Tarehe 11 Julai ni Siku ya Mtakatifu Benedikto wa Nursia na Msimamizi wa Bara la Ulaya
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kila tarehe 11 Julai ya kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Benedikto wa Norcia yaani Nursia ambaye alikuwa mmonaki wa Italia na aliyeandika Kanuni ya Utawa ambayo iliyoenea katika monasteri nyingi za Kanisa la Kilatini na hata nje yake. Wananaoifuatilia Kanuni hiyo wanaitwa Wabenediktini na Mtakatifu huyo anaheshimiwa tangu zamani kama Abati mtakatifu. Kwa kawaida Wabenediktini wanaadhimisha sikukuu yake tarehe aliyofariki dunia, lakini kalenda ya Kanisa la Roma inaiadhimisha tarehe 11 Julai, tangu Papa Paulo VI alipomtangaza kuwa msimamizi mkuu wa Bara la Ulaya mnamo tarehe 24 Oktoba 1964 na kwa upande wa Kanisa la Kiorthodox, wanaadhimisha Mtakatifu huyo kila ifikapo tarehe 14 Machi.
Wasifu wa Mtakatifu Benedikto
Mtakatifu Benedikto da Nursia, alikuwa ndugu pacha wa Mtakatifu Skolastika, alizaliwa tarehe 12 Septemba 480, katika familia tajiri ya Roma. Baba yake, Eutropius Anicius, alikuwa kapteni mkuu wa Warumi katika eneo la Nursia, wakati mama yake alikuwa Claudia Abondantia Reguardati, malkia mdogo wa kijiji hicho. Aliishi miaka ya utoto kijijini Nursia, huku akiona wahamiaji kutoka Dola la Roma Mashariki ambao katika karne III walikimbia dhuluma wakashika maisha ya kiroho katika mapango waliyojichimbia mwambani kandokando ya Kanisa dogo. Alipofikia umri wa miaka 12 hivi mapacha hao walitumwa Roma kwa ajili ya masomo, lakini walichukizwa na anasa za jiji hilo, kama alivyosimulia Papa Gregori I katika kitabu cha pili cha Majadiliano.Hivyo akaacha masomo, nyumba na mali ili avae kanzu la kimonaki akampendeze Mwenyezi Mungu tu. Alipofikia miaka 17 alihamia kwenye bonde la mto Aniene karibu na Eufide, na kuelekea baadaye Subiaco, alipokutana na mmonaki wa monasteri ya jirani ambaye kama abati Adeodatus alipokea nadhiri zake za kitawa akamuonesha pango kwenye mlima Taleo. Huko aliishi miaka 3 kama mkaapweke hadi Pasaka ya mwaka 500. Halafu akakubali kuongoza wamonaki wengine karibu na Vicovaro, lakini, baada ya kunusurika kuuawa kwa sumu, na akarudi Subiaco, alipobaki karibu miaka 30, akihubiri neno la Mungu na kupokea wanafunzi wengi zaidi na zaidi, hata akawa anaongoza monasteri 13, kila mojawapo ikiwa na wamonaki 12 na abati wake.
Kauli mbiu: Ora et labora
Karibu na mwaka 529 baada ya upinzani mkali wa padre jirani ambaye alianza migogoro kadhaa na kupotosha wafuasi wake, aliamua kuhama akaelekea huko Cassino ambapo, juu ya mlima alianzisha monasteri kubwa inayoitwa Montecassino juu ya mabaki ya mahekalu ya Wapagani. Huko Montecassino Mtakatifu Benedikto aliandika kanuni yake mnamo mwaka 540, huku akiongozwa na zile zilizotangulia, hasa Kanuni ya Mafundisho iliyoandikwa na mmonaki asiyejulikana, lakini pia ya Mtakatifu Basili Mkuu, Yohane Kasiano, Pakomi na Sesari, aliunganisha nidhamu na heshima kwa mtawa na vipawa vyake, ili kuunda shule ya utumishi wa Bwana ambapo kauli mbiu ya Shirika hilo ni Ora et labora, yaani Sala na kufanya kazi. Maisha yake yote hadi kifo chake aliishi Montecassino, akitembelewa na waamini na watu maarufu kama Totila mfalme wa Ostrogoti. Alifariki mnamo tarehe 21 Machi 547, siku arobaini hivi baada ya dada yake Pacha Skolastica ambaye alizikwa pamoja naye katika kaburi moja huko Montecasino.
