Makleri kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Makleri kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. 

Upadre Ni Wito, Fumbo na Zawadi Kutoka Kwa Mwenyezi Mungu!

Wakleri wanakumbushwa kwamba, kabla hata ya kuwekewa mikono na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu, wao kimsingi ni: waamini waliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu na kwamba, utambulisho wao wa kwanza ni waamini na wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Ushuhuda wa Shemasi Renovatus Mugisha Edward Kalemba, Jimbo la Kayanga.

Na Renovatus Mugisha Edward Kalemba, - Roma, Italia.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu wito na maisha ya Daraja takatifu ya Upadre anapenda kukazia sana umuhimu wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu; Fumbo la Ekaristi Takatifu kuwa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa kwa sababu Kristo Yesu ndiye chemchemi ya upendo kwa waja wake. Wakleri wanakumbushwa kwamba, kabla hata ya kuwekewa mikono na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu, wao kimsingi ni: waamini waliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu na kwamba, utambulisho wao wa kwanza ni waamini na wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa Kwa namna ya pekee, ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Huu ndio urithi unaojikita katika Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa. Ni ukweli ambao wakleri wanapaswa kuumwilisha katika maisha na utume wao kwa njia ya Roho Mtakatifu. Padre daima anapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake na kwamba, Ibada kwa Bikira Maria inawawezesha wakleri kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria, ili kweli waweze kuwa wafuasi na mitume hodari wa Kristo Yesu kwa kusikiliza na kutenda kama alivyokuwa Bikira Maria. Daima amekumbusha kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, ni watu wanaopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Shemasi Renovatus Mugisha Edward Kalemba, Jimbo la Kayanga
Shemasi Renovatus Mugisha Edward Kalemba, Jimbo la Kayanga

Ninaitwa Shemasi Renovatus Mugisha Edward Kalemba, kutoka Jimbo Katoliki la Kayanga, Parokia ya Mt. Petro Klaveri Bugene, ni mhitimu wa masomo ya Sheria za Kanisa (Shahada ya uzamili) katika Chuo Kikuu cha Kipapa (Urbaniana) kilichoko mjini Roma nchini Italia na ninatarajia kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 13 Julai 2024 katika Kanisa la Mtakatifu Petro Klaveri Bugene. Mimi ni mtoto wa tano na wa mwisho wa Ta Edward Kalemba Bernard na Ma. Petronilla Kagemuro. Nilizaliwa tarehe 13 Januari 1991 huko Karagwe, Kagera-Tanzania. Nilipokuwa mdogo nilitamani sana kuwa daktari wa binadamu, hivyo nilipoanza sekondari nilipendelea sana masomo ya sayansi. Kwa kuwa nilisoma shule ya serikali (Kidato cha I-IV), baada ya kuhitimu nilitamani kwenda kujiunga na shule binafsi hasa seminari ili ninufaike na malezi na maarifa yanatolewa na shule za Kanisa. Wazazi walinisadia kufanya taratibu zote ikiwemo kuongea na aliyekuwa Paroko wangu Padre Edouard Rwechungura na Mkurugenzi wa miito, Padre Fortunatus Bijura ili wanisaidie kutafuta nafasi katika seminari inayofundisha masomo ya sayansi. Nilifanikiwa kupata nafasi ya Kwenda kusoma katika Seminari ndogo ya Bikira Maria, Nyegezi Jimbo kuu la Mwanza, japo ilibidi nibalidi mchepuo badala ya kuchukua masomo ya Fikizia, Kemia na Bioyolojia (PCB), ilinibidi nichukue PCM (Fikizia, Kemia na Mahesabu) kwa sababu Bioyolojia ilikuwa haifundishwi pale Nyegezi. Nikiwa naendelea na masomo ya kidato cha V na VI, kuna mambo yalianza kunivutia, moja ya jambo lililonigusa sana ni jinsi ambavyo Mapadre walezi walivyokuwa na huruma na upendo hasa pale mseminari alipokuwa anapitia kipindi kigumu na changamoto za maisha kama: magonjwa, kufiwa nk. Kitu kingine kilichonivutia zaidi ni mavazi yanayovaliwa na Mapadre wakati wa adhimisho la Misa Takatifu, kipindi kile nilikuwa sijazoea kuwaona Mapadre mara kwa mara na wakiwa zaidi ya mmoja kwenye Adhimisho Takatifu la Misa, hivyo kwangu ilikuwa ni furaha kuwaona kila siku asubuhi wakati wa Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, wakiwa wameizunguka Altare ya Bwana kwa Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, kielelezo cha umoja na ushirika wa watu wa Mungu.

