Tanzania,Ask.Rweyongeza:Kama mchungaji muige Kristo mchungaji mwema!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Shamba la Bwana ni kubwa lakini watenda kazi ni wachache, tumuombe Bwana wa Mavuno ili apelekea watenda kazi wake. Haya kweli ni maneno ya Yesu, ambayo kila siku yanazidi kuonekana kama tone la mvua katika bahari kubwa ya Ulimwengu wa Unjilishaji. Tarehe 13 Julai 2024, mama Kanisa akimkumbuka Mama Maria Waridi la Fumbo, katika Parokia ya Mtakatifu Petro Klaveri Bugene, Jimbo Katoliki la Kayanga, nchini Tanzania, kulikuwa na tukio la kutoa daraja Takatifu la Upadre, kwa Padre mpya Renovatus Mugisha Edward Kalemba, ambaye ni mhitimu wa masomo ya Sheria za Kanisa ( kwa Shahada ya uzamili) katika Chuo Kikuu cha Kipapa(Urbaniana) jijini Roma.
Misa hiyo iliudhuliwa na mapadre, watawa, waseminari, waamini wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali, nje na ndani ya Jimbo na nchi vile vile hata wamadhehebu mengine ya kidini. Misa Takatifu iliongozwa na Mwashamu Askofu Almachius Vincent Rweyongeza wa Jimbo hilo katoliki la Kayanga. Katika mahubiri yake hasa kwa mlengwa, mpadre na kwa waamini wote watu wa Mungu, kwa kuongoza na masomo yaliyosomwa: kutoka Is 61,1-3, somo la pili kutoka 1 Tim 4:12-16 na Injili kutoka Yh 10:11-16, Askofu alitoa maelekezo 30 kuhusiana Mbwa mwitu katika utume ambapo Padre huyo anaweza kuyazingatia na kuwa makini, katika safari yake mpya anayoianza, lakini pia huku akimuomba aongezee mengine zaidi katika ulimwengu huu kwa sababu ni mengi.
Radio Vatican inachapisha mahubiri ya Askofu Reyongeza aliyotoa. Akianza tafakari hiyo, Mwashamu Askofu Rweyongeza alisema: “Wapendwa wanafamilia ya Mungu: Tumsifu Yesu Kristo…Tuimarishe Imani yetu: kwa Neno la Mungu na Sakramenti. Jumuiya Ndogo Ndogo: Moyo mmoja, roho moja katika Kristo. Bila jumuia: Maisha hayaendi! “Siku hii ndiyo aliyoifanya Mungu, tutashangilia na kuifurahia” (Zab 118:24). Tunashangilia na kuifurahia kwa sababu: Kwanza, mwanetu, ndugu yetu na rafiki yetu Renovatus atapadrishwa. Pili, tumekuja kumshukuru Mungu na kumwomba. Tatu, tumekuja kushuhudia jinsi Upadre unavyotolewa, na hivyo kuendelea kuombea Miito ya Upadre, kuichochea na kuifadhili. Nne, tumekuja kumuombea Padre mpya huduma takatifu ya altare na kuzidi kumwomba Mwenye mavuno aite vijana wengi kutoka familia zenye uchaji wa Mungu wajiunge na wito wa Upadre (Optatam Totius, na 2).
Askofu wa Jimbo Kayanga aliendelea kwa kumgeukia Mteule huyo Padre na kusema: “Mpendwa Renovatus Mugisha Edward Kalemba, tunakushukuru sana kwa kuitikia wito wa Upadre; tunakuombea huduma na utumishi mtakatifu wa Kipadre. Wewe umekuwa sababu kubwa ya kukusanya umati huu mkubwa wa Mapadre, Mafrateri, Waseminaristi, Watawa, waamini walei ili kushuhudia, ukiwekewa mikono na kupakwa mafuta matakatifu ya Krisma kwa mara ya tatu (Ubatizo, Kipaimara, Upadrisho) na kwa njia hiyo unakabidhiwa rasmi ofisi tatu: Unabii, Ukuhani na Uchungaji. Wakati huohuo wale ambao ni Mapadre tayari fanya tathmini ya ofisi hizo kama zimejaa vumbi, buibui, panya, popo, mende, viroboto! Mosi, Utapewa Ofisi ya Unabii na hivyo kufanywa nabii au mwalimu wa kuhubiri Injili, kufundisha Neno la Mungu, kuonya na kukemea maovu."
