Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya uzima wa milele.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 20 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Ekaristi Takatifu Chakula Cha Uzima wa Milele

Kuna mambo makuu matatu anayoyasema Yesu. Kwanza ni tamko rasmi likitoa maana ya Ekaristi, faida na umuhimu wake. Katika tamko hili rasmi Yesu anasema hivi; “Mimi ndimi chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, mtu akila chakula hiki ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Ekaristi Takatifu ni mwili na damu ya Yesu, chakula cha uzima wa milele. Tamko la fundisho hili lilikuwa gumu mno kueleweka na wafuasi.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 20 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika 19B yalitilia msisitizo katika suala la kupokea Ekaristi Takatifu, chakula cha kiroho kinachotupa nguvu ya kuendelea na safari ya kuuelekea mbinguni. Masomo ya dominika hii ya 20 Mwaka B wa Kanisa yanaendeleza msisitizo wa umuhimu wa Ekaristi Takatifu, chakula cha uzima wa milele. Ujumbe mahususi ni huu: Tunataka kuwa na uzima wa kimungu ndani mwetu, lazima tule Mwili wa Kristo na kunywa Damu yake.  Tukifanya hivyo tutakaa ndani ya Kristo naye ndani yetu, tutakuwa na muungano na Mungu wetu mtakatifu, na kukaa katika nyumba yake milele yote. Ndiyo maana zaburi ya wimbo wa Mwanzo inavyosisitiza uzuri na ubora wa kukaa katika nyumba ya Mungu ikisema; “Ee Mungu, ngao yetu, uangalie, umtazame uso Kristu wako. Hakika siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku elfu” (Zab. 84: 9-10). Hii ndiyo tamaa ya kila mwanadamu ambayo mama Kanisa katika sala ya mwanzo anaiomba kwa Mungu akisali hivi; “Ee Mungu, umewawekea tayari wale wakupendao mema yasiyoonekana. Utie mioyoni mwetu hamu ya kukupenda, ili kwa kukupenda katika mambo yote na kuliko yote, tupate ahadi zako tunazotamani kupita yote”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Mithali (9:1-6). Somo hili linaelezea sifa za Hekima. Katika Agano la Kale Hekima ni Neno la Mungu, ni nafsi ya Mungu. Ndiye Yesu Kristo katika Agano Jipya kama anavyosema Mwinjili Yohane; “Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukauona utukufu Wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli” (Yn 1:14). Hekima, Neno wa Mungu, alikuwako tangu mwanzo na kwa njia yake kila kitu kiliumbwa.

Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani
Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani

Mwinjili Yohane anasema hivi; “Hapo mwanzo, alikuwako Neno. Naye Neno alikuwa kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa kwa Mungu. Vitu vyote viliumbwa kwa Yeye, wala pasipo Yeye hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. Ndani Yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. Nuru hung’aa gizani nalo giza halikuishinda” (Yn.1:1-5). Yeye huyu Hekima anatualika kwenye karamu akimwambia kila mmoja wetu; “Njoo ule mkate wangu, ukanywe divai niliyoichangaya.” Ni mwaliko wa karamu ya Bwana ndiyo Ekaristi Takatifu, karamu aliyoiandaa Yesu Kristo mwenyewe. Hiki ndicho ambacho Mzaburi katika wimbo wa katikati anatusihi akituambia; “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema. Nitamhimidi Bwana kila wakati, sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, wanyenyekevu wasikie wakafurahi. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, yaani, wamchao hawahitaji kitu. Wana-simba hutindikiwa, huona njaa. Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema. Njoni, enyi wana, mnisikilize, nami nitawafundisha kumcha Bwana. Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima, apendaye siku nyingi apate kuona mema? Uuzuie ulimi wako na mabaya, na midomo yako na kusema hila. Uache mabaya ukatende mema, utafute amani ukaifuatie (Zab. 33, 8, 1-2, 9-14). Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (5:15-20). Somo hili ni mawaidha ya Mtume Paulo kwa Wakristo wa Efeso akiwasihi waishi kadiri ya hekima ya Kikristo wakitafuta furaha yao katika Roho Mtakatifu siyo katika furaha za dunia. Ujumbe huu unatuhusu na sisi nyakati zetu. Tunaaswa tutumie vizuri muda tulionao kwa kutenda mema.

Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya uzima wa milele
Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya uzima wa milele

Tusali na Mzaburi tukiomba hivi daima; “Ee Bwana, unijulishe mwisho wangu, hesabu ya siku zangu ni ngapi, nijue jinsi nilivyo dhaifu” (Zab 39:4). “Utufundishe kuzihesabu siku zetu vyema, tujipatie moyo wenye hekima” (Zab 90: 12). Tunaonywa tusipoteze muda kwa mambo yasiyofaa; tusilewe kwa mvinyo, kwani ulevi humwangamiza mtu, bali tutafute kujazwa na Roho wa Mungu. Muda wa kuishi ni zawadi tunayopewa na Mungu hivyo hatuna budi kuutumia vizuri. Kupoteza muda kwa yasiyofaa ni ukosefu wa shukrani kwa Mungu. Hivyo basi daima tumshukuru Mungu Baba kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo kwa ajili ya yote. Na siri ya mafanikio ni kufanya mem tunayopaswa kuyafanya bila kukawia. “Kwa hiyo, tukiwa bado na wakati, tuwatendee watu wote mema” (Gal 6: 9). Tukumbuke kuwa muda wa kuishi duniani ni mfupi. Tuutumie vyema kwa yanayofaa huku tukiishi kwa furaha na amani. Tupangilie vyema ratiba zetu. Tuwe na mda kusali, kufanya kazi, kupumzika, kula, kunywa na kufurahi na wengine, kucheza na kufanya mazoezi kwa afya ya kimwili, kiakili na kiroho. “Msifanye chochote kwa moyo wa fitina” (Waf. 2: 3). Fitina imejaa kulipa kisasi. Kulipa kisasi ni kupoteza muda wa kukua kiroho, kiutu na kimaadili. Kulipa kisasi ni kupoteza muda wa kusukuma gurudumu la maendeleo mbele.

Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya uwepo endelevu wa Yesu
Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya uwepo endelevu wa Yesu

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (6:51-59). Sehemu hii ya Injili ni mwendelezo wa mafundisho ya Yesu juu ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake, chakula cha uzima wa milele. Katika fundisho hili kuna mambo makuu matatu anayoyasema Yesu. Kwanza ni tamko rasmi likitoa maana ya Ekaristi, faida na umuhimu wake. Katika tamko hili rasmi Yesu anasema hivi; “Mimi ndimi chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, mtu akila chakula hiki ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Ekaristi Takatifu ni mwili na damu ya Yesu, chakula cha uzima wa milele. Tamko la fundisho hili lilikuwa gumu mno kueleweka na kupokeleka. Ndiyo maana manung’uniko yalitokea yakisema; “Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?” Baada ya hayo manung’uniko Yesu alisisitiza fundisho hili kwa tishio hili; “Msipoula mwili wa mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu”. Kumbe suala la kula na kunywa mwili na damu ya Kristo ni suala la Uhai na Kifo. Hakika tusipopokea Ekaristi Takatifu tunakufa kiroho, tunakosa uzima wa kimungu ndani mwetu. Fundisho hili lilizidi kuwa gumu zaidi alipotamka wazi wazi kuwa damu yake “ni kinywaji cha kweli”. Maana katika Agano la Kale damu ilichukuliwa kuwa ni kiini cha uhai. Tunasoma hivi; “Mwisraeli ye yote au mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye atamwinda mnyama au ndege anayeruhusiwa kuliwa ni lazima aimwage damu na kuifunika kwa udongo, kwa sababu uhai wa kila kiumbe ni katika damu yake” (Walawi 17:13). Hivyo ilikatazwa kabisa kunywa damu ya mnyama au ndege.

