Tafakari Dominika 18 ya Mwaka B wa Kanisa: Yesu Mkate wa Uzima wa Uzima wa Milele
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 18 ya mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya dominika hii umejikita katika masuala ya chakula na namna ya kula. Ekaristi Takatifu ni chakula kinachotupatia nguvu na uzima unaodumu kwa ajili ya utume wa kuujenga utu mpya wa mwanadamu. Yesu anatuonya kuwa tusikihangaike chakula cha kimwili tu kwa ajili ya tumbo, bali tushughulike na chakula cha kiroho kituleteacho uzima wa milele. Daima tukiwa na shida zinazozidi uwezo wetu, kimbilio letu liwe ni Mungu. Ndivyo anavyotuhimiza mzaburi katika wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii akisema; “Ee Mungu, uniokoe, ee Bwana, unisaidie hima. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, ee Bwana, usikawie” (Zab. 70: 1, 5). Mama Kanisa akilitambua hili, anatuombea sisi wanae kwa matumaini katika sala ya mwanzo akisali sala hii; “Ee Bwana, uwe nasi watumishi wako, utukirimie mema yako yasiyo na mwisho sisi tuombao. Uyatengeneze na kutuhifadhia mema hayo, kwa vile tunaona fahari kwamba wewe ndiwe mwumba na mfalme wetu”. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kutoka (16: 2-4, 12-15). Somo hili linasimulia jinsi Mungu alivyowalisha Waisraeli jangwani. Itakumbukwa kuwa baada ya kukombolewa utumwani Misri, Waisraeli walisafiri safari ndefu ya kuchosha. Walipofika jangwani, walitindikiwa chakula na wakakosa maji. Hivyo wakamnung’unikia Musa na Haruni wakiwaambia; “Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula hata kushiba; kwani mmetutoa huko ili kutuua kwa njaa”. Mungu akasikia manung’uniko yao akamwambia Musa; “Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate na nyama kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku. Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”
Huu ndio wema wa Mungu ambao mzaburi katika wimbo wa katikati anauimba akisema; “Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, ambayo baba zetu walituambia. Hayo hatutawaficha wana wao, huku tukiwaambia kizazi kingine sifa za Bwana, na nguvu zake. Lakini aliyaamuru mawingu juu; akaifungua milango ya mbinguni; akawanyeshea mana ili wale; akawapa nafaka ya mbinguni. Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; aliwapelekea chakula cha kuwashibisha. Akawapelekea hadi mpaka wake mtakatifu, mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume” (Zab. 78:3-4, 23-25, 54). Njaa iliwafanya wana wa Israeli wakate tamaa na maisha, wakanung’unika na kutamani kurudi utumwani Misri. Hawakuthamini kukombolewa kwao kutoka utumwani, wakaona ni aheri wangeendelea kuwa watuwa ili mradi tu waendelee kushibisha tumbo, wazime tu njaa ya kimwili. Je, sisi nasi hatuna fikra na mawazo kama haya ya kutafuta kuzima njaa ya mwili kwa kushibisha tu tumbo hata katika dhambi, na hivyo kuangamiza roho zetu? Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (4:17, 20-24). Katika somo hili mtume Paulo anatufundisha kuwa kutenda dhambi ni kuvaa utu wa zamani. Hivyo anatuonya tusienende kama watu wa mataifa wasiomjua Kristo wanavyoenenda katika ubatili wa nia zao. Maana sivyo tulivyojifunza kwa Kristo. Hivyo anatuasa tuuvue utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudangaya, ili tufanywe wapya katika roho ya nia zetu. Tuuvae utu upya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.
Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 6:24-35). Sehemu hii ya Injili inatueleza mafundisho ya Yesu juu ya habari za chakula kiletacho uzima wa milele, Ekaristi Takatifu. Simulizi linasema kuwa watu walimtafuta Yesu kwa hamu kubwa, wakamkuta ng’ambo ya bahari, na kumuuliza Rabi, umekuja lini hapa? Yesu akijua mawazo yao, aliwaambia ni kwa sababu walikula mikate wakashiba, ndiyo maana wanamtafuta. Yesu anawaonya wasikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kinachowaletea uzima wa milele. Chakula hiki ni kuishi kadiri ya mpango wa Mungu. Lakini watu walitaka ishara kama ya Musa jangwani ili waweze kumwamini. Yesu aliwakumbusha kuwa sio Musa aliyewapa mana jagwani bali ni Mungu. Hata hivyo chakula hicho kilikuwa ni ishara tu na utabiri wa chakula kiletacho uzima wa milele ndiye Kristo mwenyewe kama anavyosema; “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa naye aniaminiye hataona kiu kamwe.” Kumbe, tunaona kuwa somo la kwanza na Injili yanaungwanishwa kwa neno moja, njaa. Njaa ni kuwa na hamu, tamaa au shauku na neno, tendo, kitu au mtu. Njaa yawezakuwa ya kimwili, kiakili, kimaadili au kiroho. Njaa ya kimwili inaletwa na ukosefu au upungufu wa chakula nayo ni silaha kubwa ya maangamizi na ukosefu wa amani. Kwa maana inasababisha njaa ya kimaadili, kiroho, kiakili na kisaikolojia. Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI akishutumu wingi wa fedha unaotumika kwa silaha za kivita anasema; “Si rahisi kuzungumzia amani pale ambapo watu wanateseka kwa sababu ya njaa.” Njaa ya kimwili ni chanzo cha manung’uniko na malumbano kati ya watu na Mataifa. Njaa hii iliwafanya Waisraeli wayakumbuke masufuria ya nyama utumwani Misri, wakanung’unika (Kut. 16: 2-3). Njaa hii iliwafanya watu wamtafute Yesu ili awalishe tena kwa mikate (Yn 6:25–26).
Njaa ya kiroho ni mbaya zaidi kwani roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu. Njaa ya kiroho inawezakuwa ya aina mbalimbali kadiri ya uhitaji wa kitu, hali, au mtu. Inaweza kuwa ni njaa ya matumaini, msamaha au upendo. Mama Teresa wa Kalkuta aliwahi kusema; “kuna njaa ya upendo na kuthaminiwa katika dunia hii kuliko njaa ya mkate”. Akasisitiza; “Ni vigumu zaidi kumaliza njaa ya upendo kuliko njaa ya mkate”. Inaweza kuwa ni njaa ya kumuona yule atiaye uzima ndani mwetu, Mungu Baba. Njaa hii ilimfanya Zakayo apande juu ya mti ili kumuona Yesu. Mzee Simeoni alikuwa na njaa ya kumwona mwokozi kabla ya kufa na baada ya kumwona akasema; sasa Bwana waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani, maana macho yangu yameuona wokovu, uliowaahidia mataifa. Mtakatifu Augustino alisema; “Mwenyezi Mungu umetuumba kwa ajili yako, mioyo yetu haitulii mpaka itakapotulia ndani mwetu.” Njaa hii ya kiroho ndiyo inayotupa hamu na nguvu za kutenda kazi ya Mungu. Yesu alisema chakula chake ni kufanya na kuitimiza kazi ya Mungu (Yn 4:34). Tujishughulishe basi kila mara kuzima njaa ya kiroho ili tupate uzima wa milele. Yesu ni Mkate wa uzima wa milele anayetulisha kwa neno lake na kwa Mwili na Damu yake. Yeye mwenyewe anasisitiza katika antifona ya Komunio akisema: “Mimi ndimi mkate wa uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe” (Yn. 6:35).
Basi tusiwe na woga au kukata tamaa tunapokumbana na magumu katika maisha na kurudia nyuma katika kiimani na kuanza kuhama makanisa huku na huko tukitafuta miujiza kutoka kwa Mungu ili tumwamini. Tukumbuke kuwa kuhamahama kutoka Kanisa moja kwenda lingine kutafuta ishara na miujiza ni kutafuta mikate na sio kumtafuta Yesu, Bwana wa uzima. Kwa ubatizo tumekuwa watu wapya, tumeuvua utu wa kale, tukauvaa utu mpya. Hivyo tusitamani kurudia hali yetu ya zamani. Bali daima tujikabidhi mikononi mwa Mungu naye daima atatulinda na kutuongoza katika uzima wa milele. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala baada ya Komunio anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akituombea kwa matumaini makubwa akisali hivi; “Ee Bwana, utulinde daima na popote sisi uliotutia nguvu kwa chakula cha mbinguni. Utufadhili siku zote ili tustahili ukombozi wa milele.” Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!