Kristo Yesu ni chakula cha uzima wa milele. Kristo Yesu ni chakula cha uzima wa milele.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 17 ya Mwaka B wa Kanisa: Yesu Ni Mkate wa Uzima wa Milele

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 28 Julai 2024 inayonogeshwa na kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Sala ya mkongwe “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9 anasema, inasikitisha kuona kwamba, watu wengi wanagundua wakiwa wamechelewa kwamba, walishindwa kuwatendea vyema wazee. Ekaristi Takatifu!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 28 Julai 2024 inayonogeshwa na kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Sala ya mkongwe “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9 anasema, inasikitisha kuona kwamba, watu wengi wanagundua wakiwa wamechelewa kwamba, walishindwa kuwatendea vyema wazee. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanawaonea huruma wazee, kwa kuwatembelea mara kwa mara na kuwatia moyo, wale waliovunjika na kupondeka moyo na hivyo kujikatia tamaa ya maisha; tayari kuwarejeshea tena matumaini katika safari ya maisha yao! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu kamwe hawatelekezi watoto wake, wala haangalii kama binadamu aangaliavyo na kwamba, kimsingi Maandiko Matakatifu ni simulizi la uaminifu wa upendo wa Mungu unaofumbatwa katika huruma katika kila hatua ya maisha hata katika uzee na kwamba, uzee kadiri ya Maandiko Matakatifu ni alama ya baraka. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9.

Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele
Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele

Nyakati za Kristo mkate ulikuwa chakula cha kawaida.  Neno “Lehem” lina maana ya chakula hivi mkate ulimaanisha chakula/riziki.  Mikate ilikuwa ya aina 2, ngano na shayiri. Utengenezaji wake ulianza kwa kusaga unga (Mt 24:41), uliwekwa hamira (Mt 13:33), unga ulioumuka ulikatwa vipande vidogo na kusambazwa juu ya jiwe la moto ili iokwe na kuliwa ingali moto. Wakati wa kula haikukatwa, ilimegwa kwa mkono na kuchovywa kwenye mchuzi. Kumpa mtu mkate uliolowekwa kwenye mchuzi ilikuwa ishara ya upendo na undugu (cf. Yesu na Yuda Iskariote) na haikuruhusiwa kutupa vipande vilivyobakia. Akina mama waliwapa watoto mikate na samaki wanapoenda shule au mahali popote pa kukaa muda mrefu, ndio maana mtoto wa Injili ya leo alikuwa na mikate 5 na samaki 2, upendo kwa watoto. KRISTO MKATE WA UZIMA, makutano wanamfuata kwa wingi ili kumsikiliza, ni nyikani wanapata njaa. Anawahurumia na kufanya muujiza akiongeza mikate na samaki. Huu ni mlo wa kisakramenti sababu una viashiria vya Karamu ya Mwisho alipoweka Ekaristi… anatwaa mkate, anashukuru na kuwapa, Kwake njaa si ‘issue’ bali neema tele na hakika ya maisha mradi tunasikia Neno lake. Neno hili limesikika katika somo I (2Fal 4:42-44) Nabii Elisha akifanya muujiza kama wa Injili akiwalisha watu mia mikate ishirini tu.