Shemasi Renovatus Mugisha akiwa na wazazi wake
Shemasi Renovatus Mugisha akiwa na wazazi wake

Baada ya mwaka mmoja pale seminarini nilianza kujiuliza mwenyewe kama na mimi nastahili kuwa mmoja wa wale Mababa. Hapo ndipo nilipoanza kufuatilia kwa karibu sana na kutaka kujua zaidi ni vigezo gani anavyopaswa kuwa navyo kijana anayetaka kuwa kama wao. Hii ilinisukuma nianze kwenda kwa aliyekuwa Baba mlezi wa maisha ya kiroho wa Seminari na kumuuliza sifa kuu za Padre. Katika majibu niliyoyapata, mawili nayakumbuka hadi leo. Kwanza, alinambia Upadre hautafutwi wala kusomewa ila ni wito na zawadi tu ambayo Mungu anampatia yule aliyemchagua na jibu la pili alisema ni kwa njia ya sala na kwa mazungumzo ya mara kwa mara na baba wa maisha ya kiroho ndiyo pole pole mtu anatambua kuwa ameitwa. Baada ya kuhitimu kidato cha sita nilienda kuongea na wazazi, nikawajulisha kuwa natamani kuwa Padre, ingawa sikuwa na uhakika kama kweli ni sauti ya Mungu hivyo nilikuwa nina wasi wasi juu ya maamuzi yangu! Wazazi walinitia moyo, wakanisindikiza kuongea aliyekuwa Paroko wangu, na baadaye Mkurugenzi wa miito na baada ya kufuata taratibu zote, nikaenda kuungana na wenzangu waliokuwa tayari wamekwenda nyumba ya malezi ya jimbo. Mwaka 2014 nilichaguliwa kujiunga na masomo ya falsafa katika seminari kuu ya Bikira Maria Malkia wa Mitume Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. Mwaka 2017, nilihitimu masomo ya falsafa na mwaka 2018 nilitumwa kuja kuanza masomo ya Taalimungu na Askofu wangu Mhashamu Almachius Vincent Rweyongeza) baada ya kupewa ufadhili na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu (Propaganda Fide) katika Chuo Kikuu cha Papa Urbano wa VIII. Mwaka 2021, nilihitimu masomo ya Taalimungu na nikapewa nafasi nyingine ya kuendelea na shahada ya uzamili katika Sheria za Kanisa na sasa tarehe 24 Juni 2024 nimehitimu masomo yangu (Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kanisa, Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana).

Shemasi Renovatus Mugisha akizungumza na Balozi Mahmoud Thabit Kombo
Shemasi Renovatus Mugisha akizungumza na Balozi Mahmoud Thabit Kombo

Changamoto katika wito: Changamoto kubwa iliyonisumbua ilikuwa ni kifo cha ghafla cha Mama mzazi Ma. Petronilla Kagemuro kilichotokea tarehe 04.08.2016 kwa ajali ya gari barabarani. Nilikuwa mwaka wa pili wa falsafa, nakumbuka ni tukio ambalo sikulitegemea wala sikuwaza kama lingetokea kabla ya mimi kuwa Padre. Licha ya maumivu na majonzi ya kifo cha mama mzazi, Mungu alinisaidia na niliiona thamani na nguvu ya sala na imani. Changamoto ya pili ni kipindi nilipofika nchini Italia 2018 kuanza masomo ya Taalimungu hasa jitihada za kijifunza lugha mpya (kiitaliano) na changamoto ya utamaduni mpya, ilinibidi niwe mvumilivu kuanza kuzoa vyakula, hali ya hewa na kujifunza kuishi na watu wenye tamaduni tofauti za zetu. Changamoto nyingine ni ile hali ya kibinadamu ya kuwa na wasi wasi kama kweli huu ni wito wangu. Lakini kwa njia ya sala, imani na matumaini makubwa, changamoto zote hizi, hatua kwa hatua zilipita na hivyo kuniongezea ukomavu na imani. Mwisho, siwezi kuisahau changamoto ya afya, ambayo mara kadhaa ilinifanya niwe na wasi wasi na mashaka na kujiona kuwa sistahili kuwa mtumishi wa Bwana. Hii nayo ilinifundisha kuwa, hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu, Yeye anayetuita tumtumikie, ndiye anayetutia nguvu na kutustahilisha kusimama mbele yake na kumtumikia bila mastahili yetu.

