Tafuta

Ni Sakramenti ya umoja na upendo, kimsingi, Ekaristi ni kiini kamili katika Kanisa. Ni Sakramenti ya umoja na upendo, kimsingi, Ekaristi ni kiini kamili katika Kanisa.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya 19 ya Mwaka B wa Kanisa: Umuhimu wa Ekaristi Takatifu

Ekaristi ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Katika Ekaristi tendo la Mungu kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo na kilele cha tendo la watu kumwabudu Mungu katika Kristo hufanyika. Katika Ekaristi mna kila hazina ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe, Pasaka wetu. Ekaristi ndio ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja ule wa Taifa la Mungu ambao unalifanya Kanisa liwepo. Ekaristi Takatifu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 19 ya Mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatualika na kutusisitiza kupokea Ekaristi Takatifu, chakula cha kiroho kinachotupa nguvu ya kuendelea na safari ya kuuelekea kwenye uzima wa milele mbinguni tukiambiwa kila mmoja wetu; “Amka, Inuka ule, maana safari hii ni ngumu kwako.” Ekaristi ni kitovu na kilele cha maisha ya Kanisa, kwa kuwa kwayo Kristo anachagamana na Kanisa lake na waamini wake wote na sadaka ya sifa na shukrani iliyotolewa mara moja Msalabani kwa Mungu Baba. Kwa sadaka hii anamimina neema za wokovu kwa mwili wake ambao ni Kanisa (KKK 1407). Papa Leo XIII anasema Ekaristi Takatifu ni roho ya Kanisa (Denz.3364). Ni Sakramenti ya umoja na upendo, kimsingi, Ekaristi ni kiini kamili katika Kanisa, na Kanisa haliwezi kitu pasipo hiyo. Kwa sababu ni Kristo mwenyewe anayejitoa kweli kama sadaka kwa ajili ya Kanisa katika Ekaristi Takatifu na ni katika Ekaristi Kanisa hufikia uhalisia wake wa juu wa asili yake, yaani, kuwa linaonekana, la daima, na alama wazi ya neema ya wokovu ya Mungu iliyopo duniani kupitia Kristo. Ekaristi ni chemchemu na kilele cha maisha yote ya Kikristo. Katika Ekaristi tendo la Mungu kuutakatifuza ulimwengu katika Kristo na kilele cha tendo la watu kumwabudu Mungu katika Kristo hufanyika. Katika Ekaristi mna kila hazina ya kiroho ya Kanisa, yaani Kristo mwenyewe, Pasaka wetu. Ekaristi ndio ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja ule wa Taifa la Mungu ambao unalifanya Kanisa liwepo. Kwa njia ya adhimisho la Ekaristi tunauungana tayari sisi wenyewe na liturjia ya mbinguni na tunaanza kutangulia kushiriki uzima wa milele (KKK 1324 – 1327, 1407).

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Katika sadaka Ekaristi, Kanisa hutolea maisha ya waamini, masifu yao, mateso yao, sala zao, kazi zao na kuyaunganisha na yale ya Kristo kwa Mungu Baba. Kwa vile ni sadaka, Ekaristi hutolewa kwa waamini wote, wazima na wafu kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na kupata rehema ya Mungu. Kanisa la Mbinguni pia linaungana na matoleo ya Kristo. Daima tukumbuke kuwa uhai wetu wa kiroho na kimwili uko mikononi mwa Mungu, aliyemtetezi wetu kama mzaburi katika wimbo wa mwanzo anavyosema; “Ee Bwana, ulitafakari agano, usisahau milele uhai wa watu wako walioonewa. Ee Mungu, usimame, ujitetee mwenyewe, usiisahau sauti ya watesi wako” (Zab. 74: 20, 19, 22, 23). Mungu kama Baba yetu daima yuko nasi. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi kwa matumaini haya; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, sisi tunathubutu kukuita baba. Ututhibitishie moyoni mwetu neema ya kuwa wana wako, tupate kustahili kuingia katika urithi uliotuahidia.” Somo la kwanza ni la katika Kitabu cha Kwanza cha Wafalme (19:4-8). Somo hili linasimulia habari za kukata tamaa kwa Nabii Eliya kwa maovu yalikithiri ya watu wake kiasi cha kutamani kufa na hivyo kuwatoroka na kukimbilia mlima wa Bwana, Horebu. Akiwa chini ya mretemu, amechoka, yuko hoi, anajiombea roho yake afe akisema; “Yatosha sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.” Eliya yuko katika hali hii kwa sababu ya ukatili wa Yezebeli, mke wa mfalme Ahabu, na kuasi kwa Waisraeli. Yeye ni mtu mwema, mcha Mungu, ndiyo maana Malaika wa Bwana anamwimarisha na kumpa mkate uliookwa juu ya makaa ale na gudulia la maji anywe ili aendelee na safari hadi Horebu, mlima wa Mungu akimwambia; “Inuka, ule, maana safari hii ni ngumu mno kwako. Naye akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu ili kuongea naye ampe mwelekeo anaopaswa kuufuata katika utume wake kama nabii na namna anavyopaswa kuishi.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano

