Tanzania,Ask.Mwijage:Fungeni ndoa na epuka uchumba sugu!
Na Patriki Tibanga,Radio Mbiu,Bukoba na Angella Rwezaula – Vatican.
Ziara ya kichungaji inaelekeza njia anayotimiza mchungaji kama Askofu ambaye katika Kanisa la kijimbo ni ishara ya Kristo Mchungaji Mwema; na pia inaonesha kwamba malengo na nia ya ziara hiyo ni ya kichungaji, yanayolenga hasa kuhimiza, kusindikiza, kuimarisha, kutia moyo na kuendeleza maisha ya Kikristo ya watu binafsi na Jumuiya nzima. Ni katika muktadha huo ambapo Waamini wakatoliki wametakiwa kuiishi na kuitetea Imani Katoliki, kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa na wazazi kuwabatiza Watoto wao na kuwafundisha sala na katekisimu ya Kanisa Katoliki. Wito huo ulitolewa na Mhashamu Jovitus Mwijage Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, nchini Tanzania tarehe 5 Julai 2024 katika homilia yake kwa waamini wa Kigango cha Watakatifu Petro na Paulo kisiwani Mazinga,(moja ya visiwa vidogo vidogo vilivyomo kwenye Ziwa la Victoria, wakati Ziara ya Kichungaji kwa Parokia ya Bikira Maria, Malkia wa Ulimwengu, Kijwire Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania.
Katika homilia hiyo Askofu Mwijage alisema kwamba wazazi wanalo jukumu kubwa la kuwafundisha sala watoto kuanzia ngazi ya familia na kuwapeleka kubatiza, wakati huo huo na wazazi ambao hawajafunga ndoa kutumia fursa zinazotolewa na Parokia husika katika kupokea Sakramenti Takatifu ya ndoa, bila kujali mahitaji ya kifedha kwani kinachotazamwa ni Imani ya mtu husika na sio fedha. “Ndugu zangu mnapopewa nafasi za namna hiyo na Paroko, kuwaandikisha watoto kubatizwa na ambao hamjafunga ndoa mnatakiwa kujitokeza kwa wingi na kamwe msidharau maana ni Kanisa limefungua mlango huo, msione kwamba ninyi ni wadhambi hamuwezi kupokea Sakramenti bali muone Kristo ndiye aliyekuja kuwatafuta nyie ili mshushe mizigo ya dhambi kwake.” Alisema Askofu Mwijage katika homilia yake.
Askofu Mwijage aidha aliwataka wamini kuacha kuishi maisha ya uchumba sugu na kutumia nafasi ya mlango wa huruma iliyofunguliwa katika Kanisa kwa kufunga ndoa na kuwabatiza Watoto: “Walio wengi hampokei sakramenti ya Ekaristi kwa sababu mnakaa kwenye uchumba sugu; wewe umekaa na mtoto wa mtu muda mrefu bila kufunga ndoa hiyo inakunyima uhuru na ushiriki wa Sakramenti za Kanisa , wakati mwingine watu wanasema hatuna mali, lakini Baba Paroko amerahisisha hayo, atakuja kufungisha hapa kisiwani au kule Parokiani ni vyema mkatumia nafasi hizo, nanyi wazazi muwalete watoto wote wabatizwe hata wale wote wasiobatizwa waje kubatizwa.”Aliongeza Askofu Mwijage.
Katika ziara hiyo ya kichungaji katika vigango hivyo, Ujumbe wa Askofu Mwijage kwa ziara hiyo ulikuwa ni waamini kuwa wawazi na kujitokeza kueleza changamoto zao bila woga kwa Paroko wa Kanisa, ili kumsaidi kupokea Sakramenti za Kanisa. Askofu Mwijaga alisema: “Tunaomba ikitokea mtu hawezi kulipa mahitaji ya kanisa basi muandikie barua Paroko ili awabatize watoto hao mradi watoto hao waweze kufuatiliwa katika kuiishi Imani yao na kila mtu anayehitaji huduma ya Kanisa asaidwe kikamilifu na asibaki kulalamika na kutangatanga katika madhehebu mengine.