Shemasi Renovatus Mugisha anawashukuru watanzania kwa umoja na upendo
Shemasi Renovatus Mugisha anawashukuru watanzania kwa umoja na upendo

Shukrani: Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote anayonitendea katika maisha yangu hasa kwa zawadi ya wito huu mtakatifu. Napenda kuwashukuru wazazi wangu kwa kuendelea kunisindikiza kwa sala na kwa kuendelea kuwa Makatekista wangu wakuu na wafadhili wangu pia. Shukrani zangu za dhati zimwendee Askofu wangu Mhashamu Alamchius Vincent Rweyongeza na wasaidizidi wake, kwa upendo wake wa kibaba kwangu, kwa kuendeleza kunitegemeza, kunilea na kwa kunisomesha na kwa namna ya pekee kwa kulipokea ombi langu la kuomba kupewa Daraja Takatifu ya Upadre ambapo natarajia kuwekwa wakfu katika Misa ya Upadrisho (13 Julai 2024) na huyo huyo Askofu wangu, Mhashamu Askofu Almachius Vincent Rweyongeza, wa Jimbo Katoliki la Kayanga. Shukrani zangu za pekee kwa uongozi wote uliopita na wa sasa wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji kwa ufadhili wao na kwa nafasi waliyonipatia kuwa mmoja wa wanafamilia kubwa ya chuo cha Papa Urbano VIII. Napenda kuwashukuru Mapadre wote wa Jimbo la Kayanga, kwa namna ya pekee Paroko wangu (Padre Nicodemus Byakatonda), kwa kushirikiana na Baba Askofu kunilea na kupalilia nia yangu ya kuwa Padre. Shukrani zangu za dhati ziwaendee Mapadre, walimu na walezi wote walionilea na wanaoendela kunifadhili kuijongea altare ya Bwana. Nawashukuru sana watawa, waseminari na waamini wote ambao nimepita katika mikono yao kwa mchango wao kwangu. Napenda kuwashukuru sana waamini wa Parokia yangu ya Bugene na waamini wote wa Jimbo la Katoliki la Kayanga kwa kuendelea kuifadhili miito kwa njia ya sala na michango yao. Siwezi kuwasahu, wanadarasa wenzangu na alumni wote ambao tulikuwa wote katika hatua mbalimbali za masomo, tangia shule ya msingi, sekondari na vyuo pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote walionisadia na wanaoendelea kuniombea na kunifadhili kuijongea Altare ya Bwana.

Shemasi Renovatus Mugisha akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Italia
Shemasi Renovatus Mugisha akiagana na Balozi wa Tanzania nchini Italia

Kwa namna ya pekee napenda kuishukuru jumuiya ya watanzania wanaosoma na wanaoishi Italia kwa upendo wenu na kuendelea kunilea kama mdogo wenu na mtoto wenu, na kwa kuendelea kunifadhili kuijongea Altare ya Bwana. Mwisho, natambua na kuthamini mchango wa kila mmoja aliyekuwa sehemu ya wote walionisaidia kuifikia siku ya leo, siwezi kuwataja kwa majina maana ni wengi sana ila nawakumbuka katika sala. Naomba mwendelee kuniombea ili hicho ambacho Mwenyezi Mungu amepanda ndani mwangu kiendelee kukua na kukomaa. Karibuni sana katika Misa ya Upadrisho wangu tarehe 13 Julai 2024, Katika Parokia ya Mtakatifu Petro Klaveri Bugene, Jimbo Katoliki la Kayanga na Misa ya Shukrani 15 Julai 2024, nyumbani Cherunga-Ihanda, Karagwe-Tanzania. Shemasi Renovatus Mugisha Edward Kalemba.

Shemasi Revo Mugisha
11 July 2024, 15:39