Tafuta

Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya 21 Mwaka B wa Kanisa: Msimamo Katika Maisha

Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu! Hapa Liturujia ya Neno la Mungu linakazia umuhimu wa kuwa na msimamo katika maisha ya imani na matumaini!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 21 ya mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuasa kuwa na msimamo mmoja katika maisha, kuwa upande wa Mungu, tukimtumikia huku tukiyaishi mafundisho ya Yesu kuhusu Ekaristi Takatifu. Au kuwa kinyume na Mungu na kuyakataa mafundisho ya Yesu kuhusu Ekaristi Takatifu. Kila mmoja yuko huru kuchagua upande mmoja kwa faida yake au hasara yake mwenyewe. Faida ya kuwa upande wa Mungu ni kusikilizwa naye kila tumwitapo kama zaburi ya wimbo wa mwanzo inayosema; “Ee Bwana, utege sikio lako unijibu. Wewe uliye Mungu wangu, umwokoe mtumishi wako anayekutumaini. Wewe, Bwana, unifadhili, maana nakulilia wewe mchana kutwa (Zab. 86:1-2). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, wewe waiunganisha mioyo ya waamini katika nia moja. Uwawezeshe watu wako wapende hayo unayoamuru, na kutamani hayo unayoahidi, ili katika ulimwengu huu geugeu, mioyo yetu iwe huko kunako furaha za kweli”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Yoshua (24:1-2a, 15-18). Somo hili linahusu kufanya maamuzi katika maisha na kuchukua msimamo unaoeleweka, kuepuka undumilakuwili na kutangatanga. Yoshua anawaambia Waisraeli kuwa hawawezi kuendelea na maisha yasiyo na msimamo. Anawataka wafanye maamuzi, wachague kati ya kumtumikia Mungu aliyewaokoa toka utumwani Misri na kuwapa nchi takatifu au miungu mingine ile ambayo baba zao waliitumikia ng’ambo ya Mto, au miungu ya wale Waamori ambao wanakaa katika nchi yao. Lakini yeye ameshachagua msimamo wake na anauweka wazi akisema; “Mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana”. Waisraeli wanachagua kumtumikia Bwana, Mungu wa kweli wakisema; “Hasha! Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine.” Wakaweka msimamo wao wazi wakisema; “Sisi nasi tutamtumikia Bwana; maana yeye ndiye Mungu wetu.” Huu ukawa msimamo wa Taifa la Israeli.

Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu
Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu

Je, sisi tunamtumikia Mungu wa kweli aliyetuumba na kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi kwa njia ya mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo au tunaitumikia miungu mingine? Kama tunaishi katika dhambi tujue wazi tunatumikia miungu mingine. Lakini kama tunahofu ya kutenda dhambi na tukianguka dhambini tunahuzunika na kumuomba Mungu msamaha katika sakramenti ya kitubio basi tuko upande wa Mungu na Mungu daima atabaki nasi siku zote naye atatuokoa na taabu zetu zote. Ndiyo maana Mzaburi katika wimbo wa katikati anatushauri akisema; Onjeni, mwone ya kuwa Bwana yu mwema. Nitamhimidi Bwana kila wakati, sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, wanyenyekevu wasikie wakafurahi. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, aliondoe kumbukumbu lao duniani. Walilia, naye Bwana akasikia, akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, na waliopondeka roho huwaokoa. Uovu utamwua asiye haki, nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa. Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, haukuvunjika hata mmoja. Uovu utamwua asiye haki, nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa. Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao (Zab. 33: 8, 1-2, 15-22).

Ndoa ya Kikristo inaundwa na mwanaume na mwanamke.
Ndoa ya Kikristo inaundwa na mwanaume na mwanamke.

