Tafuta

Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, waamini wa Jimbo kuu la Tabora, nchini Tanzania, wakiongozwa na Kardinali Protase Rugambwa wamefanya hija ya kiroho huko Kategile. Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, waamini wa Jimbo kuu la Tabora, nchini Tanzania, wakiongozwa na Kardinali Protase Rugambwa wamefanya hija ya kiroho huko Kategile. 

Kardinali Protase Rugambwa: Bikira Maria Hujaji wa Imani na Matumaini

B. Maria ni hujaji wa imani, matumaini na mapendo, hija aliyoianzisha tangu siku ile alipopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu; akafuatana na Mwanaye mpendwa Kristo Yesu katika Njia ile ya Msalaba na baada ya maisha ya hapa duniani, akapalizwa mbinguni mwili na roho, ili kushiriki utukufu wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu na utukufu wa Mwenyezi Mungu, mwaliko kwa waamini kuwa ni mahujaji wa furaha na uzima wa milele, kwa mfano wa B. Maria

Na Kardinali Protase Rugambwa, Jimbo kuu la Tabora, Tanzania

Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, Mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe, kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos.” Waamini wa Kanisa la Mashariki kwa miaka mingi walikuwa wanaiadhimisha Sherehe hii ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho kama kielelezo cha kulala usingizi wa amani “Dormitio Somnum Mariae.” Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, waamini wa Jimbo kuu la Tabora, nchini Tanzania, wakiongozwa na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, tarehe 15 Agosti 2024 wamefanya hija ya maisha ya kiroho katika Kituo cha Hija cha Kategile, kilichoko kwenye Kigango cha Parokia ya Itaga, Jimbo kuu la Tabora. Hapa ni mahali ambapo watu wateule wa Mungu Jimbo kuu la Tabora wanapata fursa ya kuinjilisha na kuinjilishwa. Kituo hiki kinabeba mapokeo ya enzi kuanzia mwaka 1930-1955 kama mahali pa mapumziko kwa Mafrateli baada ya kuhitimu masomo yao Seminari kuu ya Kipalapala. Kituo hiki kiko umbali wa kilometa 30 kutoka Makao makuu ya Jimbo kuu la Tabora, kuelekea Parokia ya Ulyankulu, Jimbo kuu la Tabora. 

Bikira Maria Amepalizwa Mbinguni Mwili na Roho
Bikira Maria Amepalizwa Mbinguni Mwili na Roho

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora alikuwa na haya ya kusema, katika mahubiri yake: Wapendwa Katika Kristo, katika Kitabu cha Katekismu ya Kanisa Katoliki tunasoma kwenye namba ya kwanza kuwa Mungu amemuumba Mwanadamu kusudi aje kushiriki naye katika Maisha ya heri, na ili iwe hivyo inabidi Mwanadamu amtafute Mungu, amjue na ampende na kwa namna hiyo atakuwa katika safari ambayo mwisho wake ni kumuunganisha na Mungu katika utukufu wake na ndiyo hayo maisha ya heri.  Ndugu zangu katika Kristo, Sherehe tunayoadhimisha leo ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni Mwili na Roho, ni sherehe inayomwonesha mtu ambaye alitambua malengo ya Mungu ya kutuumba na hivyo akaanza kuifanya hiyo safari ya kumjua, kumpenda na mwisho wa safari yake ndo huo tunaoshereheka leo wa Mama Bikira Maria kupalizwa Mbinguni huko kwenye nafasi “iliyotayarishwa na Mungu” kama mwandishi wa Ufunuo wa Yohane anavyoliweka. Huko alikoenda kushiriki katika utukufu wa Mwanaye na utukufu wa Mungu wake. Ni sherehe inayotualika nasi tuwe watu wa safari na watakaofanya safari yenye kutupeleka kwenye furaha isiyo na mwisho, yaani kwenye Utukufu, huko aliko Mama yetu Bikira Maria tunayemshangilia leo. Na hayo yote tuyafanye tukiiga mfano wake. Mama Bikira Maria amekuwa ni mtu wa safari, zenye malengo mahususi, zilizoanza mara tu baada ya kuwa amepashwa habari kuwa atakuwa Mama wa Mungu.  Katika sehemu ya Injili ya Luka tuliyosikia leo, tunaambiwa kuwa Mama MKaria aliondoka, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elizabeti aliyekuwa binamu yake.

Bikira Maria hujaji wa imani, matumaini na mapendo
Bikira Maria hujaji wa imani, matumaini na mapendo

