne Wambani Wafula, fsp. – Vatican.

Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo, pia wanajulikana kama “Masista wa Vyombo vya Upashanaji Habari” kwa mwaka 2024 wanasherehekea miaka 109 ya maisha na utume wao katika mchakato wa uinjilishaji kwa kutumia vyombo vya mawasiliano ya jamii. Shirika hili lilianzishwa kunako mwaka 1915, nchini Italia na Mwenyeheri James Alberione pamoja na Sr. Tecla Merlo kama mwanzilishi mwenza, linavuma kwa njia ya kipekee katika Kanisa kwa jinsi linavyojihusisha na ulimwengu wa maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano kama sehemu ya maisha na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa. Ni katika muktadha huu, tarehe 29 Juni 2024 Mabinti wa Mtakatifu Paulo, Jimbo kuu la Dar es Salaam waliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kumshukuru Mungu kwa kupandishwa hadhi na kuwa sasa Kanda ya Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo, sanjari na uzinduzi wa Nembo ya Shirika na Utume wa Shirika. Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Padre Patrick Musumba wa Shirika la Marian Hill, akisaidiana na Padre Dennis Wigira, Dekano wa Dekania ya Mtakatifu Yosefu ambaye pia ni Paroko wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu Jimbo kuu la Dar es Salaam pamoja na Padre Dominic Mavula, C.PP.S., Mkurugenzi wa Matangazo Radio Maria Tanzania.

Ibada ya Misa takatifu ikiendeshwa na Padre Patrick Musumba.
Ibada ya Misa takatifu ikiendeshwa na Padre Patrick Musumba.

Mabinti wa Mtakatifu Paulo wamebobea katika vyombo vya mawasiliano ya jamii. Wanaendesha Vituo vya Elimu ya Mawasiliano ya Jamii, Idhaa za Radio wako pia kwenye mitandao ya kijamii. Mabinti wa Mtakatifu Paulo wametakiwa daima kusoma alama za nyakati ili waweze kuwa mstari wa mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Mwenyeheri James Alberione hakuwa kipofu kuona ushawishi uliokuwepo wa vyombo vya habari. Aliona nguvu ya vyombo vya upashanaji habari na teknolojia zinazoibuka katika kuunda maoni ya umma, kama mwelekeo ambao ungeweza kutumika kwa manufaa ya wote. Bega kwa bega alishirikiana na Mama Thecla Merlo, Sista ambaye alikuja kuwa Mkuu wa Kwanza wa Shirika. Akiongozwa na kuvuviwa na Roho Mtakatifu katika roho ya Mtume Paulo, mjumbe wa imani thabiti, Mwenye heri Alberione alianzisha Shirika la Wamisionari wa Mtakatifu Paulo (La kiume) na Mabinti wa Mtakatifu Paulo. Dhamira yao: Kutumia njia zote zilizopo za upashanaji habari za kijamii ili kumpeleka Kristo ulimwenguni. Kama vile Alberione mwenyewe alivyotangaza, "Lazima uwe Mtakatifu Paulo anayeishi leo," na Mabinti wa Mtakatifu Paulo wanajumuisha roho hii katika uhalisia wa maisha yao.

Mabinti wa Mtakatifu Paulo wakizindua Neno ya maisha na Utume wao
Mabinti wa Mtakatifu Paulo wakizindua Neno ya maisha na Utume wao

Msingi wa Maisha ya kiroho ya Mabinti wa Mtakatifu Paulo unajikita katika kujitolea kwao kwa Yesu Kristo, ambaye kwao, ni Mwalimu, Njia Ukweli na Uzima. Wanapata msukumo kwa Mtakatifu Paulo, Mtume, wakimwona kuwa kielelezo cha utume wao. Maria, Malkia wa Mitume, pia ana nafasi ya pekee katika shirika lao. Ekaristi ina nafasi ya pekee na ibada za misa kila siku huimarisha msingi wao. Walau lisaa limoja la kuabudu huwaruhusu kuombea kwa njia ya pekee ulimwengu mzima Pamoja na nia zao. "Mabinti wa Mtakatifu Paulo huendesha maduka vya vitabu ulimwenguni kote, na kuvigeuza kuwa vituo vya nuru na ukweli," Vituo hivi ni sehemu ya kukutana na nyenzo za imani, kushiriki katika mazungumzo ya maana, na kujisikia nyumbani, katika Kristu. Je, wangapi wanajua kwamba kila duka la vitabu linaloendeshwa na Masista hawa kina Kikanisa cha kuabudia Ekaristi Takatifu? Kila mmoja wao hupata fursa, katika ‘ubize’wao, walau kumwabudu Yesu wa Ekaristi kwa saa nzima kwa kupokezana. Kama Shirika, wanaamini kwamba “Baada ya sala huja utume," "na baada ya utume, sala huwasaidia kuchota ari na nguvu mpya ya kuchakarika kwenye utume.

