Tafakari Dominika 15 Mwaka B wa Kanisa: Mitume Wanatumwa Kutangaza na Kushuhudia Injili
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 15 ya mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuelekeza kuweka tumaini kwa Mungu na kumtegemea yeye pekee tukiziendea ahadi alizotupatia yaani kuurithi uzima wa milele, maana tu wateule wake hata kabla ya kuumbwa ulimwengu. Hivyo, kumuona Mungu ni hamu ya daima ya mwanadamu wa nyakati zote. Ndivyo anaimba mzaburi katika wimbo wa mwanzo akisema; “Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, niamkapo nishibishwe kwa sura yako” (Zab 17:15). Hamu hii ndiyo inayomfanya mama Kanisa katika sala ya mwanzo atuombee akisali hivi; “Ee Mungu, wawaonyesha mwanga wa ukweli wako wale wanaodanganyika, ili waweze kurudia njia ya haki. Uwawezeshe wote wanaoshika imani ya kikristu wayakatae mambo yanayopingana na jina hilo, na kuyafuata yale yanayopatana nalo”. Somo la kwanza ni kutoka Kitabu cha Nabii Amosi (7:12-15). Ili kuulewa vyema ujumbe wake ni vyema kurejea kwanza kwenye mazingira yaliyopelekea ujumbe huu kutolewa. Historia inasimulia kuwa baada ya kifo cha Mfalme Solomoni mwanae Rehoboamu akawa mfalme. Lakini ni makabila mawili tu yaliyomtambua kama mfalme, na makabila mengine 10 yaliunda ufalme wao tofauti. Kwa hiyo kukawa na falme mbili: Ufalme wa Yuda, upande wa kusini chini ya Rehoboamu, makabila mawili na mji wake mkuu ukiwa ni Yerusalemu. Na ufalme wa Israeli, upande wa Kaskazini ukiwa na makabila 10 na mji wake mkuu ni Samaria. Falme hizi mbili daima ziligombana. Vita vilinukia kila wakati.
Hata hivyo wakati wote Yerusalemu ilibaki kuwa ni kitovu cha ibada kwa falme zote mbili. Lakini Mfalme wa Israeli upande wa kaskazini, aliona kuwa watu wake wakiendelea kwenda kuabudu Yerusalemu, makao makuu ya ufalme wa Yuda upande wa kusini ni hatari kwa ufalme wake. Hivyo alijenga hekalu Betheli ili watu wa ufalme wake waabudu huko. Betheli maana yake ni Nyumba ya Mungu/mahali patakatifu pa ibada. Ibrahimu aliabudu pale alipofika nchi ya ahadi (Mwa 12:8). Yakobo aliabudu pale alipokuwa anamkimbia ndugu yake Esau (Mwa 28: 18), na alipokuwa anarudi akiwa na familia yake baada ya kujipatanishwa na ndugu yake Essau (Mwa 35:3, 6). Kumbe, Betheli ikawa mahali patakatifu kwa ajili ya ibada kwa makabila 10 ya Kaskazini. Makuhani katika Hekalu la Betheli walilipwa na Mfalme. Amazia Kuhani alikuwa mmoja wapo. Makuhani na Manabii hawa walikuwa ni wa uongo na matapeli, maana walilifanya hekalu la Betheli kuwa mradi wao wa kujitajirisha. Mungu alimchagua Amosi kutoka Ufalme wa Yuda, upande wa kusini, na kumteua awe mhubiri katika Ufalme wa Israeli, upande kaskazini. Amosi akaisikia sauti ya Mungu akaenda kuhubiri katika Hekalu la Betheli. Ujumbe wake haukupokelewa vizuri. Zaidi sana makuhani walimpinga maana walio kibarua chao kinaota nyasi kwa mahubiri yake. Ndiyo maana Amazia anamwambia aondoke Bethel, kama ana njaa akatafute chakula kwa mfalme wake katika ufalme wa Yuda, akatabiri na kula mkate huko, na asitabiri tena Betheli. Amosi alivumilia yote, akiisikiliza sauti ya Mungu aliyemtuma.
