Tafakari Dominika 21 ya Mwaka B wa Kanisa: Hili Fundisho Ni Gumu
Na Askofu Severine Niwemugizi, - Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara
“Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, ‘Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?’”. Shida ilianzia hapo, hatimaye uvumilivu ulikwisha na baadhi ya wafuasi wakasema, “Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia” Yn 6:52,60). Hawakumuona kama Mungu bali “mtu huyu”! Lazima kuamua! Leo hii kila kona ya dunia unasikia “watu wanajiondoa kanisani”! Ujerumani unasikia juu ya “austritt von der kirche”, kwetu Tanzania unasikia “wakatoliki wanajiunga na madhehebu mengine”, nk. Swali fikirishi ni: kwa nini hii inatokea hivyo? Je, hili ni jambo jipya? Ukiuliza sababu za hili kutokea, huku Ulaya na Marekani utasikia ni kwa sababu mapadre wamefanya makosa ya zinaa, hasa kuwadhalilisha watoto. Ujerumani kuna suala la kodi ya kanisa (kirchen steuer) pia. Huko kwingine unasikia ni kwa sababu mapadre wanakwaza; au wakatoliki hawashibi kwa mafundisho wanayopewa na mapadre wao, nk. Lakini hizo ndizo sababu za kweli? Jibu ni hapana. Hizo sababu nyingine ni “dhambi za mwili” nyingine ni mahitaji ya kibinadamu” (sins of the flesh and human needs), na hizo ni “visingizio” tu (scapegoat reasons). Ukiwa mgonjwa busara ikuelekeze kuwa usikatae dawa kwa kuwa anayekupa dawa hiyo naye ni mgonjwa au ana mapungufu fulani (ni mdhambi, si mkamilifu). Kwa hakika daktari anayekaribia kufa anaweza kukupa au kukuelekeza upate dawa ya kukuponya wewe! Kapteni wa meli aliye kifoni anaweza kuwaokoa abiria wanaoelea wasizame kwa kuwapa maboya au kuwaelekeza yalipo.
Tatizo lipo kwamba kila mmoja ana picha ya Yesu wake anayemtaka au kumkubali. Kuna watu wanamtaka na kumkubali Yesu anayetenda miujiza, anayeleta nafuu ya maisha, anayenipa mke au mume, anayeponya magonjwa, anayenipa mali, anayeniepusha na matatizo ya kazi na maisha. Hawamtaki Yesu anayedai kubeba msalaba, kuwajibika, kuvumilia taabu, kuacha dhambi, kushika amri, kuwa waaminifu katika ndoa au majukumu ya umma, nk. Kwa hiyo nyingi ni sababu za vionjo. Lazima tujiulize kwa nini watu huja kwa Yesu, na kwa nini huamua kumuacha? Na ili abaki na wenye dhamira ya kweli ya kumfuata alimaliza hotuba yake ya katekesi kwa swali: “Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Kwa nini baadhi huondoka Kanisani? Sababu ya msingi ni: kumkataa Mungu na mafundisho yake. Ipo mifano mingi ya watu kuyakataa maneno au mafundisho ya Mungu na maelekezo yake kwao. Na hii haikuanza leo na haitakoma leo au kesho. Ndiyo maana tangu Agano la Kale unasikia wazo la “kuamua ni yupi unayetaka kumtumikia, au kumfuata” (Jos 24:15) Mungu wa kweli au miungu wengine? Ndiyo maana tunakuta wazo la “masalia” (Isa 10:20-22) ambayo Mungu atayakusanya! Injili ya Yohane Mwanataalimungu nguri inatoa sababu ya kweli, “kutokuamini”. Anasema: “Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini” (Yn 6:64), na huo ndiyo mstari wenyewe wa kusuka au kunyoa! Yesu anapomalizia Katekesi yake juu ya mwili wake kuwa chakula cha uzima na damu yake kuwa kinywaji cha kweli, watu wamekwazika na wanaamua na kumwambia ukweli wao wa moyoni: “Neno hili ni gumu” (Yn 6:61) hakuna wa kulifuata!