Askofu alimweleza mteule huyo kuwa "Utafanya kazi hiyo Kanisani, kwenye mimbari, wakati wa Ibada. Lakini siku hizi kuna majukwaa mbalimbali ya kuhubiri Injili na kufundisha maadili kama vile: Mosi, Kwenye Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo – watembelee waamini waadhimishie Misa, wahubirie Injili – ukisaidiwa na Kipimajoto cha Jumuiya Ndogo ndogo (JNNK) kilichotengenezwa tunapoadhimisha miaka 50 ya JNNK Tanzania na Nchi za AMECEA. Pili, Tembelea watoto na vijana mashuleni na vyuoni. Mapadre tembelea mashule kila Ijumaa. Kama huwezi kufundisha dini na maadili kila darasa — Basi, kusanya wanafunzi wote wakatoliki pamoja — uwaadhimishie Misa na uwafundishe wakati wa Mahubiri — nenda umevalia kanzu lako na umejifunga sashi. Muonekano wako huo pia ni mahubiri. Wanaokuona watasema Padre alifika hapa au alipita hapa. Tatu, Vyama vya Kitume: Moyo Mtakatifu wa Yesu, Regio Mariae, UWAKA, VIWAWA, WAWATA, UTOTO MTAKATIFU, Mariae, Banyakaroli, Utume wa Fatima, nk. Vyama vya Kitume ni uhai wa Kanisa. Vitembelee wape mafungo, nk. Nne, majukwaa ya mazishi na kuanua matanga – Huko unakuta jamii mchanganyiko ya walio kusanyika kumzika marehemu. Tumia fursa hiyo kukemea maovu – ulevi, uzembe, wizi, ushirikina, mauaji, nk.”
“Pili, kwa kuwekewa mikono na kupakwa mafuta matakatifu ya Krisma utafanywa Kuhani wa Agano Jipya, ukifanya kazi ya kuadhimisha Sakramenti hasa Ekaristi Takatifu au Misa Takatifu kila siku juu ya altare. Kwa njia ya Ubatizo utaliongezea taifa la Mungu waamini wapya. Kwa sakramenti ya Kitubio utasamehe dhambi kwa jina la Kristo na Kanisa, kwa Mpako Mtakatifu utawafariji wagonjwa na kuwaponya magonjwa ya rohoni na mwilini. Mintarafu ofisi hii ya ukuhani — zingatia Sala ya Kanisa au Breviary na kwa njia hiyo kumtolea Mungu sala za sifa na shukrani kwa ulimwengu mzima. Tatu, kwa kuwekewa mikono na kupakwa mafuta matakatifu ya Krisma utakabidhiwa ofisi ya Mfalme, mtawala, yaani utafanywa Mchungaji au Kiongozi wa Taifa la Mungu ukishirikiana na Askofu — kuwaongoza watu kwa Mungu Baba kwa njia ya Kristo na katika Roho Mtakatifu.”
Askofu Rweyongeza aliendelea kueleza:“Wewe, kama mchungaji, muige Kristo Mchungaji mwema anayetuhimiza akisema: “Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Mtu wa kuajiriwa ambaye ni mchungaji feki au bandia na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa- mwitu wanakuja, anawaacha kondoo na kukimbia, kisha mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya” (Yoh 10:11-12). Mtume Petro anatuasa akisema: “Ninawasihi mlichunge lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa; mlitunze si kwa kulazimishwa bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu wote. Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo kundi. Na wakati Mchungaji Mkuu atakapotokea, ninyi mtapokea taji ya utukufu isiyofifia” (1 Petro 5:1-4).”
