Tafuta

Amri kumi za Mungu ni utambulisho wa Waisraeli, dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Amri kumi za Mungu ni utambulisho wa Waisraeli, dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. 

Tafakari Dominika ya 22 ya Mwaka B wa Kanisa: Amri za Mungu na Mapokeo

Masomo ya dominika hii yanatukumbusha umuhimu na ulazima wa kuwa wakarimu, kutenda haki na kuondoa mifumo kandamizi katika jamii zetu. Mafanikio ya hili yanatutaka tuijaze mioyo yetu upendo, upole, wema, ukarimu, haki, huruma na msamaha. Na tukifanya hivyo, chochote tutakacho mwomba Mungu kwa kumlilia atatupatia kama Mzaburi katika wimbo wa mwanzo anavyosema; “Ee Bwana, unifadhili, maana nakulilia wewe mchana kutwa." Zab 86:3.5.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 22 ya mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatukumbusha umuhimu na ulazima wa kuwa wakarimu, kutenda haki na kuondoa mifumo kandamizi katika jamii zetu. Mafanikio ya hili yanatutaka tuijaze mioyo yetu upendo, upole, wema, ukarimu, haki, huruma na msamaha. Na tukifanya hivyo, chochote tutakacho mwomba Mungu kwa kumlilia atatupatia kama Mzaburi katika wimbo wa mwanzo anavyosema; “Ee Bwana, unifadhili, maana nakulilia wewe mchana kutwa. Kwa maana wewe, Bwana, u mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili kwa watu wote wakuitao” (Zab. 86:3, 5). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu uliye na uwezo na nguvu, uliye na kila kitu kilicho chema, ututilie mioyoni mwetu upendo wa jina lako. Uyakuze ndani yetu yale yaliyo mema kwa kutuongezea uchaji; uyalinde kwa tunza yako yale uliyoyakuza”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Kumbukumbu la Torati (4:1-2, 6-8). Katika somo hili Musa anawakumbusha wana wa Israeli kuwa ili waweze kuingia na kuimiliki nchi awapayo Mungu wa baba zao na ili waweze kuishi kwa amani na furaha, lazima wazisikilize, wazishike na kuziishi amri na maagizo ya Mungu kwa moyo wao wote. Katika kufanya hivyo kuna masharti ya kuzingatia; kutokuongeza wala kupunguza neno lolote, katika amri hizo, wazishike na kuzitenda jinsi zilivyo, maana hiyo ndiyo hekima yao, akili zao, na kitambulisho chao machoni pa mataifa. Wakifanya hivyo watakuwa taifa kubwa, watu wenye hekima na akili, na Mungu atakuwa karibu nao kila wamwitapo.

Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha
Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha

Kwa Sakramenti ya ubatizo, sisi nasi tumefanywa taifa teule la Mungu, Taifa kubwa. Hivyo ili tuweze kuishi vyema sharti kuzishika na kuziishi amri za Mungu na maagizo yake kama yalivyo maana ndiyo hekima na akili atupayo Mungu. Tukifanya hivyo tutaishi kwa amani na furaha hapa duniani na kuurithi uzima wa milele, ndiko kukaa katika hema ya Mungu, kuupanda mlima wake mtakatifu. Ndivyo anavyosisitiza Mzaburi katika wimbo wa katikati kwa kuuliza maswali haya na kuyajibu; “Bwana, ni nani atakayekaa katika hema yako? Ni nani atakayefanya maskani yake katika kilima chako kitakatifu? Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, na kutenda haki; asemaye kweli kwa moyo wake. Ni yeye ambaye hakumtenda mwenziwe mabaya, wala hakumsengenya jirani yake. Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, bali huwaheshimu wamchao Bwana. Ni yeye ambaye hayabadili maneno yake, ingawa ameapa kwa hasara yake. Ambaye hakutoa fedha yake apate kula riba, wala hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo hataondoshwa milele (Zab. 15:1-5). Somo la pili ni la Waraka wa Yakobo kwa Watu Wote (1:17-18, 2, 27).  Somo hili linatueleza kuwa chochote chema na kamili tunachokifanya ni kazi ya Mungu anayejifunua kwetu kwa njia ya Yesu Kristo. Wema haubadiliki wala kugeuka geuka maana Mungu aliye wema ni wa milele. Hivyo tunapaswa kutenda yaliyo mema kwa kuwasaidia wenye shida na kujihadhari na yote yanayotutenga na Mungu. Yakobo anatuasa akisema hivi; “Wekeni mbali uchafu na ubaya wote, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani mwenu, liwezalo kuziokoa roho zenu.” Tunapaswa kuliweka katika matendo Neno la Mungu tulisikialo, na kuepuka kutenda dhambi. Maana “dini iliyo safi, na isiyo na mawaa, isiyo na unajisi mbele za Mungu Baba, ni hii: “kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao”. Nasi tukifanya hivyo tutakuwa na hazina mbinguni.

