Hii ni Karamu ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu chakula cha maisha na uzima wa milele. Hii ni Karamu ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu chakula cha maisha na uzima wa milele.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika 20 ya Mwaka B wa Kanisa: Ekaristi Takatifu: Karamu ya Bwana

Kristo Yesu anayesema “Mimi ndimi chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, mtu akila chakula hiki ataishi milele. Hii ni Karamu ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu chakula cha maisha na uzima wa milele. Hii ni Sherehe, Sadaka ya Kristo; Kumbukumbu hai ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Ni mwaliko wa ujenzi wa ushirika; ili kumtolea Mungu sifa na heshima, kwani Yeye ndiye chemchemi ya matumaini ya waja wake. Hii ni Karamu ya Neno na Ekaristi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican popote pale ulipo wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Dominika ya Ishirini ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Wazo kuu linalotolewa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Neno la Mungu ni Karamu ya Kimasiha, iliyoandaliwa na Kristo Yesu anayesema “Mimi ndimi chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, mtu akila chakula hiki ataishi milele. Hii ni Karamu ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu chakula cha maisha na uzima wa milele. Hii ni Sherehe, Sadaka ya Kristo; Kumbukumbu hai ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Ni mwaliko wa ujenzi wa ushirika; ili kumtolea Mungu sifa na heshima, kwani Yeye ndiye matumaini ya waja wake. Itakumbukwa kwamba, Ekaristi Takatifu ni Karamu inayoundwa na matukio makuu mawili: Meza ya Neno la Mungu ambalo ni mwanga na dira ya kuyaangazaia mapito ya maisha yetu. Kristo Yesu anatukumbusha kwamba, mtu hataishi kwa mkate tu bali katika kila jema litokalo katika kinywa cha Bwana. Kristo Yesu ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati yetu. Ni mkate unaomegwa kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele. Mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu. Rej 1 Kor 10:21. Kristo Yesu anatoa mwaliko akisema, “Njooni kwangu” Mt 11: 28. Sehemu hii ya Neno la Mungu inatumika katika Liturujia ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu; Karamu ya Kimasiha. Yesu anawakaribisha waja wake ili washiriki kwenye karamu yake, chemchemi ya maisha na uzima wa milele. Huu ni mwaliko wa kupyaisha tena maisha ya Kikristo kwa kusoma alama za nyakati.

Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele
Kristo Yesu ni Mkate wa uzima wa milele

Kristo Yesu anasema, Yeye ni Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, akawaambia wasipokula Mwili wake na kuinywa Damu yake azizi hawana uzima ndani mwao. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho. Haya ni maneno yaliyowashangaza sana Wayahudi waliokuwa wanamsikiliza, kiasi cha kujiuliza, inakuaje huyu kutulisha mwili wake? Inawezekanaje? Hata Bikira Maria alipatwa na mshangao mkubwa namna hii, pale alipoambia na Malaika Gabrieli kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu akamwambia Malaika “Litakuaje neno hili? Wayahudi walikwazika na maneno ya Kristo Yesu, kiasi cha kushindwa kuyaamini masikio yao! Kristo Yesu ndiye chakula kilichoshuka kutoka mbinguni: Hapa anakumbushia asili yake; Ishara inayogusia Fumbo la Umwilisho, Mateso, Kifo na Ufufuko wake kwa wafu na hatimaye, kupaa mbinguni. Mwinjili Yohane anakazia kwamba, maisha ya Uzima wa milele yanapata chimbuko lake katika Fumbo la Umwilisho, linalopata hatima yake katika Fumbo la Pasaka ya Bwana inayoadhimishwa katika Fumbo la Ekaristi; Karamu ya Kimasiha. Damu katika Maandiko Matakatifu ni alama ya uhai na agano. Kumbe, Ekaristi Takatifu ni dawa ya maisha ya uzima wa milele. Ndiyo maana Padre wakati akikomunika anasema “Mwili na Damu ya Kristo inilinde nipate uzima wa milele.” Diva ina Mkate ni kazi ya mikono ya mwanadamu.

Ekaristi Takatifu ni Karamu ya Neno na Chakula cha uzima wa milele
Ekaristi Takatifu ni Karamu ya Neno na Chakula cha uzima wa milele

Hii ni karamu ya Bwana inakita mizizi yake katika ukarimu, upendo, mawasiliano; maondoleo ya dhambi, kiasi kwamba, hata maskini wakala mkate ulioshuka kutoka mbinguni. Mwinjili Yohane anatumia fursa kuonesha umuhimu wa Karamu ya Kipasaka; alama na sheria ya kifungo cha upendo; huduma kwa maskini na kwamba, hiki ni kielelezo cha sadaka ya utii hadi kifo cha Msalaba, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Matunda ya maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni mchakato wa ujenzi wa Jumuiya ya Kisinodi inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu; ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali, tayari kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja, upendo, udugu wa kibinadamu na huduma. Karamu hii ya Kimasiha inasimikwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, hekima ya Mungu, lishe ya maisha ya kiroho. Hapa ni mahali ambapo waamini wanajengewa hofu ya Kimungu, kama inavyojidhihirisha katika somo la Kwanza kutoka katika Kitabu cha Mithali 9:1-6. Kitabu cha Hekima ni chemchemi ya akili na furaha ya kweli, yaani Neno wa Mungu yaani Kristo Yesu “ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimetiririka.” Kol 2:3. Kumbe, Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha na uzima wa milele. Ndiyo maana Mzaburi anatoa mwaliko akisema, “Onjeni mwone ya kuwa Bwana ni mwema.” Zab 33:9. Kristo Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele! Huu ni mwaliko wa kushiriki Karamu ya Neno la Mungu, hekima ya Neno la Mungu na lishe ya maisha ya kiroho. Ni mwaliko wa kushiriki Mwili na Damu yake Azizi, kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele.

Liturujia D20 Mwaka B
16 August 2024, 16:32