Tafuta

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika 15 ya Mwaka B wa Kanisa: Toba, Faraja Na Wongofu wa Ndani

Mama Kanisa katika masomo ya dominika hii anatukumbusha kuwa kwa Sakramenti ya Ubatizo na kipaimara sisi sote tumeitwa kuihuburi Injili kwa kuishi ukristo wetu vyema sio kwa sheria za maumbile bali kwa kuwa viumbe vipya ndani ya Kristo na kuona fahari juu ya Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo ambao kwao tumekombolewa. Hii ni changamoto ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalodai waamini kutembea kwa pamoja, kusikilizana na kufanya mang'amuzi ya pamoja

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mungu anatuita kuwa manabii kama Amosi na wamisionari kama Mitume ili kuleta faraja juu ya huruma ya Mungu, kuwafungua na pepo wabaya, kuwapaka mafuta wagonjwa na kupoza mateso. Tuongozwe na neno hili “akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu.” Kama mwalimu mbobezi, Kristo anawapeleka wanafunzi ‘field’ kwa mazoezi. Ajabu anaagiza wasichukue chochote kwa safari, ila fimbo tu. Je, fimbo pekee ni msaada wa kuutumainia na kuaminika? Kadiri ya Kamusi ‘fimbo’ (bakora, gongo, henzirani, mkongojo) ni kipande cha mti kinachochongwa ili kushika, kutembelea, kupigia au kuchezea ngoma. Ni msaada kwa wasioona na pia uzeeni pale mtu aliyekuwa na uwezo wa kukimbia apendavyo sasa ameinama na kutegemea labda mguu 1 na fimbo, ouh! maisha ni fumbo kuu, Ee Mungu utupe unyenyekevu tuwapo bado vijana.

UFAFANUZI: Kibiblia fimbo ni ishara ya utawala, ukuu na mamlaka “fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda” (Mwz 49:10), adhabu “mwovu na alazwe chini na kupigwa kadiri ya uovu wake kwa kuhesabu, aweza kumpiga fimbo 40 asizidishe”(kumb 25:2-3), maonyo “fimbo na maonyo hutia hekima” (Mith 29:15), ghadhabu na mateso (Omb 3:1), kiburi (Eze 7:10), silaha (Mik 5:1), faraja wakati wa shida “gongo lako na fimbo yako vyanifariji” (Zab 23:4), kifaa cha kazi (1Sam 14:43, Isa 28:27).. uadilifu “na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili” (Ebr 1:8). Mnaikumbuka fimbo ya Musa? ya kawaida lakini yenye mambo: iligeuka nyoka mbele ya Farao (Kut 4:2), ikaigawa bahari ya Shamu (Kut 14:16), ikabubujisha maji mwambani na kuponya kiu ya watu na mifugo (Kut 17:5), ni ishara ya uwezo, nguvu na mamlaka ya Mungu. Mitume wa Yesu wanatakiwa wachukue hiyo tu yaani wasitegemee msaada mwingine. Fimbo hiyo ni Neno la Mungu hivi wajenge imani katika neno hilo “hai na lina nguvu tena lina ukali kuliko upanga ukatao kuwili, hukata kabisa mpaka mahali ambapo moyo na roho hukutana… li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo” (Ebr 4:12).

Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu
Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu

Utume wa kuhubiri toba, kukomboa na pepo wabaya, kupaka wagonjwa mafuta na kuwapoza ni muhimu kwa wote. Nia ipo na tungetamani kutekeleza ila tumefungwa na wajibu nyinginezo nje ya utume huu. Huenda hatujiamini, tuna hisia za kukosa usalama labda kwa sababu ya mifumo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Tunatafuta fedha ili tuwe na nguvu, tumejenga kuta na mageti na makomeo, bunduki na risasi tukihangaikia ulinzi na usalama. Yesu anatutaka tuchukue fimbo tu, kwani “Bwana asipoulinda mji waulindao wanakesha bure”(Zab 127:1) Mara si haba tumegombana, mipango haitimii, tumedanganywa, kuonewa na kudhalilishwa, labda sababu hatukufikia malengo yetu, mfano tulitegemea watoto wema tumepata wakorofi au hatujapata kabisa, tuna mali lakini hatuna furaha sababu hatuna mrithi, tumetenda dhambi na kukata tamaa ya kusamehewa, tumefikiri haiwezekani kupatana, ndugu wanasema sisi ni wachawi tunawaloga, wanatuaibisha na kutishia kutuua, tumefikiriwa vibaya na kusingiziwa mambo ya fedha, uongozi, mahusiano nk. Katika yote haya mkristo usichukue wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni, chukua fimbo tu… inakutosha! Fimbo hiyo ni nguvu ya Neno la Mungu, nguvu ya sakramenti za Kanisa, nguvu ya Msalaba, nguvu ya neema (2Kor 12:9).

