Tafakari Dominika 14 ya Mwaka B wa Kanisa: Mwana wa Seremala
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Kwa jasho la uso wako utakula chakula…’ (Mwz 3:19) ni kauli ngumu kutoka kwa BWANA iliyofungua maisha ya kazi, jasho na damu ili kuishi. Tangu hapo mwanadamu amepasika kufanya kazi kama sehemu ya utu na heshima yake na pia utekelezaji wa neno hilo la BWANA kwa Adamu. Akina baba wa Kiyahudi walikuwa na wajibu wa kuwafundisha watoto wao ujasiri, utu, uzalendo, Torati na kazi. Familia tajiri waliwapeleka watoto kusomea fani mbalimbali Misri, Ugiriki na Roma, wengine waliwaweka watoto chini ya marabi, ila familia za kawaida zisizo na uwezo watoto walirithi kazi za baba zao. Mara nyingi ilisemwa ‘Baba asipomfundisha mwanawe kazi basi anamlea kuwa jambazi!’… Hivi watu wa Nazareti wanapomshangaa Kristo na kusema ‘huyu si seremala!’ walikuwa sawa sababu ndiyo ilikuwa kazi aliyojifunza kwa Yosefu baba yake kipindi cha ‘utoto’ wake kabla hajabatizwa na kuanza rasmi utume. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume “Redemptoris Custos” anasema: “Kama vile Mtakatifu Yosefu alivyochukua jukumu la kumtunza kwa upendo Bikira Maria na kwa furaha akajitoa katika kumtunza Yesu Kristo, vivyo hivyo ndiyo anavyolitunza na kuliangalia Fumbo la Mwili wa Kristo, Kanisa ambalo Bikira Maria ni mfano na kielelezo.” Nafasi hii ya Mtakatifu Yosefu inatekelezwa katika hali ya unyenyekevu na ukimya kabisa. Mtakatifu Yosefu anaonesha mfano bora kabisa kwa maisha yetu ya Kikristo. Daima hakusita kutimiza wajibu wake kama Baba wa familia. Pia alitimiza wajibu huu kwa uaminifu mkubwa kabisa hata katika mazingira ambayo yalikuwa ni magumu kueleweka. Tunasoma katika Injili jinsi alivyoangaika na Mama yetu Bikira Maria akiwa karibu naye kama mme wake mwaminifu wakati wa kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Mtakatifu Yosefu alijitoa mhanga kusafiri usiku kucha wakati wakimtorosha mtoto Yesu ili kuilinda familia hii takatifu ya Nazareti na mkono dhalimu wa mfalme Herode. Katika maisha ya familia kule Nazareti aliangaika kama Baba kuitafutia familia mahitaji yake ya kila siku na hii inathibitishwa na jinsi Kristo alivyojulikana kuwa ni “Mwana wa Seremala.”
UFAFANUZI: ‘Useremala’ ni neno la Kiajemi na Kiarabu likimaanisha ufundi ambao kimapokeo ulitegemea mbao lakini siku hizi hutumia vitu vingine kama metali na vioo. Mtu hujifunza kazi hii kwa kumsaidia seremala mzoefu na kwa sasa kuna vyuo vya fani hii. Katika Biblia maseremala ni pamoja na Nuhu aliyechonga safina kwa mti wa mvinje (Mwz 6:14), Bezaleli alichonga sanduku la Agano kwa mti wa mshita (Kut 37:1), maseremala walitengeneza Ikulu ya Mfalme Daudi kwa mbao za mielezi ya Lebanoni (2Sam 5:11), Hekalu la Mfalme Sulemani (1Fal 5:6, 18), wakalikarabati baada ya kutoka utumwani Babilonia (Ezra 3:7) Miongoni mwa kazi za useremala ilikuwa vifaa vya kilimo, ofisi, nyumbani na ujenzi. Hawakununua mbao ila walidondosha magogo na kutengeneza mbao kwa mashoka, nyundo, panga, misumeno (1Sam 13:20) na hivi miili yao ilikomaa na misuli kujengeka kiume. ‘Huyu si yule seremala!’ ilikuwa kauli ya dharau, kwamba wanamjua pamoja na mama na ndugu zake, kijana masikini ambaye hajasoma Misri au penginepo na hajafundishwa na rabbi yeyote hivi haya anayoyafanya ameyapata wapi? Pamoja na dharau hii useremala ilikuwa kazi muhimu hasa ukizingatia ufundi unaodhihirishwa katika hekalu lile kuu Yerusalemu na majumba ya serikali na wananchi. Baadhi ya makuhani walipaswa kujifunza useremala ili ikiharibika samani hekaluni mfano patakatifu pa patakatifu basi kuhani fundi aliruhusiwa kuingia ili kutengeneza hitilafu iliyojitokeza. Zaidi sana kazi hii ya Mtakatifu Yosefu imezipatia kazi zote heshima kuu tunavyosherehekea Mei Mosi kila mwaka hivi pamoja na kumdharau Kristo kwa kazi hii kwa upande mwingine wametoa heshima kubwa kwa kazi zetu za mikono.