Kuzeni mema yaliyomo ndani mwenu.
Kuzeni mema yaliyomo ndani mwenu.

Injili ni ilivyoandikwa na Marko (7:1-8, 14-15, 21-23). Itakumbukwa kuwa kwa Jumapili tano mfululizo tulisoma Injili ya Yohani sura ya 6 iliyohusu mafundisho ya Yesu juu ya Mkate wa uzima, mwili na damu yake, Ekaristi Takatifu. Kuanzia dominika hii tunairudia Injili ya Marko ambayo ndiyo Injili ya Mwaka B.  Katika sehemu hii ya Injili tunatufundishwa kwamba si matendo ya nje yanayomfanya mtu najisi, bali mawazo maovu yatokayo moyoni yanayotufanya tutende matendo maovu. Yesu anatoa fundisho hii kama jibu kwa swali la Mafarisayo na waandishi walilomuuliza wakisema; “Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi?” Yesu anawajibu kwa kunukuu utabiri wa Nabii Isaya kuwa wao ni wanafiki maana humheshimu Mungu kwa midomo ila mioyo yao iko mbali naye; wanamuabudu bure, wakifundisha na kuyashika mapokeo na maagizo ya wanadamu na kuiacha amri ya Mungu. Baada ya nukuu hiyo Yesu alitoa fundisha hili kuwa; “Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu”. Maana moyoni hutoka mawazo mabaya: uchoyo, wizi, uzinzi, tamaa mbaya, mauaji, wivu, rushwa, ukaidi, ulaghai, masegn’enyo, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, na upumbavu. Ndiyo maana waswahili husema; Lililo moyoni ulimi huiba. Kumbe, ukiongea neno zuri au baya, ulimi unakuwa umeliiba toka moyoni. Hii ndiyo kusema moyo ni makao ya mawazo mazuri au mawazo mabaya. Kumbe ni vyema kuulisha na kuujaza moyo yaliyo mema ili ndani mwake yatoke yaliyo mema.

Waamini wanaitwa kuishi maisha adili na matakatifu
Waamini wanaitwa kuishi maisha adili na matakatifu

Basi tuzingatie haya; Amri za Mungu ni hekima na akili kwani zinatuonyesha ni lipi la kutenda. Amri za Mungu zinatuonyesha mapenzi ya Mungu kwetu, zinatusaidia kuwa wakamilifu, kutenda haki na kusema ukweli. Amri za Mungu zi juu ya mila zetu na sheria nyingine maana zatuongoza katika kutenda mema. Jambo jema ni lile linaloendana na asili au maumbile ya kibinadamu. Amri za Mungu ndizo zatuonyesha lipi ni jema kwa sababu Mungu aliyetuumba ndiye anajua asili yetu. Kwa hiyo, sheria zozote lazima ziendane na Amri za Mungu, siasa ziongozwe na Amri za Mungu, biashara ziongozwe na Amri za Mungu, utaratibu wa nyumbani uongozwe na Amri za Mungu, sheria za nchi ziongozwe Amri za Mungu. Tukumbuke daima kuwa baada ya kifo chetu ili tuingie mbinguni lazima tuwe na jibu la ndiyo kwa maswali haya; Nilipokuwa uchi ulinivika? Nilipokuwa na njaa ulinipa chakula? Nilipokuwa na kiu ulininywesha? Nilipokuwa mgonjwa ulikaja kunifariji? Nilipokuwa gerezani ulikuja kunitazama? Kama majibu yatakuwa ni ndiyo, ndiyo, ndiyo, basi lango la kuingia katika uzima wa milele litafunguka nawe kuingia. Kama majibu yatakuwa ni hapana, hapana, hapana. Basi mbingu hautaiona kamwe. Ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu mama Kanisa anasali akiomba hivi; “Ee Bwana, sadaka tutoayo ituletee daima baraka yako, ili jambo linalotendwa kwa fumbo, likamilishwe ndani yetu kwa nguvu ya sadaka hii”. Nayo antifona ya Komunyo inasisitiza kusema; “Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao (Mt. 5:9-10). Ni wazi kwa nguvu zetu hatuwezi chochote ndiyo maana mama Kanisa anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii katika sala baada ya komunyo anaomba neema na baraka za kiekaristi zitusaidie akisali hivi; “Ee Bwana, sisi tuliolishwa mkate mtakatifu tunakuomba sana, ili chakula hicho cha mapendo kitutie nguvu moyoni, hata tuvutwe kuwatumikia jirani zetu kwa ajili yako”. Na hii ndiyo hamu ya mioyo yetu na tumaini letu.

Tafakari D22
28 August 2024, 14:59