Tafuta

Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea, tarehe 24 Agosti 2024 alimbariki na kumsimika Abate Emmanuel Mlwilo, OSB kuwa Abate wa Abasia ya Peramiho, iliyoko Jimbo kuu la Songea, Tanzania. Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea, tarehe 24 Agosti 2024 alimbariki na kumsimika Abate Emmanuel Mlwilo, OSB kuwa Abate wa Abasia ya Peramiho, iliyoko Jimbo kuu la Songea, Tanzania. 

Abate Emmanuel Mlwilo, OSB, Abasia ya Peramiho, Songea

Askofu mkuu Damian Denis Dallu tarehe 24 Agosti 2024 alimbariki Abate Emmanuel Mlwilo, OSB kuwa Abate wa Abasia ya Peramiho, iliyoko Jimbo kuu la Songea, Tanzania. Tukio hili linavunja upweke wa Abasia ya Peramiho kukaa kwa kipindi kirefu bila ya kuwa na Abate. Sasa Abasia ya Peramiho ina Baba, Mwalimu na Kiongozi wa Jumuiya hii ya Wamonaki, wanaojisadaka kuishi nadhiri ya: Ufukara, Useja na Utii kamili kadiri ya Sheria na Kanuni za Mtakatifu Benedikto!

Na Daniel Anthony Ling’wentu. JUGO MEDIA NETWORK, DSM – Tanzania

Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tarehe 24 Agosti 2024 alimbariki na kumsimika Abate Emmanuel Mlwilo, OSB kuwa Abate wa Abasia ya Peramiho, iliyoko Jimbo kuu la Songea, Tanzania. Tukio hili linavunja upweke wa Abasia ya Peramiho kukaa kwa kipindi kirefu bila ya kuwa na Abate. Sasa Abasia ya Peramiho ina Baba, Mwalimu na Kiongozi wa Jumuiya hii ya Wamonaki, wanaojisadaka kuishi nadhiri ya: Utii, uthabiti wa kudumu katika maisha ya kitawa pamoja na wongofu wa mwenendo kamili kadiri ya Sheria na Kanuni za Mtakatifu Benedikto Abate sura ya 58. Abate Emmanuel Mlwilo, OSB alizaliwa tarehe 21 Januari 1970, Manga mkoani Njombe. Baada ya malezi na majiundo yake ya maisha ya kitawa, tarehe 8 Agosti 2007 akaweka nadhiri za daima mikononi mwa Abate Lambert Doer, OSB.

Askofu Damian Denis Dallu akimbariki Abate Emmanuel Mlwilo, OSB
Askofu Damian Denis Dallu akimbariki Abate Emmanuel Mlwilo, OSB

Tarehe 10 Desemba 2007 akapewa Daraja ya Ushemasi na Hayati Askofu Emmanuel Mapunda wa Jimbo Katoliki la Mbinga na hatimaye, tarehe 19 Juni 2008 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Hayati Askofu Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki la Njombe. Katika maisha na utume wake kama Padre kati yam waka 2008 hadi mwaka 2012 alikuwa ni Baba wa maisha ya kiroho katika Hospitali ya Mtakatifu Yosefu, Peramiho na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Peramiho, Jimbo kuu la Songea. Kati ya Mwaka 2012 hadi mwaka 2018 aliteuliwa kuwa ni Paroko wa Parokia ya Mhalule na baadaye akahamishiwa Parokia ya Uwemba, Jimbo Katoliki la Njombe hadi alipochaguliwa kuwa Abate. Na tarehe 3 Juni 2024, Watawa wa Abasia ya Peramiho wakamchagua kuwa Abate wa sita na hatimaye, kubarikiwa na kusimikwa rasmi tarehe 24 Agosti 2024. Hii ni Abasia yenye watawa wa nadhiri za daima 26 na kati yao kuna Mapadre watano. Watawa wa nadhiri za muda wapo 20, wanaovisi ni tisa na wapostulanti 11.

