Tafuta

Tarehe 2 Julai 2024 Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba, OSA wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi tisa na Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Wilibrant Urio, C.PP.S. Tarehe 2 Julai 2024 Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba, OSA wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi tisa na Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Wilibrant Urio, C.PP.S.  

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Wapata Mashemasi 9 na Padre Mmoja! Yaani We Acha Tu

Katika mahubiri yake, Askofu Msaidizi Stephano Musomba amegusia kuhusu thamani ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre, kwamba, hii ni safari inayosimikwa katika malezi yanayomwezesha mwamini kuundwa kwa kile anachoitiwa, yaani Daraja Takatifu ya Upadre. Wanapaswa kujiulizwa wanaitwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni nani katika Kanisa na Shirika, Wanaitwa kuishi namna gani na kwamba, wanaitwa kufanya nini katika maisha na utume wa Kanisa. "Alter Christus."

Na Daniel A. Ling’wentu na Ndahani Lugunya, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Damu Azizi ya Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu wa ulimwengu na kwamba, ni alama ya juu kabisa inayoshuhudia upendo na sadaka ya maisha kwa ajili ya wengine. Sadaka hii inajirudia tena na tena katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha Kristo Yesu kuwakirimia waamini Mwili na Damu yake Azizi; Damu ya Agano Jipya na la milele, iliyomwagika kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujitambua kama watu waliotiwa muhuri ili kushiriki katika utume wa Kristo Yesu, ili waweze kuwa ni mwanga na baraka inayofufua na kupyaisha; mwanga unaoponya na kumweka mtu huru; tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Familia za Kikristo ziwe ni vitalu vya kulelea miito mitakatifu
Familia za Kikristo ziwe ni vitalu vya kulelea miito mitakatifu

Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., ni Shirika la Kitume lililoanzishwa na Mtakatifu Gaspar del Bufalo kunako tarehe 15 Agosti 1815 na kulisimika katika nguzo kuu tatu: Maisha ya kijumuiya, Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu na Utume. Utume: kama mhimili wa kwanza wa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ni kuendeleza utume wa Mtakatifu Gaspari wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Mhimili wa pili ni maisha ya jumuiya, ambapo Wamisionari huishi pamoja daima, hasa utume unapowaruhusu kufanya hivyo. Katika kukamilishana katika hilo, Wamisionari huunganishwa na kuongozwa na kifungo cha upendo badala ya nadhiri. Mhimili wa tatu ni Tasaufi ya Damu Azizi. Kristo Yesu aliyemwaga Damu yake Azizi ni alama ya upendo mkuu wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote.

Askofu Msaidizi Stephano Musomba wa Jimbo kuu la Dar es Salaam
Askofu Msaidizi Stephano Musomba wa Jimbo kuu la Dar es Salaam

Na tasaufi ya Damu Azizi ndiyo inayowahamasisha wamisionari mpaka leo hii kuunganisha maisha na kujenga maisha ya jumuiya wakitembea huko na huko wakiwa wameshikamana na wale wanaoteseka ili kujibu kilio cha damu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwa kifupi kilio cha damu ndiyo tasaufi dhahiri ya Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu na daima wanajitahidi kusikiliza na kutoa majibu muafaka kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Ni katika muktadha huu, katika maadhimisho ya Sherehe ya Damu Azizi ya Yesu, tarehe Mosi, Julai 2024, Mheshimiwa Padre Vedasto Ngowi, C.PP.S., Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania aliwapokea Mafrateri tisa na kuwaingiza katika Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu na kuanzia sasa wanakuwa ni Wamisionari kamili wa Damu Azizi ya Yesu wenye haki na nyajibu mbele ya Shirika na Kanisa katika ujumla wake. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Parokia ya Mwili na Damu ya Yesu, Tegeta, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Mapadre watambue kwamba wao ni Mawakili wa Kristo!
Mapadre watambue kwamba wao ni Mawakili wa Kristo!

Tarehe 2 Julai 2024 Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba, OSA wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi tisa na Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Wilibrant Urio, C.PP.S. Katika mahubiri yake, Askofu Msaidizi Stephano Musomba amegusia kuhusu thamani ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre, kwamba, hii ni safari inayosimikwa katika malezi yanayomwezesha mwamini kuundwa kwa kile anachoitiwa, yaani Daraja Takatifu ya Upadre. Wanapaswa kujiulizwa wanaitwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni nani katika Kanisa na Shirika, Wanaitwa kuishi namna gani na kwamba, wanaitwa kufanya nini katika maisha na utume wa Kanisa. Mapadre watambue kwamba, wanaitwa ili kuwa “Alter Christus yaani: “Kristo mwingine”, hadhi inayowataka Mapadre kuwa ni wanyenyekevu, kutambua udhaifu wao wa kibinadamu na hivyo kukimbilia huruma ya Mungu mara kwa mara kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Mapadre watambue kwamba, wanaishi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, changamoto kubwa ni kutambua utambulisho wao, na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu! Wachunge sana ndimi zao kwa kutambua kwamba, wao ni Mawakili wa Kristo Yesu, maneno yao yawe ni maneno ya baraka, faraja na kutia moyo; Wawe mfano bora wa kuigwa katika imani, utu wema na maadili; upendo uwe ni chachu ya huduma bora za kichungaji kwa watu wa Mungu; watangaze na kushuhudia useja; wawe tayari kusoma alama za nyakati, ili kamwe wasimezwe na malimwengu, kwani huko watakiona cha mtema kuni! Mapadre wawe ni mfano bora wa kuigwa katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Waboreshe maisha yao kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu, funga na matendo ya huruma.

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wawe ni mashuhuda wa huruma ya Mungu
Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wawe ni mashuhuda wa huruma ya Mungu

Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba, OSA amewataka waamini kuhakikisha kwamba, wanawatunza vyema Mapadre wao kwa kuwapatia mahitaji msingi, familia zao ziwe ni vitalu bora kwa Mapadre wa leo na kesho. Wakumbuke kwamba, wito wa kwanza kwa kila Mkristo ni Utakatifu wa maisha. Kumbe, Waamini wanao wajibu wa kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, ili kweli Mama Kanisa apate watenda kazi: waaminifu, wachapakazi, waadilifu na watakatifu; wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kama wanashirika wajitahidi kuishi nguzo kuu za Shirika yaani: Karama na Maisha ya Kijumuiya ili kutangaza na kushuhudia Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo Yesu, ili kujibu kilio cha damu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mashemasi wapya kwa Mwezi Julai 2024 ni: Shemasi Abias Mkwetu C.PP.S., Shemasi Andrew Mauya C.PP.S., Shemasi Alfons Gervas C.PP.S., Shemasi Cyprian Damian C.PP.S., Shemasi Deogratias Dimoso C.PP.S., Shemasi Erasmo Mlingo C.PP.S., Shemasi Francis Chrisostom C.PP.S., Shemasi Metodi Kibiriri C.PP.S., pamoja na Shemasi Wilberd Chuwa C.PP.S., na hatimaye, ni Padre Wilibrant Urio C.PP.S.

Wamisionari wa Damu Azizi
04 July 2024, 15:05