Tafuta

Kristo Yesu alikuwa anahubiri na kufundisha kwa mamlaka kama anavyozungumza Mwenyezi, kwa kuganga, kuponya na kuokoa watu. Kristo Yesu alikuwa anahubiri na kufundisha kwa mamlaka kama anavyozungumza Mwenyezi, kwa kuganga, kuponya na kuokoa watu. 

Tafakari Dominika 14 ya Mwaka B wa Kanisa: Yesu Alikuwa Akizungumza Kwa Mamlaka

Yesu anazungumza kwa Mamlaka kama anavyozungumza Mwenyezi Mungu, kwani Yesu ni Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Mungu Mwana anayeganga, kuponya na kuwaokoa watu wake! Kristo Yesu alijipambanua kama mtu mwenye mamlaka katika kutenda, kiasi cha kutambuliwa na mtu mwenye pepo mchafu, kuwa ni Mtakatifu wa Mungu. Alihubiri kwa mamlaka, akaonesha umahiri wake, mafundisho yalikuwa yanabubujika kutoka katika undani wake!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 14 ya mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatueleza kuwa katika kutimiza mpango wake, Mungu anawachagua watu wa kawaida kabisa tunaowafahamu na kuyafahamu, mazuri yao, madhaifu yao, familia zao, wazazi wao, hata kazi na kipato chao. Hawa Mungu anawatuma kwetu watuletee ujumbe wake, neema zake, baraka zake na nguvu zake za kuokoa. Lakini kwa kuwa tunawafahamu na tumewazoea wakati mwingine tunawakataa na kuwadharua na hivyo kuukataa na kuudharau ujumbe wa Mungu ambao mwisho wake ni hukumu ya milele. Kristo Yesu anazungumza kwa Mamlaka kama anavyozungumza Mwenyezi Mungu, kwani Kristo Yesu ni Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Mungu Mwana anayeganga, kuponya na kuwaokoa watu wake! Kristo Yesu alijipambanua kama mtu mwenye mamlaka katika kutenda, kiasi cha kutambuliwa na mtu mwenye pepo mchafu, kuwa ni Mtakatifu wa Mungu. Kristo Yesu alihubiri kwa mamlaka, akaonesha umahiri wake kwamba alikuwa na mafundisho yaliyokuya yanabubujika kutoka katika undani wake na wala si kama waandishi waliotegemea mapokeo na sheria walizopewa. Mafundisho ya Kristo Yesu yalikuwa yanabubujika kutoka kwa Baba yake wa milele! Kumbe, Kristo Yesu alikuwa anahubiri na kufundisha kwa mamlaka kama anavyozungumza Mwenyezi, kwa kuganga, kuponya na kuokoa watu. Kristo Yesu ni utimilifu wa Unabii, kwani anasema na kutenda kila anachosema kwani kwa hakika ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake. Kwa njia hii, anazungumza akiwa na mamlaka ya Kimungu!

Kristo Yesu alikuwa akihubiri kwa mamlaka kwa sababu ni Nafsi ya Pili ya Utatu
Kristo Yesu alikuwa akihubiri kwa mamlaka kwa sababu ni Nafsi ya Pili ya Utatu

Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa wakati ambapo Injili Takatifu inatangazwa katika liturujia ya Kanisa, ili waamini waweze kuonja ile nguvu ya neno la Kristo Yesu. Hivi ndivyo pia inavyopaswa kuwa pale mwamini binafsi, anapojisomea Injili Takatifu, huku akiwa na moyo wazi, kwani hapo mwanga na nguvu ya Kristo Yesu inapenya, inajaliwa mema, inawaangaza, inawaponya na kuwafariji. Bikira Maria alibahatika katika maisha yake, kulihifadhi Neno la Mungu na kufuatilia kwa uaminifu na uwajibikaji mkubwa kwa matendo ya Kristo Yesu. Bikira Maria awasaidie waamini kumsikiliza na kumfuata Kristo Yesu, ili kuonja katika maisha alama za wokovu wake! Ili tusianguke katika hali hii, tufuate ushauri wa zaburi ya wimbo wa mwanzo wa kutafakari daima njia zake Mungu ukisema; “Tumezitafakari fadhila zake, ee Mungu, katikati ya hekalu lako. Kama lilivyo jina lako, ee Mungu, ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia. Mkono wako wa kuume umejaa haki” (Zab. 48:9-10). Ili tuweza kufanikiwa katika hili yatupaswa kujivika moyo wa unyenyekevu. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu, kwa njia ya unyenyekevu wake Mwanao umeuinua ulimwengu uliokuwa umeanguka. Uwajalie waamini wako furaha takatifu; uwapatie furaha za milele hao uliowaondoa katika utumwa wa dhambi.”