Ibada ya Kumbariki Abate Emmanuel Mwilo, OSB Songea
Ibada ya Kumbariki Abate Emmanuel Mwilo, OSB Songea

Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea, alikazia umuhimu wa thawabu ya mtu kutafuta hekima, ili kuweza kukua kiroho na hatimaye kumfahamu Mwenyezi Mungu vizuri zaidi. Hekima iwe ni ridhaa ya kuelewa mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, ili kutafuta na kuambata ukweli na haki. Amehimiza umoja, ushirika na utume katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kama ilivyokuwa kwa wamisionari waliojisadaka kutangaza na kushuhudia tunu msingi za kiinjili kusini mwa Tanzania. Watawa watambue nguvu na karama za Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao, tayari kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha; kielelezo cha sala na kazi: Ora et Labora, kauli mbiu ya Wabenediktini. Karama na nguvu ya Roho Mtakatifu ni chemchemi ya maisha mapya.

Waamini wakishangilia tukio la kubarikiwa kwa Abate
Waamini wakishangilia tukio la kubarikiwa kwa Abate

Ili kuwapata viongozi wa Shirika, tendo hili lilitanguliwa na ibada ya kufunga, kusali, toba na wongofu wa ndani. Hii ni changamoto kwa watawa wote kushirikiana kikamilifu na Makanisa mahalia katika maisha na utume wao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu mkuu Dallu, ameonya kuhusu mashindano yasiokuwa na tija wala mashiko miongoni mwa watawa, kwani hii ni dhambi ya kuacha kutenda lile linalopasika kutendwa. Kumbe, umoja, ushirika na mshikamano wa watawa na Kanisa zima ni muhimu sana kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hii ni huduma katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Amewataka watawa, wakleri na waamini walei kutumia vyema madaraka yao na kamwe wasithubutu kuchukua nafasi ya Mungu. Madaraka waliyokabidhiwa na Mwenyezi Mungu wayatumie kwa unyenyekevu kama zawadi, kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na kwamba, madaraka yanapata chimbuko lake kutoka katika ridhaa ya watu na Katiba husika. Watu wa Mungu wasiendekeze rushwa kwani itawagharimu sana.

Askofu mkuu Damian Denis Dallu Jimbo kuu la Songea
Askofu mkuu Damian Denis Dallu Jimbo kuu la Songea

Ikumbukwe kwamba, upigaji kura ni tendo la uchaji linalofumbatwa katika kufuata dhamiri nyofu, ili hatimaye, anayechaguliwa aweze kukabidhiwa kwa Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wasipige kura kinyume cha dhamiri zao nyofu. Kazi za kimisionari zinazotekelezwa katika sekta ya elimu, afya, ustawi wa jamii na maendeleo ya wengi ni sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya uinjilishaji na wala si chanzo cha mapato na hivyo, hakuna sababu za msingi kulipizwa kodi na wamisionari kutoka nje ya nchi si wawekezaji wanaohitaji vibali vya kufanyia kazi. Kumbe, wamisionari wametakiwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia maisha ya sala, adili, matakatifu na utume unaosimikwa katika imani, matumaini na mapendo. Hivi ndivyo Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania alivyohitimisha mahibiri yake katika Maadhimisho ya kumbariki na kumsimika Abate Emmanuel Mlwilo, OSB., wa Abasia ya Peramiho, iliyoko Jimbo kuu la Songea, Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Abasia ya Peramiho ni nyumba ya watawa wa kiume wa Shirika la Wabenediktini, Wamisionari wa Mtakatifu Otilia, kutoka nchini Ujerumani lililoanzishwa kunako mwaka 1884 na Padre Andreas Amrhein kwa ruhusa ya Papa Pius XIII kama nyumba ya kuandaa wamisionari wakijerumani ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Tarehe 13, Novemba, 1887 Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, “Propaganda Fide” liliunda Zanzibar ya Kusini kuwa Eneo la Utume (Prefectura Apostolica) na kulikabidhi Shirika la Watawa wa Mtakatifu Benedikto. Kikundi cha kwanza cha Watawa hawa kilifika Pugu, Dar es salaam mwaka 1888 na kuanzisha monasteri, na mwaka 1889, wakati wa vita vya Bushiri, Monasteri hii iliharibiwa na baadhi ya watawa waliuawa, na wengine walirudi Ulaya na kurejea tena Dar es salaam pale ambapo leo panaitwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu.

Maaskofu wakiandama kuingia kwenye Ibada.
Maaskofu wakiandama kuingia kwenye Ibada.