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (5:21-32). Katika somo hili Mtume Paulo anatueleza ukamilifu wa ndoa ya kikristo kwa mfano wa mapendo ya Kristo kwa Kanisa lake. Kama vile Kristo alipendavyo daima Kanisa, Taifa la Mungu, vivi hivi inawapasa watu wa ndoa kupendana daima. Mtume Paulo anaufananisha muungano na uaminifu kati ya Mungu na watu na muungano na uaminifu wa watu wa ndoa. Jinsi watu wa ndoa wanavyoungana ndivyo na sisi tunavyoungana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu. Hali kadhalika, uaminifu wanaopaswa kuwa nao watu wa ndoa ndio tunaopaswa kuwa nao kwa Kristo. Kama ambavyo wana ndoa hawafurahii wenzi wao kuwadanganya na kuwasaliti kwa kukosa uaminifu, ndivyo ambavyo Mungu anavyochukizwa tunapomuasi na kutumikia miungu mingine. Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (6:60-69). Sehemu hii ya Injili inahitimisha sura ya 6 ya Mwinjili Yohane kuhusu mafundisho ya Yesu juu ya Ekaristi Takatifu, Mkate wa uzima wa milele, Mwili na Damu yake Azizi. Tunaalikwa kufanya maamuzi magumu, kuchagua kupokea Ekaristi Takatifu ili tuwe na uzima ndani mwetu au kutoipokea na kuwa kama wafu ndani mwetu. Baada ya fundisho la kula mwili na kunywa damu yake Yesu kuonekana kuwa ni gumu; wanafunzi na wafuasi wengine waliamua kumuacha Yesu wakisema; “Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia?” Yesu alitambua manung’uniko yao akawaambia; “Je! Neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.” Katika hali hii ya kunung’unika na kurudi nyuma kwa wafuasi wengine, Yesu anawageukia Mitume wake kumi na wawili na kuwauliza; “Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Simoni Petro alijibu akisema; “Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.”

Yesu anayo maneno ya uzima wa milele.
Yesu anayo maneno ya uzima wa milele.

Basi nasi yatupasa kufanya maamuzi kumfuata Yesu, kupokea Ekaristi Takatifu, kula mwili wake na kunywa damu yake ili tupate uzima wa milele au kutokupokea Ekaristi Takatifu, kutokula mwili wake na kunywa damu yake tufe kiroho na kuukosa uzima wa milele. Katika hili kila mmoja yuko huru, hakuna anayelazimishwa. Lakini uhuru huu ni uhuru wa kuwajibika. Kila mmoja anawajibika kwa uchaguzi wake. Mungu daima anaheshimu uhuru wa kila binadamu. Katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati tunasoma hivi: “Leo hii nawapeni uchaguzi kati ya mema na mabaya; kati ya uhai na kifo…kati ya Baraka na laana. Basi chagueni uhai ili mpate kuishi” (30:15-20). Kumbe katika masuala ya Imani tusiwe watu wa kulalamika, maana hakuna anayelazimishwa kuamini au kutokuamini kinachofundishwa. Maana kila mmoja atawajibika peke yake katika kile alichochagua kukiishi mda wake ukifika, kifo. Inawezekana nasi kumwacha Kristo na mafundisho yake kwa kutokuelewa mafundisho yake yanayotolewa na Kanisa kama ilivyokuwa kwa wale waliokuwa wanamsikiliza Yesu mwenyewe. Tukumbuke kuwa kutokuelewa kwetu hakuondoi ukweli wa mafundisho haya. Basi tujitahidi kuelewa tunachoweza kuelewa. Pale tunaposhindwa kuelewa, si kwa kutoeleweka kwa mafundisho bali kwa ufinyu wetu wa kuelewa, tupige magoti na kusema; “Nasadiki.”

Roho ndiyo itiayo uzima mwili haufai kitu
Roho ndiyo itiayo uzima mwili haufai kitu

Daima tubaki upande wa Mungu tukisema kama Habakuk kuwa; “hata kama mitini isipochanua maua; hata kama zabibu hazitazaa zabibu; hata kama mizeituni isipozaa zeituni; hata kama mashamba yasipotoa chakula; hata kama kondoo wakitoweka mazizini; mimi nitaendelea kumfurahia Mungu wangu” (Habakuk 3:17). Tufahamu kuwa mafundisho ya Kanisa ambayo ni ufunuo wa Mungu kwa wanadamu kwa njia ya Roho Mtakatifu kamwe hayatabadilika wala kubadilishwa kwa watu kuyalalamikia au kutokuyaelewa hata kama watu watalilaumu na kulilalamikia Kanisa kuwa haliendani na wakati au halisikilizi matakwa yao. Ndiyo maana Kristo Yesu hakubadili msimamo wa fundisho kuhusu Ekaristi Takatifu. Bali alisisitiza kuwa ni lazima tule mwili wake na kuinywa damu yake ili tupate uzima wa milele maana huo ndio ukweli kuwa aulaye mwili wa Kristo na kuinywa damu yake anao uzima wa milele; naye atamfufua siku ya mwisho. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 21 Mwaka B
21 August 2024, 11:04