Kuhusu kujitolea mali watu na muda wa ziada kwa Kanisa, Askofu Mwijage aliwasihi waamini kuwa na moyo wa kujitolea muda wao wa ziada kwa kulitegemeza Kanisa na kuwasaidia wale wote wasiojiweza na kumshukuru Mzee Alphonce Rugazia ambaye katika kisiwa cha Mazinga mnamo mwaka 1982 kabla mzee huyo hajabatizwa aliitoa ardhi yake hekari 3 kwa ajili ya Kanisa ili kupata sehemu ya kuweka kituo cha sala na mnamo mwaka 1999 eneo hilo likapewa hadi ya Kigango na sasa ni Kigango cha Mazinga ambacho kina jumla ya vituo vidogo vya Jumuiya 7. Askofu Jovitus Mwijage alihitimisha ziara yake ya siku 4 katika Parokia ya Bikira Maria, Malkia wa Ulimwengu - Kijwire Jimbo Katoliki la Bukoba na katika ziara hiyo akiwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Philbert Mutalemwa na Paroko Msaidizi Fridoinus Muchunguzi walifanikiwa kuzungukia Jumuiya zilizopo katika Kisiwa na vigango vya nchi Kavu huku akitazama maendeleo ya waamini wanaoishi katika visiwa na nchi kavu kwa lengo la kuwahimiza kushiriki kikamilifu katika kulitegemeza Kanisa na kupokea Sakramenti za Kanisa huku akiwaonya waepuke madhebu yanayochipuka kama uyoga.
Tukirudi katika “Ziara ya Kichungaji” tena, jina lenyewe linavyopendekeza, ni ziara kwa maana ya sasa ya neno hilo kwamba: Askofu yeyote anafanana Kwenda kutembelea nyumba za waamini mahali ambapo maisha yao ya imani yafanyika na ambapo Jumuiya za waamini zinakutana ili kusikiliza Neno linalookoa na kuumega Mkate, ili kushuhudia tumaini la uzima wa milele na kubadilishana zawadi ya upendo wa kidugu. Kwa hiyo neno “kichungaji” linaonesha wazi kwamba, ziara hiyo hufanywa na Askofu, ambaye katika Kanisa la kijimbo kwa hakika ni ishara ya Kristo Mchungaji Mwema; na pia inaonesha kuwa malengo na nia ya ziara hiyo ni ya kichungaji tu, kutaka kuhimiza na kuendeleza maisha ya Kikristo ya watu binafsi na jumuiya nzima ya waamini wake. Kama Yesu asemavyo: “Mimi ni Mchungaji mwema, na watafuta walio wangu. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, atakimbia aonapo mbwa mwito…(Yh 10:11-15). Lakini Yeye ni Mchungaji awajuaye walio wake na kuwaita majina yao.
Kwa njia hiyo Askofu akitembelea Parokia hushiriki baadhi ya nyakati za maisha ya parokia na mapadre na waamini wote kwa kujumla, hata walio wadogo, maskini, wafungwa ili kila mmoja ajisikie ndani ya zizi bila kutengwa. Na zaidi ni ukweli wa kukutana kila mmoja ambao si kama wageni, kwa sababu wote, yaani mchungaji na waamini wanashiriki imani sawa katika Bwana Yesu na ni wa familia moja ambayo ni Kanisa Mama. Ziara ya Kichungaji, kwa hakika, kwa Kanisa la Jimbo ni kielelezo na ukumbusho wa umoja, ambao Askofu ndiye “Kanuni inayoonekana na msingi katika Makanisa Mahalia.”(rej. Katiba Lumen Gentium, n. 23 ya Mtaguso wa Pili wa Vatican). Na kumbe Basi hatushangai kila mara kusikia Baba Mtakatifu ameanza ziara ya Kichungaji. Lengo la Baba Mtakatifu, na Askofu wa kijimbo ni moja hapaishani ya kuweza kuwaimarisha waamini wake. Zaidi ya hayo, Ziara ya Kichungaji ni sababu ya furaha kwa sababu, kama Kitabu cha Maaskofu kinavyosema, kuwa “ni tukio la neema ambalo kwa namna fulani linaakisi taswira ya ziara hiyo ya pekee na ya ajabu kabisa ambayo kwayo Mchungaji Mkuu, Askofu wa nafsi zetu, Yesu Kristo alitembelea na kuwakomboa watu wake” (Rej n. 166,3). Kwa hiyo, Ziara ya Kichungaji lazima iangaliwe kwa jicho la imani na kutayarishwa mapema kwa maombi.