Waamini wanakutana na Kristo Yesu kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Katika Neno lake, Sakramenti za Kanisa pamoja na kati ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii Waamini wanakutana na Kristo Yesu kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Katika Neno lake, Sakramenti za Kanisa pamoja na kati ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 19 ya Mwaka B wa Kanisa: Yesu Chakula Cha Uzima wa Milele!

Kristo Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni ili kuzima njaa na kiu ya watu wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, katika hija ya maisha yao wanakutana na Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima. Kristo Yesu anajionesha na kujifunua mwenyewe kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu: Mwili na Damu yake Azizi, Katika Neno lake ambalo ni taa ya kuyaongoza mapito yao pamoja na maskini na wote wanaosukumizwa pembeni

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

WAZO KUU "Na chakula nitakachotoa ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu" (Yn 6:51b) Mpendwa mskilizaji na msomaji, ni Dominika ya 19 katika Neno la Mungu leo tunatafakari jinsi Kristo Yesu, kwa upendo wake, anatugusa katika safari yetu ya maisha kama alivyomuimarisha mtumishi wake Eliya jangwani… Hivi, ni wapi tunapokutana na Yesu? Ni katika Ekaristi Takatifu anapokuja kwetu, anazungumza nasi na kuigusa mioyo yetu, ni ukamilifu wa manna ya kale, chakula cha kiroho “roho ndiyo itiayo uzima mwili haufai kitu; maneno niliyowaambia ni roho tena ni uzima” (Yn 6:63). Halafu tunakutana Naye katika Neno linalotujenga na kutupa uzima, linakuwa chakula. Injili inasema Wayahudi walimnung’unikia Yesu aliposema ameshuka toka mbinguni, hawakuguswa na Umungu wake, sisi tumesadiki tena tumejua ya kuwa Kristo ndiye mtakatifu wa Mungu (Yn 6:69) … hivi tulisikie, tulipokee, tulizungumze na tuliishi Neno lake. UFAFANUZI Injili  Ni Neno la wokovu, taa ya kutuongoza na mwanga wa roho zetu. Neno la Mungu ni Yesu chakula cha uzima, dira ya maisha, kiongozi, chemchemi ya ufunuo wa kimungu. Tunapolisoma tunamjua Yeye na kujitambua sisi. Latuwezesha kujua kilicho bora, kuyatambua mawazo ya Bwana na kuyaishi mapenzi yake. Linaposomwa, kujadiliwa na kupata tafakari yake linakuwa hazina isiyoelezeka iwafaayo waamini. Mpendwa zingatia uzito na uzuri wa neno hili “na chakula nitakachotoa ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu” tunataka nini zaidi? Walimwengu ni mimi, wewe, sisi. Leo na daima Kristo anatupa mwili wake kwa ajili ya uzima wetu.

Dominika ya 19 ya Mwaka B wa Kanisa
Dominika ya 19 ya Mwaka B wa Kanisa

Kristo anatupa uzima kwa kujibu sala yetu, omba kwa imani hatakuacha, mwanadamu aweza kupuuza shida za mwenzake lakini Kristo hapana, anajibu. Kwa namna mbalimbali wengi tunapikwa katika chungu kimoja na Nabii Eliya, tunapita jangwa litishalo, tumekata tamaa. Bila bahati Eliya yule hodari aliyemkabili mfalme Ahab na malkia Jezebel kwa ujasiri mwingi, akamshuhudia Mungu kwa muuji za wa unga na mafuta Salepta na kushindana na manabii wa uwongo 400 moto ukishuka toka mbinguni, amekata tamaa jangwani (1Fal 19:4-8)… “Ee Bwana uniondoe roho yangu, kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu” akajilaza afe. Mungu kaingilia kati, akapigwa bega na kuambiwa hakuna kufa hapa, amka ule safari iendelee, jamaa akala akalala tena! Akaamshwa tena “nimekwambiaje hafi mtu hapa, kula unywe safari lazima iendelee!” ndio safari lazima iendelee, hakuna wa kuzuia maendeleo yako, hakuna wa kukufukuza, kukunyamazisha, wala kukuogopesha, mwamini Mungu, amka ule, safari iendelee. Zingatia neno la Kristo “chakula nitakachotoa ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu”, najua upo jangwani na Eliya usife moyo, Yeye ndiye uzima wako. Jifunze kutumainia nguvu na uweza wake, tegemea huruma yake, jali ulinzi wake, mpokee moyoni mwako utakuwa salama ndio, “umngoje Bwana uwe hodari, upige moyo konde, naam, umngoje Bwana” (Zab 27:13-14) … jipe moyo, amka ule unywe safari ni lazima iendelee. Je, sisi tunaompokea tufanye nini? Tujitoe kwa ajili ya uzima wa wengine kama anavyojitoa kwa ajili yetu. Kujitoa kwetu kuzingatie mausia ya somo II (Efe 4:30-5:2) Mt. Paulo anapotuasa tusimuhuzunishe Roho Mtakatifu tujibidiishe kuwapenda na kuwajali wengine. Tuachane na uchoyo na ubinafsi. Hili ni bomu la wakati wetu; hatari kubwa. 

Ekaristi Takatifu maana yake ni shukrani, Wakristo wawe watu wa shukrani
Ekaristi Takatifu maana yake ni shukrani, Wakristo wawe watu wa shukrani

Kristo Yesu anapotoa mwili wake wanafamilia nao wajitoe kila mmoja kwa mwenzake. Wazazi kwa ajili ya watoto, watoto kwa ajili ya wazazi. Tudumishe maelewano na masikilizano. Tazama, tumewaacha wazazi na tumeambatana pamoja kusudi tuwe kitu kimoja. Uzuri wa sakramenti ya ndoa upo katika kuhudumiana huduma takatifu hivi inafaa kujali maana ya sakramenti hii na faida zake kiroho kuliko sherehe na mambo ya nje. Wengi tunasita kufunga ndoa sababu hatuna fedha ya sherehe. Hatujali sakramenti na neema zake, tunajali sherehe. Uzoefu unaonesha ndoa zinazofungwa kwa mbwembwe ndizo zinazoongoza kwa vitimbi na migogoro isiyokwisha. “Chakula nitakachotoa ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu…” tujitoe kama Yesu anavyojitoa kwa kushirikishana karama tulizojaliwa. Wenye vipaji vya uongozi na waongoze vema, wenye kuimba na wapaze sauti zao kumsifu Mungu, watu wa burudani na waburudishe, wafanya biashara wasitulangue na wakulima wasiuze kila kitu, akiba kidogo ni muhimu. Je, tunayaishi hayo? itakuwa heri yetu, nafasi bado ingalipo ya kuanza upya. Kristo anatutia mwamko na anatuwezesha kupata furaha katika kumsifu kwa kuwa ametuumba kwa ajili yake (Mtakatifu Augustino) kama Mungu alivyomsaidia Eliya atatusaidia na sisi, huzuni yetu inakwenda kuwa furaha, ataondoa hali ya upweke wa jangwani nafsini mwetu na kutujalia ulinzi na huduma ya malaika wake na kutupa ushindi, “maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, katika radhi yake mna uhai, kilio huja usiku lakini asubuhi huwa furaha” (Zab 30:5).

Liturujia D19 Mwaka B
09 August 2024, 15:05