Ndugu zake Kristo hawakumuunga mkono nyumbani kwake, walimsikiliza kwa masikio tu na sio kwa imani, walifunga macho ya akili zao wasitambue kuwa kati yao ni Masiha aliyesubiriwa kwa karne nyingi, wakamkwaza Kristo ‘akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao’ (Mk 6:6) na madhara yake ‘wala hakuweza kufanya muujiza wowote huko isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache akawaponya’ (Mk 6:5). Wengi tumebatizwa, tunasali na kushiriki mambo yote. Ushiriki wetu unaweza kupelekea kujisahau na kudhani tunamfahamu vema kama wale wanazareti na kuishi imani yetu kwa mazoea na kumkwaza Kristo. Lakini Je, ni kweli tunamfahamu Kristo? Kwamba ni Mwana wa Mungu sawa, na kwamba alisulibiwa, akafa na kufufuka ni kweli kabisa na tunaamini… Je, hii inatosha kusema tunamfahamu? Tumfahamuje basi? Ni kwa kujitambua wenyewe na uduni wetu mbele ya Mungu na mbele ya ulimwengu, kwamba sisi ni viumbe tu na hapa tutamtambua kama Mungu wetu, kwamba tu wadhambi na tutamtambua kama Mwokozi, kama raia katika ufalme wa mbinguni tutamtambua kama Mfalme. Tutambue kwamba ana uwezo wa kubadili maisha yetu na kutusaidia kukiri na kuiishi imani yetu kama Maria Magdalene, kwamba yupo mbinguni na anasikia sala yetu. Katika hili ni lazima tumsikilize, tufuate maongozi yake na tuige tabia zake, ndipo tutasema walau kidogo tumemfahamu. Kama Wanazareti walivyomkataa Kristo nasi huenda tunamkataa kwa namna tunavyoishi.
Mara kadhaa maisha yetu hayajampa Mungu utukufu, walaini kuhusu dhambi kiasi cha kushindwa kujizuia. Kama Kanisa huenda hatujatimiza wajibu zetu ipasavyo na hapa na pale kutenda nje ya lengo, kama taifa hatujawajali wote katika usawa, tofauti zetu zimetutenga… sera, sheria na kanuni hazijafaulu kumnufaisha mwananchi wa chini, kama familia hatujauishi upendo kwa viwango vya kimungu na kama mtu binafsi hatujawa na unyofu na utakatifu anaotarajia Kristo. Nabii Ezekiel katika somo la kwanza (2:2-5) anatukumbusha wajibu wa kusaidiana ili tuondokane na uasi wetu sababu sisi na baba zetu tumekosa juu ya Mungu. Naye Mtume Paulo katika somo II (2Kor 12:7-10) anatukumbusha kuwa tuna udhaifu mwilini mwetu na hivi tumtegemee Mungu ili tuwe na nguvu. ‘Huyu si Seremala’… tumwombe Seremala huyu wa Nazareti ili atusaidie tumtambue katika uhalisia wake, tulishike neno lake ili asitustaajabie kwa kutokuamini kwetu, useremala wa Kristo utupe shime ya kazi, ndio ‘mwibaji asiibe tena, bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia muhitaji (Efe 4:28). Mkristo hakikisha unakuwa miongoni wa wagonjwa wachache waliobahatika kupokea uponyaji nyumbani kwa Kristo Nazareti yaani ndani ya moyo wako.