Watu walimtambua Kristo kwa Mahubiri na Utakatifu wa maisha yake
Watu walimtambua Kristo kwa Mahubiri na Utakatifu wa maisha yake

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Ezekieli (2:2-5). Somo hili ni ujumbe wa Mungu kwa Ezekieli anapomtuma kuwa Nabii kwa wana wa Israeli wakiwa uhamishoni Babeli. Katika ujumbe huu Mungu anamweleza Ezekieli hali halisi ya watu anaenda kuwapa ujumbe wake kuwa wana ugumu wa mioyo, ukaidi na uasi. Mungu anamwambia hivi Ezekieli; “Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli wanaoasi, walioniasi mimi, wao na baba zao wamekosa juu yangu. Na wana wao hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni mingumu.” Mungu anamwambia Ezekieli kuwa anapaswa kujua kuwa hawa watu wanaweza kumsikiliza au wasimsikilize akisema; “Na kwamba watasikia au kwamba hawataki kusikia, maana ndio nyumba ya kuasi”. Mungu alitambua kabisa kuwa watu hawa wana shingo ngumu. Lakini ni katika hao waliopotea anamtuma mjumbe wake ili awaokoe hao. Alifanya hivyo ili kwamba hata kama hawatabadilika, walau wajue wanalopaswa kufanya na kwa jinsi hiyo wanaweza kulaumiwa kwa sababu wameambiwa wanalopaswa kutenda, lakini hawakulitenda. Mungu hachoki kututumia ujumbe wake kwa njia ya watumishi wake hata tukiwa na mioyo migumu, waasi na tusiosikia bado anaendelea kuturudisha kwake. Ni juu yetu kuipokea au kuikataa neema hiyo. Lakini tutambue siku yaja, siku ya kiama ambapo kila mmoja atasimama mbele ya kiti cha hukumu ya haki ambapo tutaitamani hii neema tusiione. Kumbe wakati ndio sasa wa kuisikia sauti ya Mungu tusifanye migumu mioyo yetu. Bali tumuinulie Mungu macho ya mioyo yetu kwa sala na sadaka kama mzaburi anavyotuasa katika wimbo wa katikati akisema; “Nimekuinulia macho yangu, Wewe uketiye mbinguni. Kama vile macho ya watumishi, kwa mkono wa bwana zao. Kama macho ya mjakazi, kwa mkono wa bibi yake; hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu, hata atakapoturehemu. Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu sisi, kwa maana tumeshiba dharau. Nafsi zetu zimeshiba mzaha wa wenye raha, na dharau ya wenye kiburi” (Zab 122).

Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha
Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha

Somo la pili ni la Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (12:7-10). Somo hili ni ujumbe wa Paulo anaeleza kuwa licha ya udhaifu wake wa kibinadamu aliweza kuifanya kazi ya Mungu kwa neema tu. Kutokana na udhaifu wa mwili wake, Paulo alijifunza kwamba kufaulu kwake katika kazi ya kuhubiri Injili si mapato ya nguvu yake mwenyewe, bali ni neema ya Mungu. Tukiwa na neema hiyo taabu za mwili si kitu. Zaidi sana tukifanikiwa katika maisha, tusijivune, maana ni kwa neema ya Mungu tu tunafanikiwa. Ni busara kuwa tukifanikiwa katika maisha, tusinyanyua mabega juu kana kwamba ni kwa nguvu na uweza wetu tumefanikiwa. Tukifanya hivyo shetani anapata mwanya na nafasi ya kutupiga kisawasawa maana tunakuwa tumeikimbia neema ya Mungu inayotulinda dhidi ya mwovu. Basi na tujinyenyekeza mbele za Mungu ili neema yake ijidhihirishe katika maisha yetu nasi tutafanikiwa zaidi. Injili ni ilivyoandikwa na Marko (6:1-16). Sehemu hii ya Injili inatueleza ni kwa namna gani na sababu gani, watu wa Nazareti walishindwa kusadiki kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu. Ni kwa sababu alizaliwa kwao, akaishi nao kama mtu wa kawaida, na hivyo wakadhani wanamfahamu, kumbe walijihadaa wenyewe. Na sababu ya kudharauliwa kwa Yesu, na watu wa nyumbani kwake si nyingine bali ni kufahamika kwake na familia yake na jamaa yake yote. Ndiyo maana wanasema kuwa ni mwana wa seremala na wanawataja waziwazi ndugu zake na wazazi wake. Walikosa moyo wa unyenyekevu. Tukitaka kusadiki na kuelewa ufunuo wa Mungu, lazima tuwe wanyenyekevu, tufungue maacho ya mioyo yetu ili neema ya Mungu ituongoze, tuweze kutambua njia na namna anazozitumikia Mungu kujifunua kwetu na kuufunua mpango wake kwetu sisi wanadamu kwa kupitia watu tunaodhani kuwa ni wanyonge, dhaifu, na tunaowafamu.

Kristo Yesu alitangaza na kushuhudia huruma ya Mungu
Kristo Yesu alitangaza na kushuhudia huruma ya Mungu

Tukumbuke kuwa nyakati zetu Mungu anaendelea kututumia wajumbe wake; Maaskofu, Mapadre, Watawa, Makatekista, Viongozi wa jumuiya na vyama vya kitume, wengine ni wanafamilia ili watuambie tunayopaswa kutenda kwa wokovu wetu. Sio ajabu kwa kuwa tunawafahamu walikotoka, familia zao, wazazi wao na hata hali zao za kiuchumi, elimu yao, utamaduni wao, na hivyo tumewazoea kama waswahili wanavyosema; “mazoea huleta dharau, mazoea yana taabu” kwa hali hiyo tukawadharau na kushindwa kuupokea ujumbe wa Mungu. Mtume Paulo anatukumbusha kuwa Mungu anavichagua vilivyodhaifu ili aviaibishe vyenye nguvu. Hii ni faraja kwa wanaoitwa na kutumwa na Mungu kuwa msiogope, maana Yesu anatuambia; “Heri yenu ninyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila neno baya kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia, maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni.” Basi na tujinyenyekeshe mbele za Mungu, tusifanye migumu mioyo yetu, tusiwe watu wa shingo ngumu wasioelezeka, wakaidi na waasi. Bali tuweni wanyenyekevu tuisikie sauti ya Mungu inayotujia kwa njia ya wale anaowachagua, itusaidie tuweze kuishi vyema maisha ya hapa duniani kwa furaha, amani, upendo na utulivu, ili mwisho wayote tuupate wokovu wa uzima wa milele mbinguni kwa Mungu Baba. Ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu mama Kanisa anasali kwa matumaini haya akisema; “Ee Bwana, sadaka tunayotoa kwa heshima ya jina lako itutakase, na ituwezeshe siku kwa siku kutenda yafaayo kuleta uzima wa mbinguni”. Na katika sala baada ya komunio tunahitimisha maadhimisho ya dominika hii kwa moyo wa matumaini maana mama Kanisa anatuombea hivi; “Ee Bwana, sisi tuliojaliwa thawabu zako nyingi sana, tunakuoma utujalie fadhili zako za wokovu; tena tusichoke kamwe kukusifu." Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 14
03 July 2024, 14:23