Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni Mwili na Roho: Imani
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Tunamfurahia Mama Bikira Maria, ametunukiwa heshima ya kutwaliwa mwili na roho, amepalizwa ili ashiriki ushindi wa Mwanawe. Tumsifu Mungu tukiimba pamoja naye ‘Moyo wangu wamwadhimisha Bwana’ tupate neema ya kuurithi uzima wa milele… basi na tutembee kwa haraka kama Maria. Kwa mwanga na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, akiwa ameungana na Maaskofu wenzake kutoka sehemu mbalimbali za dunia, Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili ni sehemu ya Mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki. Bikira Maria tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Ilikuwa ni tarehe Mosi, Novemba 1950, katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, Papa Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa Kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kwamba, “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani” kuwa ni fundisho tanzu la imani ya Kanisa Katoliki. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa maneno mengine, Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Mapokeo ya Kanisa na hasa zaidi wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431, ulipotamka kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, “Theotokos.” Bikira Maria ni Mama yake Kristo Yesu, ambaye ni Mwana wa Baba wa milele, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kweli kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Kanisa linamwita kuwa ni Eva mpya kutokana na utii wake kwa Mwenyezi Mungu. Bikira Maria ni kielelezo cha imani na ishara na utimilifu kamili wa Kanisa. Kumbe, kwa njia ya imani na utii wake thabiti, Bikira Maria akapewa upendeleo wa pekee kuweza kushiriki katika kazi ya ukombozi kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kwa utii wake amekuwa Eva mpya, Mama wa walio hai.
UFAFANUZI: Je, anastahili? Ndio… Mosi, alikingiwa dhambi ya asili iliyo asili ya kifo. Pili mwili wake ulichukua mimba ya Mkombozi, kwa uhusiano huo wa ndani Kristo asingesita kuutukuza mwili uliomchukua mimba. Tatu, ubikira wake haukudhurika bali ulitakaswa na uzazi wa Mwana wa Mungu. Nne, aliambatana na Mwanae katika furaha na uchungu wa mateso kama Simeon alivyotabiri (Lk 2:35). Tano, alisimama chini ya msalaba kwa mateso, ilifaa pia aketi kuume kwa Mwanaye Mshinda, Mfalme na Mtawala kama Malkia. Sita, kwa kumzaa Kristo amekuwa Bibi harusi wa kimbingu, ni vema akae katika vyumba vya Bwana harusi. Kwa sababu hizo, kuoza kaburini kungepingana na hali yake ya utakatifu. Huko mbinguni amefanywa Malkia, amekwezwa juu kuliko makundi ya malaika. Binti huyu Sayuni amejaa neema, Bwana yu pamoja naye. Utii na utayari wake kwa ujumbe wa Gabrieli ulirahisisha mpango wa Mungu na hivi Maria akawa sababu ya ukombozi wake mwenyewe na ukombozi wetu sisi. Bikira Maria anasifika nyakati zote, litania yake inampamba kwa sifa 49, anatajwa MAMA mara 11, BIKIRA mara 7 na MALKIA mara 12. Alama zake kibiblia ni Safina ya Nuhu, kichaka cha Musa, fimbo ya Haruni, paradisi/edeni ya mbinguni, chombo cha ibada, waridi kati ya miiba, ngozi ya Gideon, mnara wa Daudi, Sanduku la Agano, nyota ya asubuhi, makimbilio ya wakosefu, msaada wa wakristo, Tabernakulo ya kwanza, Mama ya Mungu na Mama yetu. Sherehe hii ituhamasishe juu ya uzima ujao, kwamba yeyote anayeishi ipasavyo thawabu yake ni uzima wa milele. Mungu ameweka nafasi mbinguni kwa ajili ya kila mmoja wetu. Hilo litawezekana ikiwa tutafanya kama Maria kwenye Injili ‘kuondoka kwa haraka’ bila kuogopa ubaya wa njia na ugumu wa usafiri kwenda kwa Elizabeti. Tuchangamke tusizubae shetani atatukamata. Tukwepe dhambi, tusali Rozari iliyo muhtasari wa mafumbo ya wokovu. Katika Rozari sisi na Maria tunaunganisha sala halafu Maria anaziongezea ujazo na uzito mbele ya kiti cha enzi… Rozari ni kinga ya maisha na ulinzi wa hakika.
Twende kwa Kristo Yesu kupitia Maria kwa ibada madhubuti. Mosi, ni Ibada ya kweli na ya ndani, ya moyo na akili (Lk1:49). Pili, ni nyororo/soft ikituunganisha na Maria kama Mama na watoto. Tatu, ni takatifu, inatuongoza tuepukane na dhambi na kuishi fadhila za Maria. Nne, hutuimarisha katika wema na matendo ya ibada, uhodari juu ya ulimwengu na ushindi dhidi ya majaribu na tamaa. Tano, haitafuti makuu au faida za binafsi. Bikira Maria ni mfano bora wa akina mama. Kwake mnajifunza maana ya mke mwema, mnajifunza upole, wema, uhodari, uvumilivu na uchapakazi. Injili haijasema Maria alionekana saluni akiongeaongea na mashoste zake. Hatuzuii unadhifu (mwanamke make-up bwana) lakini sukeni na kurudi, mengine achaneni nayo, jipambeni zaidi kwa utakatifu na ukunjufu wa moyo. Mama zetu mngejitoa kikamilifu katika mambo ya Mungu na Kanisa, uongozi na maendeleo ya jamii, sayansi, teknolojia, tiba, haki na amani hakika familia ya mwanadamu ingegeuka na jamii ingekuwa paradiso ya duniani. Changamoto ni pale tunaposhindwa kujasiria au kuhangaikia yasiyo na maana. Bikira Maria ni mfano wa vijana, alijua maana na thamani ya maisha akazingatia ya muhimu, alitunza afya yake, ni kielelezo cha kujitambua, malengo, usafi wa moyo na utakatifu. Kupalizwa Bikira Maria kutupatie hamu ya kufika huko. Safari ni ngumu ikijumuisha vishawishi, majaribu, tabu, adha, mateso na mengi ya kukatisha tamaa. Tusife moyo, tunaye Mama anayetukumbatia na kutusaidia. Tunazo sakramenti zinazotuunganisha na kutumiminia neema. Tunalo Kanisa linalotuongoza na kutunufaisha kwa sala na baraka. Tunalo Neno la Mungu lililo muongozo wa kila siku na tunayo maadili ya Kikristo yenye kutuonyesha lipi la kufaa lipi sio… Maria Malkia aliyepalizwa mbinguni atushike mkono bondeni huku kwenye machozi, amina.