Ni katika mukadha huu, Zaburi ya wimbo wa katikati inaasa daima tuisikilize sauti ya Mungu ikisema; “Ee Bwana utuonyeshe rehema zako utupe wokovu wako. Na nisikie atakayosema Mungu Bwana, maana atawaambia wake wake amani, hakika wokovu wake u karibu na wamchao, utukufu ukae katika nchi yetu. Fadhili na kweli zimekutana, Haki na amani zimebusiana. Kweli imechipuka katika nchi, Haki imechungulia kutoka mbinguni. Naam, Bwana atatoa kilicho chema, na nchi yetu itatoa mazao yake. Haki itakwenda mbele zake, nayo itazifanya hatua zake kuwa njia” (Zab. 84: 8-13). Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (1:3-14). Somo hili ni utenzi wa Mtume Paulo akimshukuru Mungu kwa sababu: alimtuma mwanae kwetu kutupasha habari za wokovu. Mungu ametutakasa kutoka dhambini kwa sakramenti ya ubatizo kwa zawadi ya Roho Mtakatifu anayetufanya kuwa wana na warithi wa uzima pamoja na Kristo. Kwa kutuwezesha kushiriki uzima huo tena tungali hapa duniani na baadaye katika ukamilifu wake huko mbinguni. Zaidi sana mtume Paulo anatuonesha aina sita za baraka zitokayo kwa Mungu: wito wa wateule kushiriki uzima wa wenye heri, hali ya watu katika kufanywa watoto wa Mungu, wokovu ulioletwa na Kristo msalabani, ufunuo wa siri ya mapenzi ya Mungu, uteule wa Israeli na mwito wa wapagani wapate pia kushiriki wokovu. Basi nasi tuwe na moyo wa shukrani kwa Mungu kwa mema yote anayotujalia katika maisha yetu yak ila siku. Injili ni ilivyoandikwa na Marko (6:7-13). Sehemu hii ya Injili inasimulia kuitwa na kutumwa kwa wale Thenashara, Mitume 12 wa Yesu. Mitume ndio msingi na nguzo za mafundisho ya Kanisa kwani wao ndio waliojifunza yote walioliachia Kanisa kutoka kwa Yesu mwenyewe.
Katika kuwatuma mitume, Yesu aliwapa uwezo wa kutenda miujiza kulikoambatana na kuhubiri Injili kwa watu wote. Katika kuwatuma Yesu alisisitiza mambo matatu katika kuenenda kwao; Kutangaza kuwa ufalme wa Mungu umekaribia, kuwaalika watu wafanye toba na kuachana dhambi, na kuukumbatia ufalme wa upendo wa Mungu. Katika utume wao, wasifungamane na watu au vitu. Katika hili anawaambia kwamba wasichukue mkate, wala fedha, nguo wala chochote, wamtegemee Mungu peke yake. Kazi yao kuu ni kufukuza pepo wachafu, na kuwaponya wagonjwa. Kiujumla tunajifunza kuwa Mungu ndiye anayechagua na kuwatumia manabii na wahubiri wa Injili. Wajibu wetu ni kuwapokea wale anaowachagua Mungu na kuwatuma kwetu kutuhubiria. Tukumbuke maneno ya Yesu Kristo kuhusu kuwapokea mitume na manabii akisema: “Anayewapokea ninyi, ananipokea mimi, na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma” (Mt 10:40). Paulo mtume anatushauri hivi; “Lakini ndugu, tunataka muwatambue wanaojibidisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana na kuwaonyeni, mkawastahi sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Iweni na imani ninyi kwa ninyi” (1Thes 5:12-13). Basi, tuwaombee wale wote wanaotetea wanyonge, wanaopigania haki na amani ya watu wote ili Mungu awazidishie matumaini wasikate tamaa, bali wasonge mbele wasirudi nyuma. Tuwaombee Mapadre na viongozi wa Kanisa, ili wawe tayari kutetea haki na ukweli na kuwaambia watu wanalopaswa kutenda. Mali na fedha visiwafunge midomo yao ili watufundishe kutenda haki na kuenenda katika upendo, umoja na amani tukiutumainia utakatifu na uzima wa milele anaotuombea mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu akisali; “Ee Bwana, tazama dhabihu za Kanisa lako liombalo. Nasi waamini wako utujalie tuzile tpate kuzidishiwa utakatifu”. Na katika sala baada ya Komunyo anahitimisha maadhimisho haya matakatifu akisali; “Ee Bwana, baada ya kuzipokea fadhili zako, tunaomba utuzidishie mapato ya wokovu wetu, kila tunapopokea fumbo hili”. Tumsifu Yesu Kristo!