Sisi nasi katika maisha yetu tunapokumbwa na changomoto za kimaisha kutokana na maovu ya wengine tunaweza kukata tamaa. Tunahitaji chakula cha kututia nguvu ili tuweze kusonga mbele. Chakula hiki si kingine bali ni Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo, chakula cha kiroho, kinachotupa nguvu katika safari ya kuelekea mbinguni kwa Mungu Baba. Huu ndio wema wa Bwana ambao Mzaburi katika wimbo wa katikati anatuambia tuuonje akisema; “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema. Nitamhimidi Bwana kila wakati, sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, wanyenyekevu wasikie wakafurahi. Mtukuzeni Bwana pamoja nami, na tuliadhimishe jina lake pamoja. Nalimtafuta Bwana akanijibu, akaniponya na hofu zangu zote. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, wala nyuso zao hazitaona haya. Maskini aliita, Bwana akasikia, akamwokoa na taabu zake zote. Malaika wa Bwana hufanya kituo, akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayetumaini” (Zab. 33:1-8). Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (4:30-5:2). Katika somo hili Mtume Paulo anatukumbusha kuwa kwa ubatizo, Roho Mtakatifu alitutia muhuri, alama ya kufanywa wana wa Mungu, isiyofutika milele. Hivyo tusimsikitishe Roho huyo akaaye ndani mwetu kwa kufarakana kati yetu, bali tuvumiliane na kusameheana kwa moyo wote. Mtume Paulo anasema hivi; “Msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi. Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kama harufu ya manukato.”

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 6:41-51). Sehemu hii ya Injili inatuambia kuwa Wayahudi kwa kuwafahamu wazazi na ndugu zake Yesu, walipata ugumu kumsadiki kuwa alitoka kwa Mungu, wakamnung’unikia, wakashindwa kuamini fundisho la mkate wa uzima, chakula kishukacho toka mbinguni, Mwili na Damu yake Azizi, Ekaristi Takatifu pale Yesu mwenyewe alipowaambia; “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu”. Wao walinung’unika wakisema; “Huyu siye Yesu ambaye babaye ni Yusufu mseremala, na mamaye ni Maria? Sasa asemaje kuwa nimeshuka kutoka mbinguni?” Yesu aliwaambia wasinung’unike, na ili waelewe jambo hili, wawe na Imani, waombe neema na baraka za Mungu ziwawezeshe kulitambua fumbo hili. Yesu anasisitiza kuwa; “Yeye aaminiye yu-na uzima wa milele.” Huu ndio ukuu wa Ekaristi Takatifu, adhimisho la Misa, Sadaka ya Msalaba. Mtaguso wa Pili wa Vatikano unatufundisha kuwa; kila inapoadhimishwa Ekaristi Takatifu kazi ya ukombozi wetu inakamilika. Kwa hiyo, tunaalikwa tushiriki maadhimisho ya Ekaristi Takatifu kila mara kwa wokovu wetu. Ekaristi Takatifu inatupa nguvu za kupambana na dhambi na tabia mbaya ndani mwetu kwa sababu tunakuwa na Roho wa Kristo aliyeshinda dhambi na mauti ndani mwetu.  Ekaristi Takatifu ni namna ya Yesu kukaa kati yetu kama alivyosema; “Tazama mimi niko pamoja nanyi mpaka ukamilifu wa dahari” (Mt. 28:19-20). Ekaristi Takatifu inatuunganisha na Kristo na kutufanya watoto wa Mungu. Kila tunapoipokea tunaungana na Kristo kama Yeye mwenyewe anavyosema; “aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu hukaa ndani yangu nami ndani yake.” Ekaristi Takatifu inatufanya tuwe watoto wa Mungu maana kwayo tunampokea Kristo Yesu, mwana wa Mungu. Yohana anasema; “wale wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu” (Yn. 1:12).

Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani
Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani

Ni wazi ni vigumu kuelewa jambo hili kwa akili ya kibinadamu. Lakini ni wazi kuwa tunakuwa kile tunachokula. Kumbe tunapompokea Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai tunakuwa sehemu ya mwili na damu yake, tunakuwa na ukristo ndani mwetu. Ekaristi Takatifu inatuunganisha sisi kwa sisi. Kama Ekaristi Takatifu inatufanya watoto wa Mungu basi inatufanya ndugu wa Kristo. Hivyo, sote ni ndugu. Ekaristi Takatifu licha ya kutuunganisha hivyo, inatusaidia kumwona mwenzako kuwa ndugu. Ndiyo maana Paulo katika somo la pili anasema; “uchungu wote na hasira viondoke kwenu.” Ekaristi Takatifu ni mwanzo na mwisho wa maisha ya Mkristo. Neema za kuweza kuishi vema maisha ya nje tunazipata katika Ekaristi; maisha ya nje ni mwendelezo wa sadaka ya Ekaristi yanayokamilika katika adhimisho jingine la Ekaristi Takatifu tunapotolea hayo maisha kama sadaka. Hii inaendelea mpaka Kristo atakaporudi.Kumbe basi, Ekaristi Takatifu ni amana ya uzima wa milele ndiyo maana Yesu anasema; “Yule anilaye yu na uzima wa milele.” Ekaristi Takatifu inatushirikisha maisha ya kimungu kwani ni chakula cha kutupeleka mpaka ukamilifu wa maisha ya mbiguni ndiyo maana Yesu anasema; “anilaye mimi nitamfufua siku ya mwisho.” Kama unaamini juu ya fundisho hili, inuka, jiandae vyema, ule, pokea Ekaristi Takatifu, fanya hima kuvunja kuta zote zinazokuzuia kupokea Ekaristi Takatifu ili upate amana ya uzima wa milele. Maana Yesu mwenyewe anasema hivi; “Mkate nitakaotoa mimi, ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu” (Yn. 6:51). Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 19 Mwaka B
07 August 2024, 14:31