Na hii ndiyo lugha inayotumiwa na wakataaji wa mafundisho ya Kanisa Katoliki kuwashawishi waamini kuondoka. Inafika mahali washawishi wanasema kwa kuazima lugha ya Kihangaza “bilagoye” (ni vigumu). Huo ndiyo mstari wa kuvuka. Inaonekana wapinzani wa Yesu, wanaolikataa fundisho lake na kuamua kuachana naye na kuondoka ndiyo walio sahihi, ndiyo wenye akili. Wanakuwa na ushawishi mkubwa kuwaaminisha wasikilizaji wao kuwa ule mkate anaousema Yesu siyo mwili wake kweli Yesu, ila alimaanisha tu ushirika naye kiroho siyo “kumla”! Wanayakataa katakata maneno yake mwenyewe Yesu “aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, anakuwa ndani yangu nami ndani yake”. Wanapoamua kuondoka Yesu habadili kauli yake na kuwazuia wasiondoke. Badala yake anawauliza wale “masalia” (mitume wake), “nanyi mnataka kuondoka? Anawataka waamue kubaki au kuondoka. Yesu habembelezi mtu! Kama alivyosema amekuja kuwasha moto, amekuja kuleta upanga. Au unayapokea au unayakataa mafundisho yake, katekesi yake, unabaki naye au unaondoka. Hakuna kubaki katikati, au moto au baridi! Fundisho la Kanisa Katoliki ambalo ni fundisho la Kristo kuwa Ekaristi Takatifu ni Mwili na Damu ya Yesu linalotoka kwenye Injili ya Yohane na kukamilika kwenye Karamu kuu ya Bwana kabla ya mateso yake na kifo linakataliwa hata na baadhi ya wanaojiita wafuasi wa Kristo. Ni hao wanaosema hilo fundisho “lilagoye.” Wanaamua kuondoka, na kujaribu kuwashawishi wengine waondoke. Ni hao wanaosema Yesu wa Wakatoliki hashibishi.
Wanamtaka Yesu anayeshibisha miili, anayewapa mali na utajiri, anayekidhi mahitaji ya kibinadamu. Ni hao wanasema mafundisho ya Wakatoliki hayashibishi, “yalagoye.” Usiposhibishwa na Ekaristi mengine yote unayolishwa kwingineko havitakushibisha kiroho na kama Bwana mwenyewe alivyosema hutakuwa na uzima ndani yako. “Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu” (Yn 6:53). Kuyaelewa haya lazima urejee kwenye maneno ya Karamu ya Bwana na mitume wake (Mt 26:26-29; Mk 14:22-25; Lk 22:17-20; 1 Kor 11:23-26). Bila imani hayaeleweki na hayakubaliki! Ni hao wanasema huhitaji kuangalia picha au sanamu ili kutafakari juu ya Mungu. Wanasahau ni Yesu huyo huyo aliyewakumbusha Waisraeli juu ya agizo la Mungu kule jangwani kwa Musa atengeneze nyoka ya shaba na kuitundika mahali pa juu, ili kila anayeng’atwa na nyoka aitazame sanamu ile na kuponywa. Yesu huyo huyo alinukuu akisema kama alivyoinuliwa huyo nyoka wa shaba yeye pia atainuliwa juu ya mti (msalaba) ili kila amtazamaye aponywe (Hes 21:8-9; Yn 3:14-15). Hilo wanasema ni fundisho gumu (lilagoye)! Anasema Yesu mtu atamwacha baba yake na mama yake ataambatana na mkewe. Hao wawili watakuwa mwili mmoja, na alichounganisha Mungu mwanadamu asitenganishe. Wanakuja wenye “akili” wanasema hiyo siyo kweli, fundisho hilo ni gumu, “lilagoye.” Kule Agano la Kale watu maarufu walikuwa na wake wengi, mifano ni lukuki. Wanasahau kwamba Yesu ameasisi Agano Jipya kwa “amri mpya”!
