Tafakari Dominika 16 ya Mwaka B wa Kanisa: Huruma na Mapumziko
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 16 ya Mwaka B Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika ya 15B yalitueleza wajibu wa viongozi wa kiroho wa kuihubiri Injili kwa uaminifu na pia wajibu wa waamini wa kusikiliza na kuyaishi yale wanayofundishwa ili waweze kuufikia uzima wa milele. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele. Masomo ya dominika hii ya 16 B yanawaasa viongozi wa kiroho kujitoa kiaminifu, wakiwatumikia na kuwajali watu waliokabidhiwa na Mungu kuwaongoza, wasitafute maslahi binafsi. Wakifuata maongozi ya Kristo, daima waeneze ujumbe wa kudumisha amani na umoja katika Jumuiya walizokabidhiwa na kuwapa watu matumaini pale wanapokumbwa na ugumu wa kimaisha wakiwaelekeza kumtumainia Mungu daima. Ndivyo zaburi ya wimbo wa mwanzo inavyosisikitiza ikisema; “Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu. Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu; ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema” (Zab. 54:4, 6). Utume huu sio rahisi, unahitaji moyo wa uvumilivu, unyenyekevu na ujasiri. Ndiyo maana katika sala ya mwanzo mama Kanisa aliawaombea akisali hivi; “Ee Bwana, uwarehemu watumishi wako, uwazidishie kwa wema baraka za neema zako kwa moyo wa matumaini, imani na mapendo.
Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Yeremia (23:1-6). Somo hili ni makaripio ya Mungu kwa viongozi wazembe wa Israeli, ulisababisha maadili ya watu kuporomoka, kutenda dhambi na kumuasi Mungu. Matokeo ya dhambi zao ni mji wa Yerusalemu na Hekalu lililowakilisha uwepo wa Mungu kugeuzwa kuwa magofu na watu wake na viongozi wao kuchukuliwa mateka Babeli. Wachungaji waovu na potofu watakaopelekwa uhamishoni kama mateka, watakufa huko kwa sababu ya dhambi zao. Lakini Mungu atawakusanya watu wake kutoka pande zote za uhamishoni na kuwarudisha katika nchi yao na kuwapa wachungaji wapya, watakaowalisha na kuwaongoza katika malisho bora na kuwalinda kutokana na hatari zozote za adui. Wachungaji hao watachipuka kutoka katika shina la Daudi, na huko litatoka chipuki la haki, mwingi wa hekima, atakuwa mfalme wa haki na utakatifu. Wachungaji hao watakuwa na wasaidizi ambao watavikwa haki na utakatifu, na karama ya uongozi itakuwa mabegani mwao, ili amani, haki, upendo, na utakatifu vitawale Israeli. Katika kutoa ahadi hii, Mungu anawafananisha watu wa Israeli kama kondoo. Hii ni kwa sababu wengi wao walikuwa wachungaji hivyo walitambua dhamani ya mchungaji. Maandiko matakatifu yanasema wazi jambo hili. Mafano, Yosefu mwana wa Yakobo, akimpa Farao habari za ndugu zake anasema: “Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa Baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kaanani, wamenijia, na watu hao ni Wachungaji…nao wameleta kondoo zao, ng’ombe zao na waliyo nayo” (Mwa 46:31-32). Na walipotoka Misri kuelekea Kaanani chini ya uongozi wa Musa, pamoja nao walichukua kondoo, mbuzi, na ng’ombe wengi (Kut 12:38). Daudi kabla ya kupakwa mafutwa na Samweli kuwa mfalme alikuwa anachunga kondoo za Baba yake Yesse (1Sam 16:11-13).