Wakristo wanaitwa na kutumwa Kuinjilisha
Wakristo wanaitwa na kutumwa Kuinjilisha

Wafuasi wa Yesu walitumwa 2-2 na sio 1-1, kwamba umisionari ni kazi ya wote. Asitokee mmoja kwenye Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo mwenye neno la mwisho, anayekumbatia vyote na hivi kuwa fimbo ya chuma kwa wengine bali wanajumuiya waende 2-2 yaani wafanye kazi kwa ushirikiano, upendo na amani. Tuhubiri Injili ya Kristo ili watu watubu na kuiamini Injili, tusihubiri Injili nyingine au kujihubiri wenyewe. Tutoe pepo, ni agizo la BWANA, yaani tupambane kufa kupona na nguvu za ubaya, giza, udanganyifu, uongo na yote yanayotukosesha. Twende zetu tukatoe pepo! tunaweza? Au tunaogopa vinyamkera? Ndugu unayesoma ujumbe huu jiangalie kuna pepo nyuma yako, kivipi? Kama hamsalimiani, mnasengenyana, mnadhulumiana, mnapigana makwenzi, mnaaibishana, mna... Pepo la kwanza hilo, mahusiano mabaya, kemea! Una amani katika ndoa? inawezekana mumeo/mkeo mshirikina na ameishakulisha sana madawa. Amekosa utulivu, sio mwaminifu, zikipita siku 2 hujapigwa unashangaa. Ikipita wiki hujalipa madeni ya mwenzio unashangaa. Kwamba kati ya watoto wenu 5 ni 2 tu ndio wako. Anavaa pete ya ndoa nyumbani tu akitoka anaificha na kuwa huru na wazi kwa watu wote. Maisha yenu yanahitaji zaidi uvumilivu kuliko upendo… pepo la pili, kemea!

Wakristo wanaalikwa kuwa ni faraja kwa wale wanaoteseka
Wakristo wanaalikwa kuwa ni faraja kwa wale wanaoteseka

Vipi hudaiwi? kama una madeni ya chumvi na sukari dukani jihesabu una pepo. Jaribu kulipa ukae na amani. Usitumie ujanjaujanja na kauli zisizo na ukweli. Siku unakopa uliahidi nini na sasa unasema nini. Biashara ya mwenzako inalega sababu hulipi madeni, akifunga duka sote tutakosa huduma. Pepo wa madeni anakemewa kwa kulipa. Yupo pepo mbaya zaidi, ubaguzi. Huja kwa kauli za uzawa na ugeni “sisi ndio wenyeji hapa! Wewe wakuja! Utahama kijiji!” Tumkemee! Mwl. Nyerere alisema ‘binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja’. Katika somo I (Amo 7:12-15) Amazia anamfukuza Amosi kwa kigezo cha ugeni. Anamwambia hapa pana wenyewe na wenyewe ndio sisi, wewe mgeni ondoka tu... Inawezekana tuna hofu na wageni wa maeneo yetu, tunadhani wanatunyang’anya fursa. Lakini jamii yenye maendeleo ni ile yenye mchanganyiko, tunapochangamana na kushirikishana vipaji, tunapojifunza kwa wengine na kushindana kwa nia njema kisiasa, kiuchumi na kijamii ndio kukua na kusonga mbele. Basi tusibaguane, dhambi hii ni mbaya, sio utu, sio uafrika. Kama mimi ni mbaguzi basi namkemea pepo huyo tangu leo, apotelee mbali. Tukijibidiisha katika haya tutakuwa na utulivu wa akili, nafsi na roho na hivi tutasali vizuri, tutaaminiana, tutakuwa marafiki. Hapo tutaungana na Mt. Paulo katika somo la Pili (Efe 1:3-14) kusifu na kuabudu tukisema “Atukuzwe Mungu, Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho… ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo” … rafiki tuamke, “tusichukue chochote ila fimbo tu” safari iendelee!

Liturujia 15 Mwaka B
12 July 2024, 15:40