Mabinti wa Mtakatifu Paulo wakisherehekea kumbuzi ya nadhiri na utume
Mabinti wa Mtakatifu Paulo wakisherehekea kumbuzi ya nadhiri na utume

Sala, Utume, masomo na maisha ya Jumuiya ni nguzo katika wito wao. Katika kipindi cha majiundo kwenye safari ya kuja kufunga nadhiri zao, na wakati mwingine baada ya nadhiri, wao hupata masomo ya falsafa, taalimungu, mawasiliano na mengineyo kama sehemu ya kuwaandaa kuelewa ulimwengu na changamoto zake. Utume wao unapelekea wao kukutana na kuhudumia watu kutoka matabaka mbalimbali ya maisha. Hivyo, inawapasa kuwa na maandalizi ya kutosha ili kukidhi mahitaji ya kila mmoja katika uhalisia wake. Maisha na utume wao wa kila siku, huwawezesha kuelewa zaidi nguvu na athari ya vyombo vya upashanaji habari na uwezekano wake wa kueneza Injili kwa ufanisi. Mwezi Juni una umuhimu maalum kwa Mabinti wa Mtakatifu Paulo. Tarehe 29 Juni ni Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume na miamba wa imani. Wakati Sherehe hii huadhimishwa na waamini kote ulimwenguni, tarehe 30 Juni ya kila mwaka huwapa nafasi ya kumsherehekea Mtakatifu Paulo kishirika. Mwezi huu wa Juni ni wa furaha. Walio wengi kama sio wote, huweka nadhiri zao kati ya hizi Juni 29 na Juni 30. Wengi wao husherehekea kumbukizi ya nadhiri zao shirikani. Sr. Mmoja kutoka Argentina mwaka huu, Juni 30, ameweka nadhiri za daima, akishuhudia kujitolea kwake kwa uthabiti. Isitoshe, manovisi kadhaa kutoka nchi za Angola, Congo DRC, Zambia, na Kenya, wameweka nadhiri zao za kwanza, mnamo Juni 30, 2024! Pongezi za dhati ziwaendee Mabinti wote wa Mtakatifu Paulo wanaoadhimisha kumbukizi zao, hususani wanajubilei wa miaka 25, 50 na 60 za utawa wao!

Wafanyakazi wa Duka la Vitabu, St. Joseph, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Duka la Vitabu, St. Joseph, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Kabla ya nadhiri za daima, kama sehemu ya maandalizi ya sherehe ya nadhiri za daima, Mabinti wa Mtakatifu Paulo hutembelea Parokia husika, anakotokea sista atakayeweka nadhiri za daima, na kufanya mambo mbalimbali, kwa mfano, kuzungumza na wanaparokia kuhusu shirika lao na sherehe ijayo ya sista kutoka parokiani kwao, kutafuta miito, kufanya semina za Biblia, kuhusu ujuzi na matumizi ya vyombo vya upashanaji habari na mengineyo. Zoezi hili huchukua kati ya juma moja hadi mwezi mzima kabla ya sherehe ya nadhiri za daima. Madhumuni ya hili zoezi ni mawili: kueneza ufahamu kuhusu Shirika, na kuwatia moyo vijana wanaotaka kujiunga na maisha ya kitawa.  Kushuhudia sherehe ya nadhiri moja kwa moja kunaweza kuwa cheche yenye nguvu, inayowasha ari na moto wa wito katika mioyo ya vijana wengi.

Kumbukizi za Jubilei za Mabinti wa Mt. Paulo
Kumbukizi za Jubilei za Mabinti wa Mt. Paulo

Marekebisho ya hivi majuzi ya nembo ya Vitabu na Vyombo vya Habari, pamoja na nembo mpya ya Shirika lenyewe, vinasisitiza na kudhihirisha dhamira yao ya "kusoma alama za nyakati" kwa ujasiri. Sista Anna Caiazza, Mama Mkuu, hivi majuzi aliwashirikisha masista wake ujumbe wenye nguvu na wenye kuchangamotisha, akisisitiza, "Hatuogopi mabadiliko; tunayakumbatia kama fursa ya ukuaji." Maoni haya yanahusiana sana na historia na wakati ujao wa shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo. "Nyinyi ni wabunifu kwa wito, mabadiliko haya ya mara kwa mara kwa kuzingatia dalili za nyakati kwenye mazingira ya vyombo vya habari, ni dalili nzuri" Sr. Anna Caiazza aliwakumbusha wanashirika. Kuadhimisha miaka 109 tangu shirika lilipoanzishwa, waliwasilisha dhana mpya ya mawasiliano inayoitwa "scrollytelling." Dk. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, alipongeza haswa hatua hii, akisema, "hii inaonesha uwezo wa Mabinti wa Mtakatifu Paulo kuwepo katika ulimwengu wa kisasa na lugha inayoeleweka kwa jamii ya leo." Sr. Anna Caiazza alieleza zaidi, "Tupo katika mabara yote na katika nchi zaidi ya 50...Katika Bara la Afrika, Mabinti wa Mtakatifu Paulo wamo katika nchi kumi na nne, zikiwemo, Kenya, Tanzania na Uganda. Tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu na kuendelea kuombea miito zaidi katika Shirika letu na Kanisa kwa ujumla. Endeleeni kuipa mabawa Injili ya Kristo Yesu; Mwalimu, aliye Njia Ukweli na Uzima!" Alisema Mama Mkuu wa Shirika, Sr. Caiazza. Wote wanaombwa kusali ili Bwana wa mavuno aendelee kutuma watenda kazi watakatifu, wenye bidii, juhudi na maarifa katika shamba lake la mizabibu.

Mabinti wa Mt. Paulo
01 July 2024, 15:00