Katika safari hii inaonekana wazi kile alichokifanya Mama Bikira Maria cha kumletea furaha ya pekee huyo binamu yake Elizabeti ambaye hakujizuia bali kuyasema yenye furaha aliyokuwanayo moyoni na aliyoona yanafanyika na yatafanyika kwake Mama Maria.   Bikira Maria naye Pamoja na kupeleka furaha kwa binamu yake, alifanya safari ya kimisionari akimtukuza Mungu kwa mema mengi aliyomtendea, akimwimbia wimbo wa kumshangilia wa “Magnificat.” Mama Maria kwa hayo aliyoyafanya hapa twaweza kumwita mmisionari wa kwanza, anaye safiri kupeleka Injili na Habari njema, na kweli ni yeye aliyemleta na kumpeleka Kristu Ulimwenguni akianzia hapo kwa binamu yake aliyempokea akiwa bado tumboni mwa Bikira Maria.    Baada ya safari hii ya kwanza, Mama Bikira Maria amezifanya safari nyingi na hakika amekuwa ni Mama wa safari, kumbukeni safari ambayo haikuwa rahisi aliyoifanya akielekea Bethlehemu alipokuwa na mimba ya Mtoto Yesu, baadae atalazimika Pamoja na Yosefu kukimbilia Misri wakati Herode anatafuta kumuua Mtoto Yesu. Nayo pia ni safari ambayo haikuwa rahisi. Tutamsikia tena akifanya safari za kwenda Yerusalemu ambako mtoto Yesu atapotelea na watalazimika kufanya safari ya kumtafuta wampate na baadaye wafanye tena safari kurudi nyumbani Nazareti.  Ziko safari nyingine nyingi ambazo twaweza kufikiria zilizofanywa na Mama Maria lakini hatuwezi kusahau ile safari iliyokuwa ngumu aliyoifanya na Mwanae akielekea Kalvari alikoshuhudia kutundikwa kwa Yesu Msalabani hata kifo chake.

Mahujaji wa Jimbo kuu la Tabora Kituo cha Kategile
Mahujaji wa Jimbo kuu la Tabora Kituo cha Kategile

Ndugu zangu, kama nilivyosema huko mwanzo, leo tunasherehekea safari yake ya mwisho ambayo kwetu inatupa furaha na kutualika kumpa shukrani Mwenyezi Mungu aliyemtazama kwa huruma mtumishi wake mdogo ambaye sisi sote tunamuita mbarikiwa tukitafuta kuiga mfano wake wa kutaka nasi tuzifanye safari mahsusi zitakazotuweka kwenye nafasi nzuri na ya pekee kama hiyo ya Mama yetu Bikira Maria. Mama yetu Bikira Maria, kwa kupalizwa Mbinguni ameuacha ulimwengu lakini hajaondolewa ulimwenguni. Kama Mama yetu na Mwombezi wetu, Mama Bikira Maria bado anabaki akiwa karibu nasi. Wote kama Mama Maria alivyokuwa tu wasafiri na tunakwenda kwenye sehemu mbali mbali tusizozijua na tusikofahamu.  Inawezekana kabisa tukapotea na kuikosa njia sahihi ya kufuata katika Maisha yetu ya Imani na kimaadili kumbe tunaalikwa tumtafute Mama Maria tukimwomba atuongoze na kutusaidia kuiona njia.  Njia ni ndefu na safari si rahisi kupitia kwenye “bonde hili lenye machozi” kama tunavyosali daima kwenye sala ya Salamu Malkia Mama mwenye huruma.  Hatuna budi kumbe, kumgeukia huyu Mama “aliyejaa neema” tukimsihi atuombee sisi wakosefu sasa na saa ya kufa kwetu, tukijua kuwa sote tuko wasafiri na bado mwendo ni mrefu.  

Kituo cha Hija Cha Kategile
Kituo cha Hija Cha Kategile

Nasi leo tuliosafiri tukafanya hii Hija, tumshukuru Mwenyezi Mungu leo, aliyetufikisha hapa Kategile ambako kama simulizi za historia zinavyotueleza, Waseminari kwa kusali Rosali mbele ya sanamu ya Bikira Maria, wakimuomba Mwenyezi Mungu afanikishe kupatikana kwa Padre aliyekuwa amepotelea Porini, Padre huyo alionekana siku ya tatu baada ya kuletwa na watu warina asali mpaka kwenye mazingira haya akiwa hai, na hili lilitokea baada ya kuwa Mlezi wa Waseminari aliwaalika waseminari waliokuwa hapa kuanza kusali Rosali mbele ya Sanamu ya Bikira Maria wakiwa wamejiwekea nia kwamba angelipatikana huyo Padre akiwa hai au amekufa basi muda huo huo wangepandisha Sanamu hiyo hapo ilipo ikiwa ni kuonesha shukrani zao kwa Mwenyezi Mungu pia maombezi ya Mama Maria  na kwamba iwe ni alama iliyo juu na yenye kuonekana kama dira kwa mtu yeyote ambaye angepotelea porini kwa kuitazama sanamu hii angeweza kurudi hapo na hivyo kutopotea. Kwetu sisi tuliofanya Hija hii leo, simulizi hili litukumbushe kuwa nasi katika safari zetu tunakuwa tukipotea na kufuata njia za shetani ambazo zaweza kutukosesha hiyo safari ya mwisho ya kwenda kukutana na Mama yetu katika maisha ya umilele, katika utukufu wa Pasaka tutakaoupata baada ya kuwa tumeifuata hiyo njia ya Eva mpya aliyeifuata njia ya Mwanae Yesu Kristu na daima tukijua kuwa ni kwa neema ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Mama maria na kwa maombezi yake tutaweza kufika.  Na tusali: Tunakimbilia ulinzi wako, Mzazi Mtakatifu wa Mungu, usitunyime tukiomba katika shida zetu, utuokoe siku zote kila tuingiapo hatarini, ewe Bikira Mtukufu na mwenye Baraka, Amina.

Kardinali Protase Rugambwa
17 August 2024, 14:15