Ni katika muktadha huu, tunapata Zaburi ya Bwana ndiye mchungaji mwema ambayo ndiyo zaburi ya wimbo wa katikati ikisema hivi; “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza, huihuisha nafsi yangu. Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita katikati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa maana Wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika. Hakika wema na fadhili zitanifuata, siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele” (Zab. 23). Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (2:13-18). Somo hili linatueleza kuwa katika Agano la Kale kulikuwa na tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi. Katika Agano jipya watu wote tumeunganishwa kwa njia ya Kristo mchungaji wetu mwema na mwaminifu aliyeutoa uhai wake kwa ajili yetu sote. Masimulizi yanasema kuwa katika Kanisa la Efeso, waamini wake wengi walitoka katika familia za watu wa mataifa wasio Waisraeli, familia za kipagani. Waamini kutoka familia hizi za makabila mengine walionekana kuwa duni mbele za waamini wa familia za kiyahudi. Ndiyo maana katika Hekalu la Yerusalemu kulikuwa na ukumbi wa Wayahudi na ukumbi wa watu wa mataifa walioongokea dini ya Kiyahudi. Ni wazi, watu wa mataifa hawakuruhusiwa kuvuka kwenda upande wa Wayahudi. Kuvunja sheria hiyo kuliendana na adhabu kali, ikiwemo kifo.
Paulo mtume wa Kimataifa anakemea tofauti hizi, akieleza kwamba; haijalishi unatoka katika kabila gani, unapoingia ukristo unakuwa kiumbe kipya. Kinachotuunganisha ni saramenti ya ubatizo inayotufanya sote kuwa familia. Maana kwa kifo cha Kristo, ukuta uliowatenganisha Wayahudi na watu wa mataifa umebomolewa. Hivyo basi, mgawanyiko, chuki, malumbano, mapambano na vita havipaswi kuwepo kati yetu sisi wakristo. Daima tunapaswa kupendana, kusaidiana na kuimarishana katika madhaifu yetu, kwa karama na vipawa tunavyojaliwa na Roho Mtakatifu ili tuweze kuhudumiana, kukamilishana na kujengana. Ni kwa matumaini haya mama Kanisa katika sala ya kubariki dhabihu anasali akiomba hivi; “Ee Mungu, ulihalalisha kafara mbalimbali za zamani katika sadaka hii moja iliyo kamili. Uipokee sadaka hii tunayokutolea sisi watumishi wako amini. Uibariki kama ulivyoibariki ile sadaka ya Abel, ili kitu alichokutolea kila mmoja wetu kwa kuuheshimu utukufu wako, kitufae sote kwa wokovu”. Injili ni ilivyoandikwa na Marko (6:30-34). Sehemu hii ya Injili inasimulia matunda ya kazi za mitume 12 aliowachagua Yesu ili waendeleze kazi ya kuujenga na kuusimika ufalme mpya wa Mungu chini ya Kristo Mchungaji mwema aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake. Mitume wanatoa taarifa ya mrejesho kwa kazi ya utume waliofanya wa kuihubiri Injili. Ingawa walikuwa wamechoka sana, walijawa na furaha kwani nguvu ya Kristo ilitenda kazi ndani yao. Yesu anawaambia wajitenge kidogo mahali pa faragha wapate kupumzimka. Kumbe, ni vyema kwa watenda kazi katika shamba la Bwana kujipa mda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea kutoa huduma vyema. Waamini wakiona wachungaji wamechukua muda wa kupumzika wanapaswa kuwasaidia na kuwawezesha ili wapate mazingira mazuri zaidi ya kupumzika vyema ili wapate nguvu na ari zaidi ya kuendelea kuwahudumia. Lakini ikitokea kuna huduma za dharura, kama vile mtu kuwa katika hatari ya kifo, wanapaswa kuahirisha mapumziko na kutoa huduma zinazohitajika kwa moyo wa huruma na mapendo.
Basi, tuombe neema za Mungu, tukimruhusu Roho Mtakatifu awe kiongozi wa wote ili tuweze kuisha kwa upendo na umoja na mwisho wa yote tukaurithi uzima wa milele Mbinguni. Ndivyo anavyosali na kutuombea mama Kanisa katika sala ya kuhitimisha maadhimisho kiliturujia katika sala baada ya kumunio akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uwe na sisi taifa lako. Na kama ulivyotujalia mafumbo haya ya mbinguni, utuondoe katika maisha ya zamani na kutuweka katika maisha mapya”. Na hili ndilo tumaini letu, kuisha maisha mapya mbinguni kwa Mungu Baba yetu. Tumsifu Yesu Kristo!