Scolastica ni dada pacha wa Mtakatifu Benedikto
Hata hivyo ndugu msikilizaji na msomaji ni vema tukatazama kidogo kuhusu maisha ya na dada yake mtawa Pacha ambao hawawezi kutengenishwa kila tunamfikira Benedikto. Andiko pekee linalotuambia kuhusu Mtakatifu Scholastica ni kitabu cha pili cha Majadiliano” cha Papa Gregori Mkuu (590-604). Lakini Majadiliano ni juu ya nyimbo zote za ushauri, ambazo zinapendekeza mifano ya utakatifu kwa waamini zinazolenga kusisimua na hisia, bila hata hivyo kutafuta data kamili na kumbukumbu fulani ya kihistoria. Na zaidi ya hayo, sura yake inapendekezwa tu katika kivuli cha kaka yake mkubwa, baba wa utawa wa Magharibi, Mtakatifu Benedikto. Dada pacha wa mtakatifu mkuu wa Norcia kama tulivyoona alizaliwa siku moja na kaka yake mnamo 480. Baba yake, Eutropius Anicius, mzao wa familia ya seneta ya kale ya Kirumi ya Anicii, alikuwa Jenerali wa Warumi katika eneo la Norcia. Mama huyo, Claudia Abondantia Reguardati, mtoto wa mfalme wa Norcia, alifariki mara baada ya kujifungua mapacha hao. Baba, ambaye alikuwa amejitolea uangalifu mkubwa kwa watoto hao wawili, aliapa kumpeleka kwenye maisha ya utawa. Maisha ya Scholastica na yale ya Mtakatifu Benedikto yamefungamana katika njia ya utakatifu. Kisha Scholastica alimfuata kaka yake ambaye alikuwa amekimbilia katika mtaa wa Subiaco. Wakati Benedikto alipoanzisha abasia ya Montecassino, Mtakatifu Scolastica alianzisha monasteri ya Piumarola, takriban kilomita saba kutoka katika Abasia maarufu ya Kibenediktini.
Mkutano wa Benedikto na Scolastica kwa mwara ya mwisho
Hapa, pamoja na dada zake, kufuatia utawala wa kimonaki wa kaka yake, alitoa tawi la kike la Shirika la Kibenedikitini. Hivyo kwa namna moja tawi la shirika jingine la kike lilianzishwa, yaani la Mtakatifu Scholastica na kaka yake, Benedikto, wakaamua kwamba wangeonana mara moja kwa mwaka, sehemu ya katikati ya nyumba za watawa wa sehemu mbili. Hii ilikuwa ni Mikutano ya imani ya kiroho, ya maombi, ya sifa kwa Bwana. Lakini kwa mara ya mwisho walipoonana kitu kimoja cha ajabu kilitokea. Mtakatifu Benedikto alipotambua kwamba siku hiyo ilikuwa inakaribia kuisha wakiwa wanazungumza, aliwapatia ishara wale mapadre waliokuwa wameambatana naye kwamba muda wa kuondoka ulikuwa umefika. Watakatifu hao wawili ilibidi watengane na ili waje wakutane tena mwaka uliofuata. Lakini Scholastica, hata hivyo, katika afla hiyo alimsihi kaka yake abaki na alikuwa amemweleza kuwa huo ungekuwa mkutano wao wa mwisho. Ndipo Mtakatifu Benedikito alimjibu dada yake: “Lakini unasema nini, dada yangu, hujui kuwa siwezi kulala nje ya chumba changu?" na hivi alivyokuwa mkali sana kwa sheria - alijibu kwa maneno haya kwa dada yake mpendwa. Wajibu wake ulikuwa kuondoka, na ndivyo alivyofanya. Scholastica, mara tu kaka yake alipoondoka - kwa hivyo inasemekana kwamba alianza kusali, kwa siri, kwa ukimya, kwa Mungu Wakati huo huo, Mtakatifu Benedikto na wenzake waliokuwa wamemsindikiza, walipokuwa wakirudi nyumbani, walipata dhoruba kubwa ya mvua na ngurumo na umeme.
Mtakatifu Benedikto anashindwa kurudi jumuiyani
Haikuwezekana kuendelea barabarani. Kwa hiyo ilibidi warudi nyuma na Mtakatifu Benedikto mara tu aliporudi kwenye nyumba iliyowekwa kwa ajili ya mikutano kati ya wawili hao alimwambia dada yake “Mungu akusamehe, dada yangu, lakini umefanya nini? Na kwa hivyo, yule dada - kwa tabasamu tamu - alijibu: “Nilikusihi ukae hadi kesho na hukunisikiliza; kwa sababu hiyo nilimgeukia Bwana naye akaniitikia.” Na kwa hivyo, watakatifu hao wawili, pamoja na mapadre wa Benediktini, walitumia usiku huo katika sala, siri za kiroho, katika mazoezi ya uchaji Mungu. Asubuhi iliyofuata, Mtakatifu Benedikto alifanikiwa kwenda kwenye Abasia yake ya Montecassino na wenzake. Siku tatu baada ya mkutano huo, Mtakatifu Benedikto alipokuwa akisalia, akitazama juu, aliona roho ya dada yake ikibebwa hadi Mbinguni kwa mbawa za Malaika. Kisha akaanza kumsifu Bwana. Hivyo ikawa kwamba aliwatuma mafrateri wengine kuchukua mabaki ya Mtakatifu, ili wayahifadhi kaburini mwao.