“Bwana Yesu aliwatuma wafuasi wake 72 akiwaambia: “Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache. Kwa hiyo, mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake. Sasa nendeni; fahamuni kwamba ninawatuma ninyi kama kondoo kati ya mbwa-mwitu” (Lk 10:2-3). Mbwa–mwitu wanaoongelewa si wale wa msituni au porini. Mbwa–mwitu hawa ni wajumbe wa shetani, ni nguvu za giza. Mtume Paulo anasema: “Maana vita vyetu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala mafisadi, wakuu na wenye nguvu, wanaomiliki ulimwengu huu wa giza” (rejea Efe 6:11-12). Silaha kubwa ya mapambano ni sala. Mbwa–mwitu, akiisha kunyanganya muda wa kusali, utakuwa mateka wake kwa urahisi.”
Askofu Rweyongeza alizisisitiza zaidi kuwamba: “Kuna mbwa-mwitu mamboleo 30”, lakin na zaidi japo kuwa alitaka kutaja vichache hivyo ambapo alimwomba yeye aongeze mwenyewe maana ni vingi, lakini kwa kutaja tu alianza kuorodhesha: “Mosi, Ulevi — madawa ya kulevya. Baadhi ya Mapadre ni mateka hapa. Pili, Ushoga na usagaji. Tatu, Vidhibiti mimba na utoaji mimba. Waganga wa hirizi na matambiko. Tano, Changudoa wanaokuja kujiuza kwako. Sita, Ushirikina na upigaji ramli chonganishi – baadhi ya Mapadre ni gumzo katika vyombo vya habari. Ikumbukwe kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe na atahukumiwa kadiri ya matendo yake. Saba, Wahubiri feki wanaofanya biashara ya upako na miujiza ya uponyaji kwa kutumia nguvu za giza. Nane, michezo ya Bonanza, Kasino, kubeti, kamali, pool. Himiza watu wafanye kazi masaa kumi kila siku. Wahenga wamesema: “Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe, bila jasho hupati.” “Fanya kazi kama mtumwa/mjakazi baadaye uishi kama mfalme/malkia (Sira 7:15; 2 Thes 3:6-12). Tisa, mashirika/makundi/vyama feki vya matapeli — mnakumbuka Pentagon, Pyramid, Biodisk, DECI, Q-NET: GOODMORNING, FREEMASON nk. Kumi, rushwa, takrima: utapewa kitita cha pesa kukuziba mdomo usikemee au kulaani. Kumi na moja, njaa na utapiamlo. Kumi na mbili, magonjwa na maradhi. Kumi na tatu, Ujinga — “wajinga ndio waliwao” — (rejea Hosea 4:6). Kumi na nne, manabii wa uwongo. Yesu alitahadharisha akisema: “Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwa–mwitu wakali. Mtawatambua kwa matendo yao” (Mt 7:15-16). Kumi na tano: utajiri bila kazi. Kumi na sita: starehe bila dhamiri. Kumi na saba: uchumi bila maadili. Kumi na nane: sayansi bila utu. Kumi na tisa, Ibada bila sadaka.”
Askofu wa Jimbo la Kayanga aliendelea bado na orodha hiyo: “Ishirini, siasa bila kanuni. Ishirini na moja, elimu bila tabia njema.Ishirini na mbili, “secularism” au kuabudu malimwengu. Roho ya kukumbatia malimwengu na kutawaliwa nayo. Ishirini na tatu, “materialism” au kuabudu mali. Ishiri na nne, “relativism” kuabudu akili yako — yaani ukweli ni jinsi nionavyo mimi, si mwingine Sheria haina nafasi wala nguvu maishani mwako. Hii ni kutenda bila hofu ya Mungu mfano: Kutoa mimba, kuua vibaka na wanaotuhumiwa uchawi, kutoshiriki Ibada za Dominika na Sherehe, kukaidi ushauri na maonyo. Ishirini na tano: uchoyo na ulafi. Ishirini na sita, ugaidi. Ishiri na saba: utitiri wa madhehebu uchwara. Ishirini na nane: uharibifu wa mazingira – ukataji miti ovyo, matumizi ya sumu – “paraforce” na “roundup” ya kuua magugu, na “forceup” au “glycel” kwa kuua Kwekwe. Ishirini na tisa: udini na ukabila. Thelathini: uchumba sugu, michepuko, talaka na familia nyingi kuvunjika.
