Tafuta

Kristo Yesu ndiye chakula na kinywaji cha uzima wa milele! Kristo Yesu ndiye chakula na kinywaji cha uzima wa milele!  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya 18 ya Mwaka B wa Kanisa: Njaa na Kiu ya Uzima wa Milele!

Hii ni njaa na kiu ya maisha ya milele na ni Yeye Yesu tu ndiye anayeweza kukidhi hamu ya njaa na kiu hiyo, kwa kuwa Ndiye "Mkate wa uzima" (v.35). Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuutafuta Mkate wa uzima sanjari na kujibidiisha kuwatafuta wengine wenye njaa na kiu ya maisha ya uzima wa milele. Kristo Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni, Mkate unaoweza kuzima njaa na kiu ya maisha ya uzima wa milele! Injili inazima kiu!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Katikati ya Edeni Mungu aliweka mti wa uzima na mti wa ujuzi wa mema na mabaya (Mwz 2:9), miti ya kisakramenti yenye maana. Mti wa ujuzi wa mema na mabaya uliashiria kifo, ni ishara ya kujua yote na kutenda yote bila kikomo, mema kwa mabaya, ni uwezo wa kufanyika vimiungu, lakini sisi siyo miungu ni binadamu dhaifu, viumbe, wategemezi tu wa Muumba kwa mapaji na maisha. Watu walimtafuta Kristo Yesu kwa sababu aliwalisha kwa mikate mitano na samaki wawili, wakashiba. Lakini zaidi ya njaa ya mahitaji ya kimwili,  mtu pia ndani yake ana njaa nyingine  muhimu zaidi, ambayo haiwezi kuridhishwa na chakula cha kawaida. Hii ni njaa na kiu ya maisha ya milele na ni Yeye Yesu tu ndiye anayeweza kukidhi hamu ya njaa na kiu hiyo, kwa kuwa Ndiye "Mkate wa uzima" (v.35).  Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuutafuta Mkate wa uzima sanjari na kujibidiisha kuwatafuta wengine wenye njaa na kiu ya maisha ya uzima wa milele. Huu ni Mkate wa Injili unaotolewa kwa watu wote na kushuhudiwa katika maisha mema, adili na matakatifu.

Kristo Yesu ni Mkate unaozima kiu na njaa ya maisha ya milele
Kristo Yesu ni Mkate unaozima kiu na njaa ya maisha ya milele

UFAFANUZI: Katika somo la kwanza – Kut 16:2-4, 12-15)  kujitoa bila kujibakiza, kuwaka na kuungua na kuteketea ili kuangaza! Kumbuka sio Musa atoaye manna ishibishayo njaa ya mwili bali ni Mungu mwenyewe kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Mti wa uzima ni ishara ya uhai ububujikao kutoka ‘uwepo mtakatifu’ wa Mungu na ukamilifu wa maisha ya mwanadamu. Unatajwa mwanzoni na mwishoni mwa Biblia (Mwz 2-3, Ufu 2:7, 22:2, 19), ulikuwa katikati ya bustani kuonyesha kuwa Mungu ndio kiini cha yote na kwamba uhai wa Adamu na Eva ungedumu ikiwa tu maisha yao yangebakia katika muungano wa kudumu na Mungu na pia kumtegemea kama viumbe wake. Adamu na Eva walifukuzwa bustanini na upanga ukailinda njia ya mti wa uzima.. Kristo anatufungulia njia hiyo kwa mti wa Msalaba (1Kor 15:44-49). Wanaotafuta msamaha wa dhambi katika damu ya Kristo iliyomwagika Kalvari hujipatia njia hiyo kuuendea mti wa uzima. Ni mti huo wa ajabu wa Msalaba unaotoa uzima kwa wote wachumao matunda yake (ukombozi) ukimuunganisha Mungu Mkuu na ubinadamu uliokombolewa. Majani yake yafaa kwa uponyaji wa ulimwengu… Kristo Pasaka wetu ndiye Mti halisi wa uzima akivirutubisha viumbe wote, hivi anaposema “Yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa” anamaanisha.

Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa

Mwanadamu anapenda nafuu ya mteremko, wayahudi wanamtafuta Kristo sababu kuna uwezekano wa mikate na samaki ya bure, wanatamani awe Mfalme ili mambo yawe ‘poa’ na Kristo anaona hawakuelewa kabisa maana ya muujiza ule, anawafundisha “msikitendee kazi chakula chenye kuharibika bali chakula kidumucho hata uzima wa milele” (Yn 6:27), chakula hicho ni Yeye Mwenyewe na katika hicho njaa hukoma kwa milele. Mpendwa msiklizxaji na masomaji, ni ipi hasa njaa ya moyo wako? Angesimama Yesu mbele yako na kukuuliza “Mwanangu sema utakacho kitulize njaa yako” utamwambia nini? Wapo watakaosemelea tozo za miamala au ukatili wanaofanyiwa, wengine wataomba fedha na mali ziwe nyingi, au maisha marefu na ya fanaka, furaha katika ndoa na familia zao, vyeo na madaraka, elimu, ndoto za tangu utotoni zitimie… labda tuna njaa ya umaarufu, kuishi kileleni, kuwa watu wa msaada kwa wenzetu, kuishi katika amani.. tuna njaa ya kukubalika, kuonja tunapendwa na wakati mwingine kuona tupo “juu” kuliko wenzetu... hakika tungemwambia vingi. Hata hivyo Kristo ni zaidi tena yu juu sana kuliko hayo yote, anapotualika “Yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa” ana maana inayopita na kuzidi hamu ya nafuu zote tutamanizo. Kumbuka, moyo wa mwanadamu hautosheki, hata akijaliwa kuimiliki sayari nzima ya dunia mkononi mwake bado atatamani amiliki na sayari ya Mars, akipata Mars atatamani na Jupiter na ikibidi “milky way galaxy” kama ilivyo… tusali ili tutambue hitaji halisi, njaa halisi ya roho zetu… ni ipi hiyo?

Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele
Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele

Kwa hakika ni NENO LA UZIMA liongozalo hatua zetu kwenye UZIMA WA MILELE.  Kubungua na kukonda kiroho ndicho chanzo cha udhaifu wote, huondoa kinga dhidi ya vishawishi na kuturushia dhambini. Tunapaswa kutibu ‘utapiamlo’ wa kiroho kwa Mkate wa uzima, Kristo Yesu Mwenyewe hasa nyakati za ugonjwa wa kimwili na mahangaiko ya kibinadamu. “Yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa” ni mwaliko wa kimapendo uletao faraja na pumziko. Ni neno linalotuhamasisha kuungana daima na Kristo na kujichotea neema. Hili litafanikiwa, amesema Yeye mwenyewe, ikiwa tutatenda kazi za Mungu yaani kumwamini Yeye aliyetumwa na Yeye (Yn 6:29). Sio kumtamani Kristo wa Samaki bali Kristo Mwana wa Mungu atoaye uzima wa milele, na hasa Kristo wa Msalaba, na kuhusiana naye 100% kupitia Neno lake, Sakramenti zake, Sala, ibada na kupitia wenzetu wenye uhitaji… Basi na tuyashike mahusia yake kwa kinywa cha Mt. Paulo kwenye somo II (Efe 4:17, 20-24) tukiachana na ubatili wa nia zetu, kuvua utu wa zamani unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya na kufanywa wapya katika roho ya nia zetu, tukavae utu mpya ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli… Mungu mwema na atusaidie!

Liturujia D18 Mwaka B
02 August 2024, 16:53