Wakatoliki wanampa heshima Bikira Maria wakisali Salamu Maria umejaa neema Bwana yu nawe. Wapinzani wanasema hilo fundisho ni gumu. Hawakubali kuwa sala hiyo inatokana na Injili ya Luka, ikiwa ni salamu ya Malaika Gabrieli pale alipofikisha ujumbe wa Mungu kwake Maria, lakini pia salamu ya Elizabeti Mama wa Yohane Mbatizaji alipotembelewa na Maria! Heshima tunayompa sisi Bikira Maria Mama wa Yesu haiwezi kufikia ile aliyopewa na Mungu mwenyewe! “Salamu uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe” (Lk 1:28). Wewe ukimdharau Maria huyo unamdharau Mungu aliyempa heshima ya pekee awe Mama ya Mwana wake Yesu! Shida kubwa ni kujaribu kuyaelewa na kuyaeleza au kuyahubiri mfundisho ya Yesu, ya Mungu na Kanisa lake kwa kutumia akili zao tu. Sasa hivi kuanzisha makanisa imekuwa fasheni. Kila anayejisikia ana kipaji au ujasiri wa kuhubiri anaona ni fursa kuanzisha kanisa awe na wafuasi, na apate kupeleka mkono kinywaji au hata kupata utajiri! Ndiyo maana Mtume Paulo aliwakumbusha na kuwaonya Wakorintho kwamba hakwenda kuwahubiri “siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno wala wa hekima” ili “imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu” (1 Kor 2:1,5). Mtume Petro pia anatukumbusha kwamba: “hakuna unabii katika Maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu” (2Pet 1:20-21). Ukimwacha Yesu wa Ekaristi, unajitenga na Bwana mleta uzima. Utakufa kiroho. Alikazia baada ya baadhi ya wafuasi kunung’unika: “awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule” (6:52), akasema: “msipoula mwili wake Mwana wa Adam na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu” (6:53).
Ndiyo hao leo wanaokomaa wakisema ‘hakumaanisha kumla mwili wake, ila alimaanisha ushirika naye kiroho’. Bado ubishi unaendelea hadi leo! Kugeuka kutoka kwa Ekaristi ni sawa na kutotii amri ya Bwana, kama wazazi wetu Adamu na Hawa walivyofanya. Bwana amesisitiza hata baada ya wasioamini alichofundisha kuondoka: “kuna wengine miongoni mwenu wasioamini” na “hakuna awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu” (6:64,65). Kuikataa Ekaristi (mwili wa Yesu) aliotuagiza kula inamaanisha kukataa urafiki na Yesu, kwa sababu alisema: “Ninyi ni rafiki zangu mkitenda ninayowaamuru” (Yohane 15:14). Tunayakataa maagizo ya Yesu na kuyasikiliza ya ‘watu baki wasiotumwa na Mungu, bali wanajiinua na kujiita mitume na manabii’. Mtakatifu Augustino alisema kuwa Ekaristi Takatifu ni “ishara ya umoja na kifungo cha upendo”. Kumwamini Yesu wa Ekaristi ndiyo ishara kubwa ya imani na kuwa katika ushirika naye Yesu, lakini pia na ushirika na jumuiya ya waamini. Tujihoji kama tunamwamini kweli Bwana kuwa yeye ni chakula na kinywaji chetu. Kama yeye ndiye anayeweza kuzima njaa na kiu yetu ya kiroho. Na kama tunakwazika kuisikia hiyo lugha ya Yesu basi tufahamu kuwa hatutofautiani na wale Wayahudi; imani yetu ni legelege au hatumwamini kabisa; na ufuasi wetu ni wa vionjo, siyo thabiti. Na huo hautufikishi kwenye utukufu wake Kristo Yesu. Kuamini fundisho lake Kristo ni kukubali fumbo lake la umwilisho, sadaka (mateso na kifo) na utukufu wake. Ni kukubali kuwa maneno yake ni roho na uzima. Ni kusimama na Mtume Petro kukiri kuwa yeye Bwana ndiye mwenye maneno ya uzima, hakuna wa kuwa mbadala wake. Tumwombe Bwana neema ya kutusaidia kuyapokea kwa imani mafundisho yake Yesu na Kanisa lake!