Safari Ya Peramiho. Padre Maurus Hartman, Msimamizi wa Kitume, alifanya safari ya kwanza kuja kusini mwa Tanganyika kutafuta eneo la kuanzisha utume, alivutiwa sana na Wangoni pamoja na mazingira yao. Kunako Mwaka 1897, alimteua Padre Cassian Spiss na wenzake kuja maeneo ya Ungoni ili kuanzisha utume na mwaka 1898, Padre Cassian Spiss na wenzake waliadhimisha Misa ya kwanza katika kilima cha Chiperamiho na ndipo walipofungua rasmi utume wao huko Peramiho. Wamisionari hawa wakiwa Peramiho walijikita katika uinjilishaji wa kina uliogusa mahitaji yam tu mzima katika: Elimu, Afya, Kilimo na Ufundi na hivi walifungua vituo vingine kama vile Kigonsera, Litembo na Lituhi. Lakini Vita ya Majimaji kati ya Mwaka 1905-1907 ilipelekea kuharibiwa kwa utume wa Shirika huko Peramiho na hivyo kupelekea vifo vya baadhi ya wamisionari akiwemo Askofu Cassian Spiss huko Mikuyumbu na watawa wakalazimika kuhama Peramiho kwenda Kigonsera kwa ajili ya usalama wao. Baada ya Vita hii, Wamisionari walirudi na kuanza upya, shughuli zilifanyika vizuri zaidi hadi mwaka 1916 wakati wa Vita Kuu vya kwanza vya Dunia, ambapo wamisionari kutoka Ujerumani wote walifukuzwa kutoka Tanganyika na eneo lao la utume likageuzwa kuwa ni hospitali ya kijeshi.

Takwimu 2024: Nadhiri za daima ni 20, nadhiri za muda 9 wanovisi 11
Takwimu 2024: Nadhiri za daima ni 20, nadhiri za muda 9 wanovisi 11

Baada ya muda, Wabenediktini kutoka nchini Uswisi waliruhusiwa kuja Tanganyika na kuendeleza shughuli za kimisionari Peramiho. Na mwaka 1926 Wabenediktini Wajerumani waliruhusiwa tena kufika Peramiho na kuendeleza kazi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Shughuli za kimisionari ziliendelea vizuri mpaka tarehe 31, Desemba ambapo Peramiho ikawa Abasia na Jimbo la Peramiho (Abbatia Nullius of Peramiho) ambalo mipaka yake sasa ni Jimbo Kuu la Songea, Jimbo la Njombe na Jimbo la Mbinga, na Abate Gallus Steiger akawa Abate na Askofu wa Kwanza. Pamoja na Athari za Vita kuu ya pili ya Dunia (1939-1945) shughuli za Uinjilishaji wa kina ziliendelea na hivi wamisionari waliweza kujenga Kanisa kubwa la Abasia kati ya Mwaka 1942-1948, sanjari na kuanzisha Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino-Peramiho kunako mwaka 1940. Tarehe 16, Februari “Abbatia Nullius ya Peramiho” ilimegwa na kuunda Jimbo la Njombe na tarehe 2, Februari 1969 “Abbatia Nullius ya Peramiho” ilipandishwa hadhi na kuwa Jimbo la Songea.

Abate Emmanuel Mlwilo, Abasia ya Peramiho Jimbo kuu la Songea
Abate Emmanuel Mlwilo, Abasia ya Peramiho Jimbo kuu la Songea

Vipindi Vya Uongozi – Abasia Ya Peramiho kuanzia Mwaka 1934 hadi Mwaka 2024

1.      Abate Askofu Gallus Steiger OSB (1934-1953)

2.      Abate Askofu Eberhard Spiess OSB (1953-1976)

3.      Abate Lambert Doer OSB (1976-2006)

4.      Abate Anastasius Reiser OSB (2006-2017)

5.      Prior Sylivanus Kessy OSB (2017-2020)

6.      Abate Laurent Mkinga OSB (2020)

7.      Prior Melchior Kayombo OSB (2020-2024)

8.      Abate Emmanuel Mlwilo OSB (2024-)

Abasia ya Peramiho
29 August 2024, 15:05