Ekaristi Takatifu ni Chakula cha Agano Jipya na la Milele
Ekaristi Takatifu ni Chakula cha Agano Jipya na la Milele

Tunasoma hivi; “Po pote mtakapoishi, kamwe msinywe damu ya ndege ye yote wala ya mnyama. Ikiwa mtu ye yote atakunywa damu, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake” (Walawi 7:26-27; 17:14). Hata nyama yenye damu walikatazwa kuila kama vile nyama ya mnyama aliyenyongwa au kuuwawa bila kuchinjwa – mzoga. Tunasoma hivi; “Mtu ye yote, awe mzaliwa au mgeni ambaye atakula mzoga wa kitu cho chote ama kilichouawa na wanyama mwitu ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi kwa kawaida ya ibada mpaka jioni, kisha atakuwa safi. Lakini kama hakufua nguo zake na kuoga, atakuwa na hatia kwa kosa hilo” (Walawi 17:15-16). Katika mazingira kama haya ilikuwa vigumu mno kwa fundisho hili kueleweka. Bila shaka hata siku ya Alhamisi Kuu Mitume hawakumuelewa alipotwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa…akisema, twaeni mle, huu ndio mwili wangu…. akatwaa kikombe, akashukuru akawapa akisema, kunyweni nyote…hii ndiyo damu yangu ya agano, itakayomwagika kwa ajili yenu kwa ondoleo la dhambi” (Mt. 26:26-28). Lakini fundisho hili liko wazi. Katika maisha ya kawaida uhai wa mtoto kabla ya kuzaliwa unategemea uhai wa mama. Damu ya mama ndiyo impayo mtoto uhai. Mtoto analishwa chakula anachokula mama, ambacho ni sehemu ya mwili na damu ya mama. Hivyo maisha na uhai wa mtoto hutegemea muunganiko uliopo na maisha ya mama – mwili na damu ya mama. Maisha na uhai wetu wa kiroho unategemea muunganiko wa Kiekaristi tulio nao na Yesu – Mwili na Damu yake Azizi.

Fumbo la Mwili na Damu ya Kristo Yesu halikueleweka na wengi
Fumbo la Mwili na Damu ya Kristo Yesu halikueleweka na wengi

Hii ndiyo ahadi anayoitoa Kristo mwenyewe akisema; “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.” Kumbe basi matokeo ya kuidharau Ekaristi Takatifu na kutoipokea ni kukosa uzima wa uzima wa milele ndani mwetu – tunakufa kiroho. Ndivyo anavyosisitiza Yesu akisema; “Amin, amin, nawaambieni, msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.” Basi tufanye hima kuvunja kuta zinazotuzuia kupokea Ekaristi Takatifu, tufanye hima kuipokea Ekaristi Takatifu kwani ndiyo amana ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu inatuunganisha na Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, uzipokee dhabihu zetu zinazotufanya tushirikiane nawe katika muungano mtukufu, ili tunapokutolea yale uliyotupa, tustahili kukupokea wewe mwenyewe”. Tukiwa na muunganiko na Mungu kwa kupokea Ekaristi Takatifu kwa mastahili, uzima wa milele tutaupata. Hii ni ahadi ya Yesu Kristo mwenyewe kama Antifona ya wimbo wa komunio inavyosema; “Bwana asema: Mimi ndimi mkate wenye uzima ulioshuka kutoka mbinguni; mtu akila mkate huu, ataishi milele” (Yn. 6:51). Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho ya Dominika hii akisali hivi; “Ee Bwana, sisi tuliounganika na Kristu kwa sakramenti hii, tunakuomba kwa unyenyekevu rehema yako, tufanane naye hapa duniani, tustahili kushirikiana naye kule mbinguni.” Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari Dominika 20 B
15 August 2024, 15:55