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

UFAFANUZI: Katika maisha tunapaswa kula chakula chenye kutupa uzima wa milele. Mara nyingi tumekikosa na kubaki njaa yaani tumeshindwa kutimiza wajibu. Inashangaza kuwa mkutano ule ulimfuata Yesu maili 9 bila kuchukua chakula na maji kama mtoto yule. Lakini inawezekana walikuwa na mikate ila hakuna aliyetoa, kila mmoja alijihifadhia mwenyewe. Yesu na Mitume hali wakitabasamu wanatoa kidogo kilichopo kwa ajili ya wote. Muujiza huu uliwabadili watu wachoyo na wabinafsi na kuwafanya jumuiya ya watu wamoja wanaoshiriki mkate mmoja, Yesu Kristo Bwana wetu. Hiyo ndio kazi ya Yesu, kukusanya na kutunza kinyume na ibilisi anayetawanya, kuharibu na kusambaratisha. Kristo angeweza kuwapa chakula bila kutumia kitu chochote cf. uumbaji (Mwz 1). Hata hivyo anatumia kidogo kilichopo mikononi mwao kutatua shida zao. Nasi tunapaswa kuwa na kitu mkononi cha kumpa ili akiongeze. Mfano haitoshi kusali ili tuache dhambi bila kujitahidi kwa dhati kuziacha. Kristo anajazia kutoka kidogo tulichonacho. Kama jumuiya vipaumbele vyetu ni vipi? Je, ni watu tunaopendana na kujaliana wakati wote? au wakati fulani tu? Mwanajumuiya anapokosea na kukanyaga vumbi na kuchafuka sisi tunamuonaje? Tunamsaidia aoge au tunamtimulia vumbi zaidi aabike na sisi kuonekana safi? Sisi sio sababu ya vumbi lao? Inawezekanaje mtu tunayeishi nae chumba kimoja, korido moja, meza 1, Kanisa 1, darasa 1 awe mchafu na sisi tuwe safi? Tatizo li wapi? Jumuiya ya hivi ina njaa na itakufa kwa utapiamlo. Tumpelekee Yesu nia zetu njema akaibadili mioyo yetu na kutujalia amani, umoja, maelewano na mshikamano… hii ndio maana ya ongezeko la mikate.

Dominika tarehe 28 Julai 2024 Ni Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee
Dominika tarehe 28 Julai 2024 Ni Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee

Jamii nyingi hii leo zinachechemea na ulimwengu unahadaika. Tupo nyikani hatuna mikate, njaa kali kila kona, hofu pande zote. Ni dunia iliyopoteza uzuri wa wakati wa uumbaji na kujivika magunia, imegeuka msitu huku wakaaji wake wakishindana daima, mwenye nguvu ndiye anaishi. Mwanadamu ni kama mnyama kwa mwenzake (homo homini lupus - a wolf to his fellow). Jua linakuchwa, ni jioni, dunia ina njaa. Je, wewe una njaa ya nini? Kuna njaa ya ‘amani’ (Rej. ugomvi, ukatili, uuaji) tunapochanganya amani na utulivu. Hatuwezi kusema tuna amani wakati wengi hawana hakika ya kesho, wanaishi chini ya sh. 1000 kwa siku, baridi kali, ongezeko la watu mijini, ombaomba ni wengi na wezi pia, ugumu wa maisha unapelekea mfano halisi binti zetu kufanya kazi za ndani zenye kuwadhalilisha kiutu na kijinsia, wakiisha kuonekana hawafai hutupwa nje wakiwa au wameathirika au wajawazito na kurudi kijijini wakipeleka huzuni kwa familia zao… kuna njaa ya ‘malezi bora’, wazazi wametingwa na kazi, hawana muda, watoto wanalelewa na mwalimu dunia na mitaala anaijua mwenyewe, baadaye tunanung’unikia ukorofi wa watoto… kuna njaa ya ‘upendo’, kukosekana kwa umoja na mshikamano katika familia kutokana na changamoto za usasa, kutopatana na kusalimiana sababu ya utu uzima tu, udanganyifu katika mahusiano nk... kuna njaa ya ‘uadilifu’ na kubwa zaidi ni njaa ya ‘Neno la Mungu’. Tufanye nini? Mosi tutambue kuna Yesu wa mikate na Yesu wa msalaba, si muda wote ni mteremko! Jibu tujipatie shibe katika Kristo ‘Mkate wa uzima’, ni Yeye pekee mwenye kuondoa njaa hizi kwa kutuongezea mikate ya ‘amani, upendo na umoja’ na samaki wa ‘uvumilivu na kutokata tamaa’ nasi tutakula na kusaza yaani kujiunda upya kutoka ndani na kujipatia jamii mpya ambayo watu wake hawaoni shida kuonyana na kuelekezana kindugu kwa upendo, kushikana mikono katika chungu na tamu za maisha hadi kuifikia nchi ya ahadi.

Liturujia D 17

 

26 July 2024, 16:16