Askofu Vincent aliendelea kudadavua kuwa "Katika mazingira haya, Padre anayemwomba Askofu wake eti kwenda likizo, ni Padre wa mshahara. Hivyo, wewe mtawa na wewe mkristo mlei yawapasa kutimiza wajibu nne kwa Mapadre: Kwanza, kuwaheshimu Mapadre (Sira 7:29-31). Pili, kuwatii katika mashauri ya dini. Tatu, kuwaombea katika Misa, Sala na Ibada mbalimbali. Nne, kutimiza wajibu wa kuwatunza (Sira 7:31).” Kadhalika Askofu Rweyongeza liongezea: “Wewe mpendwa Padre mtarajiwa Renovatus pokea wosia huu: Mosi, “Mtumikieni Mungu kwa furaha” (Zab 100:2) na “Usilegee katika bidii, ila uwe mchangamfu rohoni na katika kumtumikia Mungu” (Rum 12:11). Pili, “Wewe shikilia wito wako zeeka ukiwa kazini mwako” (Sira 11:20; 2 Pet 1:10-11).Tatu, “tenda vitu kwa uaminifu nawe utafanikiwa katika mambo yako yote”(Tobit 4:6); na kwa jinsi hiyo jioni ya maisha yako utasikia sauti hii ikikukaribisha mbinguni: “Vema mtumishi mwema na mwaminifu njoo ufurahi na Bwana wako” (Mt 25:21,23),”Alihitimisha, Askofu mahubiri hayo na kuendelea na taratibu zilizofuata za kiliturujia ya Upadrisho huo.
Ndugu Msikilizaji na msomaji ikumbukwe Padre mpya Renovatus Mugisha alizaliwa tarehe 13 Januari 1991 huko Karagwe, Kagera-Tanzania na ni mtoto wa tano na wa mwisho wa Edward Kalemba Bernard na Petronilla Kagemuro. Katika majiundo yake ni shule ya Msingi, sekondari na I-IV akiwa anasomea serikali na baada ya kuhitimu alitamani kwenda kujiunga na shule binafsi hasa seminari ili anufaike na malezi na maarifa yanatolewa na shule za Kanisa. Wazazi walimsadia kufanya taratibu zote ikiwemo kuongea na aliyekuwa Paroko wake Padre Edward Rwechungura na Mkurugenzi wa Miito. Mnamo mwaka 2014 alichaguliwa kujiunga na masomo ya falsafa katika Seminari Kuu ya Bikira Maria Malkia wa Mitume Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. Mwaka 2017, alihitimu masomo ya falsafa na mwaka 2018 alitumwa kuanza masomo ya Taalimungu Chuo Kikii cha Kipapa cha Urbabiana, Roma na Askofu wake Mhashamu Almachius Vincent Rweyongeza. Mwaka 2021, alihitimu masomo ya Taalimungu na akapewa nafasi nyingine ya kuendelea na shahada ya uzamili katika Sheria za Kanisa ambayo alihitimisha tarehe 24 Juni 2024 na Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kanisa, Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana.
Katika neno la Mkurugenzi wa Miito jimbo katoliki la Kayanga, Padre Renatus Ajuna, alihimiza wazazi walee miito ya watoto, lakini pia akiwaalika kila mmoja kuwa mwajibikaji wa kulea na kutunza miito. Alitoa takwimu kamili ya vijana ambao wapo katika seminari ya Jimbo lakini vile vile kuwaalika vijana wanaopenda kujiunga, huku akiwapa maelekezo ya jinsi ya kujiunga. Yafuatayo ni maelekezo ya Mkurugenzi wa miito Jimbo katoliki la Kayanga Tanzania..